Friday, January 22, 2010

RAISI AMANI KARUME NA MKAKATI WA MARIDHIANO

Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Seif Shariff Hamad na urafiki wa mashaka

Aristotle – yule mwanafalsafa wa kale wa Kigriki aliwahi kusema kwamba “man is a political animal”. Japo kumekuwa na mjadala mrefu (ambao bado unaendelea) kuhusu alichokimaanisha hasa aliposema maneno haya, tunaweza kuchukulia kijuujuu tu hapa kwamba pengine alichokimaanisha Aristotle ni ukweli kwamba binadamu ni mnyama ambaye anajulikana kwa kujiundia mifumo tata ya kisiasa na kijamii, mifumo ambayo ipo hasa kwa lengo la kuhakikisha kwamba anaishi kwa amani kulingana na sheria na amali alizojiwekea. Kutokana na ukweli huu, binadamu pia inamlazimu awe na “watawala” ambao kimsingi kazi yao ya msingi ni kuhakikisha kwamba sheria na amali zilizokubaliwa kufuatwa na jamii zinatekelezwa na kuwa kila mwanajamii anaishi kwa utangamano katika nyanja zote. Inavyoonekana, kama Historia inavyotuonyesha, utawala ni mtamu na tabaka linalofanikiwa kushika nafasi hii mara nyingi huwa halipendi kuiachia kirahisi. Ndiyo maana Historia imejaa wafalme (wa maisha), maraisi wa kudumu na hata madikteta. Ndiyo maana wengine hujaribu hata kubadili katiba ili waweze kuendelea kuwa watawala. Hata katika nchi zinazojidai kuwa na ukomavu wa kidemokrasia, tamaa ya tabaka (au chama) tawala daima ni kubakia madarakani kwa mbinu na gharama yo yote ile.

Leo nitazungumzia suala hili kwa kuangalia mbinu na ujanja unaotumiwa na chama tawala cha Tanzania (CCM) kinapojaribu kung’ang’ania madarakani kwa kuangalia kiinimacho cha maridhiano kule Zanzibar. Sina ugomvi na CCM, na kama nilivyodokeza hapo juu, hata kama chama kingine cha upinzani kingekuwa madarakani leo (mf. CUF, CHADEMA au UDP), kingejaribu pia kutumia mbinu ili kiweze kung’ang’ania madarakani. Tayari tumeshaona baadhi ya viongozi wa vyama hivi vinavyoitwa vya upinzani wanavyoupenda Uenyekiti, Umakamu Mwenyekiti na Ukatibu Mkuu wa vyama vyao kiasi kwamba hawataki kuwaachia wanachama wengine. Unafikiri wakiingia madarakani watakubali kuondoka kwa urahisi hawa? Thubutu! Hebu turudi kwenye mada yetu kuu ya leo - kiinimacho cha maridhiano Zanzibar.

Kama kuna chama ambacho unaweza kukiita chama cha watu wenye kujua kuchezea watu shere basi chama hicho ni CCM. Ndiyo maana kuna kitengo cha Propaganda kinachoongozwa na Hizza Tambwe.

Mimi siyo mfuatiliaji sana wa masuala ya kisiasa, lakini matukio yaliyojitokeza hivi karibuni katika duru za siasa hapa nchini, nimejikuta nikikaa na kutafakari sana, na hatimaye nikajiwa na kitu kama maono.

Kwa wale wanaofanya ‘meditation’ kama rafiki yangu Kamala, anafahamu nazungumzia kitu gani. Ilianza kama masihara, Rais Amani Abeid Karume akamwalika hasimu wake kisiasa Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamadi pale ikulu ili kupata staftahi.

Lakini pamoja na mambo mengine Rais Karume akaja na agenda ya kutafuta suluhu baina ya vyama hivyo viwili, kule Zanzibar, yaani CCM na CUF.

Katika stafutahi hiyo Mheshimiwa Amani Karume akaja na msamiati wa “Maridhiano”. Kama kuna chama kinachojua kucheza na misamiati ya ghiliba za kisiasa zisizo na ukomo, basi CCM inaongoza.

Awali chini ya uongozi wa Rais mstaafu Dk. Salmin Amour waliunda tume ya kutafuta ‘suluhu’ ikiwa inaongozwa na aliyekuwa katibu mkuu wa jumuiya wa madola Chifu Emeka Anyaoku, mnamo mwaka 1999, ikiwa ni mwendelezo wa mtafaruku wa chama cha CUF kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1995 ambapo Salmin Amour akaukwaa urais kwa mara ya pili.

Rais Benjamin Mkapa akishiriki moja kwa moja katika msamiati huo wa “Suluhu”. Hata hivyo baada ya mauaji ya Januari 27, 2001, serikali ililazimika kuamuru jeshi la polisi kutumia risasi za moto kuzima maandamano ya wafuasi wa CUF waliokuwa wakipinga matokeo ya mwaka 2000 yaliyompatia uongozi Rais Karume.

Hapo ndipo ukazuka msamiati wa pili wa ‘muafaka’ baina ya CUF na CCM kutoka msamiati wa ‘suluhu’ chini ya Dk Salmini Amour. Ikumbukwe ‘muafaka’ huo ulishindwa kutekelezwa kutokana na danadana nyingi. Baada ya hapo sasa upo mikononi mwa Rais wa awamu ya nne mheshimiwa Kikwete.

Jitihada za Rais Kikwete kutanzua mzozo huo uliwafikisha hadi kijijini Butiama alikozikwa baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Na hapo ndipo wakazuka na msamiati mwingine wa ‘kura ya maoni’ kama wananchi wanaridhia serikali ya mseto itakayoundwa na vyama hivi viwili(CCM na CUF).

Kwa maana nyingine ‘muafaka’ ulioafikiwa katika kamati za vyama hivyo haukutekelezwa, ndiyo maana tukaona malumbano yasiyo na tija huku CUF wakigomea mazungumzo mengine na CCM kwakuwa maazimio ya awali hayakutekelezwa.
.
Waama! sasa Mheshimiwa Amani Karume kazuka na msamiati mwingine wa nne “Maridhiano”. Hapa kama ni ndoano basi imenasa Jodari. Kwasababu ukihesabu unaona huu ni msamiati wa nne wa kulijadili jambo lilelile na watu walewale………….

Naam! wakati wa hiyo stafutahi ndipo mzee mzima Rais Karume akamweleza Bwana Shariff Hamad, ‘Bwanae!, hii Zanzibari ni yetu sote kwa nini tugombane atii?!!!... huu sio wakati wa maugomvi yakhe!!.., tuijenge nchi yetu ili watu waendelee …kulima na kuvuna Karafuu bila ghasiaaa, au wewe wasemaje?”

Sharrif Hamad naye, akajibu….’Bwana Amani Karume, (Hapo ilikuwa bado kumtambua kama Raisi), umegusa pale ninapopataka, unajua naona sasa wananchi watafikia mahali watachoka na haya mambo ya Unguja na Pemba, huu si wakati wa kuwachezea shere ati, wanifahamu?

….Huu ni wakati wa kuyamaliza mambo haya ili tuishi kama enzi zileee! tukicheza ngoma ya mbwa kachoka na Kibati wan’kumbuka sawasawa?”…

Mheshimiwa Amani Karume naye akaongeza…..‘Nakumbuka shehe wangu, sasa wewe kawakusanye wana-CUF wote pale Kibanda Maiti na kisha katangaze kun’tambua mie kama rais wa Zanzibar nami nitawakusanya wana-CCM wote pale Jambiani kisha nitatangaza kuwa tumeamua kufanya ‘maridhiano’,… waonaje hapo”??!

Seif Shariff Hamadi akajibu, ‘Hapo umenena, lakini shehe wangu, (akainamisha kichwa chini) wewe wawajua hawa Wapemba, ni wakorofi mno hawa, waweza kun’piga hawa. Itakuwaje ulinzi sasa?”…

‘Hapo shehe wangu sina nsaada, kwani nikisema nitumie polisi itakuwa vita, wataona hawa ni njama ya CCM, kwa nini usitumie wale Blue Guard wenu?!’

‘Basi ngoja nikajaribu kisha wewe utaona na kitakachotokea, lakini usisahau kunilinda shehe wangu sawa?’……

Basi huo ndio ukawa mwanzo wa kuanzishwa kwa mchakato wa ‘Maridhiano’. Kilichotokea katika mkutano wa CUF kila mtu anakifahamu, ilikuwa chupuchupu Seif Shariff Hamad atolewe ngeu na Wapemba wenye msimamo mkali, lakini akaokolewa na Blue Guard.

Baadaye Rais Amani Karume naye akaitisha mkutano na kueleza mkakati huo wa kuanzisha maridhiano na CUF. Serikali yetu ikapongeza jitihada hizo na Mataifa mbalimbali nayo yakapongeza hatua hiyo.

Huo ukawa mwanzo mpya kuelekea katika ‘Maridhiano’. Wakati wananchi wakiendelea kutafakari mwanzo huo mpya kati ya CCM Zanzibar na CUF, huku Bara akaibuka mpiga ramli mmoja anayeishi pale Magomeni Mwembe Chai.

Huyu akaja na kali kuliko zote. Kwa umaridadi kabisa bila soni akasema endapo mwana-CCM yeyote atakayechukua fomu za kumpinga Kikwete katika uteuzi wa kugombea urais ndani ya CCM atakufa ghafla.

Hii ni kwa mujibu wa utabiri wa huyu mpiga ramli anayedai kusifika Afrika Mashariki na Kati. Duh!.. watu wakataharuki, kulikoni jamani uchuro huu?. Mpaka sasa bado mjadala huu unaendelea.

Katika duru za siasa kuna watu wanaojulikana kama Political Thinkers (Wataalamu wa sayansi ya siasa au wachunguzi/wachambuzi wa masuala ya kisiasa).

Hawa Political Thinkers ndiyo hasa huwaongoza watawala wetu katika nadharia za mienendo ya wapinzani wao na wananchi(Political Behavourism au Political Behavoralism), na siku hizi wamekoleza kwa kusema ‘Post Behavoralism’. Wenyewe husema eti ni ‘The Mass’(wananchi) na ‘Political Elite’(wanazuoni wa kisiasa).

Inaeleweka kuwa ushauri wa kujenga mitandao ndani ya vyama ulikuwa wa hawa Political Thinkers ambao baadhi yao sasa wanaongoza taasisi kubwa za serikali ikiwemo chuo kikuu cha Dar es salaam.

Hawa ni watu hodari sana katika kusoma hali ya kisiasa na kutengeneza propaganda pale ambapo viongozi wa kisiasa wanapotaka kutekeleza agenda zao, ni watu ambao wakati mwingine hueneza uvumi ili kupima uelekeo wa umma(Public reaction) kabla ya maamuzi kamili.

Na maamuzi mengine hufanywa hata pale maandamano ya kupinga jambo lolote katika nchi au mgongano wa wananchi na serikali yao. Wenyewe huita ‘Divide and rule’, wagawanye na uwatawale. Kwa maana nyingine msingi mkubwa hapa ni kwamba kitendo cha wananchi kuridhia ‘maridhiano’ yale ndiyo majilio ya kuongezewa muda wa kutawala kwa Rais Karume.

Political Thinkers hawa kuna wakati pia huwatumia wapiga ramli kama Shehe wa Magomeni Mwembe Chai, yaani Shehe Yahya Hussein. Hupima uelekeo wa kisiasa na kutoa ushauri kuwa nini kifanyike pale panapotokea ombwe la kisiasa.

Sote tunajua kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwa upande Bara, Rais aliyepo madarakani bado anataka kumaliza kipindi chake cha pili cha miaka mitano.

Lakini kwa upande wa Zanzibar, Rais Karume anamaliza ngwe yake ya miaka kumi na anatakiwa kuondoka, ili aje raisi mwingine, bila kujali atatokea CCM au CUF.

Maswali ninayojiuliza ni haya; kwanini suala la ‘maridhiano’ lijitokeze wakati huu wakati Rais Amani Karume anamaliza muda wake? Je kipindi chote cha miaka tisa alikuwa wapi? Ni kwanini Seif Hamad akubali kumtambua Rais Karume kipindi hiki?

Hivi nitakosea nikisema kuwa agenda hii ya maridhiano imekuja wakati huu, mahsusi ili kutengeneza mazingira ya Rais Amani Karume kuongezewa muda wa Urais kwa kisingizio cha kuweka sawa haya maridhiano?

Kwa nini nisiamini hivyo wakati tayari Wanachama na Viongozi wa vyama vyote viwili wameshafanya maandamano ya pamoja na kumuomba Raisi Karume akubali kuongezewa muda wa Uraisi ili aweze kuyaendeleza haya Maridhiano.

Hata hivyo wakati wa Kilele cha Sherehe za Mapinduzi, Rais Amani Karume akatangaza kuwa Uraisi wa Zanzibar ni miaka kumi tu kwa mujibu wa katiba, hivyo hatagombea tena.

Hii siyo danganya toto kweli? Kwanini wamsemee eti aongezewe muda halafu mwenyewe anajidai kukataa? Je iwapo katiba itarekebishwa na kuombwa aendelee tena na Urais atakataa?.

Hili tunaomba alijibu kwa yakini ili historia imhukumu. Upande wa Bara, CCM ikiongozwa na Katibu wake mkuu Luteni mstaafu Yusuf Makamba na katibu mwenezi Kapteni mstaafu John Chiligati, wakahamaki na kudai kuwa haiwezekani katiba ya Zanzibar kuchezewa, urais mwisho ni miaka 10.

Huu sio mkakati kweli wa kujaribu kupima upepo, naamini hapo baadaye Wazanzibari wakidhamiria katiba irekebishwe ili Rais Amani Karume aendelee kuongoza, hawa kina Makamba na Chiligati hawatatueleza mambo ya Wazanzibari waachiwe wenyewe????.

Je mpaka hapo lengo halijatimia na kuongezwa muda wa kututawala??? Jamani mimi siyo Mnajimu, au msoma elimu ya nyota, bali hizi ni Porojo zangu tu! Tukumbuke kwamba, kama alivyosema Aristotle, “man is a political animal” na kwamba madaraka ni matamu. Wenye nayo wanayakumbatia na kuyaengaenga ili wayahodhi daima dumu. Nadhani hiki ndicho kinachojaribu kufanywa kupitia hiki kiinimacho cha Maridhiano!
Mwaonaje waungwana??!!

7 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Hiki kinachoendelea Zanzibar ni win-win solution kwa Karume na CCM.
Kwanza ninukuu uliposema "binadamu ni mnyama ambaye anajulikana kwa kujiundia mifumo tata ya kisiasa na kijamii, mifumo ambayo ipo hasa kwa lengo la kuhakikisha kwamba anaishi kwa amani kulingana na sheria na amali alizojiwekea."
Yaani hakuna kinachotendwa na kiongozi wa kisiasa kisicho na maslahi kwake na chama chake kisha nchi yake. Yaani hata hawa uwasikiao wanakurupuka kusema hili na lile wanatanguliza "u-wao" kwanza. Hili nadhani Profesa Matondo atalizungumzia saana maana amelizungumzia kabla.
Lakini kama ulivyosema, maigizo yao hayajawa na characters walio makini. Leo hii Mhe Karume anakubali kufanya maridhiano na Mheshimiwa sana Shariff. Na anajua kuwa yeye (Karume) harejei kugombea. Ina maana Shariff akisema aendelee na kipindi na wengine wakagoma basi Shariff ataonekana kama ambaye anapenda maridhiano na hivyo akigombea ndiye atakayepewa nafasi kubwa ya kufanya vema (at least kwa upande wa upinzani). SI ANAKUJA KUENDELEZA YALE WALIYOKUBALIANA NA MHE KARUME??? SASA MTABISHA? HAMTAKI MARIDHIANO? KAMA MNATAKA BASI MPENI "INSIDER" ALIYEKUWEPO KWENYE UANZILISHI WA MARIDHIANO HAYO NA AMBAYE "HAKUWA NA TAMAA YA MADARAKA KAMA ANAVYOPENDA MARIDHIANO" NDIO MAANA AKAOMBA Mhe KARUME AONGEZEWE MUDA (japo alijua haiwezekani)
Lakini faida ya pili ni kwa CCM ambao wanajua fika kuwa Sahariff akigombea atakuwa na chance ndogo ya kushinda hivyo walichofanya ni kumtengenezea mazingira mazuri ya mtego (set up) ili agombee, ashindwe kisha akigoma kumtambua rais ajaye ataonekana mwenye uroho wa madaraka na si msaka maridhiano.

Ooooooh!!!! I loooove POLI-TRIX.
Just Kidding....
I HATE IT.

Yasinta Ngonyani said...

Haki ya Mungu ya leo ni kali mnoooo! Duh, kazi ipo

Ramson said...

Dada Koero wewe bi zaidi ya yule Shehe wa Magomeni Mwembechai yaani Shehe Yahaya Hussein. Kwani Utabiri wako utatimia sawasa.

Kama alivyosema kaka Mubelwa hapo juu, kuna kamtego mzee Shariff Hamad ametegwa kwa hiyo asilaumu matokeo.....

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hakuna mtego hizi ni dangannya totooooooo

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...
This comment has been removed by the author.
Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

"Hata katika nchi zinazojidai kuwa na ukomavu wa kidemokrasia, tamaa ya tabaka (au chama) tawala daima ni kubakia madarakani kwa mbinu na gharama yo yote ile"

Hii imenikumbusha lile sakata la uchaguzi wa urais hapa Marekani mwaka 2000 ambapo kila mtu anajua kwamba rais Bush (II) alishindwa na Al Gore. WaRepublican walifanya kila njia kuhakikisha kwamba wanalichukua jimbo amuzi gombaniwa la Florida hata kama ni kwa kuiba kura. Na kweli kura ziliibwa na mwenzao akaupata uraisi. Kilichofuatia hapo tunakifahamu. Vita visivyo vya lazima vikaanzishwa na miaka michache tu akawa ameshaitafuna ziada ya bajeti aliyoikuta na kuitumbukiza nchi katika madeni makubwa na hatimaye uchumi kuyumba. Lakini marafiki zake walitajirika ajabu kwa kupatiwa mikataba ya kutengeneza silaha na miundo mbinu ya Iraq (Halliburton n.k.)

Kwa hivyo mchezo huu uko popote pale na invyoonekana CCM ni magwiji hasa wa kuucheza. Historia hata hivyo inatuambia kwamba hatimaye watu huchoka na michezo ya aina hii, wakainuka na kuleta mabadiliko ya kimfumo. Kinachoumiza na kushangaza zaidi ni kwamba hata hao wapya wanaopewa madaraka katika mvuvumko mpya nao huugeuka umma uliowaweka madarakani na kuishia kufanya yale yale (na hata kuzidi) ya watangulizi wao. Ndiyo maana mimi sina matumaini wala imani na hivi vyama vya upinzani (tazama hapa: http://matondo.blogspot.com/2010/01/ni-kweli-au-ni-kauli-mbiu-yenye-ombwe.html).

Kamwe usimwamini mwanasiasa hata kama ni baba yako, mama yako, mke wako au mtoto wako.

Kamwe usimwamini mwanasiasa - HATA KAMA NI WEWE MWENYEWE!

MARKUS MPANGALA said...

INDIDE JOB