Monday, September 5, 2011

MCHUMBA ANGU YUKO FINLAND!

Naelekea Uzeeni sasa!




Ni miaka 16 sasa tangu nifahamiane naye, alikuwa ndio kwanza amemaliza kozi yake ya uhasibu na kuajiria katika ubalozi wa mmojawapo ya nchi za Ulaya hapa nchini.


Alipoanza kujitegemea, alipata nyumba iliyoko jirani na nyumbani kwetu, na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana naye. Alikuwa akijiheshimu sana na hakupenda kujichanganya na watu. Alitumia muda wake mwingi nyumbani kwake na kama akiamua kutoka mara nyingi alipenda kuwatembelea ndugu zake a marafiki zake waishio maeneo ya mbali.


Nilibahatika kufahamiana naye wakati fulani ilipotokea shida ya maji, na kwa kuwa, nyumbani kwetu kulikuwa na kisima, alikuja kuomba msaada wa maji na huo ukawa ndio mwanzo wa kufahamiana.


Naam, urafiki wetu ulimea na kukua, kiasi kwamba tulikuwa tukitembeleana mara kwa mara, alitokea kufahamiana na wazazi wangu pia na walimkubali sana, kutokana na jinsi alivyokuwa akijiheshimu.


Jambo moja lililonishangaza, ni kwamba sikuwahi kumsikia akizungumzia juu ya mahusiano yake, nilishikwa na udadisi na siku moja nikamuuliza kma anaye mchumba. Alinijulisha kuwa mchumba ake yuko Finland kwa masomo, nilimdadisi zaidi kama yuko huko kwa muda gani, akanijibu kuwa ni miaka miwili sasa. Alinijulisha kuwa mchumba ake huyo anasoma kule na itamchukua miaka 3 hadi kumaliza masomo yake na ndipo atarejea nchini na kuungana naye.


Ukweli ni kwamba rafiki yangu huyu alikuwa akifuatwa na wanaume wengi tu tena wa kutosha wakitaka kuwa na uhusiano naye, nadhani ni kwa sababu alikuwa ni mrembo sana, lakini alikuwa akiwakataa kwa maelezo kwamba, anaye mchumba tayari ambaye yuko nje ya nchi kwa masomo.


Nilimuheshimu sana kwa msimamo wake. Mwaka uliofuata binti yule alihama katika numba ile na kuhamia maeneo ya Sinza. Nilipoteana naye kwa takriban miaka 16. Ni hivi karibuni nimebahatika kukutana naye, alionekana dhahiri kuwa umri umekwenda.


Alinikaribisha nyumbani kwake maeneo ya Kimara, alinijulisha kuwa amebahatika kujenga nyumba yake mwenyewe. Wiki iliyofuata nilimtembelea nyumbani kwake. Alikuwa amejenga nyumba nzuri na alikuwa ameizungushia ukuta na kuweka geti. Alinikaribisha sebuleni kwake. Alinitambulisha kwa mdogo wake wa kike aliyekuwa akiishi naye ambaye alikuwa akisoma Chuo Kikuu Dodoma, na pia kwa msichana wake wa kazi.


Nilishikwa na udadisi wa kutaka kujua alipo mume wake, na labda kama ana mtoto. Alicheka sana na kisha akanishika mkono na kunipeleka chumbani kwake. Alikuwa na chumba kikubwa chenye nafasi ya kutosha na pia kulikuwa na meza kubwa ambayo ilikuwa imepambwa vizuri na vifaa vya ofisini pamoja na lap top, kwa ajili ya kazi zake.


Aliniacha kwa muda ili niridhishe macho yangu, kisha akaanzisha mazungumzo.


Mwenzangu, alianza simulizi yake, …….. unadhani kipindi kile wakati nakwambia kuwa ninaye mchumba na yuko masomoni Finland ilikuwa ni kweli, la hasha, haikuwa kweli, bali nilikuwa nadanganya tu kwa sababu sikutaka kusumbuliwa na wanaume. Si unajua wanaume wa siku hizi wanapenda kuwachezea wanawake!, sasa mimi kwa kuliepuka hilo nikaona nitumie mbinu hiyo ili kuepuka usumbufu. Nilibaki mdomo wazi….


Basi bi dada………… aliendelea…….. nilipohama pale Mikocheni, na kuhamia Sinza, niliendelea na msimamo mwangu, sikuwapa wanaume nafasi, nilikuwa na malengo yangu na nilitaka nihakikishe yanatimia.


Ni malengo gani hayo…… nilimdadisi……


Kwanza, nilitaka nijenge nyumba yangu mwenyewe, na pia ninunue gari na kuanzisha biashara zangu na sasa nimetimiza malengo yangu, sasa tatizo linakuja.


Tatizo gani tena………..nilimuuliza.


Sitongozwi na wanaume……… na wananiogopa!..............haki ya Mungu Koero, yaani nina wakati mgumu kweli.


Mh! Niliguna…… wewe unadhani tatizo ni nini? Nilimuuliza,


Sijui sababu, lakini, naona kama vile hakuna anayevutiwa na mimi, najitahidi kuongea na wanaume lakini tunaishia kupiga stori tu, na wengine wananitongoza lakini ni waume za watu. Mwenzio naogopa kweli, mpaka nimejenga wasiwasi kuwa labda nimelogwa.


Mh……….Nilishusha pumzi……….Vumilia dada Jane, utampata atakayekufaa, muombe sana Mungu, atakupa mume aliye mwema, nilimpa moyo.


Mh, Koero, umri huu? Unajua mwakani natimiza miaka 39, mwenzio nazeheka hivyo, atanioa nani…. Nimekuwa nikibadilisha makanisa kama nini, katika kuombewa na kote huko naona maombi yangu hayajibiwi.


Marafiki zangu karibu wote wameolewa na wanaishi na waume zao, mimi tu, sijui nina mkosi gani…. Nilimuona Dhahiri machozi yakimlengalenga….


Nilimpa moyo na kumshauri asikate tamaa. Nilimwambia arudi kwenye kanisa lake la awali na ajiunge na kwaya ikiwezekana ashiriki kwenye kamati mbalimbali za kanisa na zitakazomfanya akutane na watu mbalimbali. Nilimwonya awe makini sana na wanaume walaghai kwani wapo wengine wanawezakutumia mwanya huo kummimbisha na kumtelekeza.


Alikubaliana na mimi na tukamaliza mazungumzo yetu kisha nikaondoka kurejea nyumbani…….. mweh dunia hii……. Habari ya dada Jane si kwamba tu ilinishangaza, bali pia ilinisikitisha. Yaani zaidi ya miaka 16 aliishi kwa kusema uongo ili kuwakwepa wanaume! Alichokuwa akikiogopa kwa wanaume ni kitu gani hasa?


Nilibaki nikijiuliza maswali chungu mzima na sikupata majibu. Ndio maana mie nasema wazi, jamaniee sijaolewa na wala sina mchumba Mbeya, Lundu Nyasa, Marekani wala Ulaya, niko Single, ready to mingle….leteni maombi na sifa zenu mtajibiwa…………LOL


20 comments:

sam mbogo said...

Dada,Koero. nimekusoma. tumpe polezake dada huyo kwa uchumba hewa miaka 16.ndoa nikitu kizurisana,lakini pia kina hitaji ujasiri wa hali ya juu sana.kwa huyu dada, nawewe pia kwa uzoefu,kujipa muda walini unataka kumpata mwenzi wako ni muhimu.hakikisha hamu hiyo inatoka kwako na wala siyo kwa washikaji ama ndugu jamaa na marafiki.mimi sioni kama nitatizo, muda utakapofika utaolewa,acha kulazimisha,mshukuru mungu kwa kukupa hayo maisha uliyo yataka,ila usikurupuke,pia usitafute mchumba kupitia humu tandaoni,ina uzuri wake na ubaya wake. we jichanganye nawatu ,na weka vigezo vyako mume utapata.Kaka S.

Yasinta Ngonyani said...

Kwanza kabisa naona dada Jane alitaka kutekeleza malengo yake au nisema alitaka kuonyesha kwamba hata wanawake tunaweza kufanya vitu bila wanaume...hakutaka ile au ule msema unakaa hapa tu nyumba yangu, gari langu nk. Pia naungana na kaka S. kuwa muda ukifika utapata mume wala hakuna haja ya kuangaika.

sam mbogo said...

Dada,Yasinta,ninapo kutana, ama kusoma ,makala inayo husu,mswala ya wana wake,huwa nakuwa nahamu sana ya kutaka swala husika kulizungumzia kwa undani,lakini muda tu una kuwa hautoshi,mimi ni Therapist,ndo maana wakati mwingine najibu au nachangia hoja kutokana na jinsi hoja ilivyo letwa.ila sasa nikitaka kuingia kitaalamu zaid,nakuwa na sita kidogo. sijuwi nifanyeje,hasa, hata kwa kiasi kidogo taaluma iweze kufanya kazi,nahisi kabisa sasa ndo wakati,anyway,unasemaje,nawengine,pia wanasemaje,dada koero sema.
Kaka S.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka S. Ushauri wangu kwanza kabisa fuata moyo wako unasema nini kusaidia au sio...Lakini kama ungeweza kupata muda ingekuwa VIZURI SANA KUTUPA USHAURI WAKO WA KITAALAM SISI WANAWAKE. Kuna mada ipo jikoni ninaiandaa kuhusu wanawake pia nitahitaji maoni yako/yenu pia.

sam mbogo said...

Poa nimekupata, nasubiri /tunaisubiri mada hiyo kwa usongo!
kaka S.

Koero Mkundi said...

Mie nipo tu hapa nasoma maoni yenu.........

Anonymous said...

Mwe nimecheka Koero ulivyomalizia kusema huna mchumba sijui wapi wala wapi. Hata mie nakumbuka kipindi niko msichana ndio nimeanza tu Chuo kikuu nilikuwa nawadanganya watu nina mchumba yuko mjini ili kukwepa usumbufu. Tena na pete ya uchumba niliivaa kabisa. Lakini mimi lengo langu ilikuwa kuchuja maana kipindi kile tunasoma sisi wasichana mkiingia tu mnakuta wanaume wamekaa standby wanasubiri kudaka first year. Mpaka nilipozoea mazingira ya chuo na kujipanga vizuri ndio nilipokubali kuwa na uhusiano na mtu na tena tunaendelea na huo uhusiano leo ni mwaka wa 20 sasa, na tuna familia.

Wakati mwingine ni vizuri kuweka vikwazo lakini viwe na malengo ya muda mfupi. Kama umwanamke uliye imara unaweza kuyafanya hayo yote ukiwa ndani ya ndoa. Mimi nimepata degree ya pili nikiwa ndani ya ndoa, na nimesoma kozi mbali mbali na nyumba nimejenga kwa nguvu zangu mwenyewe na nyingine kwa kushirikiana na mume. Ukifanya kama huyo dada utajikuta uko mpweke na uwezo wa kuzaa unaishia, maana biological time ina tick, utakuta mayai yameishaisha umeingia kwenye menopause.

sam mbogo said...

dada zangu,msimamo ni muhimu sana.kujuwa nini unataka,wewe nasiyo watu watasemaje.mimi naamini mwana mke ni jasiri akiamua.ila hakikisha necha,inafanya kazi yake au inachukua nafasi yake.kuwa narafiki wa kiume wakati unasoma siyo mbaya,nimsimamo wako tu.sidhani kama ukimwambia huyo jamaa yako muwe waangalifu mnapo du hata kuelewa kama kweli anakupenda. kaka s

MARKUS MPANGALA said...

Jane????? Nope, siyo yeye, bali mwingine. na mwingine huyo ni yule yule nimfahamuye. wala siyo Jane, wala siyo miaka 39, ni ile ya 26. Ni Jane? hapana, siyo yeye bali mwingine tu, ajue kuwa kuna kijiji cha Lundu kule ukanda wa ziwa nyasa. Ni huyuhuyu nanihiiiii ....... Lol, anaogopa muda kwenda machweooooo.... ... ni yeye anajua anataka kwenda Lundu, akavue samani wa nyasa. Lol..... ndiyo najua ni wewe au yule yule wa chanda chema huvikwa ...... kidude....... nibipu tu.... +255 764 936655, ewe binti wa mamba miamba, upareni sitanii.......

Fadhy Mtanga said...

anawadanganyeni huyo mchumbaake yupo Mbeya halafu ana wivu ile mbaya..shauri lenu.

chib said...

He he heeee, nyie akina M, Maana tunataja majina kwa ubini...
Hii vita haijaisha tu.
Bahati mbaya au nzuri sheikh Yahya hayupo tena, nina hakika mngeshaenda kupiga ramli ha ha haaa

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ngono jamani

Godwin Habib Meghji said...

Mi napita tu

Anonymous said...

jaman kuweka hapo wazi si kuhangaika, bora umeweka wazi, na mchumba ni popote. Unaweza pata kanisani akawa kimeo, popote Mungu alipopanga ila sio bar wala disko. mimi pia nilianza kuona wenzangu wanaolewa mi nabaki, nilichofanya ni kuomba kwa bidii na kufunga, Mungu amenijibu nimepata mume mzuri na mwema sana.
Omba sana sana, usihame dini Mungu anapatikana popote ni wewe na moyo wako, anasema nitafute maana ninapatikana, hajasema nitafute mahali fulan.. NO. Omba mpenzi tena sana.Mungu atakujibu

Anonymous said...

Vikwzo zaman, sikuhiz ukiweka vikwazo anakimbia. Ila ngono hapana. Ukifanya hivyo wataonja na kukimbia

Simon Kitururu said...

Koero sasa ninii? Umekimbia tena!:-(

nyahbingi worrior. said...

Habari za siku.
Kama mwanablogu kutoka Tanzania,nakuomba kushiriki kuchangia Mchakato wa KUFUFUA JUMUWATA(Jumuiya ya Wanablogu Tanzania).

Tafadhali naomba ufungue hii kurasa ya
http://blogutanzania.blogspot.com/
kisha upendekeze jinsi ya kufufua JUMUWATA.
Ahsante
Luiham Ringo.

Vimax Asli Canada said...

I like it this blog information, thanks for sharing

Obat Kuat Asli said...

I like it this blog information, thanks for sharing