Niliamua kurudi shamba na kuwa mkulima
Kwa kifupi sana ni hivi. Mwaka 1975 nikiwa mwalimu kijana bado, nilifanya jambo ambalo kwa wakati ule wala halikunisumbua ingawa lilikuwa baya sana.
Bila shaka, wale wanaokumbuka mfumo wa elimu wa wakati ule wanajua kuhusu wanafunzi waliokuwa wanaitwa maripita ambao walikuwa ni wale wanaoanguka mtihani wa darasa la saba shule fulani na kwenda kudurusu darasa hilo kwenye shule nyingine.
Serikali ilikuwa inakataa kabisa wanafunzi kukariri tena darasa la saba au la nyuma yake baada ya kuanguka mtihani. Nikiwa shuleni kule Mbeya mwanafunzi mmoja ambaye baba yake alikuwa na urafiki na mkuu wa shule niliyokuwa nafundisha alikuja kudurusu darasa.Siku alipokuwa anakuja kuripoti, nilikuwepo mimi ofisini kama mwalimu mkuu msaidizi.
Kijana huyo aliletwa na dada yake ambaye alikuwa anafanya kazi hospitali ya mkoa. Nilimpokea kijana yule nikijua kwamba anarudia shule.Baadaya kumpokea na kujua dada yake anapofanyia kazi, niliona nami ningepata. Kama mkuu wa shule alipata fedha kupitia Yule kijana kudurusu darasa, nilijua na mimi ningepata rushwa ya mwili.
Nilimwandikisha kijana huku nikisema kwamba, kudurusu darasa ni mbayasana. Yule dada wa kijana alisema ni kweli, lakini ni suala la kusaidiana.Nilitania kwakusema, “nasi tukija kuomba msaada hospitalini itabidi tusaidiwe.” Yule dada alisema hakuna tabu. Basi kijana alianza masomo darasa la saba nami nilianza kumfuatilia dada yake kule hospitali ya mkoa. Nilifuatilia kwa miezi miwili bila mafanikio zaidi ya ahadi tu.
Nilijua kwamba, Yule muuguzi, dada wa yule kijana alikuwa anataka tu kuvuta muda ili mdogo wake amalize masomo ili anitolee nje. Ilibidi nimwambie kwamba, kama asiponikubalia ombi langu, mdogo wake ni lazima angeanguka mtihani kwani ningekwenda kuchongea mkoani kuhusu kudurusu kwake.Yule dada aliniambia, kama hilo ndilo lengo langu, ni vizuri nikalifanya.
Kuanzia hapo sikufuatilia tena na nilipania kumchongea Yule mdogo wake, jambo ambalo sikujua kwamba, lingemdhuru na bosi wangu, yaani mwalimu mkuu. Ni kweli nilikwenda mkoani na kutoa taarifa kisiri kwa wanaohusika.Ukweli ni kwamba kijana Yule ambaye alikuwa na uwezo sana darasani alishindwa baada ya jina lake kukatwa na mkuu wa shule kushushwa cheo.
Nilifurahi sana baada ya matokeo hayo. Nilikwenda kule Hospitalini kumjulisha Yule dada mtu kwamba mimi ndiye niliyemwangusha mdogo wake.
Yule dada alilia nikiwa hapohapo, huku moyo wangu ukiwa umeridhika. Jioni ya siku ile ile, Yule kijana alikuja nyumbani kwangu hapo shuleni na kuniuliza ni kwa nini nimemfanyia roho mbaya . Nilimwambia amuulize dada yake na kumsisitiza kwamba sio mimi bali ni sheria zanchi.Yule kijana aliondoka huku akisema, Mungu ndiye anayejua kulipa au kutoa hukumu kwa haki.
Nilicheka na kumwambia aende akafie mbali. “Dada yako ni ndege mjanja amenasa kwenye tundu bovu” Nilimpigia kelele. Aligeuka na kunitazama kwa muda, halafu aliondoka. Nadhani angekuwa na nguvu angeweza kunipiga ngumi nyingi sana, lakini hakuwana ubavu.Miaka ilipita na nikawa nimesahau kabisa jambo lile. Ilikuwa ni miaka 25 baadae, mwaka 2000 ni kwamba mwaka 1995 niliacha kazi ya ualimu na kurudi kwetu Iringa. Nilianzisha biashara na kuwa mfanyabiashara.
Mwaka huo 2000 nilipata matatizo ambayo yalinifikisha mahakamani.Kesi iliendelea kwa mwezi mmoja, kabla ya kutolewa hukumu. Haikuwa kesi kubwa, wala ambayo ingenitisha kwa kweli, Haya hukumu yake kwa mujibu wa wanasheria ambao niliwauliza, hakimu alikuwa anaruhusiwa kutoa faini au kifungo cha nje. Sijui walinidanganya kunipa moyo au vipi.
Lakini siku ya hukumu hakimu alinihukumu kwenda jela miaka Mitatu adhabu ya juu kabisa ya kosa langu. Nilibabaika sana na wala sikuamini kama nimehukumiwa kwenda jela. Wakati nikipelekwa kufungiwa selo Yule hakimu aliyenihukumu alinijia na kuniambia.“Siyo mimi, bali sheria za nchi. Nadhani safari hii dada yangu sio ndege mjanja tena.” Ilinichukua muda, lakini polepole akili ilizibuka wakati nikiwa jela mwezi wa pili, ambapo nilikumbuka lile tukio la mwaka 1975. Sijui nilihisi nini, lakini niliumia sana.
Sipendi kukumbuka nilivyoishi kwa huzuni kule jela, nikijutia ufedhuli ule nilioufanya kwa kijana yule wakati ule.Baada ya kumaliza kifungo changu, bado nikiwa na harufu ya jela nilikwenda nyumbani kwa hakimu yule na kubisha hodi. Alifungua mlango na kunikaribisha ndani kwake bila kinyongo. Nilimsalimia na kumwambia moja kwa moja. “Naomba radhi kwa yale niliyokufanyia wakati ule….”Yule hakimu alinikata kalma na kusema, “hukufanya lolote baya, ilikuwa ni sheria kweli. Kama ambavyo nami nimetimiza sheria za nchi.
Wala huna haja ya kuomba radhi, labda tu kwa sababu, wewe ulikuwa unalipa kisasi baada ya dada yangu kukukataa, wakati mimi sikutimiza wajibu wangu kwa kinyongo.”Niliinuka na kutoka nje, nikielekea kwangu. Maisha yalikuwa ndiyo kwanza yanaanza na uzee umeingia . Kisa kujisahau.