Ni hivi karibuni niliandika juu ya habari ya vibaka wa pale Tandale kwa Mtogole na Manzese niliyoipa kichwa cha habari kisemacho “DAR ES SALAAM: TANDALE KWA MTOGOLE NA JARAMBA LA SASAMBUA SASAMBUA” . Niko Arusha kwa sasa na niko huku kutokana na shughuli za kifamilia.
Kwa hapa Arusha eneo ambalo unaweza kulifananisha na Tandale kwa Mtogole au Manzese ni Unga Limited, Ngarenaro, Kimandolu, na Sanawari eneo la Mbwa Chini.
Nimetolea mfano maeneo hayo kwa kuwa ndio maeneo ninayoyafahamu vizuri, lakini naamini mikoa yetu yote hapa nchini inayo maeneo fulani fulani ambayo ni korofi kwa uhalifu.
Lengo langu leo sio kuongelea uhalifu na hao vibaka, bali nataka kuzungumzia sera yetu ya elimu hapa nchini. Nilipokuwa Dar es salaam, kila nikipita katika vituo vya daladala nakuta kundi la vijana wanaopiga debe maarufu kama mateja, na hao hao ndio vibaka wanaopora watu hapo vituoni.
Katika utafiti niliofanya nimegundua kuwa kila mwaka idadi ya wapiga debe katika vituo vya daladala inazidi kuongezeka, hii ina maana gani, ni kwamba kila mwaka wanafunzi wanapomaliza darasa la saba lipo kundi kubwa la wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo ya sekondari hivyo huishia mitaani.
Je nini majaaliwa ya wanafunzi hawa? Je ni kwa nini nguvu kazi hii inaachwa ikipotea bure, hivi kupiga makelele ya kuita abiria na kujipatia shilingi mia au mia mbili ndio uzalishaji? Je kijana huyu anachangiaje pato la Taifa?
Ukweli ni kwamba sera yetu ya elimu hapa nchini imepogoka mno na haimuandai kijana kujiajiri ili kujiletea maendeleo na kuongeza pato la Taifa, na hili niliwahi kulijadili katika mada niliyoipa kichwa cha habari kisemacho “HIVI MSOMI HASA NI NANI?”
Nakumbuka wachangiaji wengi waliojitokeza kila mmoja alisema lakwake na mjadala ule uliisha bila kupata muafaka. Sina haja ya kurudia kile nilichokisema, bali leo ninayo maoni tofauti kidogo katika kulizungumzia hili.
Kuna siku nilikuwa naongea na mzee Mkundi, ambaye ni baba yangu, huyu mzee mie hupenda kumuita M-Conservative, kutokana na misimamo yake.
Siku hiyo nilimuuliza juu ya tofauti iliyopo kati ya mfumo wa elimu tulionao sasa na ule uliokuwa ukitumiwa na wakoloni, kabla ya kupata uhuru.
Baba alishangazwa na swali langu hilo, lakini hata hivyo alinijibu. Kwa mtazamo wake alisema kwamba pamoja na kwamba sera ya elimu ya mkoloni haikuwa na nia ya kutaka Muafrika ajitawale, lakini yalikuwepo maeneo ambayo sera hiyo ilifanikiwa sana.
Kwa mfano, wale wanafunzi ambao walikuwa hawana uwezo darasani lakini walionesha kuwa na vipaji, hao waliandaliwa kulingana na vipaji vyao huku wale wenye uwezo darasani waliendelea na masomo ya elimu ya juu.
Katika wale ambao walikuwa hawana uwezo darasani ndio waliokuja kuendelezwa katika fani mbalimbali kama vile utalamu wa kilimo, ufundi washi, useremala, makenika, ufundi mitambo, uhunzi na fani nyingine za michezo.
Yote hayo yalifanyika katika program maalum kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye hakuwa na uwezo darasani ambaye alitelekezwa.
Tulipopata uhuru ndio kila kitu kilipoanza kuvurugwa taratibu, katika mfumo wa elimu.
Labda kulikuwa na nia nzuri ya kutaka kubadili ule mfumo wa elimu wa kikoloni uliokuwa umejikita zaidi katika kuwaandaa makarani wa kusimamia shughuli za wakoloni na kuweka mfumo wa kizalendo, lakini mabadilliko hayo hayakufanywa kwa umakini, kwani ilitakiwa tuache yale mabaya na kuchukua mazuri kama hayo ya kuwaandaa vijana katika nyanja mbali mbali kutokana na vipaji vyao. Lakini hata hivyo mzee Mkundi alibainisha kuwa, inawezekana ni kweli makosa yalifanyika kutokana na upeo finyu tuliokuwa nao wakati huo, lakini hivi mpaka leo bado tumeshindwa kutengeneza sera maridhawa ya kuwaandaa vijana wetu ili kujiajiri?
Hayo ndio majibu ya mzee Mkundi kwa mtazamo wake, hata hivyo niliamua kumshirikisha Profesa Matondo {bonyeza hapa kumsoma} katika mjadala huu, naye alikuwa na haya ya kusema:
Ukweli ni kwamba mfumo wa elimu yetu ni mbovu na kama ulivyosema haumwandai kijana kuweza kufanya lolote mbali na kuajiriwa baada ya shule. Tatizo ni kwamba hatuna ajira za kutosha na vijana wengi wanaishia kutelekezwa. (1) Kuna shule chache sana za sekondari na vijana wengi wanashindwa kukivuka hata kizingiti cha darasa la saba. Sijui hawa ni asilimia ngapi lakini nadhani ni wengi sana pengine karibia asilimia 75. Hakuna anayejua wala kujali hawa wanakwenda wapi baada ya kumaliza darasa la saba. Wengine wanajaribu umachinga, upiga debe na bila shaka kuwa vibaka na ujambazi. Halafu serikali inajaribu kupambana na tatizo hili kwa kuajiri mapolisi zaidi. Tazama maoni yangu niliyoweka katika blogu yako hapa:
(2) Hivi ulishawahi kujiuliza ni kwa nini watu wanaofeli mitihani ndiyo tunawatuma wakawe waalimu na waelimishaji wa taifa letu? Eti ukishindwa kwenda High School (division 3 na division 4) ndiyo unapelekwa ualimu. Unaweza kupata F zote na D mbili tu au tatu tu lakini bado taifa likakupa wajibu mzito wa kuandaa vijana wake. Huu nao ni muujiza. Literally kipofu anamwongoza kipofu mwenzake. Hapo unategemea nini? Kwa wenzetu huku kuanzia mwalimu wa chekechea ni lazima awe na digrii ya kwanza ya chuo kikuu, na awe "certified". Shule za msingi ndiko hasa tunapaswa kuweka misingi na kama mtoto anaanza na waalimu wetu hawa waliopata F zote na D mbili katika masomo yao ya kidato cha nne, unamtegemea mtoto huyo atakuwaje hata katika viwango vya juu vya elimu?
(3) Suala jingine ni lugha. Miaka saba ambayo ni ya muhimu sana kwa mtoto, mtoto anafundishwa kwa lugha nyingine na kimiujizaujiza tu anategemewa kwamba anapokwenda sekondari basi atakuwa amekifahamu Kiingereza sawasawa kiasi cha kukitumia ipasavyo katika masomo yake. Watoto wengi wanakwenda kidato cha kwanza hata hawajui kujitambulisha katika Kiingereza halafu wanategemewa eti waweze kuzifahamu Newton's Laws of Motion na maana zake pamoja na manufaa yake. Hapa ndipo elimu inakosa maana na kuwa zoezi la kukariri tu. Unakariri, unakopi kwenye mtihani, unapata A unasonga mbele ingawa hujui kitu. Na hili linaendelea mpaka pale Mlimani. Unapata digrii yako, unabahatika kuajiriwa, unaboronga na mambo yanaendelea. Japo leo kuna mfumuko mkubwa wa hizi "academy" zinazofundisha kwa Kiingereza tupu, tatizo ni kwamba nyingi zipo mjini wakati walengwa wake wako kijijini; na hata huko mjini ni wangapi wanaweza kumudu gharama zake?
Mzee Mkundi yuko sawa. Wakoloni hawakumtelekeza mtu kwani walihitaji sana watu wenye ujuzi fulani kuweza kuwasaidia katika shughuli zao nyingi. Walihitaji mafundi seremala, waachi, mafundi umeme, mafundi wa magari n.k. kwani wasingeendelea kuagiza watu hawa kutoka kwao Ulaya. Sijui tulishindwa nini kuendeleza sera nzuri kama hii. Siasa ya Kujitegemea mashuleni ilikuwa na lengo kama hili lakini bila vifaa na vitendea kazi, siasa hiyo iliishindwa. Badala yake ikawa wakati wa kujitegemea watoto mnakwenda kufagia na kumwagilia maua maji!Je wadau wengine mnasemaje juu ya hili?
Tujadili kwa pamoja
TRA WAWASHUKURU GF TRUCK LTD NA LINDI EXPRESS LTD
-
Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ldara ya Kodi
za ndani, kitengo cha walipakodi wa kati Godwin Barongo pamoja na
Watumishi...
2 hours ago
6 comments:
Kwanza nasema nashukuru umeweka mjadala huu hapa. Ni kweli elimu ya zamani ilikuwa ya kuelimisha zaidi. Yaani wazazi wetu walikuwa wanajali elimu hata kama wengi wao waliishia darasa la nane. Walisoma kwa bidii zote na kuwa makini sana Lakini Taifa letu la leo hatuna ile hamu ya kusoma kwa nia fulani haya ndio matokeo ya wapiga debe kuwa wengi. Kuna hatari Taifa lijalo inawezekana ikawa mbaya sana kwani watoto huiga maisha ya wazazi/jamii. Pia tatizo ni kwamba walimu wa sasa hawana elimu ya kutosha mwl. mwenyewe hajui kusema jina lake kwa kiingireza halafu anapewa kufundisha somo la kiingireza kweli kitakuwa nini hapa. Pia jambo muhimu au mtazamo wangu mimi ningependa masomo yote yafundishwa kwa kiswahili kuanzia darasa la kwanza mpaka sec. au iwe kinyume kiingireza. Kwani huwezi kuanza na kiswahili na ghfla unaanza sec. masomo yote ni kiingereza kasoro kiswahili kwali unafikiri kuna mwanfunzi ataambua kitu hapo itakuwa linaingia sikio la kulia na kutoka sikio la kushoto.
Kwa sababu hilo jambo sio Afrika tu nimeona hata hapa akija mkuja akipata kazi wanamchukia na kusema umekuja na kuchukua kazi zetu. Lakini ni kwamba wao wenyewe hawataki kazi za kufagia au kumwagilia maua wanataka kazi za kilipa. We mwingine unachukua tu ili kuweza kuyamudu maisha.
Mimi sitaki kukubaliana na wewe kwa asilimia mia moja kuwa serikali imewasahau kabisa wale ambao hawajafanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho wa darasa la saba. Serikali ililitambua hili ndio sababu ilianzisha VETA. takwimu zangu zinaonyesha vyuo vya VETA vimeongezeka na vinaendela kuongezeka toka tupate uhuru. mwisho kabisa kutembela tovuti ya VETA walikuwa na vyuo 21 na walikuwa wanatoa elimu kwenye fani tofauti tofauti zaidi ya 40. UKWELI KABISA ELIMU YA VETA INAMUANDAA ZAIDI MUHITIMU WAKE KUJIAJIRI. na wengi wa wahitimu wa VETA wamejiajiri wenyewe. TATIZO LIPO KWENYE KUWEZESHA NA SERIKALI KUACHIA BIDHAA FEKI TOKA ASIA HUSUSANI CHINA KUJA KWENYE SOKO LETU BILA KUANGALIA ATHARI KWA WANANCHI WAKE. ukweli vijana waliomaliza na kufuzu hivi vyuo ni mafundi hodari sana. ila ushindani wa kibiashra kwa bidhaa feki zinazotoka asia zinawakwamisha sana. PIA WATANZANIA TUNAKASUMBUA YA KUBABAIKIA BIDHAA ZA JE HATA KAMA HAZINA UBORA KAMA TUNAZOZALISHA NYUMBANI. WATANZANIA hatuoni fahari kununua na kumiliki bidhaa zilizozalishwa na watanzania wenzetu.
NIRUDI SASA KWENYE FORMAL EDUCATION. Ninakubaliana na wewe kwa asiimia mia moja LUGHA YA KUFUNDISHIA NI TATIZO. kama tumeamua kuingia kwenye ushindani wa kibiashara na huu UBEPARI, hatuna budi kukubali kuwa Kingereza kitumike kwa masomo yote toka elimu ya msingi. NI VIGUMU KWA MWANAFUNZI KUELEWA MASOMO SEKONDARI WAKATI LUGHA NI TATIZO. kwa mfano mimi nilipokuwa shule ya msingi nilikuwa nasoma vitabu vingi sana vya kiada na ziada. na nilielewa sana masomo kwa sababu yalifundishwa kwa lugha ninayoijua. Kufika sekondari nikapunguza kusoma vitabu vya ziada. kwa sababu ilibidi nitumie muda mwingi kukariri ili niweze kufaulu mitihani. HILI NI TATIZO... Serikali ikaanzisha shule za watoto wenye vipaji. NILIBAHATIKA KUSOMA KWENYE SHULE HIZO. Ila ki ukweli serikali ilikosea kutoa jina. sikuona kipaji chochote zaidi ya wanafunzi kusoma masaa kibao. WATU WENYE VIPAJI WAMEACHWA KISA HAWAJAWEZA KUKARIRI VIZURI NA KUPATA ALAMA ZA A KWENYE MITIHANI YAO YA MWISHO. Kweli kabisa kufundishwa na watu waliofeli ni tatizo pia. Tanzania mtu akifeli sehemu ya kukimbilia ni ualimu. KAZI KWELI KWELI. Nakumbuka shule ya msingi nilikosana na mwalimu mmoja kwa kumkatalia kuwa TANZANIA HAIJAWAHI KUTAWALIWA NA MKOLONI YEYOTE. nakumbuka swali lilikuwa andika KWELI AU SI KWELI. Jibu la mwalimu lilikuwa kweli TZ ilitawaliwa na wajerumani na Waingereza. Kwa kumbishia mwalimu nilikuwa bakora 8. SINTASAHAU HILI. Inawezekana vipi nchi iliyoundwa 1964 iwe imetaliwa na kupata uhuru 1961. Pamoja na kumuelewesha labda alikuwa na maana ya TANGANYIKA au ZANZIBAR
Kaka Godwin naomba kutofautiana na wewe juu ya swala la VETA,
Naona kama hukuielewa mada hii, Alichozungmza Dada Koero ni sahihi kabisa, Serikali inastahili kulaumiwa. Swala hapa sio kuanzishwa kwa Veta, swala hapa ni je imewawezeshaje vijana wetu kumudu kujiajiri?
No matter vyuo vingapi vimeanzishwa na Veta, hiyo haifuti lawama hata kidogo.
Kwani kuna haja gani ya kuwa na vyuo lukuki huku kukiwa na vijana wengi mitaani wakiishia kuwa wapiga debe na ukibaka, ambapo waki graduate wanakuwa majambazi na kudhulumu roho za watu wasio na hatia?
Mimi binafsi ni zao la Veta, lakini utashangaa nikikuambia kuwa kazi ninayoifanya sio ile niliyosomea pale Veta.
Hivi unajua kuwa unaweza kuomba kusomea ujuzi fulani pale Veta halafu ukajikuta unapangiwa kusomea kitu tofauti na ndoto zako.
Nakumbuka katika darasa letu pale Veta tulikuwa tunajiita lost boys, kwa nini?
Ni kwa sababu tulijikuta wote tukiwa pale nje ya matakwa yetu, wapo alioacha kabisa kusoma na akina sisi hatukuwa na jinsi tulisoma bora liende. Bila shaka hutashangaa nikikuambia kuwa katika darasa letu hakuna hata mmoja anayefanya kazi ile tuliosomea, tulipoteza miaka yetu miwili pale Veta bure kabisa.
Kule Usa Riva, Arusha katika eneo la Leguruki kuna chuo kilianzishwa na Wajerumani, si ndio waliokuwa wakitutawala sisi Watanganyika?
Fani ya kwanza kufundishwa pale ni ile ya ufundi Seremala, na wanafunzi wa kwanza kumaliza walipewa nyenzo na mtaji kwa mkopo na kuanzishiwa kiwanda kilichoitwa UMALE, yaani Umoja wa Mafundi Leguruki.
Wale vijana ni mafundi hodari kweli na samani wanazochonga sinauzwa mpaka Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya, huko ndio kuwezeshwa, na sio kusomeshwa Veta halafu unatelekezwa bila mtaji wala nyenzo.
Kwa nini Veta isiige mfano wa chuo cha Leguruki?
Kwani inahitaji gharama kubwa kiasi gain? Tena sio kuwapa bure, kunakuwa na mpango maalum wa kuwapa nyenzo kwa mikopo na kuwasaidia kutengeneza management ili waweze kujiendesha kwa ufanisi, si ndio kuwezeshwa huko?
Na baadae serikali haitahitaji tena kutenga mtaji mkubwa kwani ule wa kwanza utakuwa unazunguka yaani hawa wakirudisha mkopo wanapewa wengine.
Haiyumkiniki kuwa hata hawa wezi wanaovunja magodown na kuiba mali zilizomo ndani ni zao la Veta, wana ujuzi lakini hawajui pa kuanzia.
Alichozungumza Mzee mkundi, Profesor Matondo na dada Yasinta ni sahihi kabisa, wakoloni hawakaumtelekeza mwanafunzi hata mmoja walikuwa wanaangalia kila mwanafunzi kama anacho kipaji gani, na kuelekeza nguvu huko ili kumuwezesha.
Tunahitaji mabadiliko makubwa katika swala zima la elimu, kwani sera yetu ya elimu imepogoka mno……
Nashukuru kupata nafasi ya kuchangia mada hii juu ya elimu ya Tanzania.
Miaka ya nyuma nilienda mkoani Morogoro, wilaya Kilombero kwa ajili ya kufuatilia habari.
Kwa bahati mbaya au nzuri jambo niliyokuwa ninaifuatilia ilikuwa ni ya kupata picha ya matokeo ya sera zinazowahusu vijana. Yaani je ni kweli sera za serikali zinawafaidisha vijana?
Bila kuchelewesha uhondo, vituko nilivyokuta huko vilinisikitisha.
eti, kwanza kupitia wizara husika, kuna mtaji wa fedha kiwango cha juu shilingi 400,000 ambao kikundi cha vijana wanaweza kujipatia ili kujinyanyua kiuchumi.
Swali ya kwanza pesa hizo huchukua muda gani kupatikana - miezi sita.
Je kikundi kinatakiwa kiwa na watu wangapi? - angalau 20
Je? laki nne itasaidia nini? Mgao wa chapu chapu kila mwanachama ajinunulie vifaa anavyo hitaji - hii ni pamoja na starehe ajaribu bahati yake. Je umeona hii.
Twende kwenye kituko kingine.
Eti kwa sababu tu wamissionari hapo zamani walijitolea kuwa honga wadau wa eneo kuhuduria kanisa walitoa nguo na misaada mingine midogo midogo hadi watu wakaamua kuacha kufanya kazi. matokeo yake misaada ilivyo katika - kama kawaida yake - wadau wakakwama hawajui wafanye nini. Basi, kwa kuwa mashamba bado yapo basi wakarudi kulima, lakini si kwa nguvu zote kwa sababu kumbe katika kipindi hicho hicho walipokuwa wana subira vya kupewa "investors" wakawa wametinga mahali hapo na kujipendelea sehemu za maana zaidi.
OK. ukuchelewa utakuta kitu si chako, matokeo ya hayo ikwa ni kwamba wazee wengine wakaamua kuwa ozesha mabinti zao kwa mwanamume - vijifulana - aliyeweza kuleta pesa za kutosha eti akamjaribu binti yake halafu ...
Je, kama mtoto ataolewa kwa riadha ya mzazi kama sheria ya nchi inavyo halalisha - shule ataenda za ngapi - na kumbe mtoto huyo huyo akirudisha baada ya pesa za bwana kuisha anasubiri bwege mwingine ajigonge na kutoa hela zake ili ajaribu naye bahati yake.
sina mengi lakini mambo ndio hayo.
SOMO TAMU SANA HILI NADHANI MJADALA UMEKOL
Hili lina ukweli, elimu yetu imepogoga mno...
Post a Comment