Wednesday, October 21, 2009

JAMANI HUU NI UTABIRI, UNAJIMU AU DHIHAKA?

Jamani mimi sio mpenzi au mshabiki wa mambo ya Nyota, kwangu mimi nachukulia kama huo ni ushirikina. Jana kuna mdau kanitumia huu utabiri au sijui niite unajimu, akinituhumu kuwa, kwa kuwa nimezaliwa mwezi wa Mei basi ninazo tabia hizi. Ukweli ni kwamba sina uhakika na hicho alichoandika, na siamini kabisa kama ninazo tabia hizo, ila waswahili wanasema Nyani haoni kundule. Kwa hiyo naomba wadau munisaidie kama unajimu huu unanihusu………….maana naona hii ni kaaaaaaaazi kweli kweli.

TABIA ZA WATU WALIOZALIWA MWEZI MEI…….HATA WEWE KOERO UMO

Mtu yeyote ambaye amezaliwa mwezi wa Mei mwaka wowote, anaweza kuwa na alama ya nyota ya Ng’ombe {Tauras} au Mapacha {Gemini}. Hapa sitazungumzia nyota moja moja, bali nitazungumzia mwezi ambao amezaliwa mtu. Kwa hiyo nitazungumzia waliozaliwa mwezi wa Mei ambapo wewe Koero ni mmoja wapo.

Watu waliozaliwa mwezi wa Mei ni wagumu, hawaambiliki wanapotaka kufanya jambo, wanapopania. Tunaweza kusema ni watu ving’ang’anizi. Lakini kwa bahati mbaya sana, kama wamempenda mtu, hakuna watu wanoporomoka kirahisi kama wao. Yaani kama wamempenda mtu wanashikwa kirahisi kuliko mtu mwingine yeyote.

Ni watu ambao wanaweza kuvumilia shida na suluba za maisha katika kiwango cha ajabu. Ni watu ambao wanamudu kuhimili misukosuko kimwili na kiakili, yaani hawachanganyikiwi kirahisikwenye misukosuko, hasa kama nia yao ya kung’ang’ania bado ipo.

Ni watu wenye uwezo mkubwa wa kumbukumbu. Kama ni uwezo wa kukariri masomo, basi ndiyo wenyewe. Lakini kwa bahati mbaya, wanapenda sana kujumuika na kujimwaga. Kwa hiyo wengi huwa hawafaidi matokeo ya vipaji vyao na wakati mwingine hata hivyo vipaji havionekani kwa sababu vinafungwa na kupenda kwao starehe.

Ni watu pia wanaofaa kwenye kazi kama zile za uhudumu katika ndege au hata mighahawani. Wana sifa ya kujua ladha ya chakula na wanamudu kutengeneza chakula kizuri sana nyumbani hata kama vifaa na fedha ni haba sana.

Ni watu ambao pia wana uwezo wa kuongoza kwenye mashirika au maeneo ya shughuli. Watu waliozaliwa Mei, inawezekana kwa nje wakaonekana kuwa na uwezo sana kuliko walionao kweli.

Hii ni kwa sababu wanajipenda sana, iwe kuvaa au hata kuwa na vitu vingine vya thamani vya nje. Mtu aliyezaliwa Mei anaweza kuwa na gari kubwa, lakini akiba ya shilingi elfu moja mfukoni hata nyumbani hana. Anaweza kuwa anavaa suti kila siku wakati hata godoro la kulalia hana.

Ni watu ambao wakipenda mtu wanakuwa kama vichaa, kwani watampa kila kitu. Kama nilivyosema, wanashikwa kabisa na kuwa kama mazuzu. Lakini wakimchukia mtu watapambana naye hadi waone kinaeleweka. Uzuri wao ni kwamba, wanapenda kukabiliana na mtu ana kwa ana, hawapendi mambo ya chini chini au njama. Wanapenda maisha ya wazi tu, hata kama ni ugomvi au uadui.

Watu waliozaliwa mwezi Mei iwe wanaume au wanawake hawatakiwi kuoa au kuolewa mapema. Hawatakiwi kufanya hivyo kwa sababu mara nyingi, kama sio zote ndoa zao za kwanza huwa wanakuwa wamekosea kuchagua. Labda ni kwa sababu wakishapenda wankuwa ni vipofu halisi. Ni watu ambao wanatakiwa wakitaka kutafakari na kuamua jambo wake wenyewe na kutafakari kimya. Hii ni kwa sababu wakiwa katika watu wengi, wantokea kuwaamini watu hao wengi na kuchukulia mawazo ya hao wengi kama yao. Ni watu ambao huchanganywa na kudanganywa kirahisi. Ni watu ambao wanapoingia kwenye hisia au upendo, hawana tena uwezo wa kufikiri vizuri.

Ni watu wenye wivu sana na mara nyingi wivu wao wa kimapenzi huwafanya kuleta vurugu au kusababisha machafuko ya wazi ya kiuhusiano. Lakini siku zote, baada ya vurugu hizo huhisi kushitakiwa na dhamira. Hujutia tabia zao za wivu lakini hawana uwezo wa kuzidhibiti kama wanavyoamini wao.

Kwenye uhusiano ukiacha wivu, ni waaminifu na wanyeyekevu kwa wapenzi wao. Wanafaa sana kuwa maafisa serikalini. Wauguzi na hata kufanya kazi za bustanini. Ni watu wazuti katika mashairi, muziki na sanaa kwa ujumla.

Kiafya ni watu wanaougua kirahisi maradhi yenye kuathiri koo, pua na mapafu pia. Kwa hiyo wantakiwa kuwa makini sana na mazingira ambayo yanaweza kudhuru koo, pua au mapafu yao. Vitu kama sigara, haviwafai watu waliozaliwa Mei

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nanukuu "Ni watu ambao wakipenda mtu wanakuwa kama vichaa, kwani watampa kila kitu. Kama nilivyosema, wanashikwa kabisa na kuwa kama mazuzu. Lakini wakimchukia mtu watapambana naye hadi waone kinaeleweka. Uzuri wao ni kwamba, wanapenda kukabiliana na mtu ana kwa ana, hawapendi mambo ya chini chini au njama. Wanapenda maisha ya wazi tu, hata kama ni ugomvi au uadui."mwisho wa kunukuu. Kaaaazi kwelikweli, Kusema kweli binafsi huwa sifuatilii sana mambo kama haya kwa hiyo sina jina kama ni tabia zako.

Mzee wa Changamoto said...

Hiki kama kioo fulani kumuonesha Koero.
Kaazi kwelikweli

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

koeroz na ndo maana anawachukia wanaume. alimpenda mmoja akampagawisha na kumtelekeza akaendelea kuwa kichaa wa kuchukia wanaume!!!

Sorrrrrrrrry

MARKUS MPANGALA said...

Watu wa mwezi mei????? duh! halafu kaka mzee wa Changamoto nakuunga mkono haswaaaa umetazama zaidi ya kilichoandikwa...... hivi ndivyo nipendeleavyo.

YASINTA: acha hizo tafadhali kuwa adabu dadangu LoL......

KAMALA: si unajua kuna kujamba kakangu? Je kujamba ni uchafu? au ajambaye anataka kwenda chooni???? LAKINI kama ni uchafu mbona tunaubeba kila mawio na machweo??? nakufikirisha tu kaka usiwaze sana.

Kwangu sijui kitu labda nina kitu, nimezaliwa mei 15, lakini hilo la starehe,mahaba, kudanganyika THUBUTU lakini inawezekana kama vile ipo kwasababu watu wapo?

Mheshimiwa mwenyekiti dada Koero, huyu aliyekuandikia anakufahamu, pengine hakumaanisha wewe hata kama ulitumiwa wewe! sijui naeleweka hapo, na labda KAMALA anaweza kurudi na kufafanua KIUTAMBUZI...... lakini kwangu ngoja niseme kikoloni kidogo au vipi......ONE ON TIME OF KOERO JAPHET MKUNDI au ONCE UPON A TIME........ ndiyo simulizi imejikita hapo.

UNAJIMU SIYO? tunasadiki ama?

MARKUS MPANGALA said...

Mheshimiwa mwenyekiti Koero, nimerudi kwasasbabu maalumu. Nayo ni kuguswa kwangu na simulizi ya SAID WA MBEKENYELA. Najua nimetoka nje ya mda hapa ila nimkwisha kuchangia.

NAOMBA ILE SIMULIZI YA SAIDI MAKONDOMU ituwajie hapa dadangu utanikuna sana kwa hilo maana ni tamu. tafadhali msomaji wako naiomba hiyooooooo usisahau