Wednesday, April 15, 2009

ONGEZEKO LA WATU NA UHARIBIFU WA MAZINGIRA- SEHEMU YA PILI

Eti tunaambiwa tusizaane!
Wiki mbili zilizopita nilizungumzia ongezeko la umasikini duniani, na niliahidi kuwa nikipata muda nitajadili kuhusu ongezeko la watu na uharibifu wa mazingira duniani.

Makala hii ni muendelezo wa makala ya kwanza, bofya hapa kuisoma.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, inaonesha kuwa kwa wastani, kila sekunde moja wanazaliwa watoto watano hapa duniani, na wakati huo huo watu wawili wanafariki dunia, achilia mbali zile mimba zinazoharibika.

Maana ya tofauti hiyo kati ya vizazi na vifo ni kwamba watu watatu wanaongezeka duniani kila sekunde moja. Ukizidisha idadi hiyo utagundua kwamba kuna ongezeko la watu 11,000 kwa saa na watu 265,000 kwa siku na hii inafanya dunia kuwa ongezeko la watu milioni 100 kwa mwaka.

Hivi sasa dunia ina watu wapatao bilioni 6.7. Mwaka 1750 kulikuwa na watu milioni 800 tu duniani. Kufikia mwaka 1850 idadi iliongeka na kufikia watu bilioni 1.8.
Mwaka 1950 idadi ya watu ikawa bilioni 2.5. Ilichukuwa miaka 50 idadi ya watu kufikia bilioni 6 yaani mwaka 2000. Inakisiwa kwamba mpaka kufikia mwaka 2010 idadi ya watu hapa duniani itafikia watu bilioni 7, ikiwa ni ongezeko la watu bilioni 1 kwa muda wa miaka 10.
Ukiangalia mtiririko wa takwimu hizo utagundua kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kwa kasi hapa duniani kuanzia karne ya 19.

Kwa mfano nchi yetu ya Tanzania iko chini ya kiwango cha ongezeko la watu hapa duniani ukilinganisha na nchi nyingine zilizoko dunia ya tatu.
Tanzania ina ukubwa wa eneo la mraba mita la 342,100, karibu sawa na Misri ambayo ina ukubwa wa mita za mraba 384,300.

Pamoja na kwamba tofauti ya ukubwa kati ya nchi hizi mbili ni ndogo sana lakini Tanzania imezidiwa kwa idadi ya watu karibu mara mbili na Misri. Kwani wakati Tanzania ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 38, Misri ina idadi ya watu wapatao milioni 71.

Ikiwa utaiunganisha Tanzania na nchi ya Benin iliyoko Afrika Magharibi ukubwa wake utalingana na nchi ya Misri, kukiwa na tofauti ndogo sana. Ukijumlisha idadi ya watu wa nchi ya Benin wanaokadiriwa kufikia milioni 7 na idadi ya watu wa Tanzania unapata idadi ya watu wapatao milioni 45, ikiwa bado ni chini ya idadi ya watu wa nchi ya Misri.

Hii inaonesha bado nchi hii ina kiwango kidogo sana cha idadi ya watu ukilinganisha na nchi nyingine zilizo katika dunia ya tatu.
Kwa hiyo sioni sababu ya serikali yetu kupiga kelele sana kuzuia watu wasizaane, Je tunataka hayo mapori yaliyoenea hapa nchini wakae kina nani?

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, imekadiriwa kwamba watoto milioni 1.6 huzaliwa kila mwaka hapa nchini. Na kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na wizara ya afya zinaonesha kwamba watoto wanaosajiliwa ni 140,000 kila mwaka ikiwa ni asilimia 10 tu ya watoto wanaozaliwa, hii inaonesha kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wanaofia tumboni, na wale wanaofariki baada ya kuzaliwa inakuwa haijachukuliwa na kuingizwa kwenye takwimu za serikali.
Hata hivyo inakadiriwa kwamba watoto wapatao 51,000 hufariki baada ya kuzaliwa hapa nchini, na wakati huo huo 43,000 hufia tumboni kila mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu hizo inaonesha kwamba bado tunayo safari ndefu ya kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa hapa nchini, kabla hatujaanza kupiga kelele ya watu kuzaa kwa mpango.

Ni hivi karibuni tumesikia Nchi ya Australia ikipiga la mgambo kuwaalika wahamiaji ili kujaza mapori yaliyo matupu.

Unajua sababu ni nini?

Wenzetu wamepambazukiwa na kung’amua kwamba watu ni rasilimali kama nguvu kazi ikitumika vizuri.
Wakati sisi tunapiga kelele watu wasizaane, wenzetu wanapiga kelele wahamiaji waende wakaijaze nchi, hapa napata kizunguzungu.

Hata hivyo chapisho hilo linabainisha kwamba mataifa makubwa yameanza kuonesha wasiwasi juu ya ongezeko la watu hapa duniani.
Mataifa hayo yanadai kuwa ongezeko la watu linasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, na hivyo kutishia dunia isiwe salama.

Kwani kumekuwa hakuna udhibiti wa kutosha kiasi kwamba watu wamekuwa wakitawanyika kwa ajili ya kutafuta makazi na hivyo kuvamia maeneo ya misitu ya asili na vyanzo vya maji na kufanya uharibifu mkubwa mkubwa wa mazingira.

Imebainika kwamba iwapo watu hao watasogezewa miundo mbinu kama vile Barabara, shule, hospitali, na huduma mbali mbali za kijamii, ina maana ya kuhalalisha uharibifu wa mazingira.

Pia wataalamu hao wanadai kwamba ongezeko la watu haliendi sambamba na ujenzi wa miundo mbinu ambayo itasaidia kulinda uharibifu wa mazingira.

Labda niwaulize ndugu wasomaji, hivi nchi masikini na zile nchi tajiri zenye viwanda ni zipi hasa zinazoifanya dunia hii isiwe salama? Wao wana viwanda wanazalisha sumu kila uchao huku wakitulisha vyakula na madawa yenye sumu ili kujikusanyia utajiri, halafu leo wanasema kuwa nchi masikini ndizo zinazochangia uharibifu wa mazingira na kuifanya dunia isiwe salama, huu ni uonevu wa hali ya juu.

Hebu tuangalie upande mwingine wa shilingi wa kadhia hii.
Kuzungumzia ongezeko la watu, unazungumzia ongezeko la soko, kwa maana ukuaji wa biashara, nguvu kazi, na ongezeko la viwanda, na hivyo ukuaji wa uchumi kuongezeka. Kwani kwa jinsi idadi ya watu inavyozidi kuongezeka na ndivyo uchumi unavyozidi kukua, hebu angalia nchi kama ya China, India, Marekani na iliyokuwa Urusi kabla haijasambaratika, ukuaji wa uchumi katika nchi hizo ulitokana na kuwa na idadi kubwa ya watu.
Ila naomba nitahadharishe kidogo hapa, ninapozungumzia ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi nazungumzia nchi kutumia nguvu kazi katika kuzalisha na kuwa na serikali makini inayowawezesha wananchi wake kufikia malengo yao na sio watu kuwa wavivu wakisubiri kila kitu kifanywe na serikali.

Naomba nikiri kwamba aina ya maisha tunayoishi hapa nchini hatuwezi kupiga hatua kimaendeleo hata kama kukiwa na ongezeko la watu. Watanzania tu-wavivu mno kiasi kwama tunashindwa kutumia fursa zilizopo na matokeo yake wageni ndio wanaozichangamkia, huku sisi tukibaki kuwa watazamaji.

Wengi tunapenda njia za mkato katika kujiletea maendeleo na ndio maana vitendo vya rushwa na ufisadi vinaiyumbisha nchi.
Kama tunataka maendeleo ya kweli yatupasa kubadili namna yetu ya kufikiri, la sivyo tutazaana na kujikuta tukibaki kuwa ombaomba ndani ya nchi yetu.

Katika kipindi hiki ambacho dunia imetikiswa kutokana na kuyumba kwa uchumi duniani, inabidi kila mtu ajiulize afanye nini ili kujiletea maendeleo na sio kukaa na kulalamika na majungu, haitatusaidia zaidi ya kupoteza muda huku dunia ikiendelea kusonga mbele kwa kasi ikikuacha ukiwa umesimama.

8 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Rasilimali. Hapo umenena. Angalia Botswana wanavyotumia mifugo na maji kujinufaisha. Tatizo kwetu ni kuwa tuna tofauti ya efinition ya rasilimali. Wakati zinasemekana kuwa za umma, zatendeka kama za watu binafsi.
Ntarejea nikijaaliwa

Yasinta Ngonyani said...

Tukiacha kuzaana sasa itakuaje?

Simon Kitururu said...

Nchi nyingi zilizoendelea zina mfumo ambao unahitaji daima kuwe na damu mpya ya kuuendeleza hasa kama watakaostaafu wataendelea kufaidika na pensheni zao. Kwa hiyo kwa wana demogarafia hujaribu kuhakikisha kuwa wazee wanapostaafu kuna vijana wanao kuja kuendeleza kazi ili kuendelea kufanya mfumo uruhusu wazee kustaafu na kuhudumiwa. Kwa hiyo kama vijana na nguvu mpya haipo ni lazima tu watataka wahamiaji watake wasitake.

Kuhusu tuzaliane ili kujaza mapori mie naamini ni mtazamo tu wa kibinadamu wa kuamini dunia ni ya binadamu pekee. Nahisi mapori ni muhimu pia yabakie mapori kama si lazima binadamu wajazane huko.

Ngojea nirudie kusoma tena Part 1 ya hii article ili ni kae mkao wakuendeleza hoja.
Baadaye!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aisee . watu wenine bwana!

wao walizaliwa, wakaishi sasa wanaona nongwa kuzaliwa kwa wengine. binadamu wa leo amekuwa mchoyo mno kiasi cha kutaka kuhodhi vitu hata asivyohitaji ndio maana analilia raslimali!.

maumbile (Mungu?) yanajua jinsi ya uridhisha viumbe vyake wawe watu au wanyama.ebu fikiri, kuongezeka kwa wanyama kama vile ngombe, kunguru, mbuzi nk, sio tishio lakini binadamu ni tishio, anamtisha nani?

taizo ni ujinga wa kujifanya kujua kila kitu. tuna viwanda vya siraha vya kuuuana na kuchafua mazingira. angalia vita siku hizi kama za marekani kule Iraq au afganistan, hawapigi watu kama Osma, bali wanapiga na kuharibu kila kitu. wakifyatua bomu, wanaua watu, wanyama, wadudu, miti, majani na ardhi yenyewe. ni uchizi unaoleta matatizo haya ya kujifanya wajuaji wakati tunajiua sis wenyewe.

Ongezeko la watu sio tishio lingekuwa tishio hao wanaojiita wataalamu basi wasingezaliwa au wangeuwawa ili kupunguza tatizo.

MARKUS MPANGALA said...

Hakuna nchi zilizoendelea wala zile zinazoendelea, kama vipi waache ugunduzi wa vitu au kitu chochote wanachokiona kianleta sura mpya ya jamii yao.

jamii hubadilika kila leo hakuna ambaye anaweza kusema kwamna jamii hii ni ya nchi zilizoendelea au hizi ni zile zisizoendelea. WAMETUDANGANYA SANA SASA INATOSHA.

kwanini tumekuwa masikini kila leo, kwanini tupo katika hali hii kama tunaweza kubadilika wenyewe bila wao.

JIKOMBOE< MAPINDUZI YA KWELI ANZA HAPO ULIPO

VUKANI JAMANIIIIIII

Bennet said...

Mimi kama mwana mazingira hii mada imenigusa sana, nchi kama yetu Tanzania haina haja ya kupunguza kuzaliana ila watu wafuate uzazi wa mpango ili kulinda afya ya mama na mtoto.
Tatizo kubwa ni jinsi ya kutumia rasilimali zetu na kuziendeleza, mfano miti tunaikata tu wakati hatupandi mingine.
Mfano mwingine ni mifugo, nchi yetu ni ya 3 Afrika kwa wingi wa mifugo lakini sisi wenyewe hatuli nyama kwa kiwango kinachotakiwa na nyama ni ghali sana (kilo tsh 4000 = na dola 3)
Cha muhimu ni kulima chakula kingi na kufuga sana kisha tuendelee kuzaliana tu madhali uwe na uwezo wa kulea watoto wako.

Mwanasosholojia said...

Vukani, makala yako imenigusa!Nakubaliana kwa mapana na marefu juu ya hoja unazozijenga. Ni kweli tuna matatizo, lakini naomba kidogo nitofautiane na kifungu hiki katika makala yako...nanukuu.."Watanzania tu-wavivu mno kiasi kwama tunashindwa kutumia fursa zilizopo na matokeo yake wageni ndio wanaozichangamkia, huku sisi tukibaki kuwa watazamaji"..mwisho wa kunukuu. Natofautiana vipi na kifungu hiki?

Pamoja na kuchukulia kwa ujumla kuwa watanzania tu- wavivu mno, mimi nafikiri hii ni "generalization" ambayo inasahau kuwa miongoni mwa watanzania wapo wachapakazi thabiti lakini mfumo uliopo (wa kuwakaribisha wageni- wanaoitwa wawekezaji) unaziba uwezekano wa watanzania hao kuendelea. Tunayo rasilimali watu na hata mawazo ya maendeleo, tatizo ambalo naliona ni kuwa uhusiano wa kizalishaji (relation of production)unaamriwa na wamiliki mali (owners of means of production)ndani ya mfumo wa kinyonyaji (exploitative system). Ni vigumu sana kwa mtanzania huyu mwenye mawazo na nia ya kuendelea kujikwamua kutoka katika mfumo huu akiwa peke yake. Inahitajika nguvu ya pamoja na wenzake ambao tayari wanapaswa kuwa wameng'amua ukweli (wana true consciousness). Mara nyingi huwa nasema, sisi hatumjui adui yetu wa kweli. Tunadhani kuwa umasikini ndio adui yetu wa kweli!Lakini umasikini unaletwa na nini?Uvivu?Uzembe? au mfumo kandamizi na wa kinyonyaji?Jambo hili ni la kihistoria, na kila siku linabadilisha shape na majina. Kulikabili inabidi tuanze kwanza kuuvunja mfumo huu, hapo tukiweka juhudi hata umasikini hatutausikia tena!

Pole kwa kuwachosha kwa falsafa hizi, lakini nawasilisha!

Koero Mkundi said...

Dada Koero, Nimeshindwa kuweka maoni yangu nadhani mtandao haukuwa mzuri
sana huku danganyika kama huko kwenu tanzania!! Naomba unisaidie kuyaweka
hewani.

Chacha
================
Bandugu, hii habari ya kupunguza idadi ya watu mimi inanishangaza na kwa
kweli kwa kuwa wengi wetu (hasa viongozi wetu) si wafukunyuzi wa haya
masuala kiasi kwamba wanakubali tu blindly kwa kila kitu wanacholetewa na
hao baba zetu walioko ulaya .

Suala la udhibiti wa watu lilianza October mwaka 1916 na mwanamke aitwaye
Margaret Sanger (mwanzilishi wa IPPF) ambaye alikuja na hoja ya 'kila mtu
anayo haki ya kufanya mapenzi' na hivo kuleta kitu kinachoitwa 'sex
education program'. Hii program ya huyu mwanamama mwendawazimu ndiyo
ilianzisha IPPF ambaye kuwadi wao hapa Tanzania ni UMATI (kwa wanaojua
kiswahili kuliko mie mkurya watajua kuwa umati maana yake ni nini lakini
wanachofanya ni kinyume).

Hatua ya pili ya IPPF ilikuwa birth control. Mlolongo wa haya mambo
yalifuata hivi:sex education, birth control, safe abortion for hard cases
and safe abortion for everyone. Wote mnajua stage tuliofikia kati ya hizo
hapo juu.

Mbinu za IPPF/UNFPA katika kuhalalisha uharamia huu ni:
1. contraceptives lowers the no of arbortions
2. vitanzi, vidonge n.k are not arbortions
3. Family planing saves money
4. over population problem
5. Sex education reduces teens pregnancies!
6. safe sex

Hayo ndo yanapiganiwa na IPPF na makuwadi wao akina Marie Stoppes ambaye
naye ana nadharia ya kuondoa kizazi kibaya na kuleta kizazi chema duniani.


Dada Koero, umeongelea kipengele cha 4 cha hawa maharamia wa ulimwengu cha
tatizo la idadi ya watu. Umejaribu kuweka takwimu mbalimbali kuhusiana na
jambo hili. Tunakushukuru kwa hilo. Nami naongezea upande wa pili wa
shilingi kukataa uongo wao kuwa dunia inajaa watu. Tuchukuwe mfano wa
takwimu za mwaka 1995. Kulikuwa na watu 5.75 bilioni. Tukichukulia pia
familia ya huko pwani kwenu (siyo kwetu ukuryani) yenye watu 6 (baba, mama
na watoto 4). Kwa mahesabu ya haraka haraka tufanye kuwa watu hawa
watahitaji nyumba yenye vyumba 5 na yenye ukubwa wa 22.86m x 27.43m (75ft
x90ft). Nyumba hiyo itakuwa na eneo la futi za mraba 6750 ama mita 627.05
za mraba.

Ulimwengu mzima (sijui ni dunia ama?) utahitaji nyumba 958,334,000 ambazo
zitajengwa katika eneo la futi za mraba 6,468,754,500,000) ama mita
600,923,330,000 za mraba ambazo ni sawa naeneo la maili za mraba 232,035
ama hekta za mraba 60,092,333.

1. Nchi ya Mexico ina eneo la maili za mraba 756,000
2. Peru ina eneo la maili za mraba 496,225
3. Venezuela ina eneo la maili za mraba 352,000
4. Jimbo la Texas (USA) lina eneo la maili za mraba 262,840
5. Jimbo la Alberta (Canada) lina eneo la maili za mraba 255,285

Tanzania mtajaza wenyewe.

Hii ina maana kuwa watu wote wa ulimwengu (dunia?) wa 1995 wangeweza
kusundikwa mexico mara mbili, na bado ardhi ikabaki kwingineko kwa ajili
ya kulima. Hizo nchi nyingine na majimbo niloyataja yanaweza
ku-accommodate watu wote na tukabaki na eneo lukuki la kulima viwanda nk.

Mbona hamuelewi ukweli huu? Kwanini mnang'ang'ania kusikiliza wendawazimu
wa ulaya? Siongei kwa sababu ni mkurya napenda kuoa wake wengi na kuzaa
watoto wengi bali kutokana na ukweli kwamba hawa mumiani washatuona siye
hatuna akili za kutosha. Mwl. Nyerere alisema' mtu akikushauri jambo la
kipumbavu, na wewe unajua ni la kipumbavu ukalikubali, basi atakuona wewe
hamnazo'.

Koero, umesema kuwa Australia inataka watu. Sombeni wamachinga muwapeleke
huko basi!!! Nimesikia kuwa Ujerumani inahamasisha watu wake kuzaa na
ukirogwa ukazaa mtoto anakuwa si wako tena bali wa state...atalipiwa kila
kitu na wewe mwenyewe utalipwa.

Nimalizie kwa maneno haya ya Mother Thereza 'A nation that destroys the
life of an unborn child who has been created for living and loving, who
has been created in the image of God, is in tremendous POVERTY'

========
Chacha Benedict Wambura
P.O. Box 854
Musoma Mara Tanzania
Tel/Fax: +255 28 2620 575
Mobile: +255 787 945 414, +255 713 235 146
Email: info@foundationhelp.org
Website: www.foundationhelp.org