Monday, January 11, 2010

ILIKUWA NI SAFARI ILIYOJAA VITUKO

Ni mara yangu ya kwanza kusafiri kwa ndege kwenda nchi ya mbali, kwani nchi ambayo niliwahi kwenda kwa ndege ni Afrika ya Kusini tu. Ni safari ya ghafla mno ambayo sikuitarajia. Niliondoka jijini Dar mida ya saa nne usiku na ndege ya KLM, hadi Amsterdam, pale niliunganisha ndege nyingine hadi Stockholm Sweden katika uwanja wa ndege wa Arlanda. Hali ya hewa hapa ni ya baridi kweli na ingawa nilibeba makoti mazito ya baridi lakini nilihisi baridi ikipenya katika maungo yangu barabara.

Nilichukua taxi hadi kwenye Hoteli ambayo baba yangu alinifanyia booking. Safari yenyewe ilikuwa haijafika ukingoni kwani nilitakiwa kesho yake nisafiri kwa treni kwenda mji wa Uppsala ambapo ndipo chuo nilichotarajiwa kujiunga nacho kilipo.

Nililala pale na siku ya pili niliondoka na taxi hadi kituo cha treni ambapo kwa msaada wa dereva wa taxi nilikata tiketi yangu na kuingia kwenye treni. Ilituchukua takribani dakika arobaini na tano kufika katika huo mji, naambiwa kuwa kwa kawaida ni nusu saa tu, lakini kutokana na hali ya barafu iliyojaa katika njia ya reli ilibidi tutumie hizo dakika arobaini na tano.
Nilifika katika huo mji wa Uppsala na kuchukua taxi ambayo ilinipeleka hadi chuoni, na nilipoangalia saa yangu ilinionyesha kuwa ni saa sita za mchana, niliopokelewa na kupelekwa ofisini kwa mkuu wa chuo ambapo nilipata maelekezo yote ya pale chuoni kisha nikakabidhiwa kwa mama mmoja wa makamu ambaye nadhani ndiye msimamizi wa zile apartment pale chuoni, alinipeleka hadi kwenye chumba changu ambapo nilimkuta binti mwingine ambaye alijitambulisha kwangu kuwa ni raia wa Finland, tulisalimiana na akapewa maelekeza kuwa tutakuwa tukiishi pamoja katika chumba kile hadi tutakapomaliza masomo. Kusema kweli alinipokea kwa bashasha, na kutokana na kusikia sifa nyingi juu ya nchi yangu ya Tanzania pamoja na sifa za mlima Kilimanjaro, binti huyu alikuwa ana hamu ya kutaka kujua mengi juu ya mlima huo na pia mbuga zetu za wanyama.
Binti wa kizungu akaanza maswali yake akitaka kujua habari za mlima huo uko upande gani wa nchi yetu, una urefu gani, ukitaka kupanda itakuchukua muda wa siku ngapi, je mbuga za wanyama nazo, ziko ngapi, ukitaka kwenda utafikaje, na itakugharimu kiasi gani kulipia kiingilio ili mradi yalikuwa maswali lukuki.

He! wenzangu nikaona naumbuka sasa, nilichojibu ni upande ambapo mlima Kilimanjaro upo ambapo ni mashariki mwa nchi yetu yaani mkoani Kilimanjaro, mengine nilitoka kapa, na kuhusu mbuga za wanyama nilizungumzia tu mbuga ya Ngorongoro ambayo niliwahi kuitembelea mwaka jana mwanzoni, zaidi ya hapo maswali mengine nilimwahidi kumjibu wakati mwingine, kwani nilijifanya kuwa nimechoka na safari, lakini moyoni nilipanga nikipata muda niende ubalozini kwetu nikatafute zile taarifa ili kuepuka fedheha ugenini, maana hawa wazungu wanadhani kwa kuwa nimezaliwa Tanzania basi nafahamu kila kitu.

Kwa kuwa ilikuwa ni ijumaa hapakuwa na ratiba yoyote kwa sababu chuo ndio kilikuwa kikiendelea kupokeaa wanafunzi kutoka nchi mbalimbali. Niliamua kujipumzisha kidogo.Niliamka majira ya saa kumi jioni, nikaelekea katika café ya pale chuoni ili kupata kahawa kupunguza baridi, nilipofika pale café niliona call box, nikaona huo ndio wakati muafaka wa kumpigia dada yangu Yasinta simu ili kumjulisha kuwa niko Sweden kwa masomo.

Kwanza dadaYasinta hakuamini alidhani namtania, lakini baada ya kumweleza mahali nilipo yaani Uppsala aliniamini na aliniahidi kunifuata siku inayofuata yaani jumamosi ili anipeleka kwake. Dada Yasinta alifurahi sana na hata baada ya kuongea naye kwa simu nilipotoka pale nilirudi chumbani kwangu na kwa kuwa pale chumbani kwetu kuna computer room, niliingia hapo tukachat kwa takriban masaa matano, tulizungumza mengi na aliniambia kuwa familia yake imefurahia ujio wangu kwani hatimaye sasa watamuona Koero live.

Ni kweli siku iliyofuata majira ya saa nne, nilikuwa bado niko chumbani kwangu nikipitia makabrasha ya maelekezao ya namna ya kuishi pale chuoni pamoja na malezo mengine juu ya kozi yangu nitakayoichukua. Ghafla nikapigiwa simu na sekretari wa mkuu wa chuo kuwa nina wageni wako mapokezi.
Nilitoka haraka kwani nilijua tu kuwa huyo angekuwa ni dada Yasinta. Anitembeee nani hapa Sweden zaidi yake? Nilipokaribia mapokezi nilimuona dada Yasinta akiwa na mumewe na nyuso zao zilikuwa zimepambwa na tabasamu pana, walikuwa wamesimama mahsusi kunipokea na nilipowafikia dadaYasinta hakusubiri, alinirukia kwa furaha na kunibeba, na hivi nina kamwili kadogo , alinibeba utadhani mama aliyembeba mwanaye, kila mtu pale mapokezi alishangaa, lakini mumewe yaani baba Camilla alisema kitu kwa kiswidish, nadhani alikuwa akiwaeleza jambo kuhusu mimi.

Tulizungumza kwa kifupi na bila kupoteza muda niliomba fomu maalum ya kuomba ruhusa ya kutoka nje ya chuo na baada ya kuijaza fomu hiyo tuliondoka pale chuoni na gari walilokuja nalo wenyeji wangu. Njiani tulizungumza mambo mengi sana juu ya blog zetu, tuliwazungumzia wana blog wenzetu kina kaka Mubelwa, Kamala, Kitururu, Markus aka Mcharuko, Da’ Subi, Da Mija, Da Schola Mbipa, kaka Bwaya, Da’ My little world, Ka Godwin Meghji, na wengine weeeengi tu.
Ingawa safari ilikuwa ni ndefu kiasi, lakini niliiona fupi kutokana na mazungumzo. Tulipofika nyumbani nilipokelewa na Camilla na Erik kwa bashasha na walinifurahia sana. Nyumba yao ni nzuri ikiwa imezunghushiwa uzio mfupi hivi huku ikiwa imenakshiwa na maua ambayo yalikuwa yameanza kunyauka kutokana na barafu, tulipoingia ndani nilikutana na hali ya joto kutokana na hita zilizowashwa ili kupunguza baridi.
Dada Yasinta alitengeneza chai haraka haraka na tukajumuika pale mezani kupata chai huku tukiendelea na mazungumzo, pamoja na kwamba kuna dinning room lakini jiko la dada Yasinta ni kubwa kiasi kwamba kulikuna na meza kubwa na viti ambapo hutumika wakati mwingine kwa ajili ya kulia chakula pale pale jikoni.

Nililipenda sana jiko lao na mpangilio mzima wa nyumba yao. Tulizungumza sana na kutaniana na shemeji yangu huku dada Yasinta akiandaa chakula cha mchana.Dada Yasinta alinifahamisha kuwa jioni walikuwa na mpango wa kwenda kucheza mchezo wa kuteleza kwenye barafu, yaani skiing, waliniuliza kama nitaongozana nao, niliwakubaliana na walifurahi sana.

Jioni ilipofika tulifungasha mizigo yetu ambapo ilikuwa ni vifaa vya kutelezea katika barafu, kisha tukaondoka na gari hadi kwenye eneo linalotimika kwa mchezo huo, tulipofika tulikuta watu wengi sana wakicheza mchezo huo, Muafrika nilikuwa ni mimi na dada Yasinta pekee wengine walikuwa ni wazungu watupu. Tulivaa vifaa vyetu na kutokana na kuwa mgeni wa mchezo huo, Dada Yasinta alinielekeza namna ya kutumia vifaa hivyo , kisha tukaanza kuteleza.

Ingawa nilikuwa nikianguka mara kwa mara, lakini shemeji yangu Torbjorn alikuwa akinisaidia kuninyanyua na kuniekeleza namna ya kutumia vifaa hivyo, mpaka nikamudu. Nilikuwa nateleza kwa uhodari mpaka kila mtu akawa ananishangaa.

Nilikuwa nateleza kwa kasi sana, mara nikajikuta nikiwaacha wenzangu hatua kadhaa nyuma, mara ghafla nikajikuta nikielekea kwenye mteremko mkali, nilishindwa kujizuia, kumbe kulikuwa na kibao kilichokuwa kikitahadharisha kuwa mbele ya lile eneo kuna bonde na ilikuwa hairuhusiwi kuvuka pale, nilisikia watu wakipiga kelele nyuma yangu lakini nilishindwa kujizuia, nikajikuta naelekea bondeni , “ mama wee nakufaaaaaa” nilipiga kelele, lakini ghafla nilisikia mtu akiniita kwa sauti “Koero nini” Nilishtuka na kuamka, huku mapigo ya moyo yakinienda mbio na jasho likinitoka, nilimuona mama akiwa pembeni yangu.
Kumbe nilikuwa nimelala na ile ilikuwa ni ndoto tu. Mama alinijulisha kuwa nilikuwa nikipiga kelele mpaka wakaamka wakidhani labda nimevamiwa. Kwa kuwa huwa sifungi mlango wangu wa chumbani. ilikuwa ni rahisi kwake kuingia chumbani kwangu ili kuangalia kama nimepatwa na nini.

Nilipoangalia nje kulikuwa kumepambazuka, nilimuomba mama maji ya kunywa na na baada ya kunywa, nikamsimulia juu ya ile ndoto. Mama alicheka sana akanimbia kuwa ni kweli baba amenitafutia chuo nje ya nchi na si muda mrefu nitaondoka nchini kwenda kukariri ujinga wa wengine.

8 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Awesome. Just awesome
Blessings

Yasinta Ngonyani said...

Nimesoma hii habari mara tatu na naona kama nami naota ndoto na pia nakuona kama upo hapa karibu yangu. Na najua ndoto yako siku moja itatimia tu utakuja kukutana nami na itakuwa siku ya furahja sana. Koero mdogo wangu ama kweli wewe ni mwandishi mahiri. Karibu sana Sweden mdogo wangu.

Faith S Hilary said...

Hahahahahahahahaha jamaaaaaani!!!! Dada Koero please kitabu ooooooooooh! Hehehe yaani hii hadithi nimeipenda kweli, I just read it over and over again na still mwisho mwisho nacheka.

Godwin Habib Meghji said...

Kwa hili nimekuweka kwenye Kundi moja na wakina MUSIBA na BEN MTOBWA. umenikumbusha hadithi za kina WIlly Gamba na Joram Kiango. KIPAJI NA UWEZO UNAO. Vipi kama utatupatia kitabu. Imenikumbusha sana kitabu kimoja cha BEN nilisoma nikiwa shule ya msingi FEDHA ZAKO ZINANUKA. Nimeipenda na Ninafurahi kuwa utarudi shule

Mija Shija Sayi said...

Kuanzia leo nitakuwa nakuita Koero binti kipaji. Kipaji hiki usipokiendeleza ni lazima ujibu mashtaka.

Stay blessed binti kipaji.

Yasinta Ngonyani said...

Da mija hapo umenena maana kila siku mi namwambia haniamini huyo binti kipaji, jina nzuri sana naungana na Da Mija.

Mzee wa Changamoto said...

Tatizo Koero M'BISHIIIIIIIIIIIII
Hataki kukubali. Anasahau kuwa KUTOTUMIA KIPAJI ULICHOPEWA NI DHAMBI.
Shauri yake. Atajiju akikosa nafasi ya kwenda mbinguni kwa kuwa hakuandika kitabu.

Markus Mpangala. said...

@ NAKUNUKUU MZEE WA CHANGAMOTO
........."Tatizo Koero M'BISHIIIIIIIIIIIII
Hataki kukubali. Anasahau kuwa KUTOTUMIA KIPAJI ULICHOPEWA NI DHAMBI.
Shauri yake. Atajiju akikosa nafasi ya kwenda mbinguni kwa kuwa hakuandika kitabu"

naongeza @ TATIZO Koero a.k.a MAMA MATATIZO