Nathubutu kukubaliana na mtaalamu wa sayansi ya siasa Harold Laswell katika taaluma hiyo. Mwanazuoni huyu alikwisha kusema maana halisi ya siasa na wanasiasa, kwamba ‘Politics is the Art of Possible”. Pale ambapo mwanasiasa anatarajiwa kutenda jambo fulani, hatendi lakini asipotarajiwa hutenda. Na hili limekuwa zuri kwa wanasiasa hata Harold Laswell akawachambua katika maana nzima ya siasa.
Karl Marx naye hakubaki nyuma, alishaeleza kuwa siasa na wanasiasa kuwa ni watu wanaofanya mambo kwa matakwa yao,mahitaji yao kwa faida zao. Tunaweza kuwa na maoni tofauti lakini msingi wetu ni kuchambua jambo lilelile.
Kwa msingi huo, leo naomba niwe mtabiri wa kile kitakachotokea katika uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba 25 mwaka huu. Hivi karibuni tumeshuhudia chama kipya cha siasa kinachoitwa Chama cha Jamii (CCJ) kimepewa usajili wa muda, wengi wamekihusisha chama hicho na Vigogo wa kupiga vita ufisadi ndani ya chama tawala yaani CCM almaarufu ‘Mitume 12’. Inaelezwa kuwa ‘mitume hawa 12’ ndiyo waanzilishi wa chama hicho.
Yamesemwa mengi na kukifanya chama hicho kuwa gumzo katika medani za kisiasa. Ni aghalabu ikapita siku pasipo vyombo vyetu vya habari hususan magazeti kuandika juu ya CCJ. CCM nacho katika nyakati tofauti viongozi waandamizi wakiongozwa na katibu wake mwenezi Kapteni mstaafu John Chiligati na Katibu wake mkuu Luteni Yusuph Makamba ambao awali walionekana kukibeza chama hicho, lakini sasa inaelekea kuwatikisa.
Jana katibu mwenezi Kapteni mstaafu John Chiligati, amesambaza waraka kwa wana- CCM nchi nzima kuwatahadharisha kujiepusha na chama hicho, vinginevyo wataharibikiwa.
Hiyo ni ishara tosha kuwa joto la CCJ limeanza kuitikisa na kuitekenya CCM.
Nirejee kwenye utabiri wangu, nionacho ni kwamba, tumeshuhudia Makundi ndani ya CCM, ambayo yamesababishwa na vita ya ufisadi ambayo ilianzishwa na Chadema. Lakini bila soni baadhi ya wabunge wa CCM wakaiteka nyara na kuigeuza mtaji wao wa kisiasa. Wakajivika jina la ‘mitume 12 wa kupambana na ufisadi’, huku wakishindwa kuitoa orodha ya mafisadi hao kama ilivyofanywa na Dk Wilbroad Slaa pale Mwembe Yanga, ambaye anastahili pongezi kwa ujasiri wake.
Ni busara za wazee hasa rais mstaafu wa awamu ya pili Mzee Ali Hassani Mwinyi na Rais mwenyewe Jakaya Mrisho Kikwete, ndizo zikaweza kumnusuru na rungu la mafisadi, vinginevyo hatma ya Spika wa bunge ingekuwa mashakani.
Hawa ndio ambao watakuwa na maamuzi ya kupitisha majina ya wabunge watakaogombea ubunge kupitia CCM, hata baada ya kupita katika kura za maoni, kamati kuu ya CCM chini ya mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete inayo maamuzi ya kupitisha majina ya walioshinda katika kura za maoni katika kinyang’anyiro cha kugombea ubunge kupitia CCM.
Hapa ndipo penye hekima na akili, hapo ndipo kwenye mashaka makubwa kwani mwanachama anaweza kushinda katika kura za maoni lakini jina lake likaondolewa katika kikao hicho pale ambapo wajumbe wasiporidhishwa na jina la mgombea aliyeshinda. Hapo inategemea zaidi maoni ya wajumbe wa kamati kuu ya chama. Hili ndilo alilofanyiwa Dk Slaa aliyeamua kujiunga Chadema au hata Stephen Wassira(kabla hajarejea CCM), wawili hawa walikumbana na ‘mkono wa kamati kuu’.
Ikumbukwe kuwa kuna wabunge ndani ya CCM ambao wameisumbua sana serikali hasa katika sakata la kashfa ya kampuni ya Richmond, ambayo hata hivyo mpaka sasa maamuzi yaliyofikiwa na kushauriwa na kamati ya bunge, bado hayajatekelezwa na serikali imeendeleza ngonjera na kupiga danadana.
Ngonjera hizo ndizo zinazowafanya baadhi ya waandamizi washindwe kumwelewa mwenyekiti wao, licha ya kuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri(kwa maana alijua zabuni hiyo na kuidhinisha), lakini amekuwa kimya huku taarifa za kiserikali kwa mujibu wa waziri wa nishati na madini, William Ngeleja zikisema watuhumiwa wameonywa tu.
Kelele za wabunge wa CCM hususan wale vinara wa vita vya ufisadi kukikana chama hicho hadharani ni kauli za kisiasa tu katika kuweka mambo yao sawa ndani ya CCM. Nani anayeweza kuukata mkono wake unaomlisha?, ni vigumu kukiri hadharani kukiunga mkono chama fulani ukiwa ndani ya CCM. Hilo ameweza kufanya mbunge wa Kigoma kwa tiketi ya Chadema Mheshimiwa Zito Kabwe peke yake ambaye siyo mnafiki.
Nina hakika hawa wabunge wa CCM wanaokikana chama cha CCJ leo hii, lakini wakienguliwa na kukimbilia katika chama hicho watasema wameombwa na wapiga kura wao hapo ndipo unapokutana na msemo wa ‘Politics is art of possible’. Ni nani asiyejua kuwa wanasiasa ni watu wasiotabirika, wanaweza kuahidi kujenga daraja mahali pasipo na mto, wanaweza kudondosha machozi kana kwamba wanauchungu, lakini wakipewa kura hutimka na hapo kuonekana ni mwaka wa uchaguzi.
Mwanasiasa anaweza kukuonesha bakuli akakwambia ni bilauri, mkabishana kweli kweli lakini ukimthibitishia kwa kutumia hata mashahidi atakwambia kuwa ni kweli ulikuwa sahihi kuwa ile ni bakuli, lakini kama ukikosa bilauri unaweza kuitumia bakuli hiyo kama bilauri. Naomba nimalizie kwa kusema kuwa Mwaka huu tutashuhudia matukio mengi ya kushangaza na haya ni majilio tu.