Sunday, April 5, 2009

JE HILI NALO LISEMWE NA NANI?

Tunavumilia mengi

Ni siku ya Ijumaa niko ofisini kwangu nimekaa nikiendelea na kazi zangu kama kawaida mara napata mgeni. Mgeni huyu ni rafiki yangu Farida mwenyeji wa kule Arusha niliyesoma nae kidato cha tano kule Morogoro, ingawa baadae mimi nilihamia shule ya binafsi hapa jijini Dar es salaam na kumuacha rafiki yangu kule Morogoro akiendelea na kidato cha sita.

Ni takribani miaka mitatu imepita bila kuonana na rafiki yangu huyu kwani kwa mara ya mwisho tulikutana pale baraza la mitihani mwenge wakati tulipofuatilia result slip zetu.

Ilikuwa ni furaha isiyo kifani kukutana na rafiki yangu huyu ambaye wanafunzi wenzetu walikuwa wakituita pacha wakidai eti tunafanana. Tangu wakati huo tulipoachana pale baraza la mitihani hatukuwahi kuonana wala kuwasiliana.

Nilimuuliza Farida kwamba yuko wapi na anafanya nini? Simulizi zake ndio zilizo nifanya nipate mada ya kuweka humu bloguni leo. Ukweli ni kwamba jambo ninalotaka kuzungumzia si geni sana kwa wasomaji wa blog hii, kwani ni jambo ambalo lipo sana, labda tu niseme kuwa siku za hivi karibuni limezidi kukua tena kwa kasi ya ajabu. Nimeona kama tusipolisemea sisi wanawake, hali inaweza kuwa mbaya sana hapo baadae.

Baada ya kumaliza kidato cha sita Farida hakupata alama nzuri za kumuwezesha kujiunga na chuo kikuu, lakini hata hivyo aliamua kujiunga na chuo cha Kimoja maarufu hapa jijini (Naomba nisikitaje) ili kusoma masomo ya biashara na masoko.
Chuoni hapo Farida alikutana na unyanyasaji mkubwa wa kijinsia, ambao ni vigumu mtu kuamini ukisimuliwa. Vinara wakubwa wa unyanyasaji huo wa kijinsia ni walimu, kwani wakimtaka mwanafunzi hawatarajii kukataliwa na kama mwanafunzi akimkataa mwalimu atarajie kufeli katika somo la mwalimu huyo.

Farida anabainisha kuwa kuna ushirikiano mkubwa miongoni mwa walimu katika kuwafelisha wanafunzi jeuri wasiokubali kutoa penzi kwa walimu hawa wakware, na cha kushangaza hata walimu wa kike ambao ndio wangekuwa msaada kwao lakini hali haiko hivyo nao wanashirikiana na walimu wa kiume kuwakandamiza wanafunzi wa kike.

Ingawa amefanikiwa kumaliza na kufaulu lakini haikuwa rahisi sana kwani ilimlazimu kurudia masomo mawili zaidi ya mara mbili ili kuweza kufaulu. Naamini wote mtakubaliana na mimi kuwa unyanyasaji wa kijinsia upo sana, na sio tu kwenye Elimu bali pia kwenye ajira kuanzia serikalini hadi kwenye sekta binafsi kote huko hapafai kumechafuka ile mbaya.

Swala hili limekuwa ni gumu kushughulikiwa kisheria kutokana na matukio mengi ya namna hii kutoripotiwa katika vyombo vya dola kutokana na kwanza Polisi wetu kutoyapa uzito unaostahili matukio ya namna hiyo na pia waaathirika kuona aibu kuripoti juu ya udhalilishwaji wanaofanyiwa kwa kuhofia swala hilo kuripotiwa kwenye vyombo vya habari na hivyo kuogopa kuchekwa na jamii. Tatizo lingine ni mazingira ya kupatikana kwa ushahidi wa kutosha wa kuwatia hatiani wahusika kutokana na vitendo hivyo kufanywa kwa usiri mkubwa.

Inapotokea mwalimu anamfanyia mwanfunzi wake vitendo vya unyanyasaji kijinsia au kumbaka, inakuwa ni vigumu kwa mwanafunzi kutoa taarifa kwa sababu anamuona mwalimu kama ndiye ameshikilia mustakabali wake wa maisha kielimu.

Kusema ukweli athari ni kubwa sana kuliko tunavyofikiria kwa sababu wanafunzi wengi wa kike wanaathirika kwa kupata ukimwi, au maradhi mengine ya zinaa au kupata ujauzito na kuachishwa shule, na matokeo yake wanafunzi hawa huumia ndani kwa ndani na kupata matatizo mengi ya kiakili.

Hata wakuu wa shule au vyuo vyenye unyanyasaji huu wa kijinsia wakiulizwa mara nyingi hukanusha vikali kuwepo kwa tatizo hilo katika shule zao au vyuo vyao, zote hizo zikiwa ni juhudi za makusudi kulinda umaarufu wa shule au chuo husika.

Hebu muulize mwanamke yeyote wakiwemo wale ambao wanashikilia nafasi za juu serikalini kuhusu jambo hili, kama hutashangazwa na kile utakachosikia kutoka kwao, utakuta kama hawakukutana na udhalilishwaji wa kijinsia walipokuwa shule ya msingi, sekondari au chuoni basi itakuwa ni katika ajira, kote huko hapafai, hali ni mbaya kweli kweli. Sasa sijui na hili gonjwa la ukimwi, tutapona kweli?

Nilipoamua kujiajiri niliangalia mambo mengi na hili likiwemo, ingawa mimi haikunitokea kwa kiwango cha Farida lakini pia nilijikuta nikiwa na wakati mgumu wakati fulani, nikitakiwa rushwa ya ngono ili nipate ajira ( rejea makala yangu ya
JAMANI HIVI HALI HII MPAKA LINI?)
Ukweli ni kwamba kuna aina nyingi za unyanyasaji wa kijinsia lakini nitaelezea aina tatu za unyanyasaji wa kijinsia ambao ndio ulioshika kasi hapa nchini.

Aina ya kwanza ni unyanyasaji wa mwanamke kuombwa rushwa ya ngono. Hapa mwanamke analazimika kumkubali mwanaume ili apate haki yake. Kwa maana kwamba mwanaume ananufaika kwa kumpata mwanamke ili amsaidie kupata huduma fulani ambayo ni haki yake.
Aina ya pili ni ile ya kumnyima raha mwanamke kwa kumnyanyasa mara kwa mara au hata kumpa adhabu isiyostahili kwa kosa dogo , kwa sababu tu alimkataa mhusika kimapenzi.
Aina hii hutokea sana mashuleni na vyuoni, na hii inawaathiri sana wanafunzi wa kike kisaikolojia, kwa sababu uwezo wao kimasomo unashuka na wakati mwingine kushindwa kuendelea na masomo.
Aina ya tatu ni ile ya kumtomasatomasa, kumbusu, kushika sehemu za siri au hata kumfanyia mwanamke vitendo vya kimapenzi bila ridhaa yake. Vitendo vya namna hii mara nyingi vinafanyika kama utani, hasa huko maofisini.
Mara nyingi mwanamke anayefanyiwa vitendo vya namna hii asipoonesha kukerwa ndivyo mhusika atakavyoendelea kumfanyia vitendo vya udhalilishaji zaidi, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kumfedhehesha ndani ya jamii .
Unaweza kushangaa kuona kwamba miongoni mwa waathirika wa unyanyasaji wa aina hii ni wake za watu ambao wameshindwa kujistahi kwa kutoweka mipaka ya utani. Unyanyasaji wa aina hii unaweza kuepukwa kabisa kama sio kukomeshwa kabisa iwapo tutaweka mipaka ya utani.
Kujistahi ni jambo la heshima sana na mwanamke yeyote anayeweka msimamo wake wazi kwa kumkemea mwanaume yeyote anayejaribu kumfanyia vitendo vya udhalilishaji wa aina hii, bila kujali kuwa ni mwalimu wake au mkubwa wake kikazi, anakuwa anajijengea heshima kubwa.

5 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Koero; mfumo dume bado unatawala. Kusema kweli mtoto wa kike anazo changamoto nyingi mno kwani tangu akiwa mdogo ipo mijibwa imekenua meno tayari tayari kumuuma na kumharibia maisha yake. Kuna wakati hata huwa namshukuru Mungu kwa kuniumba mwanaume! Nitatoa mifano michache tu hapa. Kwa tuliopita JKT tunajua mambo ambayo dada zetu walikuwa wanakumbana nayo kule kutoka kwa maafande wakorofi waliosoma sana na kutembea mpaka Egypt na Misri. Mimi niliapa kwamba kama ningekuwa na mtoto wa kike au dadangu KAMWE nisingemruhusu aende JKT. Halafu nenda katika vyuo vyetu. Katika nchi nyingi vyuo vikuu ndiyo chimbuko la fikra mpya na mitazamo mipya katika jamii. Katika vyuo vyetu vingi mambo ni kinyume kabisa. Maprofesa ni miungu watu na wanachokitaka lazima wakipate. Vinginevyo kuna "kushikwa" na hata "kudisko" Ungebakia chuoni mwenyewe binafsi ungekumbana na changamoto hizi kama ulikuwa bado. Cha ajabu ni kwamba kama ulivyosema kila mtu anajua kuhusu mambo haya lakini hakuna anayeyasema wazi. Kwangu mimi hata mabinti pia nawavisha lawama. Niliyoyaona wakati nikiwa chuoni ni kwamba mabinti wengine tamaa zimewazidi na wanataka maisha ya kiwango cha juu wakati wametoka katika familia za kikulima. Tamaa za kupata TV kubwa, masystem ghali ya muziki, simu za bei mbaya, majiko mazuri na wapenzi wenye magari watakaowaokoa na daladala kunawaponza mabinti wengi sana. Kuna waliokuwa wakiahidiwa kubakizwa kama ma-TA hata kama walikuwa bongo lala, kuna waliokuwa wamepangishiwa vyumba n.k. Kama kweli wangesimama kidete na kukemea unyama huu kwa umoja naamini mambo pole pole mambo yangebadilika. Kutokana na ujasiri ulio nao sidhani na wala nisingetegemea kwamba Koero Mkundi "ninayemfahamu" na kumsoma katika blogu hii angekubali kufanyiwa ukware na maprofesa ambao wengi wao wanaweza kuwa hata mababu zake kwa sababu tu eti ya MAKSI!!!

Farida, ulilofanya ni jambo jema na umeilinda heshima yako kama binadamu na binti mwenye hadhi. Kama asemavyo Da' Mija - wewe ni mwanamke wa shoka!

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli inasikitisha sana kuona wanawake/mabinti jinsi tunavyonyanyaswa. Nakubaliana na matondo kwa sisi wanawake/mabinti wakati mwingine tamaa zinatuzidi mno. Lakini pia kwa nini wanaume hawatosheki, Nina maana hao walimu, mabos,maprofesa kwa nini wasiridhike na wake zao.Basi nao pia wana tamaa.

Albert Kissima said...

Kama alivyoongelea Masangu na dada Yasinta kukandamizia, kina dada wengi wanaponzwa na tamaa.Mimi naamini kuwa kida dada wote wa vyuo wangekuwa na msimamo mmoja, unyanyasaji huu kwa kiasi kikubwa ungeweza kukomeshwa

Bila shaka Farida alijitetea yeye kama yeye, tujiulize, ni wenzake wangapi walioathiririka na ukware kama huu? labda kwa kufukuzwa chuo,kubebeshwa mimba, kuambukizwa ukimwi na magonjwa ya zinaa? Hakika kulingana stori hii, ni wengi wamekutwa na kati ya niliyoyaainisha hapo juu.

Farida aliwezaje kukabiliana na hali hii na wengine washindwe?

Koero,Farida,wanawake wote pamoja na wanaume wote hali hii ya unyanyasaji tunaiona, tusiilazie damu, kila mmoja atafakari ni kwa namna gani hali hii itakomeshwa.Tusiishie tu kutoa maoni mazuri ambayo hayatawekwa kivitendo.

Wito wangu kwa kinadada/wanawake/mabinti wawe imara ktk hili ikiwezekana waweke mitego ambayo itawaweka hadharani wakware hawa,mitego kama ile inayotumiwa na "takukuru"
kwani hata unyanyasaji huu ni rushwa ya kimapenzi.

Mzee wa Changamoto said...

Justine Kalikawe aliwahi kuimba akisema "chanzo cha tatizo ndilo tatizo. Ukijua chanzo cha tatizo utapata ufumbuzi wa tatizo". Nakubaliana naye kwa asilimia zote. Lakini nakubaliana naye nikiamini katika UMOJA. Yaani najua kuwa ile "divide and rule" ndiyo inayowaponza wengine. Kuna mabinti ambao wanafahamika kwenye taasisi hizo kuwa wao ni watu wa starehe na sherehe na bado wanafaulu. Si kwa kusoma sana, bali kwa kutoa hiyo rushwa ya mwili. Kwa hiyo hawa ni miongoni mwa chachu za kuendekeza fikra hizi na inakuwa na itakuwa vigumu kuwasihi kinadada kuwa na msimamo mmoja kupinga hili maana wale wapenda starehe na maksi nzuri hawawezi kuungana nao. Lakini kama tujuavyo kuwa SI KILA MAKUBALIANO YANAHITAJI KURA ZOTE. Kwa hiyo wakiwa wengi wenye msimamo na kusaka njia halisi za kutatua, hakuna shaka kuwa litafika kikomo.
Pole kwako Farida na wote mkumbanao nayo.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

najiulizaga maswali mengi juu ya maisha yetu na maisha ya dada zetu na kunyanyaswa.

silielewi sana hili la manyanyaso ya kijinsia. "niliawahi kuambiwa kuwa simuheshimu mwanamke, nilishangazwa na shutuma hizo. yaani mtu ninayeweza kumvulia nguo unaniambia simuheshimu? mbona simvulii mama, baba, wewe, nk lakini namvulia mwanamke? naheshimu basi"

anasema bwana cholaje wa tabata dsm

tusiitafute weak point bwana hizo zote ni changamoto za maisha kuwa sisi kama wanawake tunatamaniwa, tunapendwa na tuepuke vyema bila kujiona disadvantaged