Wednesday, January 26, 2011

KUSENGENYA: TABIA ISIYO NA MWISHO MZURIHebu chukulia umechelewa kufika kazini , unapofika ofisini unasikia sauti za wafanyakazi wenzako wakizungumza kwa ndani, unapofungua mlango na kuingia, ghafla wananyamaza na kukuangalia kwa mshangao!
Jiulize walikuwa wanazungumzia nini?

Kwa kuangalia mfano huo kwa haraka utagundua kwamba walikuwa wanazungumzia jambo linalokuhusu au walikuwa wanakusengenya. Kwa mujibu wa watafiti mbalimbali, imethibitishwa kuwa wanawake na wanaume wote wanasengenya, labda kinachowatofautisha ni uwiano kwamba wanawake ndio wasengenyaji wazuri zaidi ya wanaume.

Hebu jaribu kutembelea kwenye saluni za kike, utakuta hakuna kinachozungumzwa huko zaidi ya kusengenya, tena kibaya zaidi ni usengenyaji wa kubomoa na kuharibu umaarufu wa watu wengine. Kama wamemtembelea mwenzao au kuhudhuria mazishi ya msiba unaomhusu mwenzao, shuhudia mazungumzo yatakayotawala wakati wanarudi.

Njia nzima mjadala utakuwa unahusu maisha ya mwenzao, kwamba hana hiki , hana kile, au mazishi hayakuwa mazuri kama ya fulani, pia hata kulinganisha thamani ya jeneza la maiti na umaarufu wa mhusika. Utawasikia wakisema “kuringa kote kule kumbe si lolote wala si chochote, ndani kwake kubaya, hana hata kitu cha thamani ukilinganisha na mavazi yake na umaarufu wake”.

Litazungumzwa hili na lile ilimradi tu kumbomoa mhusika. Hivi karibuni niliamua kufanya kautafiti kadogo pale ilipo biashara yangu kwa kuwauliza baadhi ya wateja wangu na wapita njia wengine. Nilizungumza na baadhi ya wanawake pamoja na wanaume kadhaa kuhusu hili suala la kusengenya. Dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Sharifa, alithibitisha kuwa ni kweli sisi wanawake tunaongoza kwa kusengenya, lakini alitetea kuwa kuna tofauti ya kusengenya na kumzungumzia mtu au watu kwa mazuri na mafanikio yao.

Sharifa alibainisha kuwa sio vibaya kumzungumzia mtu kutokana na mafanikio yake, kwani hiyo kuwapa fursa ya kujifunza kulingana na mafanikio ya mwenzao, pia hata wanapozungumzia mapungufu ya mtu, hiyo ni kwa ajili ya kujifunza kutokana na mapungufu ya mwenzao. Dada mwingine aitwae Bupe, alisema kuwa hata wanaume nao husengenya, yeye alishawahi kumfuma mvulana ambaye punde tu alitoka kufanya naye mapenzi akiwasimulia wenzake jinsi yeye (Bupe) alivyo awapo kitandani, kuanzia mwili wake hadi namna anavyofanya mapenzi.

Ukweli ni kwamba hakuamini tukio lile kwa sababu mvulana aliyemwamwini na kuamini kumkubali kuwa mpenzi wake baada ya kumtongoza kwa muda mrefu, angeweza kusimulia yale yote aliyoyasikia. Kibaya zaidi hata wale waliokuwa wakisikiliza ule utumbo walionekana kwa nje, kuwa ni watu wenye busara. “Usiwaone wamekaa kwenye makundi wakizungumza ni wasengenyaji wazuri sana, tena usidhani wanajadili jambo la maana, sanasana wanazungumzia wanawake wale waliotembea nao alisisitiza Bupe”.

Kijana mmoja aitwae Dikupila ambaye anamiliki saluni ya kunyoa nywele jirani na ofisi yangu, kwa upande wake aliyewatetea wanaume kuwa siyo wasengenyaji, kwani hayo ni mambo ya wanawake. “Sisi wanaume kusengenya! Haiwezekani, hayo ni mambo ya wanawake, sana sana ukikuta mwanaume anajadili udhaifu wa mpenzi wake hadharani basi ujue huyo jamaa anamatatizo makubwa ya kiakili” alisema Dikupila.

Watu wengi wa jinsia tofauti niliobahatika kuzungumza nao walikuwa wanakiri kusengenya lakini walikuwa wanajaribu kutengeneza fasili ya neno kusengenya kwa namna ya kukidhi haja zao. Kwao kusengenya walisema ni mtu kutafuta namna ya kujifunza kuwa bora kupitia makosa ya wengine. Je tabia hii inaweza kuachwa? Wengi walikiri kwamba siyo rahisi tabia hiyo kuachwa kwani imekuwa ndiyo sehemu ya maisha, kwamba haiwezekani watu kukaa pamoja na kuacha kuzungumza matukio na yanapozungumzwa matukio, ni lazima yatawahusu watu hivyo kujikuta watu wanasengenya.

Na tabia hii imejikita kila mahali kuanzia nyumbani, mitaani, hadi maofisini, mashuleni na vyuoni. Binafsi naamini kwamba tabia inaweza kuachwa kwa watu wakijikita zaidi katika kufanya kazi na kuwa wabunifu, hasa maofisini. Kama ni suala la mazungumzo iwe ni ya kuleta ufanisi na tija katika kazi kwani waajiri hulipa mishahara kutokana na ufanyaji wetu wa kazi na uzalishaji.

Utakuta mtu anafika kazini amechelewa na akifika anaanza kusengenya, atazungumzia hili na lile wakati muda unaenda na muda wa kazi ukiisha anafunga kazi na kuondoka. Ukichunguza utakuta tangu asubuhi hakuna chochote alichofanya zaidi ya umbea. Watu wa aina hii wanakuwa wa kwanza kulalamika mishahara ikichelewa. Yapasa watu kubadilika na kutia shime katika ubunifu.

Majumbani na mitaani vilevile nako hapafai. Kwa mfano utakuta mtu ana saluni yake na ana wateja wengi wanasubiri kuhudumiwa lakini wahusika utawakuta wanatumia muda mwingi kusengenya na hivyo kupoteza muda bure. Wale wateja wenye haraka kwa kawaida huwa wanaondoka na kutafuta mahali pengine. Hivyo ikiwa watu watajirekebisha kwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha tabia ya kusengenya naamini nchi hii uchumi wake utakua kwa kiwango kizuri na kila mtu atafaidi matunda ya jasho lake.

Ni vema kama mtu hawezi kusema jambo lolote zuri kuhusu mwenzake akakaa kimya, kwani ni njia bora ya kusitiri heshima yake.

Makala hii niliwahi kuiweka mwaka juzi Febuari 2009, na leo nimeikumbuka na kuona sio vibaya tukijikumbusha.

9 comments:

Goodman Manyanya Phiri said...

Mdogowangu Koero weee!Umepata joto na jasho juu ya jambo dogo, jambo la kawaida tena jambo la kimaumbile ya akili kwa binadamu.


Mi na sema anayesengenya ni mtu mzuri kwani anakupasha na kukutaarifu. Mtu mbaya ni yule anayesikiliza hizo habari PAMOJA NA UTUMBO WAKE USIYEKUWA NA MAANA YOYOTE ILE. Niulize kivipi?


Mie nauza mandazi, na kwenye kibao juu ya hayo mandazi SIKU MOJA GHAFLA unakuta na kusoma:

"Mandazi haya leo nimetia sumu kusaidia wanaotaka kufa haraka".


Je, utanilaumu mimi mfanyabiashara wakujitafutia pesa nchini huru au utajilaumu mwenyewe kwa kuyanunua? Ni kosa kunilaumu mimi kwani kama nia yako nikujipeleka huko peponi haraka, utajinyonga tu kwa vyovyote vile mandazi yapo mandazi hayapo!

Ya mwisho, kuwa na wasiwasi mkubwa na maisha yako watu wanapoacha kukusengenya... inamaana umekwishakufa. Lakini kama mtu mwingine anakuja kwako kumsengenya mwingine nawe hapo hufurahii tendo hilo, VUMILIA TU mpaka msengenyaji amalize kwani hio inamsaidia kuondoa STRESS yake, unajua!


Anapomaliza tu, mpigie simu yule aliyekuwa anamsengenya naye aje na mpe tena "msengenyaji" fursa arudie mbele zake yale aliyekwambia wewe awali labda "msengenyiwa" anaweza akamfafanulia zaidi "msengenyaji" kwanini hali ilikuwa kama alivyoyiona yeye ni "STRESS".


Lakini tuseme tunapiga marufuku tendo la kusengenya haiji kabisa! Ni maumbile yetu sisi binadamu! Na hapohapo watu wanahaki kabisa kutoa maoni juu ya mazishi nyumbani kwako...kwanini wasitoe?

chib said...

Kuna mtu alisema bila kusengenya kijiwe hakinogi, na mwingine alisema kazi ya ususi inachukua muda mrefu, hivyo kupiga stori za maendeleo watu huchoka, hivyo huchombeza misengenyo kupitisha muda.
Na kuna wengine wakitaka habari za umbeya au udaku, basi hujongelea mikusanyiko iliyobobea kwa misengenyo.
Bahati mbaya mikusanyiko inayoweza kuchanganua misengenyo inawahusu wanawake hususan katika ususi wa nyele, na mikeka, mtoni kwenye kufua, kupakaa hina, nk. Wakati shughuli za wanaume ni chapchap kama kunyoa nywele, kukutana kwenye pombe (muda mfupi tu kumbukumbu kwisha), sehemu nyingine ni za kazi ngumu kama kugonga kokoto, kubeba mizigo, kupiga debe nk, na kwa sababu kazi hizo zinaendana na ka-bangi kidogo kuzimua misuli, basi misengenyo ya wanaume hao huishia kutukana matusi mazito.

Markus Mpangala said...

“kuringa kote kule kumbe si lolote wala si chochote, ndani kwake kubaya, hana hata kitu cha thamani ukilinganisha na mavazi yake na umaarufu wake”.
>>>>>>>>>>>>>>
nimenukuu sentensi hii lakini maoni ya kaka zangu yamenibadilisha sana
@Godwin, heshima kwako kaka.
@kaka Chib, vijiwe vyetu toka Ikulu hadi huko kwetu Nyasa wanasengenya, Ila sijui ni kwanini watu tunafikiria kuna kusengenya na kusengenywa, lakini ni muhimu kueleewa tu kwamba WATU WANA MAMBO

@Koero uliwahi kusema MBOMBO JILIPO, nami nakukumbusha neno hilohilo.

wakati nahamia kaofisi ka pale Samora a.k.a kona ya daily news, ngumi ya kushoto ya Habari Leo nilipata taabu sana ya kucheka. Nilishtukia tu kina dada mtu Bee, aise ilikuwa kazi ngumu sana. Lakini siku moja nikasema, wasengenyaji WANASHIBA HEWA. Miminashiba chakula. mwisho wa siku duh! jamaa hatukukupa pale mwanzoni kumbe ndio wewe.

kudadadekiiii nikapotezea mbaliiiiiii, Lol.

ha ha ha ha ha LAKINI HII MADA INANOGA SANA UKICHORA PICHA YA SALUNI ZA KIKE sijui huko kukoje maana sijawahi kutimba miguu.

asante Mama Mchungaji Koero kwa kuchunga kondoo wako.

Yasinta Ngonyani said...

nanukuu "Ni vema kama mtu hawezi kusema jambo lolote zuri kuhusu mwenzake akakaa kimya, kwani ni njia bora ya kusitiri heshima yake."mwisho wa kunuu. Nakubaliana kabisaaa fanya kazi kwa kumjadili fulani wewe yako nani anayajua?

Koero Mkundi said...

Kaka Markus, kweli Mbombo Jilipo, maana juzi niliwakuta mashoga zangu fulani wamemkalia shoga yao mwngini KIGWENA wakimsengenya, yaani niliwashangaa sana, lakini cha kushangaza zaidi, ni pale mmoja wa mashoga wale alipoondoka kibao kikamgeukia, wakaanza kumsengenya na yeye, .....mweh! nikawauliza 'hivi nyie hamna kazi za kufanya? kulikoni kuwasengenya wenzenu?' nilipewa jibu moja tu nikajiondokea.... 'bibi wewe mwanamke kusengenya ni suna kama hupendi chapa mwenndo utuanche na stori zetu'
kusema kweli huwa nakwazika sana niwaonapo watu wakisengenya.

naomba tubadilike...............

emu-three said...

Kuna watu wammechunguza kuwa wanapokutana watu zaidi ya mmoja, kama watakaa kuzungumza zaidi ya nusu saa, lazima watasengenya...sizungumzii mikutano yenye ajenda...mazungumzo ya kawaida tu...
Imekuwa na hulka ya binadamu kusengenya, kuteta..nk, na hili ni dhambi, lakini mmmmh, ...sijui

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hata kanisani humsengenya shetani!

Goodman Manyanya Phiri said...

@kamala

Mtundu sana weeMkuu!

Na ""umenivunja mbavu?? (YOU HAVE GOT MY STOMACH IN STITCHES) hapo kuhusu jinsi Shetani naye anavyosengenywa huko kanisani!!!

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___