Kuna jambo moja lilinikwaza sana wakati fulani. Hivyo nimeona ni vyema nikasema hisia zangu humu ili wanablog wenzangu wanisaidia mawazo.
Mimi ni miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu waliorudishwa majumbani kutokana na migomo iliyovikumba vyuo vikuu vingi hapa nchini kutokana na madai mbali mbali.
Sitaki kujadili kuhusu hilo kwa sababu si sababu ya kero niliyokumbana nayo.
Baada ya kurudishwa nyumbani baba alinishauri nikaripoti ofisini kwake anipangie kazi ya kufanya, kwani kuna kazi nyingi na anahitaji msaada wangu.
Labda niweke wazi kuwa baba yangu anamiliki kijikampuni chake kinachojishughulisha na utoaji huduma mbalimbali za kijamii.
Ukweli sikukubaliana na wazo la baba kwa sababu sikupenda kufanya kazi karibu na baba na badala yake nilitaka nitafute kazi ili baadae na mimi niwe na kitu changu mwenyewe kama vile na yeye alivyotafuta na kuwa na kitu chake mwenyewe.
Pia sikupenda kuwa kuajiriwa na baba kwani nadhani baadhi ya wafanyakazi wa mzee hawatajisikia vizuri na uwepo wangu pale ofisini.
Basi baada ya kubishana sana na baba, ilibidi akubaliane na mimi.
Ukweli ni kwamba baba yangu ananiheshimu sana kwani mimi ni mtaalamu wa kujenga hoja na kuitetea, ni mara chache sana alikuwa akinishinda linapokuja suala la kutofautiana kimtazamo.
Hivyo niliamua kutafuta kazi, niliamua kutumia muda wangu mwingi nikiwa kwenye mtandao pale nyumbani nikijaribu kutuma maombi yangu ya kazi kwenye mashirika tofauti tofauti na wakati mwingine nilipeleka maombi yangu kwa mkono au kwa njia ya Posta, ilimradi kutaka kujaribu kila mahali.
Kuna wakati nilipokea simu moja kutoka kwa mtu nisiyemfahamu, alinijulisha kwamba ameona maombi yangu ya kazi na anataka kunisaidia, hivyo alitaka tukutane tuzungumze kabla ya kufanya usaili ili aweze kunisaidia mambo fulani.
Nilijaribu kumuuliza kwa nini ameamua kunisaidia mimi, mtu ambaye hanifahamu na si ndugu yake, au mtu mwingine, alinijibu kwamba ameona anisaidie kwani amevutiwa sana na CV yangu na ameona kuwa ni mtu ambaye ninafaa kuajiriwa katika shirika lao.
Alitumia muda mwingi kujieleza na kunihakikishia kwamba anayo nia nzuri ya kutaka kunisaidia.
Nilipomuuliza tukutane wapi, alinitaka tukutane kwenye hoteli moja maarufu iliyoko maeneo ya katikati ya jiji.
Nilisita kumkubalia , lakini baada ya kutafakari niliona nimkubalie, hivyo nilikubali ule mwaliko wa yule mtu aliyejitambulisha kwamba ni mmojawapo wa wakurugenzi waandamizi wa lile shirika nilikopeleka maombi yangu.
Siku iliyofuata majira ya jioni nilikwenda pale Hotelini kama tulivyo ahidiana, sikuwa mgeni na mahali na ile Hoteli kwa sababu nilishawahi kwenda pale mara kadhaa kuhudhuria semina wakati nilipokuwa nafanya kazi kwa muda kwenye NGO moja kabla sijajiunga na Chuo kikuu.
Nilipofika pale nilimpigia simu na alinielekeza mahali alipo, nilipofika nilikutana na baba mtu mzima anayeweza hata kunizaa mara tano.
Alijitambulisha na mimi nikajitambulisha, mara akamuita muhudumu na kunitaka niagize kinywaji chochote ninachotaka, niliagiza maji tu, alinitaka nagize mvinyo au pombe yoyote ambayo ninakunywa, lakini nilimkatalia.
Hata hivyo nilimuomba afupishe maongezi kwa sababu baba yngu huwa anapenda sana kufika pale Hoteli na marafiki zake, kusikia hivyo akadakia na kunijulisha kuwa ameandaa mahali pa faragha kwani amechukuwa chumba tutachofanyia maongezi, kisha akanikabidhi kadi ya kufungulia mlango ambayo ilikuwa imeandikwa namba ya chumba.
Nikamuuliza, kwani hatuwezi kufanyia mazungumzo yetu pale mpaka twende chumbani?
Akadai kwamba anataka kunilinda kwa hiyo nisihofu nitakuwa salama.
Nitakuwa salama!!!? mimi na yeye chumbani!!!? Nilimkatalia na kumtaka tufanyie mazungumzo yetu pale la sivyo niondoke zangu, alikubali japo kwa shingo upande.
Mara akaanza kujiongelesha, “ooh unajua wewe ni mzuri sana na una sifa zote za kupata kazi pale lakini unaweza kukwamishwa kwa sababu utatakiwa utoe kitu kidogo, kwani kazi yenyewe imeombwa na watu wengi, na wote wanasifa, lakini nilipoona CV yako nikavutiwa na wewe, hivyo naomba ukubaliane na mimi kiutu uzima ili na mimi nikusaidie”
Nilipomuuliza nikubaliane na yeye kiutu uzima kivipi? kwani kama ni rushwa mimi siwezi kutoa kwa sababu si lazima nifanye kazi kwenye shirika lao.
Ndipo akaniambia nikubaliane nae tukafanye mapenzi, ili aweze kunisaidia.
Nilibaki nikiwa nimeduwaa kwenye kiti, nisiamini kile nilichosikia kutoka kwa yule mzee, alionekana kutokuwa na wasi wasi kabisa wakati akitamka neno lile, na hiyo iliashiria kwamba hiyo ndio tabia yake.
“Unashangaa nini?” aliniuliza bila hata kuonesha dalili ya aibu usoni pake. Nisaidia na mimi nikusaidie, kwani ulimwengu tulionao ni wa kusaidiana, wewe unahitaji kazi na mimi nahitaji mwili wako tatizo liko wapi?
Niliimkatalia, kata kata na kumuonya kwamba asirudie tena kunipigia simu la sivyo nitamuadhiri mpaka ashangae, kwani mimi sio malaya kama anavyofikiria.
Huo ulikuwa ndio mwanzo wa matukio mengine yanayofanana na hayo kunitokea, kwani katika baadhi ya makampuni au mashirika niliyoomba kazi nilikutana na viashiria au mazingira ya kuombwa rushwa ya ngono.
Wengine walikuwa makini sana walikuwa wanatumia njia ya mzunguko katika kufikisha ujumbe kwamba wanachohitaji kutoka kwangu ni Ngono!!!!.
Jamani hivi ni kwa nini hali hii?
Najaribu kuangalia wale wasichana wenzangu ambao wanatoka katika familia duni ambazo mustakabali wa kuendesha maisha yao na ya familia zao ni wao kupata vibarua.
Je kwa hali hii watapona?
Mimi si mtetezi wa haki za wanawake na watoto, ila nimelisema hili kwa sababu limenikuta, nikamudu kukabiliana nalo, kwa sababu mimi ni zaidi ya mwanamke.
Hivi sasa nimefungua kijimradi changu sikosi shilingi mbili tatu, huku nikisubiri mustakabali wa kurudi chuoni kuendelea kukariri kile mtambuzi alichoita maarifa ya wengine pasipo kubuni maarifa yetu wenyewe.
IGP WAMBURA AFUMUA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI
-
*Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus M. Wambura amefanya mabadiliko
madogo kwa Wakuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani. Amemhamisha Naibu...
6 minutes ago
10 comments:
koero, sitosema pole. nitasema hongera. hongera yangu ni kwa sababu leo umewakilisha maelfu ya watoto wa kike wanaolazimishwa kuitoa miili yao ili waajiliwe. haya mambo yanatokea, yanatokea sana. natamani sauti yako itoshe kuwakemea wote. natamani iwe hivyo. ahsante kwa kuongea hilo. wanaume, tufikie mahali tubadilike. ni hayo tu!
Koero mimi binafsi nimesikitika sana na jambo kama hilo, kwakeli dunia imegeuka,ila cha msingi tunatakiwa kuwa makini wote haijalishi kwa mtoto wa kike peke yake bali hata wakiume nao pia wanashawishiwa na jambo kama hilo.
Kwa upande wako mwanablogu mwenzangu napenda kukusihi usikubali kushawishiwa na mambo hayo jitunze, kama Mungu amekujalia kupata kazi nzuri utapata tu bila hata kutoa rushwa ya ngono.
Ahsate.
Dah!! Yaani namaliza ku-post habari yangu ya leo (ama niseme toleo la leo) nakutana na hii. Umemuombea huyo? Ama umemshukuru? Unadhani amekuwa changamoto kwako kuanzisha mradi unaokupa kiasi kidogo lakini ni wako? Unadhani ungefikiria kuanzisha mradi huo bila kukumbana na hayo? Unadhani yaliyokukuta na kwa kuanzisha mradi wako baada ya kusimama imara si msingi mzuri na mafundisho kwa wengine? Nashukuru kuwa sio tu umeshinda "majaribu" bali pia umepata njia m'badala ya kuepukana nayo moja kwa moja, na zaidi umejua kuwa ikitokea watu wakaja kama alivyokuja huyo mzee, unaweza kupata njia nyingine. Tatizo ni namna ya kujikwamua na tatizo kwa namna tulionavyo. Ulimwengu una mengi ambayo tukifikiria kwa umakini yatalipa. Lucky Dube alisema "it is a give or take world, so you gotta take what you can, when you can make the best of it". Swali ni kwamba ni kipi unachotaka ku-make the best of it? Huyo Baba na wewe nyote mnataka ku-make the best out of life opportunities you have, lakini mmoja ana akili za kutumia vibaya. Umeweza kukwamuka, simaa imara, muombee huyo mzee atambue kuwa hajakuangusha bali kasimika mzizi wa uimara ndani yako, kisha mshukuru aliyekuwezesha kuwa na ujasiri (nikimaanisha Mungu kama wamwamini) na baada ya hapo ungana wote walioshinda majaribu ku-CELEBRATE LIFE.
Nimeeleweka lakini?
See you "next ijayo"
Blessings
Koero nakupa hongera sana kwa kuandika mada hii. Ni kweli kabisa wasichana tunadhalauliwa sana.
Endelea hivyo hivyo na nakutakia mwaka mpya. tutaonana mwakani basi!!!
Duuh! aise hii sasa TOO MUCH ingawa ni kawaida. huwa najiuliza vipi akina dada warembo wote wanatetendewa hivyo? lakini nadhani nakupa PONGEZI tu maana mimi naamini UNAWEZA ndiyo maana uliweza.
Nadhani umejifunza kitu hata hivyo nashindwa kusema sana shauri wengi wamemaliza mengi wamesema yenye hekima
Koero hongera sana kwa kuweza kuandika habari hii. Umeonyesha ujasiri. Kwa wengine, isingewezekana.
Pole kwa yaliyokutokea. UamuzI wako ni wa kupongezwa. Je, ni wasichana wangapi wamefanyiwa hivi? Tunakwenda wapi Tanzania? Mambo haya ni ya kufikirisha sana.
POLE DADA, TATIZO WANUME WENGI WANENDESHWA NA MWILI, BADALA YA AKILI.
KAMA ALIVYOSEMA KAKAMTWIBA, INABIDI TUMUOMBEE.
HIVI INGEKUWAJE KAMA UNGEMTEGESHEA KUPITIA TAKUKUKURU?
UNGEPANGA NAE SIKU NYINGINE HALAFU UKAWATAARIFU TAKUKURU.
Nawashukuru wote kwa maoni yenu, Kaka fadhy, dada Yasinta,kaka Mtwiba, Fita, kaka Bwaya, Kaka Mpangala,na mzee wa Utambuzi.
Maoni yenu ni muhiu kwangu na yamenisaidia kunipa ujasiri, wa kuendelea kupambana na changamoto za wanume wakware.
Awali nilihofu kuweka hii habari hapa barazani, nikidhani labda wasomaji watani Critisize.
lakini kumbe wasomaji wa blog hii ni waungwana sana na hiyo itanifanya niwe muwazi kwenu, kwani mimi napenda sana challenge, hasa za maisha.
ok, let me say. thank you once again for your support.
Huo unaitwa ufisadi wa ngono,na umetapakaa sana.Kwanza hongera kwa ujasiri wako.Dada zetu wengine huwa wanashindwa kuwa na ujasiri kama wako.Ni tatizo la kimfumo pia kwa vile sikumbuki lini mara ya mwisho vyombo vya dola vimemwadabisha bosi aliedai rushwa ya ngono.Kwa kuweka stori hii hapa unaweza kuwafungulia mlango akinadada wengine kuweka kero hiyo hadharani.Inaweza isiondoe tatizo hilo mara moja lakini in a long run inaweza kuleta mabadiliko.Again,hongera kwa ujasiri wako.
OMBI nakuomba dada Koero kama una kitu kinachokutatiza uweke hapa maana tunasaidiana sana kadiri nionavyo. wala usiogope kama ulivyosema awali ulipatwa na hofu pengine tutakushambulia. HAPANA hapa mimi naiita kijiwe cha MASWALI MAGUMU lakini yanajibika, ebu angalia BWAYA, KALUSE,KALAMA, MARKUS, SIMON, YASINTA,FADHY, FITA, MZEE WA CHANGAMOTO, na wewe KOERO= hakika tutaweza kushauriana mambo mazuri tupu na kupeana changamoto kidogo.
haya kazi njema karibu nyasa
mimi mnyasa wa nyasa mvuvi hodari
Post a Comment