Wednesday, September 1, 2010

YATOKANAYO NA WASIFU WA DK. BEN CARSON

Dk. Ben CarsonDk
Nimependezwa sana na maoni ya wasomaji wa kibaraza hiki kuhusiana na mada niliyoiweka wiki iliyopita ya wasifu wa Dk. Carson.

Naomba nikiri kuwa maoni ya kaka yangu Mubelwa Bandio yalinifanya nijiulize maswali kadhaa ambayo ningependa kuwashirikisha wasomaji ili tutafakari kwa pamoja:

Maswali yenyewe ni haya yafuatayo:

*mama yake aliolewa akiwa na umri wa miaka 13 na mchungaji mzee kwa kukimbia shida za pale nyumbani kwao, ambapo pia aliachika na kuachiwa kuwalea watoto wawili pake yake.

*mama huyu aliishia darasa la tatu, ambapo sio kiwango kizuri cha elimu cha kujivunia, lakini kwa shida sana alilazimika kufanya kazi zaidi ya tatu ili ahakikshe anawatengenezea wanae hao future.

*Carson alikuwa mbumbumbu darasani, lakini kutokana namsimamo wa mama yake wa kuwalazimisha kusoma libarary, alipata mwamko na kusoma kwa bidii hadi kufikia kuwa daktari bingwa wa upasuaji.

Haya ni mafanikio makubwa kwa mama huyu (Mwanamke huyu) ambaye hakupata elimu kubwa. Je kuna wazazi wangapi ambao wana elimu ya kutosha tu lakini malezi kwa watoto wao yamewashinda?

Hata hivyo kuna jambo moja nimeliona kwa upande waserikali ya Wamarekani, nalo ni lile la kutambua mchango unaofanywa na wataalamu mbalimbali nchini humo.

Pamoja na Carson kupata tuzo nyingi, lakini Rais wa Marekani wa wakati huo G W Bush alitambua mchango wake na kumwalika Ikulu na kumpa tuzo ya Uhuru ambayo ni tuzo kubwa kutolewa nchini humo na Rais.

Je ni wataalamu wangapi au niseme ni Watanzania wangapi ambao wanatoa au wametoa mchango mkubwa hapa nchini hata wengine wakapoteza maisha yao au wakawa wameathirika kwa kiasi kikubwa lakini mpaka leo hii hawajawahi kupewa tuzo yoyote na Rais au hata kutambuliwa na Serikali?

Je hakuna haja ya kuliomba bunge lijalo litunge sheria itakayounda jopo la watu ambao kwa kuzingatia vigezo maalum wateue mtu mwenye sifa fulani kulingana na kile alichokifanya katika jamii na kukabidhi jina lake kwa rais ili apewe tuzo kubwa na ya heshima?

Tuzo hiyo isiwe ni tuzo tu ya kawaida bali pia iwe ni tuzo itakayoambatana na fedha za kutosha na kuwe na sherehe maaluma wakati wa kukabidhi tuzo hiyo.

Hilo naamini litawezekana kwani huko mikoani kuna watu wamefanya mambo makubwa lakini kutokana na urasimu yanaishia kwenye makabati ya wakuu wa wilaya au wenyeviti wa vijiji.

Nataka kuwasha moto......

2 comments:

emu-three said...

Tunashukuru kwa nyongeza hii, ni kweli wapo watu wamefanya mengi katika jamii yetu, lakini jinsi gani wanaweza kuwekwa kwenye vitabu vya kumbukumbu inakuwa ni mtihani.
Labda kwasababu `kizuri' ni kile alichogundua au kutengeneza `mzungu'. Na ya kuwa sisi hatuna utaratibu wa kuweka kumbukumbu za wema waliopita wa kitanzania, labda wawe wameandikwa na wenzetu, kama walivyoandikwa akina Mkwawa na wengineo.
Swali ni je hatuna `wanafikira wa kitanzania, ambao waligundua vitu, au maisha yao ni marejeo ya kukumbukwa?'

Yasinta Ngonyani said...

nanukuu "Je hakuna haja ya kuliomba bunge lijalo litunge sheria itakayounda jopo la watu ambao kwa kuzingatia vigezo maalum wateue mtu mwenye sifa fulani kulingana na kile alichokifanya katika jamii na kukabidhi jina lake kwa rais ili apewe tuzo kubwa na ya heshima?mwisho wa kunukuu.

Swali hili ni nzuri sana. Kwa kweli inasikitisha sana kuona sisi waafrika tunaiga mambo yasiyo na maana lakini yale ya maaana tunaacha hivi tuna kasoro gani? Tunaiga, tunaiga na tunaiga na kuna wengine sasa wanaiga hata lugha eti mimi siwezi kuongea kiswahili, mimi si mngoni, kaazi kwedlikweli. Kwa nini tusiige kusoma vitabu au kwa nini tusiige kuwatunukia waliotenda ugunduzi? Siamini kuwa Tanzania yetu hawapo wapo sana tena wengi tu. AAAhhhh hili kwa kweli ni tatizo nadhani hasira zimenishika naacha nisije nikaharibu hapa....