Saturday, January 16, 2010

DADA YASINTA NIMEISHITUKIA JANJA YAKO

Dada yangu akiweka mikakati
Kwa dada yangu Yasinta,

Nimesikitishwa sana na kile ulichobandika katika blog yako ukidai kuwa wewe hutaki kuwa mwanaharakati wa kututetea sisi wanawake na watoto zetu, kama nilikunukuu vizuri umesema kuwa kuandika kwako makala za kutetea haki za wanawake sio kwamba unayo dhamira ya kuanzisha NGO.

Umedai kuwa hujawahi kuota na wala kuwaza kufanya kazi hiyo, bali unaamini kwamba, kuwa mwanaharakati haimaanishi kuwa na Organization. Kwamba huwezi kuwatetea wanawake na watoto isipokuwa mpaka uwe na NGO.

Pia ukabainisha kuwa umeamua kuweka mambo hadharani maana kuna vimbelembele washaanza kujifanya yule shehe wa Mwembe chai aliyetabiri kuwa mwana CCM yeyote atakayechukua fomu za kutaka kugombea urais kwa kumpinga Rais wa sasa Muheshimiwa Kikwete basi atakufa ghafla kwa kubanwa na ngiri. Vimbelembele hao wamekutabiria kuwa kwa kuandika kwako vimakala vya kujifanya una huruma sana na wanawake wanaonyanyaswa na waume zao ni kamchakato kako ka kuelekea kuanzisha Organization ya kuwatetea wanawake nchini.

Duh! Samahani dada nilisahau kukupa heshima yako. Nakupa shikamoo zako wewe na mumeo. Habari za huko ughaibuni mlipo, nasikia kuwa kuna baridi sana kiasi kwamba mabarafu yamejaa kila mahali mpaka chooni. Samahani kwa kutaja chooni, nimesahau kuwa hilo sio neno la kistaarabu, nilikuwa namaanisha toilet.

Dada kama nilivyoanza katika utangulizi wa barua hii, ni kwamba nimeishitukia janja yako. Unajua tangu uhamie ughaibuni dada umekuwa na akili sana.

Sio wewe mwaka juzi ulipokuja huku nyumbani ulianzisha NGO ya kutetea haki za wanawake na watoto kwa kushirikiana na yule binamu yako anayezaliwa na yule shangazi, ambaye analazimisha undugu baada ya kusikia kuwa umeolewa na mzungu kwa kudai kuwa eti zamani alikuwa akimbeba baba yako wakati bibi na babu yako wakienda shamba.

Huyu binamu yako ambaye inasemekana alifeli zaidi ya mara saba kuingia kidato cha pili huko Songea katika ile shule iliyoko pale Mfaranyaki, karibu na ule muembe dodo unaotumiwa na mafundi baiskeli ndiye uliamua kumshirikisha kuanzisha NGO yenu wenyewe ambayo mliipa jina la Ruhuwiko NGO for woman and children crying everyday.
Taasisi hiyo ambayo imesajiliwa na katibu kata ilikuja kwa kasi ya ajabu na inatishia kuvunja ndoa za watu, na mojawapo ya ndoa iliyovunjika ni ile ya yule mzee Ngatura mwenye wake saba.

Ndao iliyovunjika ni ya yule binti machepele wa saba kuolewa na yule mzee. Nadhani unamkumbuka yule binti aliyewahi kufumaniwa na mke wa mwalimu wa kufundisha ngoma za asili pale shuleni, na kutokana na umahiri wa kucheza lizombe yule binti alipewa Umanju wa kuongoza ngoma na mwalimu na kutokana na kupewa cheo hicho mwalimu wa ngoma akamgeuza kuwa kijumba kidogo chake na makutano yao yakawa kule kwenye shamba la kijiiji, na kama unavyojua wambea wa kijiji wakamjuza mke wa mwalimu wa ngoma na hivyo kuwekewa mtego na kufumaniwa. Si unakumbuka jinsi alivyopigwa mpaka akachaniwa nguo zote? Basi kutokana na aibu si ndio akahamishiwa katika shule ya jirani na baba yake ili kukwepa aibu.

Basi huyu binti baada ya kuachika huku akiongozwa na binamu yako wanataka mali za yule mzee zigawanywe sawa kwa sawa la sivyo kesi inapelekwa mahakaam kuu.
Hivi ninavyo kuandikia kuna mashauri zaidi ya wanawake 30 wanaotaka kuachana na wanaume zao kwa kutegemea kugawana mali walizochuma na wanaume zao. Kampeni hiyo ya kuachanisha wanandoa inaongozwa na hiyo NGO yenu na anayeingoza uasi huo wa kuvunja ndoa za watu ni huyo binamu yako.

Hivi sasa hali ni tete pale kijijini na wazee wa kijiji wameitisha kikao cha dharura kujaldili hali hiyo na wanatishia kuchangishana nauli ili waje Dar kumuona muheshimiwa rais ili anusuru ndoa zao zinazoelekea shimoni. Pia wanataka binamu yako huyo aondolewe haraka pale kijijini kwa ile staili ya kuwekewa karantini asikanyage tena pale kijijini iwe ni kwa sherehe au misiba.

Hata hivyo katika utetezi wake binamu yako huyo amejitetea kuwa eti hiyo kampeni ya kuachanisha ndoa za watu ni idea yako yaani kwa kiingereza suggestion yako maana alidai kuwa yeye siye msemaji mkuu wa hiyo NGO, bali ni mtekelezaji wa kile unachokiagiza ukiwa huko ughaibuni.

Sasa dada kwa kutaka kutuchota akili unajidai kuwa hutaki kuwa mwanaharakati wakati tayari ulishakuwa mwanaharakati tangu mwaka juzi. Kwa kuwa unatafuta umaarufu ili kutengeneza mazingira ya kupanua wigo wa hiyo NGO yako kutoka kijijini hadi kuwa NGO ya kitaifa baada ya kuona kule Ruhuwiko umeanza kupoteza umaarufu na ndio maana unataka kupata maoni ya wasomaji wako katika ile staili ya mchomeko, yaani ku bip kwa kiingereza.

Dada samahani naomba univumilie kwa haya ninayoyasema maana mie sitaki uje kuumbuka baadae, kwani Dar es salaamu sio sawa na Ruhuwiko, huku kuna ushindani wa hii biashara ya NGO, usipoangalia utatapeliwa wewe, kuna watu huku ni wasanii ile mbaya, anaweza kuja mwanamke akajidai amegombana na mumewe, na akipata msaada huyooo anaenda kuendelea na ndoa yake kama kawaida. Ukitaka kupanua wigo wa NGO yenu ihamie huku Dar inabidi utafute mganga ambaye anaweza kumwangalia mteja akajua kama huyu ana matatizo kweli au msanii tu.
Dada huku Dar NGO ni mradi wa watu wajanja ambao hutumia staili ya matatizo yenu ndio tijara yetu, na wengi wao ni wale walioshindwa kutofautisha ile dhana kujiajiri na kujitolea. Kwa wao kuitolea maana yake ni kuwekeza kwa kutumia matatizo ya wengine.

Yaani siamini kuwa na wewe umeingia katika kamtindo hako kwa kutafuta fedha kwa kutumia matatizo ya wengine. Nashawishika kuamini kuwa na wewe umefulia kimawazo, kwani hiyo mbinu yako nimeishitukia dada. Hapa Dar humpati mtu labda Kamala na Chacha kwani nao eti ni wanaharakati wa kuwatetea vijana…….LOL

Kwa leo naomba niishie hapa nikipata muda nitakujuza mengi juu ya NGO za hapa Dar.

Nakutakia siku njema.

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Kwa kweli ni jambo la kujivunia kuwa na mdogo kama Koero. Unapendwa sana na familia yangu Yaani basi tu. Nadhani nimekosa la kusema lakini nimesema.

Mija Shija Sayi said...

Koero binti kipaji.

Bennet said...

Nimecheka sana leo, umefanikiwa kuitengeneza siku yangu

MARKUS MPANGALA said...

ngoja kuna washawasha hapa najikuna nitasema kitu baadaye............................................................................................................................................
MCHARUKOOOOOOOOOOO nimeshutukia Koero ni fundi wa kuandika WRITE UP za NGO ha ha ha ha ha> Ngoja kama unaweza kuamini jambo lazima ulifahamu kwanza na kulipima......nadhani mmepima sana kuhusu SIDANGANYIKI haya semeni wenyewe sasa kabala sijacharukaaaaaaa.

NASUBIRI KITABU CHA SIMULIZI ZAKO Mama Matatizo

Kibunango said...

Interesting...