Nakumbuka alikuwa na kawaida ya kuja pale ofisini kwangu, maeneo ya mjini na kunisaidia shughuli za usafi na kumlipa ujira kidogo. Kama nilikuwa nataka kununua kitu nilikuwa namtuma. Ni kijana mchapa kazi kweli na mcheshi kupindukia.
Akiwa ni mzaliwa wa Lindi katika kijiji cha Mbekenyela, kijana huyu ambaye ningependa kumwita Saidi *{Sio jina lake halisi}hakubahatika kumuona mama yake. Anasimulia kuwa mama yake aliolewa akiwa na umri mdogo sana miaka 15 na mzee mmoja aliemzidi kwa miaka 50, aliolewa katika zile ndoa maarufu za Korosho. Ndoa ambazo hufanyika sana mara baada ya msimu wa korosho.
Anasema kuwa kule kwao Lindi, kila baada ya msimu wa korosho wazee wengi ambao wana mashamba makubwa ya Korosho hukimbilia kuoa vibinti vidogo kwa kuwa wanazo fedha za mauzo ya Korosho, kuna wakati watoto wa kike hulazimika kuachishwa shule ili kuozeshwa kwa vibabu hivyo visivyoisha tamaa, na mara nyingi ndoa hizo huwa hazidumu kwani fedha zikiisha na ndoa huingia katika misukosuko na hatimaye kuvunjika kutokana na vizee hivyo kushindwa kumudu gharama za malezi ya wake wawili au hata watatu.
Hali hiyo imesababisha familia nyingi mkoani humo kuwa na vijukuu baada ya mama zao kuachika na kurudishwa nyumbani, hivyo kufanya hali ya maisha katika familia nyingi kuwa ngumu.
Mama yake Saidi alifariki wakati akijifungua, hivyo saidi hakumjua mama yake na hivyo kulelewa na bibi yake. Alipokuwa darasa la tatu babu yake alifariki, na maisha pale nyumbani yakawa magumu kweli. Saidi aliamua kwenda kwa baba yake aliyekuwa akiishi kijiji cha jirani, kule alikutana na mateso ya ajabu kutoka kwa mama zake wakambo na hivyo kulazimika kurudi kwa bibi yake mzaa mama.
Hata hivyo alijitahidi kuendelea na masomo, huku akifanya vibarua vya hapa na pale ili kumsaidia bibi yake ambaye alishakuwa mzee kujikimu. Alilazimika kuacha shule na kukimbilia mjini Lindi ili kujitafutia kipato. Alipofika mjini alikuwa akiishi stendi huku akifanya vibarua vya kubeba mizigo ya abiria na shughuli nyingine za kuosha magari ili mradi mkono uende kinywani.
Siku moja alipata wazo aje Jijini Dar, hiyo ni baada ya kusikia sifa nyingi kuhusiana na jiji hili, kwa kuwa alikuwa na vijisenti vyake alivyojiwekea alikata tiketi na kuja mjini. Alipofika awali alifikia pale ubungo stendi na kama ilivyokuwa Lindi alijishughulisha na shughuli zile zile za kubeba mizigo ya abiria na kuosha magari, baadae alihamishia shughuli zake maeneo ya Posta. Kati kati ya mji, na hapo ndipo nilipotokea kufahamiana naye.
Ni kijana mwenye heshima na muaminifu, siku moja kama kawaida yangu nilianza kumdadisi kwani kutokana na umri wake niliona alistahili kuwepo shuleni, na ndipo aliponisimulia historia ya maisha yake. Ukweli ni kwamba nilishikwa na huzuni sana na wakati ananisimulia kuna wakati nilijikuta nikitokwa na machozi kutokana na kuguswa na maisha magumu aliyoapitia.
Nikisema nisimulie historia yake yote, nitakuchosha wewe msomaji lakini kwa kifupi ni kwamba, Saidi alipitia maisha magumu sana, na yanayosikitisha na kuhuzunisha. Baada ya kusikiliza simulizi yake juu ya maisha yake, nilikata shauri nimsaidie. Nakumbuka kipindi cha nyuma kuna wakati nilikwenda kwa mama yangu mdogo anayeishi maeneo ya Kigogo, pale jirani na anapoishi nilimkuta kijana mmoja anafunga vifuko vya karatasi kwa kutumia unga wa ngano. Alikuwa akitengeneza vifuko vya saizi tofauti tofauti kulingana na matumizi na kisha kuviuza katika maduka ya dawa na wakati mwingine maduka ya kawaida na hata kwa wale wauza CD za muziki kwa ajili ya kufungia bidhaa zao.
Kutokana na udadisi wangu kama kawaida niliweza kuongea na yule kijana mtengeneza mifuko, na ikatokea tukazoeana sana, na hapo ndipo nikajifunza kutengeneza hiyo mifuko, ingawa sikujua kama najifunza ili iweje.
Baada ya kuongea na saidi nilipata wazo la kumfundisha ile kazi yakutengeneza mifuko ya karatasi, na baada ya kumweleza alifurahi sana. Kazi yenyewe haikuhitaji mtaji mkubwa, hivyo nilimpa kazi ya kupita katika maduka ya stationary na kuokota makaratasi na kisha aniletee. Na mimi nilipita pia kwenye maduka ya aina hiyo ambayo yalikuwa jirani na ofisi yangu na kuwaomba wawe wananihifadhia makaratasi wasiyoyatumia kwa kuwa nilikuwa na shida nayo, kwa kweli walinipa ushirikiano, kwani mpaka jioni nilikuwana lundo la makaratasi, naye Saidi kwa upande wake aliweza kukusanya makaratasi mengi sana, hatua ya kwanza ikawa imekamilika.
Tulipanga siku inayofuata ndio darasa letu lianze. Na siku iliyofuata nilinunua unga wangu wa ngano katika duka moja la jirani kule nyumbani kiasi cha kilo moja hivi, niliona hiyo ingetosha kuanzia, na nilipofika ofisini nilimkuta saidi ameshafika na kuanza shughuli zake za usafi kama kawaida, ila siku hiyo alikuwa ni mchangamfu sana. Baada ya kumaliza shughuli za usafi nilikaa naye na kuanza kumfundisha hatua kwa hatua mpaka akamudu kutengeneza mfuko, nilimuacha akiendelea kutengeneza mifuko yake na mimi nikawa naendelea na bishara zangu pale ofisini lakini nilikuwa naikagua kazi yake mara kwa mara na kuitoa makosa madogo madogo, na hatimaye alimudu.
Mpaka kufikia jioni alikuwa ametengeneza mifuko inayofikia mia sita ya saizi tofauti tofauti na huwezi kuamini ndugu msomaji, wateja alianza kuwapatia pale pale. Na huo ndio ukawa ndio mwanzo wa Saidi kuinuka.
Nililazimika kuibinafsisha ofisi yangu kwa kumuachia rafiki yangu aiendeshe na mimi kuhamia Arusha kwa muda katika kutekeleza majukumu ya kifamilia. Hivi karibuni nilitembelea ofisi yangu, nilipofika pale nilipata ujumbe kuwa Saidi ananitafuta sana na aliacha namba yake ili nikipita pale nimpigie, kwa kuwa sikuwa na simu rafiki yangu alimpigia na kumjulisha kuwa niko pale, Saidi aliniomba nimsubiri kwani alikuwa maeneo ya Kariakoo, niliamua kumsubiri kwa shauku ili kujua sababu ya kunitafuta.
Hata hivyo yule rafiki yang alinijulisha kwamba Saidi mambo yake sio mabaya kwani amenenepa na ana pesa sana simu hizi, kwanza simuamini nikajua ananitania. Haikupita muda Saidi alifika mahali pale, awali sikumjua kabisa mpaka alikiniita kwa jina langu huku akicheka kama kawaida yake. Alinieleza mengi kuhusu maisha yake, baada ya kuwa nimemuanzishia ile biashara. Aliniambia kuwa, ile biashara ilimnyookea na mpaka kufikia wakati ule alikuwa amemudu kufungua duka lake la kuuza CD maeneo ya Tandika na duka lingine la vitenge, khanga na vitambaa vya magauni hapo hapo Tandika pia ameoa na ana mtoto mmoja na amefanikiwa kununua shamba la eka mbili maneno ya Mkuranga, nilimdadisi kama ameanza ujenzi, akanijibu kuwa hajaanza bado lakini yuko kwenye harakati za kuanza, nilimuahidi kumnunulia mifuko kumi ya cement ili aweze kuanza hata msingi, alifurahi sana.
Akisimulia namna alivyomudu, anasema kuwa, kutokana na biashara hiyo ya mifuko kumpatia faida kubwa, rafiki yake mmoja alimshauri aweke fedha zake Saccos, ili akuze mtaji, alianza kuweka kila siku shilingi elfu kumi, na baada ya mwaka mmoja alikuwa amejikusanyia kiasi cha shilingi 3,650,000 kiasi ambacho hakuwahi kuota kuwa nacho.
Mpaka kufikia hapo alikuwa na uwezo wa kukopa shilingi milioni tisa na ushee, lakini hakuwa na dhamana kulingana na mkopo wa kiasi hicho, hivyo alianza na shilingi milioni moja ambapo alianza kwa kufungua biashara ya kuuza kanza na CD kule Tandika na baadae aliweza kuanzisha biashara nyingine ya kuuza vitenge na khanga hapo hapo Tandika. Hata hivyo Saidi anasema kwamba hajaacha biashara ya kuuza mifuko, anaendelea nayo kwani ndio iliyomuwezesha kufikia hapo alipo.
Nilizungumza na Saidi mambo mengi na kusema kweli alionekana kuwa na matarajio makubwa sana, hata mimi alinishangaza sana.
Mafanikio ya Saidi siwezi kujivunia kama sitamtaja yule kijana wa Kigogo ambaye ndiye aliyenifundisha kazi hiyo. Lakini kuna jambo moja najiuliza, hivi kuna watoto wangapi walioko mitaani leo wanaoshi katika mazingira magumu? Bila shaka ni wengi sana, Hivi si tunalo shirika letu la SIDO? Nazungumzia shirika la viwanda vidogovidogo. Hivi hawa wameshindwa kabisa kubuni miradi itakayowawezeka hawa vijana wa mitaani kujiajiri na kumudu maisha ya kujitegemea na hata kuchangia pato la Taifa badala ya kuiacha nguvu kazi hii ikipotea bure.
Tukumbuke kwamba hawa ndio kesho wana Graduate na kuwa vibaka na hata majambazi ambao huishia kupora na kudhulumu roho za watu. Watashindwaje kufanya hivyo ili hali tumewatelekeza watoto hawa. Jamii imewatelekeza, na hata serikali yao imewatelekeza, kwa nini tunakosa ubunifu.
Naomba tutafakari………….