Saturday, June 26, 2010

KINJEKITILE NGWALE NA HISTORIA YENYE UTATA!

Kulikuwa na mateso na kulimishwa kwa nguvu.

Leo katika kupekua kwangu mtandaoni, nimekutana na historia mbili tofauti zinazomzungumzia Kinjekitile. Kilichonivutia hadi kuamua kuwashirkikisha wasomaji wa kibaraza hiki ili tutafakari kwa pamoja ni kutokana na kupingana kwa historia hizo.

Wakati historia moja ikihoji kuwa Kinjekitile alikuwa shujaa au mshirikina? ambayo iliandikwa na mwandishi Aloyce Menda katika gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 21,2006, nyingine ilikuwa ikidai kuwa historia yake imepotoshwa, ambayo nayo iliandikwa na mwandishi Evaristy Masuha katika gazeti hilo hilo la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 21, 2008.

Kwa historia hizo mbili kunaonekana kuwa na walakini na ni vyema historia hii ikawekwa sawa kwa manufaa ya vizazi vijavyo, la sivyo tutajikuta tukiwa tumepoteza kumbukumbu hii muhimu kwa vizazi vyetu.

Naomba tuwekane sawa katika swala hili, Je ni yupi yuko sahihi kati ya waandishi hawa wawili?

***************************************

KINJEKITILE - Jemedari shujaa kweli au mshirikina laghai tu?

Na Aloyce Menda

Ijumaa, Septemba 21,2006


'Wakoloni wa Kijerumani waliita Vita ya Majimaji kuwa ni uasi wa Majimaji au Majimaji Rebellion kwa Kiingereza. Kwa Wakoloni, Kinjekitile alikuwa mhaini aliyekuwa anapinga utawala halali. Kwa dhana hiyo, Kinjekitile alikuwa shujaa kwa kupigania uhuru wa watu waliokuwa chini ya ukoloni.

Lakini kwa kutazama kwa kina mbinu za ukombozi alizotumia kupigania huo uhuru, sioni ushujaa wake. Vitabu vya historia vilivyoandikwa na wakoloni na hata vya wazalendo vinaonyesha wazi kwamba Kinjekitile alilaghai mamilioni ya watu wasioelimika, kwamba risasi za moto kutoka katika magobore ya askari wa Kijerumani zinaweza kugeuzwa maji na kuishia kulowesha tu miili yao bila madhara yoyote.

Kinjekitile alilaghai watu kwamba yeye anafahamu sayansi ya kijadi itakayotumiwa na ‘watu wake’ katika vita dhidi ya Wajerumani na kushinda. Sayansi yenyewe aliifundisha yeye mwenyewe kilaghai na kuisambaza kutoka Kilwa hadi Songea.

Watu wengi wakapotoshwa na kuamini kwamba risasi za moto zitageuka maji katika vita, kasha wakahamasishwa kuanzisha vita bila kujiandaa kwa mbinu nyingine za ziada! Silaha zao za jadi zilikuwa ni mawe, marungu, mundu, pinde, mishale na mikuki butu. Hatari iliyoje hiyo!
Kinjekitile mwenyewe hakwenda mstari wa mbele katika vita halisi, wala hakudiriki kusitisha mapambano alipoona maelfu ya ‘watu wake’ wakiteketezwa kwa risasi. Badala yake, alikaa mafichoni huku akiendelea kutuma wasaidizi wake kushawishi watu waamini ulaghai wake, na kwamba waliokuwa wanakufa kwa risasi hizo ni wale tu ambao hawakutimiza vyema masharti ya ‘sayansi’ yake aliyowapa.

‘Shujaa’ Kinjekitile alikuwa tapeli hatari sana kiasi kwamba, hakuwa na himaya maalumu ya kuishi, tofauti na walivyokuwa kina Chifu Mkwawa, Mtemi Mirambo and Mangi Sina. Bila shaka alikuwa anafahamu fika kwamba siku moja ulaghai wake utafikia mwisho, ambapo watu wangemgeukia na kumtoa roho yake, hivyo alijihami kabla kwa kuishi mafichoni kama afanyavyo gaidi Osama bin Laden hivi sasa.

Vita ilipokaribia mwisho wake kwa wazalendo wengi kufa kama sisimizi, Kinjekitile alitokomea pasipojulikana na hadi leo haifahamiki ‘shujaa’ huyo alizikwa wapi.

Mamilioni ya wazalendo kusini mwa Tanzania walikufa kwa njaa, maradhi na kukosa makazi baada ya vita hii. Wakoloni wa Kijerumani waliteketeza mashamba yao, mifugo na nyumba na kuhakikisha wanavunja misingi yote ya kiuchumi kama mbinu ya kujihami dhidi ya ‘maasi’ mengine.’

Unaweza kubofya hapa ili kuisoma historia hii kwa undani

Vita ya Majimaji: Historia iliyopotoshwa

Na Evaristy Masuha

Alhamisi, Agost 21, 2008


‘Leo napenda kuchimba zaidi ukweli huo huku nikijarijbu kutoa ukweli mwingine ambao utathibitisha historia hii huku nikiendelea kuwakumbusha Watanzania ambao watakuwa aidha wamesahau au hawakupata nafasi nzuri ya kuijua vita hiyo iliyokuja kujulikana kama “Vita ya Majimaji”.


Vita hiyo ilianza Julai mwaka 1905. Pigano la mwisho lilifanyika katika maeneo ya mpaka wa Tunduru na Masasi katika Kijiji cha Lusesule.

Mwaka 1907 wakati vita hiyo iliyokuwa kati ya serikali ya Wajerumani na Waafrika waliochoshwa na utawala wa suluba ikiendelea, Waafrika ambao walikuwa ni muungano wa makabila ya kusini hadi pwani ya Tanganyika, walikuwa wakipiga mishale na mikuki yao huku wakitamka neno ‘mashe’.

Neno hilo lipo kwenye lugha ya Kimatumbi ambalo tafsiri ya Kiswahili, ni ‘maji’, kama walivyoelekezwa na kiongozi wao hayati Kinjekitile Ngwale. Hiyo ndiyo iliyokuja kuzaa jina la ‘majimaji’.

Mwisho wa vita, Waafrika walishindwa vibaya na wengi wao kuuawa. Hapo ndipo historia ikaja kumtambua Kinjekitile kama kiongozi wa vita aliyewaahidi askari wake ushindi kutoka kwenye dawa aliyoamini ingeweza kubadilisha risasi kuwa maji, kitu ambacho hakikuwa kweli.

Historia hiyo tuliipokea na ndiyo tunayowafundisha vijana wetu na inatamka wazi kwamba dawa haikuwa kweli, kwani hakuna risasi hata moja iliyogeuka kuwa maji na matokeo yake Waafrika wengi walipoteza uhai wao.

Hapo ndipo nakosoa historia hiyo kulingana na mlolongo wa matukio yaliyofuatia hadi mwisho wa vita hiyo ambayo mwanzo ilikuwa ya ushindi mkubwa kwa Waafrika.

Historia hii ina tuambia kuwa Vita ya Majimaji ilianza mwaka 1905 Julai na mwezi mmoja baadaye yaani Agosti 24, mwaka 1905 Kinjekitile alinyongwa katika Kijiji cha Mhoro, Rufiji.
Tangu hapo wapiganaji wa Kiafrika wakaendelea kupigana bila kiongozi wao hadi Januari 1907.

Kwa mtazamo kama huo, tunaweza kupata picha ambayo itatufikisha katika ukweli wa historia ambayo walio kuwa na jukumu au uwezo wa kuhifadhi historia hiyo walilifanya makusudi kabisa ili tuamini kile walichokitaka wao.

Mwanzo wa Vita ya Majimaji huko Umatumbini ilikuwa ni mwendelezo wa vita ya muda mrefu kati ya utawala wa Wajerumani na Wamatumbi ambao walikuwa wamechoka kabisa kutawaliwa.

Hiyo ilitokana na Wajerumani walioingia kama marafiki, kugeuka kuwa wakatiili. Waafrika walichukizwa na kitendo cha kufanyishwa kazi katika mashamba ya Wajerumani kutwa nzima bila malipo.


Hali hiyo ilijenga chuki kati ya Waafrika na Wajerumani, hivyo Wamatumbi walianzisha vita iliyokuwa ya Mzungu na Mwafrika popote pale walipokuwa wakikutana.
Hali hiyo ilishtukiwa na Wajerumani na hivyo wakaamuru Wamatumbi wote kuepukana na asili yao ambayo ilikuwa ni kutembea na fimbo au mkongojo kwani ilikuja kugundulika kwamba, mikongoja hiyo ndiyo ilikuwa ikigeuka silaha dhidi ya Wajerumani.

Hiyo ilikuwa mwaka 1896, baada ya serikali ya kikoloni kuweka mkazo na sheria kali dhidi ya Mmatumbi yeyote anayepatikana akitembea na aina yoyote ya mti. Mwaka 1898, Wamatumbi wakagundua mbinu nyingine ambapo sasa maboga waliyokuwa wakilima zaidi kugeuka kuwa silaha.

Wamatumbi ambao kwa asili walikuwa watu jasiri sana, walianza kupambana na kila Mzungu waliyekutana naye kwa kumponda kwa boga. Vita hiyo ambayo inajulikana kwa Kimatumbi kama ‘Ngondo ya Mayawa’, yaani vita ya maboga.

Staili hiyo iliwashitua Wajerumani ambao sasa walianza kupambana na Wamatumbi kwa mtutu wa bunduki pamoja na sheria za kufungwa na wengine kuhukumiwa kunyongwa. Hapo tena Mmatumbi akawa amekubali kushindwa.

Kwa mtiririko wa matukio kama hayo ambayo sasa yalielekea kuwakatisha tamaa Wamatumbi, ndipo mzee hodari na mganga maarufu sana kwa ukanda huo, mganga aliyekuwa na mifugo mbalimbali nyumbani kwake, ikiwamo nyoka na samba, alisimama na kuwaahidi Wamatumbi kuingia katika vita aliyoiita vita ya ushindi.

Mzee huyu ambaye vitabu vya historia vinamtambua kama Kinjekitile, ukweli halisi wa jina lake aliitwa Kinjeketile, yaani kimeniitikia kwa lugha ya Kimatumbi.


Kwa mjibu wa imani ya Wamatumbi, mzee Kinjekitile aliyewarejesha Wamatumbi katika roho ya ujasiri kutoka katika roho ya kukata tamaa, alizama ndani ya Mto Rufiji na kuibuka baada ya siku mbili, akiwa na mizizi ya dawa hiyo. Hiyo ilikuwa mwaka 1903.’

Unaweza kubofya hapa ili kuisoma historia hii kwa undani.

6 comments:

Anonymous said...

Da' Koero sio historia ya Kinjeketile tu iliyopotoshwa. Kuna historia nyingi sana zimepotoshwa hapa nchini, tulichosoma huko mashuleni ni tofauti kabisa na ukweli halisi.......

Markus Mpangala said...

NILISOMA MUDA MREFU HII MADA. lakini nadhani Aloyce hajasema ni kitu gani kilichopotoshwa bali amesimamia kuhusu nomino za dhahania za ushirikiana na ulaghai. alitakiwa aseme ulaghai huu umefanyika kwa kiasi gani. na ushirikina ulifanywa kwa kiasi gani. lakini hana hoja ya kusema historia imepotoshwa. VINGINEVYO NAMTAKA AJIOME saikolojia kuelewa mantiki ya ulaghai na ushirikina anaoai ulifanywa na kinjeketile. nimesoma historia inayotaja kinjeketile ngwale kwahiyo kwa Masuha hakuna jipya sana kuhusu jina hilo. nampongeza Masuha kwa kutoa historia nzuri na ambao anadai imepotoshwa. huyu anastahili kusifiwa kw akile alichokusanya. lakini kwa kaka Aloyce sioni kitu zaidi ya hisia zisizo za kihistoria. alipaswa kueleza kwa kina kama ambavyo Masuha ametamka.

kupotoshwa kwa historia siyo vita ya majimaji BALI BIBLIA NAYO imejaa mambo mengi ya kipotoshaji ila nashindwa kuhukumu sana lakini wapagani waliingiza mafunzo yao na sasa yanaimbwa sana tu. vinginevyo mungu ajaibu hoja za kupotoshwa huko. yako mengi ndani ya biblia ambayo wengi wansadiki tu kwakuwa wanatishwa na wachungaji na walimu wao. ngoja niishie hapa halafu nimwambia kaka aloyce alete hoja siyo vioja. tena aende jumba la makumbusho pale songea akaona na kusimuliwa kisha apelekwe maeneo husika asiniletee vioja hapa

Anonymous said...

Mwe! Ndio maana watu wanaambiwa wasikilize simulizi za wazee wao zaidi kuliko simulizi za wazungu. Huyu Aloyce ndio wale wanaoamini kuwa mila na desturi zetu ni za kishenzi na ushirikina, na kuabudu vya wazungu. Laiti angepata exposure ya kuona ya wazungu, hivi karibuni walishiriki huko kwenye mawe ibada yao ya SOLASTICE, yaani siku ndefu ya Jua, wakiabudu jua je nao huu si ushirikina? Kinjekitile Ngwale alikuwa ni mganga tena aliyepewa uwezo wa ajabu na Mungu, Aloyce ajiulize kama alikuwa tapeli na watu wengi walikufa kwa nini vita haikuisha baada ya mwezi, badala yake iliendelea zaidi ya mwaka mmoja? Vitu vingine huhitaji kuwa genius kupata majibu yake, wajerumani walileta askari wa kukodiwa kutoka Sudan na Ethiopia kuwasaidia kupambana na uasi huo.

Kati ya askari hao wamo babu wa mama yangu pamoja na mjomba wake! Mjomba wa mama yangu ambaye ni marehemu babu yangu mimi alikufa mwaka 2000, na alikuwa anatupa simulizi nyingi sana za matukio hayo wakati wa hiyo vita yeye alikuwa teenager! Kwa hiyo mtu unapotumia kalamu kuandika jaribu kufanya kautafiti kidogo ama sivyo utajikuta unaandika vitu ambavyo watu wanashangaa hata hiyo tasnia ya habari umefikaje. Ndio maana BM anawaponda kila siku kwa kulipua bila kufanya utafiti wa kina!

Bi Mkora

Anonymous said...

Ni kweli kama wasemavyo wengine; wazungu waliandika historia yetu wakitumia Euro-centric approach. Wanahistoria wetu wanatakiwa waiandike kwa kutumia Afro-centric approach. Niliishi Kilwa mika 6 na nilipoongea na wazee wa Kilwa Kisiwani kuhusu Hassan bn Ally kwamba eti alikinunua kisiwa cha Kilwa kwa kutumia majora ya nguo toka kwa Lord of Kilwa (kama tulivyosoma ktk Short History of Tanganyika (kitabu cha mzungu fulani) wazee wale walinishangaa sana. Wakasema ulizeni sisi wazee tuwaeleze ili mkaandike upya. Wakanieleza mambo ya ajabu sana. Sina muda kwa sasa lakini mtu akitaka, tuwasiliane kwa email hii:p.kopweh.1@research.gla.ac.uk. Tunaweza tukajadil ikwa kirefu.

Abby Thabit said...

Kweli kabisa.

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___