Friday, November 26, 2010

CHAI YA MKANDAA NA MUHESHIMIWA!

Siku hiyo ikifika!

Ijumaa ya leo nimeamka alfajiri na mapema, niliamka majira ya saa kumi na moja alfajiri, nje kulikuwa na dalili ya mvua kwani kulikuwa na wingu zito ajabu. Naam kitambo kidogo nikiwa nimesimama dirishani nikiwa bado nimevaa gauni langu jepesi la kulalia nikaona manyunyu ya mvua yakidondoka katika ardhi hii ya mwenyezi mungu. Yale manyunyu yalikuwa yakidondokea juu ya maua yaliyopandwa upenuni mwa nyumba yetu na yalikuwa yakichirizika taratiibu na kudondoka chini na kupotelea ardhini. Kwa kuwa ardhi ilikuwa kavu sana yale matone ya manyunyu yalikuwa yakimezwa na ardhi sawia.


Nikiwa pale dirishani nikiwa nimetumbua macho yangu nje, naam, nikaanza kuwaza, na kuwaza huko kulikuwa kama masihara hivi, ni jambo ambalo sidhani kama linawezekana lakini nilijikuta tu nawaza. Niliwahi kusoma katika blog ya kaka yangu Mtambuzi Shaban kuwa sisi wanaadamu huwa tunapitiwa na mawazo kati ya 5000 mpaka 6000 kwa siku, na ndio maana sikushangaa sana kujikuta nawaza juu ya jambo hilo.


Nilikuwa najiuliza, hivi itakuwaje siku moja itokee Muheshimiwa Rais anialike Ikulu ili kupata naye chai japo ya mkandaa? Sijui ni kwanini niliwaza hivyo, lakini nilijikuta tu nawaza juu ya jambo hilo. Lakini kama itatokea siku nikipata mwaliko huo…….kwanza sidhani kama nitalala, kwani nitakuwa nikiwaza jambo la kumweleza muheshimiwa, najua yapo madhila mengi sana yanayotukabili, lakini je nianze na lipi?


Je nianze kwa kumweleza madhila yanayowakabili wanawake na watoto? Lakini anaweza kunikata kalma na kunipa ushahidi kuhusiana na jinsi anavyojitahidi kuwawezesha na kuwapa vyeo wanawake na ninajua hatasita kumtaja Spika mpya wa Bunge mama Anna Makinda. Hapo nitaonekana sina jipya, Je kuhusu huduma za Afya? Hapo anaweza kunikumbusha kuwa katika kampeni zake ameahidi kujenga hospitali za rufaa kila mkoa.


Ebo! Sasa nitamweleza jambo gani….Niliendelea kuwaza……… Eheeeee… nimekumbuka Kilimo, nitamweleza kuwa siku hizi mtu kuitwa mkulima ni kama kumtusi, kwani kilimo kimepuuzwa sana na serikali, lakini hilo nalo anaweza kunishangaa, anaweza kuniuliza, hivi sijawahi kusikia kampeni za Kilimo Kwanza ambapo serikali imeelekeza nguvu nyingi katika sekta hiyo ili kuhakikisha kuwa tunafanya mapinduzi ya kijani? Pia anaweza kuniambia kuwa hata waziri wa wizara hiyo amemteua mjomba wangu Jumanne Maghembe.


Mweh! Sasa nizungumzie nini? Ok, hapa naona nitakuwa nimepatia, nitamuuliza kama atawachukulia hatua wale wote waliotuhumiwa kwa ufisadi bila kujali kuwa ni marafiki zake……… lakini hili nalo anaweza kuniruka kimanga, ‘ we huwaoni kina Basili Mramba, Yona na Mgonja wana kesi mahakamani?’ anaweza kusema hivyo..…….


Nadhani nitakuwa nimeishiwa na hoja……..Hebu nisaidieni wasomaji na wanablog wenzangu, hivi siku kama jambo hilo likitokea nizungumzie nini?

8 comments:

Ramson said...

Binti unawaza mambo makubwa weye...., Nakuombea ndoto yako iweze kutimia, ila jiandae kwa kweli maana usije ukajikuta unashikwa na kigugumizi, matatizo tuliyo nayo ya msingi ni mengi na kikubwa zaidi mshauri asione haya kutumia sera za CHADEMA ambazo kwa kweli ziliwavutia wapiga kura wengi kwa mfano kushusha bei ya cement, mabati na elimu bure mpaka kidato cha sita, akiamua kubana matumizi ya serikali yake na kupunguza misamaha ya kodi atamudu.

yapo mambo mengi ya msingi ambayo hata yeye anaweza kukiri kuwa wakati wanatunga ilani yao ya uchaguzi mwaka huu walikuwa na makengeza na hawakuyaona na ndio maana wakajikuta wanapigwa kumbo na wapinzani.

Yasinta Ngonyani said...

Nadhani wakati mwingine la kusema linatokea pale unapokutana na mtu kwa hiyo usihofu la kusema litakuwa na litakuwa la muhimu sana ndoto nzuri K.

Simon Kitururu said...

Mmmh!

Mija Shija Sayi said...

Yapo mengi ya kumuuliza ila muulize, pindi amalizapo muda wake je kumbukumbu gani chanya atakayoiachia nchi? kwa maana nyingine anadhani atakumbukwa kwa lipi la msingi alilowafanyia wananchi?

Albert Kissima said...

Mwulize kama anaona kuna umuhimu wa kuwa na katiba mpya yenye kutoa mwongozo sahihi ktk mambo mbali mbali na hasa hasa kwenye sheria za uchaguzi na tume ya uchaguzi.

Unknown said...

Naungana na dada Yasinta, mara nyingi inatokea kuwa unapokutana na mtu mambo kibao ya kuzungumza yanakuja..Siku hiyo ikitokea, utapata mengi tuu, hapata kuwa na shida kabisa.Nakuombea mema!!
Weekend njema!!

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

mmmh! Haya nenda mwana nenda!

Da Mija, nadhani hiyo ni simpo kabsaa..kuchekacheka kwa sana hata kwa mambo ya msingi ndo atatuachia :-(

Jacob Malihoja said...

Hamjambo Blogers? nimefurahi kuona mawazo ya Koero, mimi nina hoja moja tu ambayo kwa Koero na yeyote atakayepata nafasi ya kuonana na rais ni muhimu kumuuliza;

Maelezo: "Siku za muvua maji hujenga desturi ya kuzusha mikondo katika majumba ya watu" Swali: "Lipi jema kati ya kujengea mfereji maji yaende yanakotafuta kwenda ama kuziba mkondo huo?"

Akisha kupa jibu, malizia chai yako na uondoke, usubiri miaka mitano itakwishaje.