Wednesday, May 25, 2011

NI MIAKA 26 SASA TANGU AZALIWE, LAKINI MIKASA, VISA NA VIJIMAMBO, VIMEENDELEA KUMTIA NGUVU.




Ilikuwa ni siku ya Jumamosi ya Sabato ya May 25, 1985, majira ya saa nne usiku ndipo binti huyu alipozaliwa. Alizaliwa akiwa na afya njema na uzito wa kuridhisha, ambapo siku iliyofuata mama wa binti huyu aliruhusiwa kutoka na kurejea nyumbani na kichanga chake.


Kalikuwa ni katoto kazuri ka kike ambako kalileta faraja katika familia ile ambayo tayari ilikuwa na watoto watatu wa kike na wawili wa kiume na hivyo kakawa kameongeza idadi ya watoto wa kike na kuwa wanne na kufanya idadi ya watoto katika familia hiyo kuwa na watoto sita.


Naambiwa kuwa binti huyu alikuwa na kipaji cha ajabu, hadi kiliwatisha wazazi wake, zile hatua za makuzi ya mtoto alizipitia lakini akiwa amewahi zaidi, kwa maana ya kuwahi kukaa, kusimama, kutembea na hata kuongea.


Akiwa na umri wa miaka miwili, tayari alikuwa amemudu kuwasha luninga na kubadilisha channel atakavyo, na si hivyo tu, alikuwa ni mdadisi na alikuwa ni mtoto anayependa kujifunza kila jambo.


Binti yule aliendelea kukua kwa umri na kimo huku akiwa na afya njema. Ni pale alipofikisha umri wa miaka mitano ndipo jambo lisilo la kawaida lilipomtokea binti huyu na kubadilisha kabisa historia ya maisha yake.


Inasimuliwa kuwa ilikuwa ni majira ya usiku ndipo binti huyu alipopatwa na homa kali sana, ambayo iliambatana na kile kinachoitwa degedege.


Kuumwa ghafla kwa binti yule kuliistua familia ile, na katika jitihada za kutaka kuokoa maisha yake alikimbizwa hospitali ya binafsi iliyopo jirani na pale kwao.


Alipofikishwa Hospitalini mama wa binti huyu alishauriwa na Daktari amkande na maji ya baridi ili kushusha joto la mwili ambalo lilikuwa limepanda kiwango cha kutisha. Daktari yule alitoa ushauri kuwa itakuwa ni jambo la hatari kuanza matibabu huku mgonjwa akiwa na joto kali kiasi kile.


Kwa kuwa Daktari alikuwa amemaliza zamu yake aliondoka nakuacha maagizo kwa Daktari na Muuguzi waliokuwa zamu akiwaelekeza hatua za kuchukua kulingana na maelekezo aliyoyaandika kwenye cheti.


Baada ya joto la mwili kupungua mama alimwita yule Muuguzi wa zamu na kumjulisha kuwa joto la mwil limepungua. Yule Muuguzi akiwa bado ana hali ya kuonesha kuwa katoka usingizini alisoma cheti na kisha akaenda kuchukua dawa.


Alirejea akiwa na vichupa vya dawa na sindano, na kumchoma sindano binti yule. Ile sindano ilisababisha binti kupoteza fahamu. Kuona hivyo alikimbia kumwita Daktari wa zamu.


Daktari wa zamu alipofika alimpima binti yule na kutoa maelekezo achomwe sindano nyingine haraka na kisha atundikiwe Drip. Maelekezo ya daktari yalifanyiwa kazi lakini binti yule hakuzinduka, ilibidi zifanyike Juhudi za kumhamishia Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambapo alipelekwa moja kwa moja chumba maalum kwa wagonjwa mahututi (ICU). Alikaa kule kwa siku tano, na alipopata nafuu, akarudishwa kwenye wodi ya watoto na kuendelea na matibabu.



Binti aliendelea kupata nafuu, lakini kulikuja kugundulika kuwa amepatwa na tatizo lingine, nalo ni la kupoteza uwezo wa kusikia. Juhudi za Madaktari wa masikio kumtibu binti huyo zilishindikana, lakini mwishowe wakasema kuwa lile ni tatizo la muda tu, na limetokana na sindano ya kwinini aliyochomwa katika zahanati aliyotibiwa awali, hivyo ikiisha nguvu atarudisha uwezo wake wa kusikia.


Habari ile haikuwafurahisha wazazi wa binti, lakini wafanye nini, na limeshatokea. Walisubiri kwa taktiban mwaka mzima, lakini hapakuonekana dalili yoyote ya kupona wala kupata nafuu. Ni dhahiri sasa walizidi kupata wasiwasi, kwani binti yao kipenzi alikuwa hana uwezo wa kusikia na ule uchangamfu, udadisi, na utundu aliokuwa nao, ulitoweka. Hali hiyo iliwanyima usingizi.


Hawakukata tamaa, wakageukia kwenye maombi, lakini maombi yao hayakujibiwa haraka kama ambavyo watu wengi wangependa. Wakakata shauri kwenda nchini Afrika ya Kusini, kwa matibabu zaidi. Walipofika kule, Daktari aliyewapokea, alimfanyia binti vipimo na kwa kushirikiana na Madaktari wenzie walitoa pendekezo wamfanyie binti upasuaji, ili kurekebisha ile hali.


Lakini siku iliyofuata, ambapo ilikuwa afanyiwe vipimo zaidi kabla ya upasuaji, yule Daktari alibadilisha uamuzi na badala yake akatoa pendekezo binti anunuliwe vifaa vya kumuwezesha kusikia, (Hiring aid) halafu baada ya mwaka mmoja warudi kwa ajili ya vipimo zaidi.


Kwa kifupi walisema kuwa ni mapema mno kukimbilia upasuaji kwa kuwa waliamini kwamba kuna uwezekano mkubwa binti akapata uwezo wa kusikia baada ya dawa aliyochomwa kuisha nguvu.


Walirudi nchini, na kuendelea na maisha, na baada ya mwaka mmoja hali haikuonekana kutengemaa, waliporudi Afrika Kusini maelezo yalikuwa ni yaleyale. Waliambiwa warudi Tanzania na kama kutakuwa na tatizo basi waende Muhimbili, kwani tatizo la binti linaweza kutatuliwa hapo. Juhudi mbalimbali za kitabibu zimefanyika lakini bado hazijazaa matunda.


Hali hiyo imemfanya Binti huyo kuwa mbali na mawasiliano ya simu hususan za mkononi akitumia zaidi Ujumbe wa badala ya kuongea, kutokana na tatizo hilo. Mawasiliano mengine anayopendelea anapotaka kuwasiliana na ndugu jamaa, wanablog, wasomaji wa blog na marafiki ni kwa kutumia barua pepe, kwani hiyo imemjengea marafiki wengi na amekuwa akiwasiliana nao kiurahisi zaidi.


Leo hii ni miaka 26 kamili tangu alipozaliwa binti huyu, na ni miaka 21, tangu alipopatwa na tatizo hilo ambalo ki-ukweli bado linaaminika kuwa lilisababishwa na muuguzi ambaye alimchoma sindano ya kwinini, badala ya kumtundikia Drip, kama alivyoandikiwa na Daktari aliyempokea binti huyo.


Bado anawaza ni wangapi baada ya mkasa wake wamepata matatizo kama haya? Ni wangapi wamesababishiwa maumivu, ulemavu na hata kifo kwa maamuzi finyu ya kutofuata maelezo ya Madaktari?


Anawaza ni wauguzi ama Madaktari wangapi ambao wametenda makosa kama haya na kuonywa ama kuwajibishwa kwa namna yoyote ile ili matatizo wanayosababisha kwa jamii yasiwe kitu kinachotokea kila mara?


Anawaza ni wangapi ambao tofauti na yeye hawawezi kuendelea na masomo kwa kuwa hawawezi kupata HEARING AID kulingana na gharama zake? Na hivyo kushindwa kuonyesha vipaji vyao halisi kwa matumizi ya nchi na dunia?


ANAWAZA namna ambavyo mimi nawe tunaweza kuwa suluhisho la matatizo haya ambayo YANAUMIZA SANA. ..........


Hata hivyo hali hiyo haikumkatisha tamaa kwani alimudu kusoma katika shule mbalimbali za kawaida huku akitumia vifaa maalum vya kusikia, ambapo alimudu kufika hadi kidato cha sita. Binti huyu hakutaka kuendela na elimu ya juu, na badala yake aliamua kujiingiza katika biashara akiwa ni mjasiriamali mchanga lakini mwenye matarajio makubwa.


Si hivyo tu, bali pia amekuwa ni mwelimishaji katika tasnia ya Blog akiwa anamiliki Blog yake ambayo imekuwa ikiibua mijadala mbalimbali yenye kufurahisha, kuhuzunisha, kuelimisha na ujinga kidogo, lakini pia pamoja na yote anaamini kuwa blog hiyo imeleta changamoto na migongano ya mawazo, jambo lililowa “amsha” wengi na ndio maana akaiita VUKANI.


Hata hivyo hawezi kujivunia hapo aliopofikia katika tasnia ya Blog bila kuwataja wanablog wote wenye kumiliki blog za kiswahili, wasomaji wa blog, wazazi wake, marafiki na wale ambao kwa njia moja ama nyingine walifanikisha uwepo wa blog hiyo ya VUKANI. Hata hivyo HASITI kuwataja Kaka Markus Mpangala, kaka Mubelwa Bandio, na Dada Yasinta Ngonyani, hawa amekuwa akiwasumbua sana pale anapohitaji ushauri kabla ya kuweka bandiko katika kibaraza chake.


Asingependa kuwasahau Mzee wa Mataranyirato Chacha o'Wambura, Ngw'anambiti, Kamala Lutatinisibwa, Fadhy Mtanga, Christian Bwaya, Simon Mkodo Kitururu, Godwin Meghji, Evarist Chahali, Dada Subi, Faith Sabrina Hilary, Shaban Kaluse, Mwanamke wa Shoka Mija Sayi, Mariam Yazawa, Emuthree, Ramadhan Msangi, Salehe Msanda, Ma-Annonymacy............. na wengineo wengi, ambao kwa kweli wamekuwa mstari wa mbele katika kuifanya blog hiyo ya VUKANI kufikia hapo ilipo


WAKATABAHU


NI MIMI KOERO JAPHETI MKUNDI

23 comments:

Ramson said...

Mh… nimeshusha pumzi, kwa kweli hujafa hujaumbika.

Nimesoma habari hii lakini nilikuwa natamani hitimisho litutie faraja kuwa umeshapona, lakini nikajikuta nikijisemea moyoni……..”ohh …..noooo!!!” kumbe haikuwa vile nilivyotarajia!


Naomba nikupongeze kwa uandishi huu mahiri na kuwa muwazi, mwanzoni wakati naanza kuisoma habari hii, nilidhani inamuhusu mtu mwingine, kumbe muhusika mwenyewe ndiye msimuliaji! Ni uandishi wenye kuleta tafakuri kwa kweli.

Simulizi yako inahuzunisha, inasisimua, na inaelimisha kwa kiasi kikubwa, na kama habari hii ataisoma yule aliyesababisha, tatizo ulilo nalo, (kama bado yuko hai maana miaka 21 si haba) ni dhahiri hata yeye habari hii itamgusa na haiyumkini akakutafuta na kukuomba radhi, kutokana na madhila aliyokusababishia.


Kama ingekuwa ni mimi (Yaani msimulizi wa habari hii), labda hitimisho langu, lingekuwa ni kumsamehe yule muuguzi aliyenisababishia kadhia hii.

Hiyo yote ni kutaka kumuonesha kuwa sina kinyongo naye, na pia ingekuwa ni ujumbe muhimu kwake kuwa sikusimulia habari hii kama kumtupia lawama kwa kile alichokifanya miaka 21 iliyopita, bali nilitaka kutoa tahadhari kwa Madaktari na Wauguzi kuwa makini sana pale wanapowahudumia wagonjwa kwa kuwa afya ya mwanaadamu sio karakana ya kufanyia majaribio.
Kwa mara nyingine, nakupongeza kwa simulizi hii ambayo naamini itawaelimisha wengi na kuwafunua wengi. Na ninamuomba Mwenye enzi Mungu akupe uponyaji, na Inshaallah utapona na kurejea katika hali yako ya kawaida.


Nakupa pole dada yangu Koero, na ninakutakia kila la kheri kwa kila ufanyalo, Mungu akutie nguvu uendelee kutuhabarisha kupitia kibaraza hiki cha VUKANI.

Yasinta Ngonyani said...

Koero mdogo wangu kwanza kabisa napenda kusema HONGERA SANA KWA SIKU YA KUZALIWA KWAKO.HII NI SIKU MUHIMU SANA KATIKA MAISHA YAKO.HONGERA MDOGO WANGU WA HIARI.
Pili napenda kukusifu sana kwa kuwa muwazi na kutupa wengi habari kama hii ambayo si nzuri, umeiandika kwa ustadi sana. Mwenyezi Mungu na azidi kukupa nguvu na pia ayasikie maombi yetu kwako.
Akubariki pia kwa kila utakalo lifanya uwe na mafanikio katika maisha yako.
Sina budi kusema NAJIVUNA SANA KUWA NA MDOGO WA HIARI kama wewe Koero Mkundi. PAMOJA DAIMA na kumbuka UNAPENDWA SANA.
hONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA.

EDNA said...

Hongera sana mdada kwa kuongeza miaka.Mungu na akulinde ili uweze kuishi miaka mingi.HAPPY BIRTHDAY KOERO

Mija Shija Sayi said...

Happy Birthday Koero mwanamke wa shoka. Napenda kukpa hongera kwa jinsi unavyojua kukabiliana na matatizo, maelezo yako yamenipa picha kwamba wewe si mtu wa kulialia kirahisi unapopatwa na matatizo bali ni mtu wa kukabiliana nayo.

Hongera sana na Happy Birthday tena. Mungu akubariki wewe na wazazi wako.

Unknown said...

Imenigusa kwa kweli, lakini hatuna haja ya kusikitika kwa tukio hilo la miaka 21 iliyopita, huo tayari ni mzoga.
Kikubwa zaidi ni kusherehekea siku hii muhimu kwako ya kuzaliwa.

Hilo kwetu ndio lenye tija kwa sasa. lakini hata hivyo kumbukumbu hii imetufundisha mambo mengi sana hususan kwa wataalamu wetu wa tiba, yaani Madaktari na Wauguzi.

Ingawa wapo wanaofanya kazi yao kwa uadilifu, lakini naomba nikiri kuwa watu wenye taaluma hizo wanalalamikiwa sana katika jamii kiasi kwamba sifa hizo mbaya zinafunika sifa nzuri za wale waadilifu. Binafsi napingana sana na methali isemayo "Samaki mmoja akioza, basi wote wameoza" Napingana na methali hiyo kwa kuwa inatumika kuwahukumu waliomo na wasiokuwemo, hivyo basi nisingependa kuwahukumu Wauguzi au Madaktari wetu hawa kwa ujumla wao, kwani majaaliwa ya Afya zetu ziko mikononi mwao na nitakuwa siwatendei haki.

Nakupongeza kwa kutuwekea ushuhuda huu na ninakutakia Birthday njema. Mungu akubariki kwa kila ufanyalo.

MARKUS MPANGALA said...

Ni asubuhi na mapema, baada ya kujiweka sawa kwa kutoa jasho kidogo naamua kukaa kwenye kompyuta.
Huku nikiwa bado nahema kutokana na na kuweka afya vema ili kuanza siku. Baada ya hapo najipa dakika ya kuipa upendeleo blog ya VUKANI kwasababu nilijua ndiyo siku ya Koero Binti Mkundi kuzaliwa, nilitaka kuona ametuletea tunu gani.
Hata hivyo nilichokiona baada ya kusoma nilibaki na simanzi. Uvumilivu ukanishinda machozi yakanilenga, mwili ukasawajika. Harara ya kuwasiliana na wadau wa VUKANI ikaanza.
Na kwakuwa nilikuwa kasi mno kuwahi majukumu, nikamuomba kaka Kaluse yapata saa moja hiyo asubuhi asome Blog ya VUKANI.
Nikamweleza na mtani wangu Fadhy, asome VUKANI. Nilipokuwa naandika maoni, ghafla Waziri Ngeleja na Tanesco wakachukua umeme wao, ikabidi nisubiri mgawo.
Nikiwa naelekea kwenye majukumu, yapata saa mbili na dakika 29 asubuhi mtani wangu Fadhy alinijulisha atasoma VUKANI aone kuna nini.
Lakini nikamwomba anipe mawasiliano ya ya simu binti Mkundi kwakuwa namba niliyonayo kwa kweli inaninyima raha, simpati Koero.
Mtani wangu Fadhy akasema hana. Yapata saa 6 na dakika 10 mchana, Kaka Kaluse ananijulisha, “Nimesoma kaka. Imenigusa sana”.
Hakika Koero alinigusa hata mimi sio Kaluse peke yake, na Mtani wangu Fadhy. Nilijua Dada yangu kipenzi Yasinta atasoma mapema tu.
>>>
Koero u mzima,
Tatizo hakuna,
Ni shida ndogo,
Wala isikupe kihoro,
Mwaka 2009 mimi,
Mshituko nilipata,
Daktari akasema,
Markus dar haikufai,
Hukuugua masikio,
Leo yamekusibu,
Kubali hilo,
Nikasema si tatizo,
Bali uwezo umepungua,
Wala sihitaji kifaa,
Kwani naweza kuwasiliana vema,
Ila kuna wakati yanauma,
Yanapunguza uwezo kusikia,
Kama homa ya vipindi,
Nimeshazoea mimi.
Koero ijali afya,
najua umekubali hali,
Hadi leo umetuambia,
Imenigusa mno,
Imewagusa wengi hapa.
Mzee wa Lundunyasa anasema,
Koero tuko pamoja kwa shida na raha.
Tena umekuwa sehemu ya furaha ya wanablog,
Hongera mzee Mkundi
Kutuletea binti Mjuzi,
Mwenye vipaji pomoni.

Mwanasosholojia said...

HONGERA SANA KWA KUMBUKUMBU HII MUHIMU KOERO! Sio siri, sikujua yote haya hadi muda mfupi uliopita baada ya kusoma ujumbe wako. Mimi ni mmoja wa wafuasi wa VUKANI, na hata kama kuna kipindi sichangii, huwa takribani kila siku lazima nipite hapa ili kujua kuna lipi jipya. Ni moja ya Blogs nizipendazo. Leo ndiyo nimetambua upande mwingine wa maisha yako KOERO. Kama walivyotangulia kusema wengine, endelea na ujasiri wako na nasisitiza, wewe ni jasiri na mwenye vipaji lukuki ulivyokirimiwa na Mungu, endelea kuvitumia KOERO na jina lako litabaki kuwa lulu siku zote! Nakutakia maisha mema na yenye nmafanikio.

Goodman Manyanya Phiri said...

Ni furaha tupu! Na tele!

Mimi kama mzee nakuona mtoto. Lakini mabinti wenye umri wa miaka kumi na nane wakuona Dada.

Huo ndio utamu wa maisha.

Nakutakia afya nzuri, Koero; ukue na utupate sisi wazee (kama tukilaza damu lakini na sidhani!!!)

Simon Kitururu said...

Hongera Koero kwa siku ya KUZALIWA!

Pole na yalolkukuta katika safari ya ukuaji na MUNGU akuzidishie KHERI Maishani!

chib said...

Kwanza hongera sana kwa kuvuka ukurasa wa miaka.
Pili, pole kwa masahibu ya kupungukiwa na uwezo wa kusikia kutokana na juhudi za tiba zikiwa zimechanganywa na bangi!
Nina imani uwezo wa kusikia umepungua na sio kutoweka kabisa, hicho kidogo kilichobakia tunamshukuru mwenye heri anayetupa uzima.
Kwa simulizi hili, limenipa picha fulani na kujibu maswali kadhaa niliyokuwa nayo, nakutakia kila la heri na mafanikio katika shughuli zako.

Mzee wa Changamoto said...

Dearest DADA
"YOU'RE WHO YOU ARE BECAUSE OF YOUR PAST AND FOR YOUR FUTURE"

I GIVE THANKS AND PRAISES to the ALMIGHTY for who you are and what you do to spread HIS GLORY in you."

HAPPY EARTHDAY
Love you plenty

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Happy birthday Da Koero!


Yalotokea ni kwa ajili ya kukuwezesha kusonga mbele! Songa mbele..hakuna kurudi nyuma!

Rachel Siwa said...

Mmmhhh Mdogo wangu pole sana kwa yaliyokukuta,Mungu ni mwema na hakuachi hata siku moja,yani nimesoma na nimejifunza sana kupitia wewe dada Koero binti wa Mkindi.

Hongera kwa kuongeza mwaka mwingine na Mungu akubariki katika yote.

Christian Bwaya said...

Koero,

Simulizi hili linagusa. Pole sana kwa uliyokutana nayo. Ndivyo maisha yalivyo. Tunakuwa tulivyo, kwa mchango wa vingi. Ni habari njema kuwa maisha yanaendelea.

Nakutakia furaha tele, afya njema, miaka mingi zaidi, hekima zaidi na kila aina ya hatua njema mbele kufikia kule unakotamani kufika.

Mungu-Mwenyezi akubariki sana!

mama Jeremiah said...

Hongera kwa kukumbuka siku yako ya kuzaliwa. Napenda kukupa pongezi nyingi kwa miaka uliyofikia na ninakutakia mafanikio mema kwenye mipango yako ya baadaaye.
Asante kwa kutushirikisha historia fupi ya maisha yako. Nimesikitika, lakini zaidi sana nimefarijika. Umenifundisha kitu kikubwa sana maishani mwangu!. Kuwa na bidii wakati wote. Tusiwe wa kukata tamaa. Mapungufu tuliyo nayo yawe chachu ya kutaka kuendelea zaidi, kufanya mengi zaidi, kujifunza zaidi.

Ubarikiwe sana dada mpendwa.

Asante tena kwa kutushirikisha historia ya maish yako

emu-three said...

Hongera sana dada Kaole, kwa siku yako ya kuzaliwa, NA JAMBO LA KUMSHUKURU MUNGU KWA KUFIKIA UMRI HUO. Na pili nakupa pole kwa mtihani huo ulikupata yote ni majaliwa ya Muumba.
Kuna jamaa mmoja alifika hospitali akiwa kalemaa mguu, alikuwa kila siku analaani, siku hiyo alipofika hospitalini wakatii anasubiri zamu yake, akamkuta jamaa anaingia akiwa anatembea kwa mikono, hana miguu kabisa.
Unajua alifanya nini, alitoka pale kwenye kiti na kusema docta nimepona!
Kwanini nimenena hili, ni kuwa kila jambo hutokea ili iwe sababu, ili likujaze imani, ili likupe kipaji fulani ambacho huenda ungekuwa huna hilo tatizo usingeliweza kulifanya, ungelizarau! Yote ni maisha na yote ni majaliwa ya muumba!
Pole sana kwa hilo, na nakupa heko kwa kuwa muwazi, pili kuwa rafiki kwa kila mtu.
Sina zaidi TUPO PAMOJA DADA YETU MPENDWA!

Anonymous said...

Hongera sana kwa kuwa muwazi, hadithi yako mwanzo nimefikiri ni hadithi ya kufikirika lakini nami ni kitu kilichonipata 22 yrs ago, nikiwa na darasa la sita. ni magumu mengi nimepitia namshukuru Mungu kwa kunipa uhai na baraka zote alizonijalia japo cjafanikiwa sana kama ambavyo naamini naweza kufanikiwa bado nikiangalia wengi wenye tatizo kama langu naona nimebarikiwa wengi maisha yao yameathirika kutokana na kukosa jamii iliyowakubali wengi hawakupata elimu

Anonymous said...

Hello nimeona blog yako nakusoma hii habari. Pole kwa yaliyokukuta lakini ningekuambia kama nikumsamehe huyo DR basi umsamehe kwa vile mimi ninakwambia inaweza kuwa wala sio hiyo sindano aliyokudunga kama tunavyofikiriaga nyumbani. Ndio kuna dawa zinafanya masikio yasisikie lakini chanzo kikuu kwa waoto ni high fever. Kama homa ilikua juu sana basi hata hiyo sindano usingechomwa inawezakana the coutcomes could be the same.
Rafiki yangu mwanae ana miaka minne na yeye alipata infection siku moja akiwa na miaka miwili. Kukimbiza hospital cha kwanza alipewa fever reducer, drops, the whole works...Alipewa matibabu yote haraka haraka na alilazwa kama week lakini kwa yote hayo the damage was already done.
Dr wakamwambia kuna chance ataweza kuregain lakini mpaka leo huyu mtoto hasikii sauti kubwa sana au ndogo sana hivyo anatumia hearing aids..Na cha kusikitisha huyu mtoto alikua ndio anaanza kujiufunza kuongea. Hivo sasa hivi wanamfanyia maspeech therapy kibao lakini bado kwa umri wake bado yupo nyuma sana.

Inasikitisha lakini yote ni mipango ya Mungu and what doesn't kill you make you stronger...
Tushukuru Mungu kwa kila jambo...

Unknown said...

pole sana mungu yuko nawe.

Pelangsing cepat said...

I like it this really good information.
I visited several web pages however the audio quality
for audio songs existing at this website is truly fabulous.

Vimax Asli Canada said...

I like it this blog information, thanks for sharing

Obat Kuat Asli said...

I like it this blog information, thanks for sharing

poker said...

PROMO DELIMA
poker online | Agen Domino | Agen Poker|Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | bandar qiu | Judi online terpercaya

Bonus yang kami sediakan :
* TO (Turn over) sebesar 0.3% yang akan di kami bagikan setiap hari senin
* Bonus referal sebesar 10%

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat.
Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: Facebook
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___http://www.delimapoker.com/?ref=19860605