Saturday, August 22, 2009

DAR ES SALAAM: TANDALE KWA MTOGOLE NA JARAMBA LA SASAMBUA LA SASAMBUA

Niliamka alfajiri na mapema, ilikuwa ni kama saa 10:30, na kujiandaa, pamoja na kuandaa uji wa mgonjwa. Ni wiki sasa mama yangu amelazwa Hospitalini Muhimbili akisumbuliwa na Presha pamoja na kisukari.

Hivyo ndivyo alivyoanza rafiki yangu Zulfa, katika email yake aliyonitumia jana, akinisimulia masaibu aliyokutana nayo juzi jijini Dar es salaam.

Baada ya kujiandaa majira ya saa 11:00 nilitoka na kuelekea kituoni cha basi pale Magomeni Makanya, nilipofika pale nilikuta abiria kadhaa na nikajiunga nao kusubiri daladala, haikuchukua muda daladala moja aina ya Toyota Coster likafika na abiria wote tuliokuwa pale kituoni tukapanda, nilipata siti ya mbele karibu na dereva nikakaa na abiria wote walipoingia tuliondoka. Daladala letu lilikuwa likienda huku likipakia abiria wengine njiani.

Tulipofika maeneo ya Tandale kwa Mtogole basi letu likasimama ili kupakia abiria, na waliingia abiria saba, wanawake watatu waliokuwa wamevaa mahijabu yaliyofunika nyuso zao kama maninja na wanaume wanne waliokuwa wamevaa kanzu.

Walipoingia wote kabla basi halijaondoka, mwanamke mmoja miongoni mwa abiria wale alikwenda moja kwa moja kwa dereva na kuchomoa panga kutoka kibindoni na kumuwekea dereva shingoni na kisha kuzima gari na kuchukua funguo, wakati huo huo miongoni mwa wale abiria mwenye kanzu alimuamuru kondakta akae kwenye kiti huku akiwa amemshikia panga vile vile, wale abiria waliokuwa na mahijabu, tuliodhani kuwa ni wanawake, kumbe walikuwa ni wanaume. Walitandika kitambaa cheupe na kutuamuru abiria wote tuliokuwa ndani ya lile daladala kila mmoja aweke kila alicho nacho pale katika kitambaa akianza na simu. Walikuwa wakiimba ule wimbo maarufu huku Pwani unaotumika wakati wa kumtunza bi harusi kabla ya kuolewa uitwao sasambu sasambu, wakitaka kila mtu asasambue alicho nacho na kukiweka katika kile kitambaa.

Baada ya kuona kama vile tunachelewa walianza kutupiga kwa ubapa wa upanga na kutisha kuwa atakayekuwa mbishi au kujitia ujanja watamuua kwani hawana cha kupoteza, wanawake wote tulinyang'anywa mikoba yetu na cha kushangaza hata kile kikapu klichokuwa na uji wa mgonjwa walikibeba.

Kuna mzee mmoja hakuwa na simu na hiyo ilimgharimu, kwani walimpiga kwa ubapa wa upanga mpaka akajifanya amezirai ndio wakamuacha, wakati zoezi hilo likiendelea vibaka wengine walikuwa nje na kazi yao ilikuwa ni kutishia daladala nyingine zilizotaka kusimama katika eneo lile zisisimame.

Ilikuwa kila daladala likitaka kusimama wanapiga mapanga kwenye bodi ya daladala hilo na kutoa lugha ya vitisho hivyo hakuna daladala au gari lolote lililosimama katika eneo hilo kutokana na eneo hilo kuthibitiwa na vibaka hao.

Baada ya kuhakikisha wametupora kila kitu walitokomea kusikojulikana wakiwa na funguo za gari, na kutokana na juhudi za dereva wa basi lile na kondakta wake walifanikiwa kuliwasha basi letu na tukaenda moja kwa moja hadi kituo cha polisi pale Tandale.

Tulipofika na kutoa ripoti, askari wa zamu waliokuwepo pale kituoni walimshambulia dereva wa basi letu na kondakta wake kuwa ni wazembe kwa kuwa lile eneo linajulikana kuwa ni hatari kwa vibaka ambao hupora hata mchana kweupe inakuwaje yeye asimame kituoni hapo alifajiri yote hiyo? Walidai kuwa madereva wote wa mabasi yanayopita njia hiyo wanalifahamu eneo hilo ambalo wamelipachika jina la mahakama ya simu kutokamna uporaji wa simu uliokithiri katika eneo hilo la Kwa Mtogole.
Karibu abiria wote tuliokuwa pale kituoni ambao tumeporwa tulishikwa na mshangao, kumbe eneo linajulikana kuwa lina vibaka, sasa kwa nini hawathibitiwi na kituo cha polisi hakiko mbali na eneo hilo?

Tuliandikisha maelezo yetu kisha kila mtu akashika njia yake, mimi ilibidi nirudi nyumbani ili kutengeneza uji mwingine wa mgonjwa kwani uji niliokuwa niupeleke kwa mgonjwa umechukuliwa na vibaka.

Basi dada Koero huo ndio mkasa ulionipata mwenzio, na mama yangu sasa hivi ameruhiusiwa na anaendelea vizuri.

Huo ndio mkasa uliompata rafiki yangu Zulfa, na ndio akanitumia email hii ili niweke katika kibaraza cha VUKANI ili kuwahabarisha wasomaji wa kibaraza hiki waishio Dar Es Salaam wachukue tahadhari.

Hiyo ndiyo hali halisi iliyotamalaki katika eneo hilo na hata Manzese. Nakumbuka hivi karibuni nilipokuwa Dar Es Salaam mama mmoja rafiki wa mama yangu anayeishi Kimara, aliporwa hand bag yake akiwa ndani ya daladala wakati akienda kazini asubuhi, tena huyo kibaka aliingia kwenye daladala hilo kama abiria na alichukuwa hand bag ya mama huyo na kushuka bila wasiwasi kama ya kwake huku abiria wakimuangalia.

Pamoja na yule mama kupiga kelele za mwizi lakini hakuna hata abiria mmoja aliyejishughulisha kumkamata kibaka huyo na alitokomea zake bila wasiwasi, wale abiria walimlaumu yule mama eti ni uzembe wake kwani eneo hilo linajulikana kwa vibaka na ndio maana wanawake wanashauriwa kuweka hand bag zao chini ya miguu, na hairuhiusiwi kushika simu mkononi katika eneo hilo na kama ukipigiwa simu si vyema ukapokea kwani ukipokea hiyo simu itachukuliwa na wenyewe wenye simu yao, yaani vibaka.

Naambiwa hali ni mbaya sana katika eneo hilo na tukio kama hilo lililompata rafiki yangu Zulfa sio la kwanza kutokea katika eneo hilo na hata Polisi wetu wanafahamu vizuri sana juu ya matukio ya uporaji yalivyokithiri katika maeneo hayo, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Naamini hatua zisipochukuliwa na jinsi pengo la wenye nacho na wasio nacho linavyozidi kukua basi tutarajie vibaka hawa kupora mchana kweupe kwa staili ya kufunga mtaa.

6 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Heaven Help Us all
Labda wangekamatwa wangekutwa na sare za askari maana wanavyotetewa yawezekana wakawa haohao wanaostahili kulinda.
Tunahitaji KUAMKA

Ramson said...

Koero, sitaki kuamini kuwa hali ya uhalifu katika maeneo hayo imekuwa mbaya kiasi hicho, na sitaki kuamini kuwa hata askari wetu ambao mishahara na marupurupu yao yanatokana na kodi zetu wanakiri udhaifu kuwa hawana uwezo wa kukabiliana na vibaka hao.
Nadhani kuna haja ya kufanya maandamano wakazi wa Dar ili kufikisha kilio chetu kwa wahusika. hivi ni njaa gani hiyo, ya kupora hata uji wea mgonjwa. kunahitajika mikakati endelevu kupambana na uhalifu wa aina hii. mungu atuepushe na hili balaa.

Tram Almasi said...

Hali hii inatisha sana, lakini kinachonitisha mimi ni kuona askari ambaye anajua kabisa uhalifu wa eneo hilo anawalaumu na kuwatishia waliofanyiwa uhalifu!Nafikiri kuna haja ya kupeana taarifa juu ya tukio hili.

Godwin Habib Meghji said...

Tram Almas, unashangaa kwa askari pekee. wananchi wenyewe wamekubali hali hiyo, ndio maana ukiibiwa wanakwambia wewe ulikuwa hujui kuwa sehemu hii ina vibaka. Sasa kwa hali hiyo nani atadai haki yake, kama hajui usalama ni haki yake. Kweli dola imeingia ubia na vibaka. HIYO NDIO NCHI YETU NA HAO NDIO WATU TULIOWAPA DHAMANA YA ULINZI WA RAIA

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli inasikitisha nami pia naona kwa nini serikali/polis kama wanalijua hili jambo wasiwaweke baadhi ya polisi katika eneo hili? Au basi hiyo njia ifungwa au hicho kituo.

MARKUS MPANGALA said...

wanaiba madhabauni washindwe kuteka nyara daladala?
nimepita wiki jana eneo hilo....lakini niliskia habari za aina hiyo kwahiyo washkaji waksema kuwa makini.

wizi upo na naelewa uhusiano wa polisi na wezi hao ama madereva kwani polisi wanaelewa madereva ni walinzi wao wasaidizi na hakuna jipya waposema eneo fulani kuna wezi.......