Friday, September 17, 2010

KOERO UTAOLEWA NA NANI? BADO NI KITENDAWILI, LAKINI LABDA MARKUS AU MTANGA…………….LOL

Najua wengi watashangaa maana wanajua mie sioleki, lakini naamini mmeona wenyewe jinsi wanaume hao wawili wanavyojifaragua, kwa mie binti kimwana.

Nakumbuka kuna mdau mmoja aliwahi kudai tena humu humu kwenye kibaraza cha Vukani kuwa mie sifai kuolewa na sitakuwa na ndoa imara kwa sababu eti nina kiherehere na kiroho papo cha kudai haki za wanawake.

Lakini Waswahili walishawahi kusema kuwa kama ni kibaya waachie wenzio……… sasa je kiko wapi?

Najua wahafidhina watatia fitina (hata hivyo nimeshawazoea) lakini wakae wakijua kuwa bahati imenidondokea….LOL

Ila kuna jambo moja, niliwahi kumuuliza bibi Koero kuhusiana na swala la wapiga emcheku kugongana kwa binti mmoja, Je inakuwaje? Jibu lilikuwa ni rahisi sana……. Ni kwamba watakaribishwa mmoja baada ya mwingine kupata mlo na baba mkwe na yule atakayekuwa anakata matonge makubwa ya ugali aka nguna na kula ugali mwingi unaofikia kilo moja kasorobo ndiye atakayepewa jiko,kwani hiyo ni ishara kuwa huyo atakuwa ni mkulima hodari na binti yao hatakufa na njaa.

Hivyo nawaomba wamezea mate na wasalandiaji waanze kuchukua mazoezi ya kumega matonge makubwa…. La sivyo hakuna ndoa….LOL

Na kwa maandalizi, wiki ijayo mwanamwali nawekwa ndani kusubiri hatima ya ndoa yangu……..je ni nani atapata bahati ya kujivinjari na kimwana……. Usikose kusoma hapa.

35 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hapa kuna utamu hapa sijui itakuwaje maana nimeoona Markus na Mtanga wanaitana SHEMEJI na sasa wanamgombania mdogo wangu wa hiari aisee kaazi kweli kweli mie nasubiri kuona huyu atakaye weza nanunukuu:- "kula ugali mwingi unaofikia kilo moja kasorobo ndiye atakayepewa jiko,kwani hiyo ni ishara kuwa huyo atakuwa ni mkulima hodari na binti yao hatakufa na njaa."

Fadhy Mtanga said...

Kwa vigezo hivyo vilivyoainishwa, namshauri shemeji yangu mtani Markus aanze kutafuta ustaarabu mwingine. Hii ngoma keshaikosa.

Markus Mpangala said...

Kabla sijaandika katika KIJIJI changu cha KARIBUNI nyasanilifanya uchunguzi mara kadhaa, nimesoma mawasiliano yangu na huyu Koero, nikahitimisha 'ndiye nilikuwa nikimsaka miaka yote hii'. Asinidanganye mtu wala Mtani a.k.a SHEMEJI, Koero ni bonge la dhahabu SIPENDI wanawake wanaotazama vidume kama ndiyo mwisho wa maisha yao.
Koero napiga magoti NAOMBA TUOANE achana na mtani wangu Fadhy..... mie sina jingine sina cha kupindisha wala nini KOERO unatafutwa na mzee wa lundunyasa. sitanii kuna vitu nimegundua na nimeviona. ngoja nitaandika tena. HEBU FIKIRIA KWANINI NILIAMUA KUANDIKA HADHARANI DHAMIRA YANGU YA DHATI KUKUCHUMBIA na UWE MAMA WATOTO WANGU. nina hakika napigania nafasi yangu kwako. NAPIGA GOTI KWAKO binti Mkundi.
USISAHAU KUNISOMA PALE KIJIJI KWANGU karibuni nyasa.

Anonymous said...

Ha ha ha haaaaaaa....Duh ugali kilo moja kasorobo....naamini akitokea msukuma itakuwa kaaazi kweli kweli, maan ataomba na nyongeza.......

chib said...

Ha ha haaa, nimecheka.
Sipendi kuingilia chochote hapa, maana naona kama usiku wa kiza, kwani kuna wakati watu waliambiwa wameangukia pua kwa tamaa zao, sasa..... naona wameanikwa tena ha ha haaaa.
Kutokana na kusoma haraka haraka, basi yaonekana wote watatu mmepania, yaani Markus, Fadhy na Koero, na kuna wengine wameshawasha indicator na kuanza kutamba kabisaaaaaa, he he heeeee, nani alisema haolewi mtu.. ha ha haaa.
Ebu yamalizeni wenyewe nyuma ya pazia, sie tutakuja kuwaunga mkono kwa hali na mali katika kufanikisha muungano huo, ambao mpaka sasa bado ni wa kufikirika, ha ha haaaa

John Mwaipopo said...

hadi raha vile. koero una visa wewe

Anonymous said...

Halo haloooooo..... kule Tanga wanasema "mamie mwali tandika kwani mgeni anaingia" nami nasema Mama Koero jiandae Koero amepata jiko.......LOL

Anonymous said...

Halo haloooooo..... kule Tanga wanasema "mamie mwali tandika kwani mgeni anaingia" nami nasema Mama Koero jiandae Koero amepata jiko.......LOL

SIMON KITURURU said...

Mmmmh!

Bwaya said...

Nimecheka. Matonge makubwa? Uhusiano wa matonge makubwa na kazi wapi wapi?

Lakini Koero, kama mwanaume mmoja anaweza kuoa wanawake zaidi ya mmoja; na kwa kuwa Koero wewe ni mtetezi wa usawa na haki za wanawake; huoni kwamba unaweza kabisa kuolewa na wote wawili ili kupunguza usumbufu wa hao jamaa kushindana kukata matonge?

Fadhy Mtanga said...
This comment has been removed by the author.
Fadhy Mtanga said...

naona shemeji yangu mtani Markus unajieleeeeza weee utadhani tupo kwenye jukwaa la ubunge.
mie siyo fundi wa maneno, bali vitendo.

natoa ushauri kwako shemeji uanze tu kucheki ustaarabu mwingine, hii ngoma ushaikosa.

Koero Mkundi said...

Kaka Bwaya, kwa kuangalia tu Historia ya hapa Nchini, hivi ni kabila gani linasifikia kwa wanaume wao kuwa na Nguvu za kufanya kazi? Bila shaka ni Wanyamwezi na Wasukuma, Je wakijua chakula chao kikuu?

kaka Matondo nisaidie.......

kaka Bwaya Ugali Uliopikwa na Msukuma au Mnyamwezi ni mgumu kama jiwe na ndio maana walichukuliwa Manamba kwa wingi kwenye mashamba ya mkonge na mashamba ya Miwa.

Nenda Tanga au Kilimanjaro na kwingineko kunakolimwa mkonge au kwenye mashamba ya miwa utawakuta wamejaa tena kwa idadi ya kutosha.

Kaka Bwaya Iwapo Binti yako ataolewa na Msukuma au Mnyamwezi basi hatakufa njaa Bro.....LOL

Bado natafakari sifa za hao watangaza nia wawili.......

Ramson said...

jamani na mie naomba nijiunga na kinyang'anyiro, mweh! unajua sifa ya mwanamke mzuri huwa anagombewa...LOL
Haya Koero andaa uwanja wa kuonyeshana ubabe mie naahidi kumaliza ugali kilo moja

Markus Mpangala said...

Mtani wangu Fadhy una mkwara weyeeee, lakini mimi nasema hivi, raha ya ubwabwa utandu, utamu ukizidi sema bandu bandu......

Najieleza kama sinema ya kihindi, lakini kumbuka bila mimi kuandika pale KIJIJINI kwangu hata Koero asingeliandika.

Najieleza, na nimemtumia ujumbe chonde mtose mtani wangu fadhy, nipe mie hilo jambia la maisha yako nilishike nikulinde.

Koero napiga MAGOTI NIPO CHINI YA MIGUU YAKO. NAOMBA TUOANE. ila naomba usiseme mie mtangaza NIA.

nimekuja tayari naomba TUOANE

Yasinta Ngonyani said...

Mie yangu macho nasubiri mshindi, ili tunywe ugimbi na kucheza limgambusa na lizombe....kaazi kwelikweli

chib said...

Kwi kwi kwiiii, nakushukuru Koero kwa kutufanya tuhamie huko wanapopaita busy kwa msongo wa mawazo. Mie nipo tayari kumpa tiba ya kisaikolojia atakayeangukia pua kwi kwi kwi

Fadhy Mtanga said...

nasema hivi Koero huyo mtani wangu shemeji Markus hana lolote. waswahili wanasema chema chajiuza, kibaya chajitembeza.

huyo jamaa hapo hana lolote ndo maana anatumia maneno mengi akisahau kuwa barafu haijengi nyumba.

maneno matupu hayavunji mfupa.

kwanza huyo jamaa ni mvivu sana Koero. halafu hajui kujali. kama anabisha mwambie aniruhusu niseme kisa cha yeye kufukuzwa kwa kimada wake wa awali.

mie wala sihitaji kumpaka matope ili nishinde kwani najua tayari wewe ni wangu na hivi karibuni nitakwenda kumsabahi bibi Koero.

ninachague mimi kwa kuwa ninastahili kuwa wako.

Markus Mpangala said...

Wakati naandika pale KIJIJINI kwangu nilifanya tafakuri anuai. najua mtani wangu fadhy nitakufichulia hapa hapa.
Koero weweeeeeeee ebu angalia pale KIJIJI kwani kuna watu wawili wanatembea kwa mahaba wameonyesha migongo. halafu muulize mtani wangu fadhy wale ni nani.

Kama ni wako basi anakudanganya,hakujali anakuzuga na busu la alfajiri, lenye ukakasi anuai.

NIPE MIMI, kwani sifanani na stori za makande ya saidi mnyamwezi na mipasho ya wazua methali.
NIPE MIMI ila usinihurumie.

Ramson ni kijana wa hadaa, anaweza kukupeleka kuzimu bureee.

NIPE NIPE NIPE MIMI MIMI
kama sukari nitalamba na asali nitaonja. ujumbe na radha vyote ni vyangu pomoni mdomoni. Koero KWAKO SISEMI WALA SIHEMI..... najua mtani wangu fadhy anakupa maneno machache lakini mimi nakupa mengi kwakuwa najua UTAMU WA PENZI NI MANENO MURUA yenye kila viungo vya STORI ZA MAKANDE zisizo na umahiri wa kusimulia kitakatifu.

PENZI akupaye ni yule aimbaye kwa lugha tamu ya MAHABA ile lugha ya kuomba ridhaa, ile lugha ya kukata rufaa, ile lugha ya kuimba kihindi au kunena kwa lugha. kumbuka NITAKUANDIKIA TENA PALE KIJIJINI KWANGU jinsi unavyonikorohua nafsi.

Mtani wangu Fadhy; dume lenye uhakika halimchungulii mkewe...... inakuwaje ukaombea kitoweo chako kwa jiraniiiii....... haya twende na stori za makande zipo kuleeeeeeeee eee

Fadhy Mtanga said...

mie si fundi wa maneno kwa kuwa si mwanasiasa kama mtani wangu na shemeji yangu Markus.

ila tu nakupa angalizo, ndoa siyo majaribio kama mashindano ya mpira ama michuano ya urembo. kama utaamua kuijaribu ladha ya ndoa iliyoshindwa, basi ambatana na huyu kijana shemeji yangu.

unakijua kisa cha mie kuamua kumwita jina la shemeji kama nyongeza ya jina la mtani?

angalizo jingine, huyu jamaa anatokea lile kabila ambalo ukiwapa pesa wanafikisha kwa uaminifu, ukiwapa........utavuna mabua.

kama kawaida mie siongei sana kwa kuwa najua ushanichagua.

Markus Mpangala said...

Mtani wangu shemeji yangu duh!!! uliwaza nini na wakinipa nini mweeeeeeeeeeeee rahaaaaa si unajua ukipewa kwa ridhaa wala hukati rufaa, bila chambi chambi au? Mtani una mamno weyeeee, lakini najua STERINGI ANAKUFA PICHA NDIYO INAANZA. Koero NIPE MIMI

John Mwaipopo said...

utani utani mara mmoja wao anachukua

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

mmmh!

Anonymous said...

Sasa mimi kama mzee mzima, inabidi nitumie busara kuweka mambo kwenye mzani.

Napenda kujua ni nani ni bachelor au spinster kati ya wachangiaji hawa hapa ili niweze kutegeu kitendawili hili, Kusema ukweli Koero amenipa mtihani mgumu katika mada zaka zinazofanana na hili. Hapa lazima jambo lifanyanyike! Binafsi najitolea kuwa mwamuzi au refari kwa lugha ya kisoka.

Markus Mpangala said...

Kaka Mwaipopo hakika SITANII naomba niwie radhi ukidhani huu ni UTANI, hakika mie toto la kinyasa sina neo jingine zaidi ya KUMPENDA KWA DHATI binti Mkundi.

Nipo kwa shida na raha, utamu wa penzi ni ridhaa na raha murua, Najua kuwa penzi Muwali ndilo hulizala AU tamu ya HUBA na maisha ya ndoa adhimu,
ni raha kumtakia UMPENDAYE TOKA MOYONI hakika sina jingine nipe raha na amani Koero tafadhali Koero. sina chambi chambi wala jembe la la kuchimbia harara bali NIMEUMBWA na harara zenye kila aina ya MANUKATO YA PENZI....

Koero mwana wa Mkundi, nipo makini ninenacho wala sitangazi nia hapa bali dhamira ya KUISHI NAWE DAIMA. kwa kweli ningeweza ningekupa mlima Kilimanjaro, lakini hadidu rejea nitakupa MOYO wangu uchukue UINGIE ndani uone PENZI LANGU..... Mtani wangu shemeji usiniwekee kiwingu maana wanipa jakamoyo ...

Koero sina AMALI nitakupa HUBA KAMILI.

Fadhy Mtanga said...

Mpenzi Koero,

Usimsikilize Markus,
Hajiamini kajaa wasi,
Bure ajitakia kesi,
Saizi yako hajaifikia.

Koero nichague mie,
Ili maishani nikufae,
Matamu nikupatie,
Mapenzi ya kufurahia.

Markus atakupoteza,
Mrembo atakuchakaza,
Kwangu utakula utasaza,
Na afya njema pia.

Mie kutunza najua,
Kwa Markus utaugua,
Kijana atakusumbua,
Uteseke na dunia.

Mpenzi wewe ni wangu,
Ua la ulimwengu,
Markus aondoe kiwingu,
Najua ushanichagua,

Mtani nakupa tu pole,
Rudi katafute wale wa shule,
Mfupa umekushindale,
Mwenye meno ukaniachia.

Koero mrembo Koero,
Markus kajawa kihoro,
Atakulisha wewe kiporo,
Ni mvivu kujitafutia.

Nashukuru umenielewa,
Nami umeshanichaguwa,
Raha tele utapewa,
Raha iliyozidia.

Wasalaam mpenzio,
Kijana Fadhy.

Markus Mpangala said...

Najua dhima ya penzi
koero daima nitakuenzi,
penzi zaidi ya enzi,
sisemi wala sihemi,

Koero binti mkundi,
mrembo unipaye amali,
nikuonapo hakika silali,
katu nitakuoa ewe mwenzi

Fadhy Mtanga said...

Katu nitakuoa ewe mwenzi,
Kiswahili tu hakiwezi,
Atakuletea jinamizi,
Usiku kucha kukusumbua.

Koero tafakari hilo vema,
Kumtosa ndiyo hekima,
Markus kamwe si mwema,
Kila siku utalia.

Huyo mwanaume suruali,
Hawezi kuvunja majabali,
Utalala na njaa ile kali,
Mrembo mwiliwo kupungua.

Markus anajua tu kuchonga,
Maneno mengi achonga ngenga,
Si mume bali kibaramchanga,
Ukweli sasa ninakwambia.

Mwanaume gani chaukarange,
Anaendeshwa na nazo bange,
Hakufai huyo umpinge,
Njoo kwangu mtoto ukatulia.

Wewe ndiwe ua lilochanua,
Markus hajui hata kumwagilia,
Ukimkubali mbona utalia,
Njoo kwangu utafurahia.

Markus nasema hatokufaa,
Utakonda mrembo ukasinyaa,
Njoo kwangu hakika utang'aa,
Maana najua kuhudumia.

Koero Mkundi said...

Ha ha ha ha haaaaaaa..... naona mpambano umefika patamu...duh! hadi Mashairi! hakika Ngoma inogile mwayego.....LOL

Haya waungwana kuna marekebisho kidogo ya masharti ya kumpata kimwana mie Koero Binti Mkundi.

Ngoja nifanye summary maana ni marefu kweli kwani mzee mkundi anataka kuhakikisha kuwa naangukia katika mikono Salama.

Nipeni muda nitaweka bandiko hivi punde na hilo ndilo litakalotujuza mshindi......LOL

Markus Mpangala said...

Mtani huniwezi,
upupu au kwenzi,
dola au dinari,
pauni au shilingi,
nalijua penzi,
lile muwali,
daima nilienzi,

Mtani wajua mepes,
wajua ile sentesi
kwangu ni parandesi,
hadidu zaidi ya fenesi,

Fadhy mwana wa Mtanga,
hujui kulea kimwana,
punguza lukuma,
wajua toto la kinyasa,
daima uvivu lakana,

chambichambi,kukusanya,
siyo wewe mwana bodaboda,
kila siku kiguu na njia,
Tramp wasafiri kumwacha mwana,

baridi kujiumizia,
katu siyo mume wa maana,
kivuli watembelea,
ati kujitafutia,

ukwasi haujengi penzi,
ukata haujengi penzi,
Koero nipe penzi,
Mtani hatakuenzi,

FADHY MTANGA a.k.a shemeji mtani wangu daima

nisikize kiinglishi, mwana naonngeza kubonga,
sina bichikoma,
navaa tu bugaluu sana,

Eti mtani wangu....
Shall i campare the to a summer's day?
Thou art more lovely and more temperate;
rough winds do shake the darling buds of may,
and summer's leave hath all too short a date.....

Koero binti mkundi,
wajui ninalo penzi,
hakika nienzi...

Markus Mpangala said...

sentesi ya kwanza nimekosea mtani wangu, inasema Shall i compare thee to a summer's day?

Fadhy Mtanga said...

leo nimepita tena hapa na kuangua kicheko vibaya mno. katika kublog kwangu, hii ni posti iliyonivunja mbavu kila nikija kusoma na kuacha maoni...
sisi wote watatu, koero, markus nami ni marafiki wazuri sana.
ahsante sana Koero kwa kuchngamsha umati.

Fadhy Mtanga said...

Jamani Koero mbona umeadimika hivyo?

Fadhy Mtanga said...

Leo Nimepita tena hapa. Nimecheka sana.

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___