Saturday, June 6, 2009

MIMBA MASHULENI BADO NI TATIZO!

Wengi huchanganyikiwa

Kuna wakati katika mojawapo ya makala zangu humu bloguni niliwahi kueleza juu ya mimba za utotoni. Makala hiyo niliipa kichwa cha habari kisemacho “VIBINTI NA MIMBA ZA UTOTONI!”

Hivi karibuni nimeandika kuhusu mkasa uliompata binti mmoja niliyempa jina la Anita, ingawa halikuwa ni jina lake halisi. Sioni sababu ya kurudia au kukumbusha kile nilichoandika kwa sababu naamini kuwa wasomaji wangu bado wanayo kumbukumbu ya mkasa uliompata binti huyo.

Kwa kuwa binti huyo alipata ujauzito akiwa ndio kwanza ameingia kidato cha pili na hivyo kukatisha masomo, nimeona ni vyema leo nizungumzie tatizo la mimba mashuleni.
Tatizo la mimba masuleni si geni sana kwetu, ni tatizo lililokuwepo na lipo na linaendelea kuwepo japokuwa wanasiasa na wanaharakati kadhaa wanaendelea kulipigia kelele.

Binafsi katika kusoma kwangu kuanzia shule ya msingi mpaka nilipomaliza kidato cha sita nimeshuhudia wasichana zaidi ya 40 wakishindwa kuendela na masomo kwa kupata ujauzito, Hapa nazungumzia wasichana niliosoma nao aidha darasa moja au shule moja kwa ujumla wake, achilia mbali wale waliofanikiwa kutoa na kuendelea na masomo, hapa nazungumzia wale walioshindwa kabisa kuendelea na masomo na ndoto zao kutoweka kwa kuporwa mustakabali wa maisha yao na wanaume wakware.

Tatizo la mimba mashuleni limekuwa ni sugu kuanzia shule za msingi, sekondari mpaka vyuoni kote huko hapafai. Yaani ni jambo la kawaida kabisa kusikia kuwa mwanafunzi fulani ana mimba ya mtu asiyemfahamu.
Kila mwaka kuna maelfu ya mabinti wa shule wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata mimba na hili sio tatizo la hapa nchini peke yake bali ni tatizo la bara la afrika, kwani ukiingia mtandaoni na kusoma takwimu kutoka vyanzo mbalimbali vya habari katika nchi nyingi za Afrika utakutana na mambo ya kutisha humo, kuna wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kujazwa mimba.

Hili tatizo sio tu linawasikitisha wazazi waliotumia fedha zao nyingi katika kumsomesha binti husika aliyepata ujauzito bali pia wanakuwa wameongezewa mzigo wa malezi ya mtoto asiyejulikana ni wa nani. Hii huwakatisha tamaa sana wazazi na ndio sababu wazazi wengi wanahofu ya kuwaendeleza watoto wao wa kike na elimu ya sekondari kwa kuhofia kupoteza muda na fedha zao bure. Kama tulivyoona kwa baba yake Anita alipokataa kumuendeleza mwanae na kutaka kumuoza kwa kile alichodai kuwa watoto wa kike hata wakisomeshwa hawainufaishi familia husika na badala yake hunufaisha familia ya wakwe zake, ingawa haikuwa hivyo kwa Anita, lakini mzee yule hatajiona kuwa alikuwa sahihi kwa kiasi fulani kutokana na binti huyo kupata ujauzito akiwa tu ndio ameingia kidato cha pili?
Hebu tuangalie sababu ambazo zinachangia wanafunzi kupata ujauzito:

Kwa kawaida mtoto yeyote wa kike akishafikisha umri wa kuanzia miaka 9 mpaka 12 anashuhudia mabadiliko katika mwili wake ikiwa ni pamoja na kuziona siku zake, hapa ndipo wazazi wanapopaswa kuzungumza na mabinti zao na kuwaelimisha juu ya kuyapokea mabadiliko hayo na namna ya kupambana na vishawishi vya wanaume na bila kusahau kuwaeleza ukweli kuhusu uwezekano wa kupata ujauzito iwapo watashiriki kufanya ngono. Namshukuru mama yetu alikuwa ni muwazi sana kwetu kiasi kwamba mimi na dada zangu tumemudu kuvuka hizo changamoto mpaka tumeweza kumaliza shule na wengine mpaka vyuoni.

Kama inavyotokea kwa mabinti na ndivyo inavyotokea kwa wavulana, nao wanapofikisha umri wa kubalehe hushuhudia mabadiliko kadhaa katika miili yao.
Nakumbuka mama aliwahi kutuambia wakati fulani, kuwa analolisema kwa watoto wake wa kike ndilo atakalolisema kwa watoto wake wa kiume vile vile, alisema hapo zamani angeweza kusema “huyu si mtoto wa kiume, yeye hana tatizo kwa sababu yeye ndiye anayefanya” lakini hali haiko hivyo siku hizi, kwani kuna gonjwa la ukimwi! Akichelea mwana ataishia kulia……
Mama yetu aliwahi kutuambia kuwa mapenzi ni kama umeme. Wote tunafahamu kuwa umeme ni nguvu inayotumika katika nyanja mbalimbali kuanzia majumbani mpaka viwandani na hutusaidia katika kurahisisha mambo mengi, lakini unapokuja vibaya ajali yake inaweza kuleta maafa makubwa na ya kutisha.

Vile vile hata swala la mapenzi nalo, iwapo mapenzi yatafanywa kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa iwe ni kimila au kidini, hakuna tatizo, lakini yakifanywa hovyo, matokeo yake wote tunayajua, ni kuishia kupata ujauzito, na katika hali ya kuchanganyikiwa mabinti wengi hufiria kutoa mimba hizo na matokea yake hupoteza maisha, wapo wanaojiuwa kwa kuwahofia wazazi, wapo wanaofariki wakati wa kujifungua kwa kifafa cha uzazi kutokana na kutohudhuria kliniki na kupata chanjo.

Wazazi wengi hawawajibiki katika kuwaelimisha mabinti zao na badala yake jukumu hilo wanawaachia waalimu ambao nao wanayo majukumu mengi ya kuandaa masomo na kufundisha,na hivyo maisha ya mabinti hao huwekwa rehani kwa wanaume wakware wenye ndimi zenye asali.


Mabinti wengi wamejikuta wakipata ujauzito kutokana na kutojua kuwa kucheza na wanaume ni sawa na kucheza na moto, na hiyo inatokana na kutopata elimu juu ya mabadiliko ya mwili na hisia za kimapenzi wanapokuwa wamevunja ungo kutoka kwa wazazi wao.

Kwa leo naomba niishie hapa, nikipata muda nitaendelea na mada hii wiki ijayo.

3 comments:

casa da poesia said...

"Negema wangu binti!

casa da poesia said...

"Negema wangu binti"

Yasinta Ngonyani said...

Koero asante kwa hili darasa:-
Ni hivi Nami nilikuwa nafikiria mara nyingi jambo hili la wasichana kukatishwa masomo yao. Huu mtindo wa wasichana kukatishwa masomo yao wakipata mimba, ni sheria mbaya sana kama ipo sheria. Kwa sababu msichana anafukuzwa shule peke yake. Na yule kijana aliyempa mimba anaendelea na masomo yake. Kwa huyu msichana hapo ndio mwisho.

Jambo hili linawafanya wazazi wengi wapuuzi kuwasomesha mabinti zao. Kwa vile wanafikiri ni kupoteza pesa bure. Wao wanaona ni watoto wa kiume ndio wana haki ya kusomeshwa. Kwa mimi naona watu wote wana haki ya kupata elimu na watu wote ni sawa kabisa.

Kama ni hivi basi kungekuwa na sheria ipitishwa na asifukuzwe mmoja wakukuzwe wote.Inashangaza sana Wizara ya elimu inawaza nini?
Pia nadhani kumekosekana somo la kujijua jinsi mabadiliko ya mwili wa msichana na mvulana unavyokuwa. Kwa sababu wengi wanasema wakishavunja ungo(balee) najaribu siku moja tu haifanyi kitu. Kwa hiyo kama angepata hili somo jinsi mzunguko wake unaendaje labda wasichana wengi wangeweza kuyamudu masomo.
Ila nao baba,kaka zetu nao wamezidi kuwa na tamaa. Vibiti vidogo mpo navyo.
Hili hapa nimeshuhudia katika Secondary moja jina nalihifadhi headmaster alimpa mwanafunzi mimba ambaye alikuwa kidato cha nne mwaka wa mwisho. Cha ajabu yeye mwenyewe alichukua hatua na kumfukuza yule msichana.

Najua wenge mtasema wasichana tunazidi kuwa na tamaa pia. Lakini mkiendelea/tukiendelea hivi hatutasonga mbele. Na kingine cha kushangaza utakuta wanaume wanasema mi nataka kuoa mke mzuri na msomi au mke mtaka maendeleo. Je? manafikiri hao wake watatoka wapi kama tunakatishwa masomo mapema na haturuhusiwi kuendele na masomo tena?