Tuesday, February 3, 2009

NILISHINDWA KUMSAIDIA ZINDUNA: SEHEMU YA PILI

Hawawezi kupiga kelele kama hivi

Hivi karibuni niliandika habari iliyohusu kifo cha rafiki yangu Zinduna ambacho kilitokana na kujiua kwa kunywa idadi kubwa ya vidonge vya Klorokwini.
Mnamo Januari 24, 2009 ndio alikuwa ametimiza miaka mitatu kamili tangu kufariki kwake.
Niliandika habari ile kama kumuenzi, lakini pia nilikuwa na dhamira ya kutaka kujadili kuhusu tatizo la Depression ambalo kaka Mubelwa Bandio kanisaidia kulitafsiri kwa Kiswahili kuwa linajulikana kama tatizo la Msongo wa mawazo.
Ahsante kaka Mubelwa kwa kunielimisha.

Sababu zinazotajwa kupelekea msongo wa mawazo ni nyingi, lakini kubwa kabisa zinazompelekea mtu kupatwa na msongeko ni hizi zifuatazo;

· Kupoteza ajira au kuwa na wasiwasi wa kupoteza ajira,
· Kuwa na umasikini wa kupindukia kiasi cha kukosa matumaini ya kujikwamua,
· Kutoridhika na hali ya kiuchumi na kushindwa kukabiliana nayo kutokana na shinikizo la watu wanaokuzunguka,
· Migogoro isiyokwisha ya ndoa au ya kifamilia,
· Matukio kama yale ya vifo vya wazazi, kutekelezwa utotoni, udhalilishwaji wa kijinsia na maradhi sugu.

Dalili za msongeko zinatofautiana kati ya mtu na mtu, lakini nitajaribu kutaja chache;
· Kukosa usingizi au kua na usingizi mzito usio wa kawaida. Kukosa raha,
· kujiona ni mwenye hatia,
· Kuwa na wasiwasi, Kuishiwa na nguvu kusiko kwa kawaida, Kukosa hamu ya kula au kuwa na hamu ya kula sana na hivyo kupelekea kupungukiwa na uzito au kuongezeka uzito,
· Kukosa matumaini na kuyaona maisha kama hayana maana,
· Kuwa na mawazo ya kuuwa au kujiuwa ya mara kwa mara na mara nyingi dalili hii inaweza kudumu akilini kwa miaka mingi bila mtu kujua.
· Na hata kama mwathirika anatamka haja ya kufanya hivyo inakuwa ni kama kufanya masihara, kwa mtu asiye elewa, lakini lazima ifahamike kwamba wanaotamka hivyo wamedhamiria.

Mara nyingi watu wanaotamka kutaka kujiuwa au wale wanaofanya jaribio la kutaka kujiuwa ni kwamba wanapiga kelele za kuomba msaada ili wasikilizwe, na kama wakipuuzwa matokeo yake ni kutekeleza kile walichodhamiria.

Wapo watanzania wanaosumbuliwa na tatizo hili la msongeko, lakini labda kwa sababu hatuna takwimu sahihi ndio sababu tatizo hili limekuwa halifahamiki. Wapo watu wengi sana wameuwa au kujiua kutokana na tatizo hili la msongeko, lakini kwa bahati mbaya sana watanzania wengi hulihusisha tatizo hili la msongeko na imani za kishirikina. Kuhusisha hali hii na ushirikina hakuna ukweli wowote na matokeo yake wengi wamejiua na kuuwa kutokana na kutopata tiba muafaka.

Yatupasa sasa kuyaangalia matatizo ya aina hii katika mkabala tofauti badala ya kukimbilia ushirikina, hiyo haiwezi kutusaidia na badala yake itatuletea maumivu zaidi.

Ukweli ni kwamba, kuna wakati dalili za msongeko hujitokeza kwa njia ambayo ni vigumu kwa mtu kujua kwamba mwenzio anakabiliwa na tatizo hili. Hata hospitalini inahitaji wataalamu wazuri sana kubaini baadhi ya dalili na hata wanapobaini bado kuna suala la ugumu wa kutibu msongeko. Huweza kutibu msongeko kwa dawa za hospitalini peke yake bila msaada wa ushauri.

Tukumbuke kwamba wengi wetu tunaishi kwenye maisha ya ushindani na mabadiliko ni ya haraka sana, kuna migogoro mingi ya kindoa na kuvunjika moyo kwingi kimaisha. Hivyo kila mmoja anaweza kuingia kwenye kusongeka.

Kwa upande wa matibabu hakuna matibabu ya moja kwa moja yanayotajwa kutibu msongeko, bali wataalamu wa magonjwa ya akili wanaweza kutoa dawa kulingana na tatizo la magonjwa yanayoonekana. Hata hivyo inapendekezwa mgonjwa kufanyishwa mazoezi ya viungo pamoja na ushauri nasaha au ushauri wa kisaikolojia(psychotherapy)

Kama ukiona mtu wa karibu yako ana msongeko unashauriwa hatua ya kwanza ni kumpunguzia hali ya kutokua na matumaini na kumpa moyo wa subira kwa kuyaona matatizo aliyonayo kama changamoto za maisha.

Pia inashauriwa sana kuwa naye karibu, isitokee hata mara moja akaachwa peke yake. Hata kama inaonekana kukerwa na kile kitendo cha kumchunga na kuwa mkali, hiyo isikutishe na wala usikasirike kwani hizo zote ni dalili za msongeko.

Narudia tena kusema kwamba, watanzania wengi wana msongeko ingawa hawajui. Kujiua kwingi kunatokea sana hivi kunatokana na msongeko. Hata ukisoma ujumbe unaoachwa na wale wanaojiua kama ule ulioachwa na Zinduna unaweza kuligundua jambo hili.

Ujumbe kama vile “nimeona maisha hayana maana”, “ugumu wa maisha umenishinda”, au “hawanitaki hivyo nimeona sina maana” ama “amenikataa na hivyo naondoka nimpe nafasi”.

Lakini kama nilivyosema, yanapotokea haya, maelezo yatakayotolewa ni kwamba, amelogwa. Mara nyingi watu wanaojiua wanakuwa wameshafanya majaribio ya kujiua hata mara mbili huko nyuma, kama tulivyoona kwa Zinduna.

Lakini cha ajabu hakuna anayejali kuchukua hatua za matibabu mtu anapofanya majaribio ya kujiua, kwani huonekana kuwa baada ya kuokoka kwenye jaribio la kujiua hatarudia tena. Hivyo sio kweli.

4 comments:

SIMON KITURURU said...

Asante kwa hili kwa maana huwa mara nyingi linarukwa katika maongezi yetu Wabongo.Ngojea nijisikilize , nisije nikawa mimi mwenyewe na MSONGEKO BURE!:-(

Markus Mpangala said...

Mmmh hapo sawa kabisa. ngoja nitaanza kula sasa maana hii hali duh!

Kissima said...

Kuna watu wenye matatizo makubwa sana lakini wanaishi kwa raha kiasi kwamba akikwambia matatizo aliyonayo hutaweza kuamini.
kwamba,kuna watu ambao tunaishi tu pasipokutegemea kuwa kuna siku maisha yanawezakuwa kinyume na tunavyotarajia kwa maana kwamba huwa tunaangalia upande mmoja tu wa kuwa na mafanikio tu na kusahau kuwa kuna matatizo.

Kulifanya tatizo kuwa ni siri ni kati ya mambo ambayo huchangia hali hii.

Wakati wote tuwe tayari kukabiliana na changamoto za maisha.Fahamu kuwa Tatizo ulilolishindwa wewe mwenzako anaweza kulitatua.


Mtu anapokuwa ktk msongo wa mawazo,ina maana kwamba anajaribu kutatua tatizo,si kivitendo bali kwa kuwaza kupita kiasi, na wakati mwingine ktk kuwaza huku sio kwamba anatafuta suluhisho bali matokeo ya tatizo.

Kukabiliana na tatizo hili ni uamuzi wa mtu binafsi. Uzuri ni kwamba anayeangukia kwenye msongo wa mawazo huwa anakuwa ni mtu ambaye ameshajitambua, kwani kama mtu hajajitambua, kwa chochote kibaya atakachofanyiwa au kila kitu atakiona ni cha kawaida hata kama kina madhara ktk maisha.

Yaone matatizo uliyonayo kama changamoto za kimaisha tu,kabiliana nayo.

Mimi nafikiri "KIFO" ndio tatizo kubwa kabisa kwa mwanadamu hapa duniani, lakini tatizo hili tumelirahisisha kiasi kwamba tunaendesha maisha yetu vizuri tukiwa na plani nyingi na za muda mrefu.

Kwa nini changamoto hizi nyingine ndogondogo tusizirahisishe kama tunavyokirahisisha kifo?


Amua wewe mwenyewe!

Usikubali kwamba iko siku eti utakutana na tatizo ambalo itakulazimu kujiua,kwani kuna wanaosema kuwa anayejiua hakupenda,hata anayesema kuwa ati hatakaa kujiua siku moja anaweza kuja kujiua .Zote hizi ni dalili za kukubali kushindwa.

kamala J Lutatinisibwa said...

mimi nasisitiza tukichoshwa na miili basi tuivue, tuitupilie mbali tutapewa mingine. lakini wa buddha wanaamini hata ukijiua kabla ya kufanya kazi yako iliyokuleta duniani, utakutawahuni fulani wanafanya ngono za kihuni na wewe utarudi duniani tena kupitia wao.

ila msongeko waweza kuhusishwa na ushirikini kwa kiasi chake kwani ushirikina unatisha sana hata kama hauna unguvu. kama ulivyosema wabongo wengi tuna msongo huo.
wewe kama una msongo karibu kimara rombo, utauacha pale