Friday, December 26, 2008

MWANASAYANSI LONGO LONGO.

Jana katika kupitia Blog mbalimbali ili kupata hekima za wenzangu, nimekutana na Blog mbili zinazoshabihiana kimtazamo, Yaani ile ya Utambuzi na ya Jielewe.

Katika blog hizo nilikutana na mada mbalimbali, lakini mada iliyonivutia ni hii ya mjadala wa mwanzo wa mwanaadamu. Nimekutana na mjadala mzito wenye rejea za wanasayansi mbalimbali na nadharia zao.

Mimi si mwanasayansi na sitaki kuingia kwenye huo mjadala kwa sababu siipendi sana Sayansi.

Hata hivyo wakati napitia Maktaba ya baba nilikutana na Kitabu kinachozungumzia mambo hayo hayo ya Sayansi, Maana Baba yangu nae anapenda sana kusoma, na ukiingia kwenye Maktaba yake utakutana na vitabu mpaka vya Kilatini.

Tuyaache hayo, ngoja niwasimulie kisa cha mwanasayansi mmoja ambaye nimesoma habari zake kutoka kwenye kitabu hicho cha mzee, ambaye ningependa kumuita Mwanasayansi Longo Longo.

Katika mojawapo ya sijui niite utafiti au utabiri, mwanasayansi huyo wa Ki-Irish,
Dk. Dionysius Lardner aliyeishi kati ta Mwaka (1793-1859) aliwahi kusema kwamba, Garimoshi halitaweza kwenda kasi hata siku moja.
Alisema garimoshi litaendelea kuwa na kasi ndogo sana, kwani likienda kwa kasi kubwa, abiria wataweza kufa kwa tatizo linalifahamika kitaalamu kama Asphyxia, yaani kukosa pumzi.

Pamoja na kwamba alikuwa ni mwanasayansi, Lakini nadhani alikuwa hajui anachokisema kwa wakati ule.

Kwa nini?

Kwa sababu leo hii kuna magari moshi yanayosafiri hata kilomita 500 kwa saa.

Sasa sijui mwanasayansi huyu alikuwa anatumia ubongo huu tulio nao katika tafiti zake au alikuwa anatumia nini, mimi sijui.

Ningependa kuchukuwa nafasi hii kuwatahadharisha kaka
Bwaya na kaka Mtambuzi kuwa wawe makini na nadharia za baadhi ya wanasayansi, kwani pia walikuwepo wanasayansi wengine waongo, kama mwanasayansi huyu wa Ki-Irish.

Hata hivyo nazifagilia kazi zao.

9 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Nimesoma sehemu za historia yake na sina hakika kama alikuwa mwanasayansi kwelikweli, mchumi ama vipi? Lakini nadhani watu wa hivi wanahitajika wakati mwingine ili kuweka CHANGAMOTO katika kusaka ukweli wa kile wapingacho. Sasa alipinga na wakajitahidi kum-prove wrong na pengine hilo liliharakisha evolution ya mwendokasi wa garimoshi. Twahitaji watu wa hivi maana si wajua bila wajinga werevu hawataonekana na pia bila wachelewaji hakutakuwa na muwahiji.
Kazi njema na asante kwa hili
Blessings

Unknown said...

Du, hapa iko kazi.
Mi yangu macho!

Fadhy Mtanga said...

Nami nitie neno. Sijui kama nitatofautiana na wenzangu. Yap, wacha niandike.
Mi nadhani (kudhani ni kuzuri?) nadhani hakuwa longolongo, sitomwita hivyo. Nadhani tatizo ni wakati. Pengine kwa wakati ule na pengine kutokana na maendeleo madogo mno ya teknolojia jambo hili halikuwa likiwezekana. Inawezekana, kwa treni zile, tena steam engine aliona na kwa dhahiri ni vigumu kwa kitu hicho.
Ni sawa na leo katika maktaba zetu tukakutana na mwanafalsafa kwa mfano, labda wa Uingereza wa karne ya 15 labda, huyo akasema haitotokea kamwe kwa ndoa za jinsia moja Uingereza.
Niongeze mfano? Ama kwa mwanafalsafa labda aliyekuwepo Uchina miaka ya 60, pengine naye angeapa kuwa dini haitotia mguu kamwe China. Hatutowaona uchwara, kwani wakati ndiyo umeyageuza mambo haya. Wakati, umebadili mfumo wa maisha. Nani aliyeishi hata tu kipindi cha mapinduzi ya viwanda hapo karne ya 18 angeweza kubashiri kuwa kutaja tokea barua pepe?
Nimalize sasa, nataka sema nini? Ok, kuwa pengine kiwango cha maendeleo cha wakati huo kilimsukuma kuamini hivyo.
Ni hayo tu!

Christian Bwaya said...

Koero,

Nakubaliana na mawazo yako. Kwamba nadharia (zikiwemo za wanasayansi) hupitia nykati za kwanza kukubaliwa. Hapa nadharia hizo huchukuliwa kama ukweli mkamilifu usiohojika. Lakini baada ya muda, kupitia matokeo ya tafiti za watu wengine, nadharia hizo hupitia kipindi kingine cha pili cha kuangaliwa upya kwa sababu ya kujitokeza maswali mengi. Baada ya kupimwa kwa muda, nadharia hizo hukanwa na kuonekana kuwa haziwezi kuwa kweli kwa mazingira mapya. Zinaonekana kuwa uongo mkamilifu.

Maana yake ni kwamba ninachoonekana ukweli leo hii, chaweza kuwa uongo wa kesho. Muhimu ni kuuchungua huu unaoitwa ukweli wa leo. Tufanye hivyo kwenye sayansi. Dini. Imani. Na kadhalika. Tuangalie kila kitu upya. Kwa huenda tumedanganywa kiasi cha kutokujua kuwa tumedanganywa.

Lakini pia tufahamu kuwa hatuwezi kukanusha kitu bila kwanza kuuangalia kwa makini na kukielewa vyema hicho kinachoitwa ukweli. Ukikanusha bila kujua unakanusha nini unaweza kuwa unausimika uongo bila kujua.

Karibu sana Koero. Ujio wako umeleta changamoto mpya.

Mzee wa Changamoto said...

Dada. Unajua kwenye profile yako hakuna e-mail? Sina hakika kama unaogopa usumbufu ama la, lakini si kila "sifa ama kukosoana" baina yetu bloggers hupitia sehemu ya maoni. Mfano ni huu ujumbe wala nisingeupitisha hapa kama kungekuwa na email yako kwenye profile.
Ni hayo tu kwa sasa. Unatakiwa mwisho mwema wa wiki

Yasinta Ngonyani said...

kazi nzuri koero, endelea vivyo hivyo. Tutaonana

MARKUS MPANGALA said...

ama kweli tuna vipaji ila wadau ni wanyonyaji watunyonye kisha watuvishe mataji..... ni mistari ya kiugumu mambo ya hip hop mwanawane au vipi. Dada KOERO njoooooooooooo karibuuuuuuuuuu ndaniiiiiiiiiiiiiiiii nitamwambia baba NDESANJO MACHA kwamba hata kama hataki kublogu ATAJIJU SIKU HIZI{natania} maana tayari dada KOERO huyooooooooooo..... lakini kuhusu hii sayansi mimi nasema labda jamaa hakuwa FREEMASONS/MASONIC ndiyo maana kasema na pengine ni hivyo alivyosema kaka Fadhi Mtanga.

Mengineyo karibu ndani dadangu..... samahani nimeweka picha yako kuonyesha msisitizo wa karibu yangu

Fita Lutonja said...

Dada Koero kuna haja gani kuzungumzia nadharia na kushindwa kufanya uchunguzi zaidi ili kujua kwa undani zaid.

Nimefurahi karibu tuunde mtandao, nimefurahi na kazi yako.

Koero Mkundi said...

Du changamoto zimekuwa ni nyingi, sikujua kama haka ka mjadala kanaweza kuleta changamoto nyingi namna hii.

Hebu ngoja nitafakari.

Wote naweza kukubaliana na ninyi lakini mifano ya kaka Fadhy inanitia mashaka kidogo.
Hivi kumbe tafiti nyingi za wanasayansi wa kale ni za kutiliwa mashaka!!!

Yaani haya tunayokaririshwa huko vyuoni yaliyoumbuliwa na wanasayansi wa karne zilizopita huenda yalikuwa yanafanya kazi kwa mazingira ya wakati ule?
Hivyo ndivyo kaka Fadhy anavyotaka niamini?

Any way ngoja niseme hivi, labda nikubaliane na kaka Bwaya aliposema Kwamba nadharia (zikiwemo za wanasayansi) hupitia nyakati za kwanza kukubaliwa.

Hapa nadharia hizo huchukuliwa kama ukweli mkamilifu usiohojika. Lakini baada ya muda, kupitia matokeo ya tafiti za watu wengine, nadharia hizo hupitia kipindi kingine cha pili cha kuangaliwa upya kwa sababu ya kujitokeza maswali mengi.

Baada ya kupimwa kwa muda, nadharia hizo hukanwa na kuonekana kuwa haziwezi kuwa kweli kwa mazingira mapya. Zinaonekana kuwa uongo mkamilifu.

Hivyo kuna haja ya kuangalie kila kitu upya. Kwa kuwa huenda tumedanganywa kiasi cha kutokujua kuwa tumedanganywa.
Mpaka hapo nakubaliana na kaka Bwaya, lakini kama nilivyosema tangu awali kwamba mimi sio mwanasayansi hivyo nachelea hoja hii isije ikanielemea.

Wadau ahsanteni kwa maoni yenu.