Tuesday, December 30, 2008

HIVI KWA NINI TANGU MWAKA 1947 HADI LEO MGOGORO HUU HAUISHI?

Juzi wakati naangalia taarifa ya habari kwenye Luninga nilikutana na habari inayohusu mashambulizi ya anga yanayofanywa na na Israel katika ukanda wa Gaza ambao unamilikiwa na kundi la Kipalestina la Hamas.

Mpaka wakati huo naangalia taarifa ya habari kuliripotiwa kuwa mashambulizi hayo yaliyorindima kwa takriban masaa 24 yamesababaisha vifo vya Wapalestina wapatao 271, huku Israel ikiwa imepoteza askari wake mmoja tu! Kwa kuwa mashambulizi hayo bado yalikuwa yanaendelea sijui ni roho za watu wangapi zisizo na hatia zitakuwa zimepotea.

Hata hivyo Israel imejitetea kwamba imefanya mashambulizi hayo kwa nia ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Hamas.

Wakati huo huo Umoja wa mataifa ulikemea mashambulizi hayo na kuitaka Israel kukomesha mashambulizi hayo mara moja.

Wakati nikiwa sekondari mwalimu wetu wa somo la Historia aliwahi kutufundisha kwamba kabla ya mwaka 1800 hakukuwa na taifa linaloitwa Israel.
Nakumbuka kwamba topiki hiyo sikuipa uzito unaostahili wakati ule, nadhani ilitokana na sijui utoto au kutokuchukulia mambo kwa uzito unaostahili.

Siku hizi nimekuwa ni mdadisi sana, kwa hiyo natumia muda mwingi kwenye maktaba ya baba nikipekua pekua ili kupanua wigo wa uelewa wangu.

Hata baba yangu huwa ananishangaa kwani tabia hii niliyoianzisha sikuwa nayo hapo kabla, lakini nadhani imetokana na kukua na kupambazukiwa, kwani ukishafika ngazi fulani ya elimu unakutana na nadharia nyingi za watu waliokufa ambazo nyingine hazikupata kuhojiwa wala kuchunguzwa.

Hebu ngoja niachane na hilo nisije nikakuchosha wewe msomaji wa blog yangu hii isiyokosa vituko kila uchao.

Basi baada ya kuangalia taarifa hiyo ya habari niliingia katika maktaba ya baba kutafuta kitabu chochote cha kujisomea, katika pekua pekua yangu nikakutana na kijitabu kilichoandikwa historia ya Israel, kwa bahati mbaya kijitabu hicho hakina hata jalada lake la juu hivyo msije mkaniuliza kinaitwaje.

Kutokana na kile nilichokiona kwenye taarifa ya habari muda mfupi uliopita nilivutiwa kukisoma kile kitabu.

Kumbe kwenye miaka ya 1800 ndipo kulipozuka swali la ni kwa namna gani wayahudi wataepuka kuuwawa kwa sababu ya chuki kule Ulaya?
Kwani wakati huo wayahudi hawakuwa na makazi, isipokuwa walikuwa wakitangatanga kule Ulaya.

Basi yale maandiko ya Biblia ya nchi ya ahadi, yakageuka harakati za kisiasa ya kutafuta makazi ya kudumu kule Mashariki ya Kati, kwenye eneo ambalo lilikuwa likikaliwa na wapalestina.

Kutokea mwaka 1920 hadi mwaka 1947, himaya ya Waingereza ndiyo iliyokuwa na mamlaka na Palestina. Wakati huo Palestina ilikuwa ni eneo lote la Israel ya sasa na maeneo yote yanayokaliwa kimabavu hivi leo na Israel. Maeneo hayo ni Gaza na Kingo za Magharibi.

Ongezeko la Waisrael kwenye eneo ambalo wenyewe wanaamini ni nchi yao ya ahadi, kwa mujibu wa maandiko ya Biblia takatifu, kitabu kisichohojiwa ingawa kiliwahi kukosewa mara kadhaa katika kuchapishwa kwake, kulianza kujenga hofu na wasi wasi kwenye eneo hilo.

Kwa hiyo ukichunguza sana utagundua kwamba hawa wanafiki Waingereza wamehusika sana katika kujenga mashariki ya kati ya leo isiyoisha migogoro, kisirani na wendawazimu ambao binadamu wa karne ya 21 kuushudia ni jambo la aibu isiyo na mfano.

Kwa ujumla migogoro ya kijiografia na kisiasa iliyozikumba na nchi za mashariki ya kati imechangiwa kwa kiasi kikubwa na nchi za Ulaya pamoja na Marekani.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia, umoja wa mataifa ambao ndio kwanza ulikuwa umeundwa ukiwa na nchi chache changa, uliamua kwamba, Palestina igawanywe na kuwa mataifa mawili.

Katika mgawanyo huo wayahudi wachache walipewa eneo kubwa kuliko wenye nchi, yaani Wapalestina.

Katika mgawanyo huo Wayahudi walipata asilimia 57 ya eneo, huku Wapalestina wakiambulia asilimia 43. Na Mji wa Jerusalem uliwekwa chini ya umoja wa mataifa.

Marekani ndio iliyokuwa kinara wa mpango huo na iliutilia nguvu na kuushabikia sana, Rais wa wakati huo Harry Truman, ambaye ndiye aliyeruhusu matumizi ya kwanza ya bomu la Atomic lililopigwa Hiroshima na Nagasaki nchini Japan hapo mnamo tarehe 6 na 9 mwaka 1945, na kusababisha kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Rais huyu alionekana kuguswa na maisha ya ukimbizi ya Wayahudi na aliseam wazi kwamba Wayahudi kugaiwa eneo ambalo sio lao ilikuwa ndio muarobaini wa madhila waliyokuwa wakiyapata huko Ulaya.

Hata hivyo Rais huyo alipingwa sana na wasaidizi wake wa masuala ya kigeni kuhusu kuunga kwake mkono jambo hilo. Wasaidizi hao walikuwa wanaogopa kuharibu uhusiano kati ya Marekani na nchi za kiarabu na walihofia kwamba Urusi inaweza kuteka nchi za Kiarabu.

Labda niwakumbushe kwamba wakati ule Dunia iligawanywa kati ya Urusi (Ukomunisti) na Marekani (Ubepari)

Taifa la Israel lilitangazwa au kujitangaza rasmi hapo mnamo Mei 14, 1948, lakini mataifa ya Kiarabu yalipinga kugawanywa kwa Palestina na kukataa kulitambua taifa hilo la Israel.
Majeshi ya Iraq, Syria, Lebanon, Saudi Arabia, Yemen na Misri, Yaliishambulia Israel, lakini yalishindwa na Wamarekani.

Israel isingeweza kuyashinda majeshi hayo, kwani ilikuwa bado ni kanchi kachanga.

Wakati Waisrael wakiendelea kujiimarisha, Wapalestina walijikuta wakiwa ni wageni kwenye ardhi yao, na suala la Jerusalem kuwa mji wa Kimataifa, yaani kusimamiwa na umoja wa mataifa nalo likafa.

Mwaka huo huo wa 1948 Wapalestina walitimuliwa kutoka katika maeneo yao na kulazimishwa kuishi ukimbizini kwenye nchi za Jordan, Misri, Lebanon na nchi nyingine.
Inadaiwa kwamba, zaidi ya Wapalestina 750,000 wanishi ukimbizini.

Historia ya mgogoro huu ni ndefu na nikisema nisimulie yote kama nilivyosoma katika kijitabu hicho pamoja na mtandaoni vile vile, nitawachosha.

Lakini swali ninalojiuliza hapa, ni kwamba ina maana dunia hii imekosa wastaarabu kadhaa wanaoweza kumaliza mgogoro huo.

Jamani yaani kizazi na kizazi bado tunaendelea kushuhudia ujinga huu wa mgogoro usioisha!!!

Nadhani kuna haja ya Wapalestina na Waisrael yakiwemo Mataifa makubwa pamoja na umoja wa mataifa kuona haya na kuangalia mustakabali wa Taifa hilo.

Kwani damu imemwagika sana, He! tangu mwaka 1947!!!!

11 comments:

A Khudori Soleh said...

salam from khudori

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

tabia yako ya kudadisi cjui niite utu uzima! lakini itakupelekea kujua mengi. tafta chakula cha akili na baadaye chakula cha roho.

hawa waisrael na wapalestina mambo yao wanayajua wenyewe. nashanga kanisani huwa tunaimba nyimbo za ninatamani kwenda Yerusalemu, jiji lenye vita na umwagaji damu kuliko maelezo. harafu tunaambiwa wayahudi ni taifa teule la mungu! Mungu huyu anawateuaje wagonvi na waonevu wakati yeye ana upendo?

Mzee wa Changamoto said...

Dah!! Kwa mujibu wa rafiki yangu ambaye ni msomi na mwamini na ambaye nadhani alifanya utafiti wa huu mgogoro, ni kuwa kuna mkanganyiko mkubwa wa maamuzi ya kiimani na kiutawala. Yaani yatakiwayo na Umoja wa Mataifa si yale yaaminiwayo na Israeli. Sina hakika na hili na ntatumia msemo waliowahi kutuambia nikiwa nafanya kazi kwenye media house moja hapo home kuwa "no research, no right to say"
Naacha maana sijachunguza hivyo sina haki ya kusema

MARKUS MPANGALA said...

Sawa! mzee wa changamoto nimekuelewa, lakini jambo hili sidhani kama UN wamelaani maana huwezi kuilaani Israel kwa dhati bali wanaigiza tu yaani wanafiki. Mzozo wa mashariki ya kati nimekuwa nikisoma baadhi ya vitabu hadi nahisi kuchanganyikiwa. Mfano someni kitabu cha Teach yourself MIDDLE EAST(samahani nimesahau jina la mwandishi) mimi ninacho na natamka anayekihitaji nitamwazimisha au ukifika maktaba ya taifa angalieni katika shelfu za reference books kama unaingia mlango wa chumba cha watu wazima cha kujisomea. Lakini nasema tena anayetaka aseme tu nitmpatia asome.

KWA UFUPI
mzozo wa Israel ni kweli kama asemavyo dada Koero kwamba Israel haikuwapo hadi pale mwaka 1948 iliposimikwa rasmi. mzozo huo upo katika masuala ya JUDAISM, ISLAMIC,CHRISTIAN,........... jaza hapa nimesahau ya nne au nitarudi kesho kujijaza. Mambo hayo yamechangia kutofautiana kwa eneo hilo. jamani nitarejea kuna mambo nayachanganya samahani NITARUDI KWA AYA ZA MOTO kwani mpango wa ROADMAP wa Marekani ulikuwa unafiki tu. Nihitimishe hata kama nitaudi tena. MGOGORO WA ISRAEL NA PALESTINA AU MASHARIKI YA KATI UTAKWISHA TU MPAKA MAREKANI, UINGEREZA NA ISARAEL WATAKAPOTAKA.

Fita Lutonja said...

Kwahili ninaomba unisamehe dada yangu kwani baba yangu amesomea tiolojia hadi akafikia falsafa ambapo sasa hivi anafundisha katika chuo kikuu cha wheatonjimbo la texas nchini Marekani kwa hiyo nikichangia mada hii itasababisha ugomvi mkubwa kati yangu na baba yangu.

Kwa hii mada naomba munisamehe sana.

Koero Mkundi said...

Ahsanteni wote mliochangia mada hii, Kamala, Mpangala, na mzee wa changamoto.
Maoni yenu ndio msingi wa kuboresha blog hii.
Nawashukuru sana.

Fita nilichoandika mimi sijanukuu kutoka katika vitabu vitakatifu. ni maoni yangu binafsi kama nilivyoona kwa mtazamo wangu. siogopi kutofautiana kimtazamo au changamoto kutoka kwa mtu yeyote. Bwaya aliwahi kusema kwamba kutofautiana ndio kujifunza.

Karibu uwanjani mzee, na ulete changamoto zako hapa huna haja ya kuogopa, kwani hapa hatugombani bali tunarekebishana na kuelekezana.

Hii mada bado haijafungwa.

Evarist Chahali said...

Nadhani mgogoro huu una mtizamo wa kisiasa na kidini.Kwa kifupi sana,kisiasa lawama ziende kwa League of Nations na Waingereza,kwa kuwapora Wapalestina haki na ardhi yao na kusapoti makazi ya Wayahudi kutoka sehemu mbalimbali duniani.Kidini,eneo hilo ni nchi ya ahadi ya wana wa Israeli kwa mujibu wa maandiko matakatifu.Siasa na dini ni mchanganyiko hatari.

Heri ya mwaka mpya dada yetu.

Christian Bwaya said...

Kikristo waisrael waliamriwa na Mungu kuwaua Wapalestina wote kipindi kile wamerejea kutoka uhamishoni Misri. Yoshua alitakiwa kuongoza mauaji ya halaiki (Wenyeji,wapelestina) ili kutokomeza kizazi chao kuwaruhu wao kuichukua nchi hiyo. Bahati mbaya tunaambiwa, waisrael wenyewe kwa huruma zao waliwaacha baadhi yao. Mungu akaambia "hawa jamaa watawatesa maisha yenu yote!".

Kibiblia, mwenye haki ya kuua ni mwisrael na si mtu wa mataifa. Ila yeye akiua, hilo si kosa. Ni kuujenga ufalme wa Mungu. Huo ndio mtazamo wa kidini.

MARKUS MPANGALA said...

Bado nakuja dada Koero wala usitie shaka nipo nipo kwanza. hakika nitaweka maelezo marefu sana hapa. NITAKUJA TU MSIHOFU

Sophie B. said...

Blog yako nzuri inaelimisha. Keep it up!Kuhusu hili nakubaliana na Mzee wa changamoto kuwa "no research, no right to say" Harafu sikubaliani kabisa na comment ya Kaka Bwaya. Pia nafikiri watu tuwe makini kucomment kama haandiki backing facts maana inapelekea kupotosha ukweli. Kwa ufupi Israel ina haki ya kujitetea na kulinda usalama na maslahi ya watu wake. Ifanyeje mtu akisema hivi: soma http://news.bbc.co.uk/2/hi/middle_east/4378948.stm. Jamani tutafute first hand info kabla hatujacomment, namna hii tutakuwa tunaelimishana vizuri. Endeleza blog yako nzuri.Nawasilisha,
Mama wa M-Israel

sbobet online said...


agen poker
poker online
pagen poker terbaik
agen poker terpercaya
poker uang asli

sabung ayam
adu ayam
ngadu ayam
laga ayam
permainan adu ayam
ayam petarung
ayam sabung
ngadu ayam jago
adu ayam online
taruhan ayam
sabung ayam terbaik
judi online ayam
ayam sabung online
judi adu ayam
situs sabung online
judi sabung online
permainan laga ayam
sabung online
sbobet
agen sbo
agen sbobet
agen sbobet terbaik
agen sbobet terpercaya
sbobet asia
ibcbet
agen ibcbet
agen ibcbet terbaik
agen ibcbet terpercaya
ibcbet online
sbobet online