Jiulize ni kitu gani hasa utaandika katika kuueleza wasifu wako ili huyu mtu msiyefahamiana kabisa akufahamu kupitia maandishi yako?
Kwa mfano labda utaanza kwa kusema, “mimi ni mwanamke au mwanaume, ni mwanafunzi; mfanyakazi au nimejiajiri nakadhalika nakadhalika.
Labda utaeleza juu ya vitu unavyovipenda na vile usivyovipenda, pamoja na tabia yako kama vile ni mwenye aibu, chakaramu, mtu wa kujirusha, mkimya, mpole, na tabia nyingine ambazo zinaweza kumfanya mtu atakayesoma wasifu wako akufahamu vizuri.
Jaribu kuchunguza tabia za marafiki zako wote pamoja na ndugu na jamaa waliokuzunguka, Je unadhani yupo japo mmoja ambaye mmetokea kufanana kwa kila kitu?
Sidhani, na kama yuko labda itakuwa ni baadhi ya vijitabia fulani mnafanana lakini haiwezi kutokea mkafanana kwa kila kitu.
Vipi kuhusu ndugu mliozaliwa tumbo moja, yawezekana kweli mkafanana kwa kila kitu? Jamani si tumezaliwa na baba mmoja na mama mmoja, Kwa nini sasa tusifanane kwa kila kitu?
Hii nadhani haiwezekani, na haitatokea iwezekane hata siku moja.
Kwa mtazamo huo basi, naamini kwamba kuna Koero mmoja tu hapa duniani, naye ni mimi, kama kuna mtu anatumia jina la Koero, basi hiyo ni coincidence, lakini hawezi kufanana na mimi hata kidogo, tembea dunia yote hii, Koero ni mimi tu. Kwa hiyo mimi ni mtu maalum kama ulivyo wewe na mwingine.
Binafsi najivunia kwa jinsi nilivyo na najikubali kwa kila kitu, kama ninayo kasoro, basi wewe ndio umeiona kwa mtazamo wako lakini mimi sijaiona.
Hivi karibuni nimetofautiana na mama yangu juu ya mustakabali wa maisha yangu.
Eti anataka nirejee chuoni ili kuendelea na Masomo, wakati nimeshadata na Biashara zangu. Baada ya lile zengwe la kurejeshwa nyumbani na chuo kufungwa nimejikuta nikipata uamuzi mwingine wa kuendesha maisha yangu, na nimeona niwe mfanyabiashara.
Elimu niliyoipata ya Kidato cha sita inatosha sana kwani nimeshajijua kuwa mimi ni nani na hata nikiendelea na masomo ya chuo kikuu sidhani kama itanisaidia sana katika kufikia malengo na matarajio yangu. Na hata kama nikisoma na kupata shahada kumi sidhani kuwa hayo ndio malengo yangu, sana sana naona ni kupoteza muda bure.
Nimeona nijikite kwenye biashara, kwa sababu naona kuwa ni kipaji changu na nina matarajio makubwa sana hapo baadae ya kuwa mmiliki wa kampuni kubwa yenye matawi karibu nchi nzima, hivyo ndivyo ninavyoiona biashara ya yangu.
Nadhani utaniuliza kama utaalamu wa kuendesha hiyo biashara nitauapa wapi? Jibu ni rahisi sana, nitaawajiri hao wasomi wenye shahada zao na kwa hakika bishara yangu itakuwa ikiendeshwa kwa ufanisi, kwani naamini naweza kuajiri hata Profesa, si ilimradi nimlipe mshahara mzuri na marupurupu?
Kwani hamjui kuwa nchi hii watu wanasoma ili wajiriwe badala ya kujiajiri?
Kwa nini mama yangu anakazania nisome? Anatafuta kuridhisha nafsi yake. Mama yangu anao ndugu zake ambao wamesomesha watoto wao mpaka vyuo vikuu na wanazo nafasi kubwa wengine wakiwa serikalini na wengine wakiwa wameajiriwa na mashirka ya kimataifa wakiwa wanashikilia nafasi za juu, sasa wakikutana kwenye vikao vyao vya ndugu, kila mmoja huanza kujisifu kuwa wanae wamesoma au wanaendela na masomo ya elimu ya juu, ilimradi kutaka kujionyesha kwa wengine kuwa watoto wao ni wasomi.
Kwa upande wa familia yetu dada zangu na kaka zangu wote ni Graduate, mimi tu ndiye nimechomoa kuendelea na elimu ya juu.
Kwa kweli baba yangu hana tatizo na uchaguzi wangu, lakini mama, Duh! Ameng’ang’ania kweli nirejee kusoma, na mimi nimekataa kabisa.
Mimi naamini kila mtu anao wasifu wake na malengo yake haihitaji mtu aje akukamilishe kwa kukupangia kuwa ufanye nini juu ya maisha yako.
Mtu kukubali kupangiwa nini cha kufanya juu ya maisha yako ni kupotea njia, ni sawa na kupanda basi la kwenda Mtwara wakati nia yako ni kuelekea Arusha!
Ukweli ni kwamba wako vijana wengi wanakabiliwa na changamoto inayonikabili sasa. Binafsi nimeweza kukabiliana nayo na ninaamini nitashinda kwani baba yuko upande wangu, lakini ningependa kuwashauri vijana wenzangu kwamba tusikubali kuburuzwa na matakwa ya wazazi, sisi ni watu kamili hatuhitaji wazazi watukamilishe.
Samahani nimeandika makala hii nikiwa na mchanganyiko wa hasira na msongo wa mawazo, hata hivyo naamini watambuzi watanielewa.