Monday, June 20, 2011

NIMEULIZWA TENA HILI SWALI: KWA NINI NILIAMUA KUITA BLOG YANGU VUKANI?

Vukani


Blog hii itakuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo. Pamoja na yote naamini pia italeta changamoto na migongano ya mawazo, ndio maana nikasema VUKANI.




KWA NINI NILIAMUA KUIITA BLOG YANGU, VUKANI?


Neno VUKANI nimelitohowa kutoka katika lugha ya mama yangu ya kipare.
Neno hili lina maana ya AMKENI, nadhani kaka Mkodo Kitururu atakuwa anafahamu vizuri kwa kuwa ni lugha yake.

Nakumbuka wakati fulani nilikwenda likizo kijijini huko upareni kuwasalimia bibi na babu yangu wanaomzaa mama yangu, basi kila siku asubuhi bibi alikuwa na kawaida ya kutuamsha ili tusali pamoja na alikuwa akitumia neno Vukani. Nilipouliza maana yake nikaambiwa ni Amkeni au kwa msisitizo wa kiingereza WAKE UP. Basi kuanzia siku hiyo nikatokea kulipenda sana hili neno, sijui ni kwa nini lakini lilikuwa linanihamasisha sana kuamka kifikra badala ya kuamka asubuhi tu.

Wakati nilipokuwa nafungua Blog yangu nilikuwa tayari nimeshachagua jina hili, na cha kushangaza nilipoliingiza kwenye mtandao nikagundua kwamba neno hili linatumiwa na makabila mawili ya Ki Zulu na Ki-Xhosa ya nchini Afrika ya Kusini, likiwa na maana moja, yaani Amkeni.

Si hivyo tu bali pia lipo gazeti moja maarufu nchini humo, linaloitwa Vukani.

Kwa maelezo zaidi bofya hapa.

Amkeni nionavyo mimi sio kuamka kutoka usingizini tu bali ni kuamka kifikra na kuhoji kila tulichofundishwa au kuambiwa kama kina ukweli kiasi gani? Si hivyo tu bali pia ni kuamka na kuachana na ile tabia ya kufikiri kwa mazoea na kutenda kwa mazoea. Kila jambo unalolifanya ujue sababu ya kufanya hivyo, sio eti kwa sababu, mama, baba, bibi, babu, mjomba, shangazi, na jamii iliwahi kufanya hivyo.

Nakumbuka wakati fulani nilihudhuria semina ya mambo ya uongozi, basi yule mwezeshaji kutoka nchini Marekani alitutolea mfano mmoja wakati alipokuwa akitufundisha namna ya kuepuka kufanya mambo kwa mazoea.

Kisa chenyewe ni hiki:

Kulikuwa na mama mmoja alikuwa na tabia, kila akitaka kuoka samaki ni lazima amkate mkia kabla ya kumuweka kwenye kikaango, ndipo amuoke. Hata kama samaki mwenyewe ni mdogo.


Siku moja binti yake aliyekuwa na umri wa miaka 10 akamuuliza mama yake sababu ya kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka, mama yake akamjibu kuwa mama yake alikuwa na kawaida ya kufanya hivyo. Alipomuuliza kama aliwahi kumuuliza mama yake sababu ya kufanya hivyo, mama yake akajibu kwamba hakuwahi kuuliza.

Basi wakati fulani bibi yake alipokwenda kuwatembelea, kama bahati mama yake alikuwa akiandaa samaki ili amuoke kama ilivyo kawaida akamkata mkia, binti akaona huo ndio wakati muafaka wa kuujua ukweli maana bibi yupo. Ndipo akamuuliza sababu ya mama yake kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka.

Si mnaona watoto wa wenzetu walivyo wadadisi?

Bibi akamwambia akamuulize mama yake sababu ya kufanya hivyo, yule binti akamjibu bibi yake kwamba, mama yake alimwambia kuwa yeye yaani bibi, ndiye aliyemfundisha kukata mkia wa samakai kabla ya kumuoka. Yule bibi akafikiria kidogo, kisha akamjibu, kwamba alikuwa akikata mkia wa samaki kwa sababu kikaango chake kilikuwa ni kidogo, hivyo ili samaki aweze kuenea kwenye kikaango alikuwa analazimika kukata mkia.

Yule binti akamwambia bibi yake, “Mbona sisi kikaango chetu ni kikubwa na isitoshe tunavyo vikaango vingi tu vya saizi tofauti tofauti, je kuna ulazima gani mama aendelee kukata mkia wa samaki kabla ya kumuoka?

Bibi akamjibu kwamba hakuna ulazima wowote.
Basi kuanzia siku hiyo yule mama akawa hakati tena mkia wa samaki.

Si mnaona jinsi mtoto huyu alivyokataa kulishwa kitu bila ya kijua sababu?
Naamini kwamba wote mtakubaliana na mimi kwamba sisi tumelelewa hivi, tunaambiwa tukate mikia ya samaki kabla ya kuwaoka na tunafuata, na wala hatuulizi sababu.

Kwa hiyo ninaposema VUKANI ninamaanisha AMKENI, ili muweze kuhoji baadhi ya mambo tunayofundishwa au kuambiwa ambayo hayana mantiki.


Monday, June 6, 2011

AKATUPA KILE KIATU!

Akakitupa hapa!




Alikuwa yuko Bar moja maarufu iliyoko maeneo ya Kinondoni hapa jijini Dar na hawara yake ambaye ndio nyumba yake ndogo pamoja na marafiki zake kadhaa wakikata maji (Pombe), Bwana Tesha (sio jina lake halisi) alikuwa na furaha siku hiyo kwani alikuwa amefanikiwa kupata tenda moja ya bajeti kubwa ambayo ilimhakikishia kupata faida ya kutosha.




Bwana Tesha anamiliki kampuni yake ya Ujenzi hapa jijini na alikuwa bado ni kijana mdogo, lakini kwa muda mfupi tangu amalize masomo yake ya Chuo Kikuu pale Mlimani alimudu kujiajiri katika sekta ya ujenzi na kupata mafanikio makubwa katika sekta hiyo.



Akiwa bado anakata maji na marafiki zake pamoja na hawara yake alipigiwa simu na mkewe. Kwa kuwa kulikuwa na kelele za walevi katika Bar hiyo aliamua kwenda kupokelea simu ile ndani ya gari lake. Simu ile haikuwa na taarifa nzuri, alijulishwa na mkewe kuwa mama mkwe wake yaani mama wa mkewe amefariki ghafla kwa presha huko Moshi mkoani Kilimanjaro.


Alirudi kwenye meza aliyokuwa amekaa ma wenzie na kuwajulisha juu ya taarifa ile, wenzie walimpa pole na kumshauri arudi nyumbani ili kumfariji mkewe. Hata hivyo alilazimika kwanza kumpeleka hawara yake nyumbani kwake maeneo ya Mwenge ndipo aende nyumban kwake maeneo ya Mbezi ya Kimara.



Wakati huo hawara yake alikuwa amelewa chakari na alikuwa hajitambui, hivyo ilimlazimu kumbeba na kumuingiza ndani ya gari yake aina ya Toyota RAV 4. Aliondoka hadi kwa hawara, aliteremka na kufungua mlango wa nyumba kisha akambeba hawara yake ambaye alikuwa hajitambui hadi ndani na kumlaza kitandani. Kwa kuwa alikuwa na funguo za akiba, alifunga mlango na kuondoka zake kuwahi nyumbani kwake.



Alifika nyumbani kwake majira ya saa nne usiku, na kukuta baadhi ya ndugu zake na ndugu wa mkewe. Baada ya mashauriano, walikubaliana yeye na mkewe waondoke kesho alfajiri, kwa kuwa yeye hahitaji kuomba ruhusa kazini.


Baadhi ya ndugu zake na ndugu wa mkewe alipanga kuondoka baadae na mabasi baada ya kuomba ruhusa kazini kwao. Walifungasha haraka haraka usiku huo huo kisha wakalala. Ilipofika alifajiri ya saa kumi za usiku waliondoka kuelekea Moshi. Ndani ya gari walikuwa wanne, mwanae wa kwanza wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 12 alikaa kiti cha mbele, mkewe pamoja na mwanae mwingine wa pili wa kike aliyekuwa na miaka 7 walikaa kiti cha nyuma. Kwa kuwa bado walikuwa na usingizi, wote walilala, na kutokana na ufinyu wa nafasi mama aliweka miguu yake katikati ya viti vya mbele na kujiegemeza kwa nyuma akimuacha mwanae wa kike amlalie mapajani mwake.



Mzee Tesha aliendesha gari kwa tahadhari sana ili kuepuka ajali. Wakati kunapambazuka alikuwa amekaribia maeneo ya mto Wami, na alijisikia kubanwa haja ndogo. Alilazimika kusimama na kuteremka ili kuchimba dawa. Alimaliza kuchimba dawa na kurejea ndani ya gari, lakini kabla ya kuondoa gari akashangaa kuona kiatu kinachofanana na kile alichovaa hawara yake usiku wa jana kikiwa chini ya kiti cha mbele cha abiria. Bwana Tesha akashtuka, akajua kile ni kiatu cha hawara yake ambaye atakuwa amekiacha mle katika gari kwa kuwa alikuwa amelewa chakari. Akageuka na kumwangalia mkewe aliyekuwa amelala kiti cha nyuma.



Aliwakagua wote ili kutaka kujua kama wamelala, na alipohakikisha kuwa wote wamelala, alikichukua kile kiatu na kukitupilia mbali, kisha akaondoa gari, akiwa amefarijika kuwa kiatu kile hakijaonwa na mkewe ambaye wanaaminiana sana tangu waoane miaka kumi iliyopita.


Aliendesha gari kwa mwendo wa wastani na ilipofika saa nne asubuhi walikuwa wako Segera, walisimama pale ili kupata staftahi. Baada ya kupaki gari aliteremka na wanae wawili na kutangulia mghahawani na kumwacha mkewe nyuma akijiweka sawa kabla ya kuteremka ndani ya gari.



Akiwa ndani ya mghahawa mkewe alimpigia simu na kumtaka aende kwenye gari kuna dharura, alitoka mghahawani na kumfuata mkewe kule kwenye gari, ili kujua kulikoni. Alipofika, alishtuka kumkuta mkewe kashikilia kiatu kimoja kinachofanana na kile alichokuwa amevaa hawara yake usiku wa jana walipokuwa kule Bar, akajua siri imefichuka, lakini akawahi kuficha mshtuko wake, na kumuuliza mkewe, “Vipi kuna nini mke wangu?”


Mkewe akamwambia kuwa ameshangaa haoni kiatu chake kimoja. Bwana Tesha akajua kiatu kisichoonekana ni kile alichokitupa kule mto Wami. Lakini alikuwa mwerevu….




“Mke wangu ana uhakika ulivaa viatu vyote viwili?” Alimuuliza mkewe akiwa na mshangao.



“Mume wangu pamoja na kuwa nimefiwa na nina uchungu sana lakini sijapoteza fahamu zangu kiasi cha kujisahau na kuvaa kiatu kimoja.” Mkewe alimjibu kwa upole.


Bwana Tesha alijifaragua akijifanya anakitafuta kiatu cha mkewe kwa bidii hasa, baada ya kupekua sana alikuja na ushauri mwingine, ambapo alimshauri mkewe wanunue kandambili avae kwa muda kwa madai kuwa wakifika Moshi watakitafuta kwa umakini.



Mkewe alikubali, lakini bado alikuwa na mashaka kidogo juu ya tukio lile. Walinunua kandambili na baada ya kupata kiamsha kinywa waliondoka. Walipofika Korogwe, Bwana Tesha alisimama na kwenda dukani ambapo alimnunulia mkewe Viatu vingine kisha wakaondoka kuwahi Mazishi.




Baada ya kufika Moshi habari ya upotevu wa kiatu kimoja ilisimuliwa na cha kushangaza tukio lile likahusishwa na mambo ya kishirikiana sambamba na msiba ule. Na hiyo ndio ikawa ndio salama ya Bwana Tesha kuepukana na fedheha ile ya kutupa kiatu cha mkewe baada ya kukifananisha na kiatu cha hawara yake.



Wednesday, June 1, 2011

AKANIAMBIA NIKIZEEKA NA KUWA BIBI KIZEE NISIJE NIKAMUOMBA UGORO!

Ni jana majira ya jioni nikikatiza mitaa ya Msasani, nikakutana na mateja wako wachafu wamekaa kijiweni wakipiga soga. Mara akaijitokeza teja mmoja na kuanza kuniita kwa sauti ya mlegezo (sauti ya mlegezo ni voice tone inayotumiwa na mateja), “Oyaa sister eee..hebu nisubiri basi nikuulize” mie sikumjibu wala kugeuka, niliendelea kuchapa mwendo.



Oyaa sister unajifanya uso wa mbuzi sio (hata sikumwelewa ana maana gani), niliendelea kuchapa mwendo bila kugeuka, na mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwa woga maana niliona dhahiri anaweza kunikaba, kwani nilipita vichochoroni.


Baada ya kuona simjibu wala kugeuka, akaanza kumwaga maneno ya kifedhuli…….


Unajifanya mzuuuri kumbe huna lolote, uzuri wenyewe uko wapi? Sana sana unatumia mgorogo tu, we nini bwana ….. unadhani tuna shobokea mademu sisi,…… shika time yako, huna lolote mshamba tu wewe……


Tena sikiliza…. Ukizeeka na kuwa bibi kizee usije ukaniomba ugoro, maana hamkawii nyie, ukizeeka na kimkongojo chako……(akainama kuonesha mfano wa bibi kizee na mkongojo) lazima utakuja tu …. Kisha akaanza kuigiza sauti ya bibi kizee na kusema, “Mzee naomba kaugoro hapo nitulize kiu yangu”


Sitakupa ng’oooo…….. Ishia huko………


Mie na watu waliokuwa karibu tulivunjika mbavu kwa kicheko, maana ilikuwa kama mchezo wa kuigiza vile.