Sunday, July 4, 2010

TAFAKARI YA LEO: WALIPOKUTANA WANABLOG HAWA, JE WALIPANGA AU ILIKUWA NI NASIBU TU?

Walipanga au ilikuwa ni nasibu tu?

Ilikuwa ni siku ya Jumamosi May 15, 2010, pale katika Hoteli ya Kimataifa ya nyota tano iitwayo Movenpick Royal Palm, ndipo mahali ambapo wanablog hawa walikutana.
Kusema kweli sijui hata mpango wa kukutana kwao uliandaliwa vipi, ila katika hali ya kustukiza kupitia kibaraza cha kaka Fadhy tukajulishwa kwamba wanablog wamekutana pale Movenpick. Unaweza kubofya hapa kujikumbusha

Ulikuwa ni mwanzo mzuri na nilidhani kwamba milango itakuwa imefunguliwa kwa wanablog kukutana na kubalishana uzoefu hasa pale itakapotokea wale walioko Ughaibuni wanaporejea nyumbani.

Siku za hivi karibuni nikapata habari kuwa wanablog wenzetu walioko huko ughaibuni wako hapa nchini. Habari ambazo sijadhibitisha kwa kuwa hazina vyanzo maalum ni kwamba, Profesa Mbele alikuwepo au bado yupo hapa nchini, na pia Godwin Meghji naye yupo hapa nchini, vile vile Profesa Matondo naye nasikia yupo hapa nchini na inasemekana baada ya kukaa hapa Arusha kwa siku kadhaa ameelekea Shinyanga kuwaona wazazi wake. Sina uhakika kama bado yupo au kesharejea huko ughaibuni.

Ni bahati mbaya kwangu kuwa sikupata bahati ya kukutana naye alipokuwa hapa Arusha kwa kuwa nilikuwa huko milimani upareni nilipokwenda kumuona bibi yangu Koero ambaye alikuwa ni mgonjwa.

Niliporudi Arusha nikawa kila siku najaribu kusoma mitandao mbali mbali hususana vibaraza vya kaka Fadhi Mtanga, Chacha o’Wambura Ng’wanambiti na kaka Chib bila kusahau kibaraza cha kaka yangu Shabani Kaluse, nikitarajia kuziona sura za wanablog hawa pamoja na ugeni huu wa wanablog wenzetu kutoka ughaibuni, lakini mpaka leo sijapata taarifa rasmi kama wanablog hawa walikutana ama la.

Ni jana usku nilipokuwa nimejipumzisha nikitafakari juu ya ukimya wa blog zetu hizi hasa katika kipindi huki muhimu cha kuelekea uchaguzi mkuu, na ndipo nikawa najiuliza hivi kukutana kwa wanablog hawa pale Movenpick lilikuwa ni jambo la kupangwa au ilikuwa ni nasibu (Coincidence) tu?

Bado natafakari………..

7 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nadhani ilikuwa bahati nasibu tu! Ngoja nami nije nikutane na mtu..lol

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Mama Mchungaji hongera kwa kuuliza swali swali zuri!

Ukweli ni kuwa mambo mengine huwa hatuvipangi ila vinajitokeza automatically!

Mimi nimekutana na Prof. Matondo Arusha na kuteta naye kwa muda wa masaa kadhaa.

Labda papaa Fadhy atajibu.

Inaonekana una wivu sana ama gubu...lol!

Christian Bwaya said...

Kama walienda pale kila mtu kwa wakati wake bila kujua nini kinaendelea bila mawasiliano yoyote, ila tu wakajakugundua kuwa wanafahamiana; basi hiyo ilikuwa bahati nasibu.

Ila kama kuna juhudi zilifanyika hata kwa 'kubipiana' tu kutafutana, basi nadhani ulikuwa ni mkakati wa makusudi kukutana na uliofanikiwa.

Ushauri wangu ni kwamba mfano waliouonyesha wenzetu hao, tuuige. Tuanze kutafutana na kubadilishana mawazo uso kwa uso. Inapendeza ati!

MARKUS MPANGALA said...

Muwe mnauliza kwanza.Ninachoajua ni kwamba kila kitu kiliandaliwa na watu wawili yaani Shaban Kaluse na mtani wangu Fadhy Mtanga. Kwahiyo mkisema ni bahati mbaya ni lazima tujiulize ilikwuaje hata Yasinta kutoka Sweden akaunganishwa hapo? Ilikuwaje hata Mtakatifu Kitururu akaunganishwa kutoka Nairobi? Je mlisoma vema maelezo ya Fadhy kuhusu mjumuiko huo? nilitumiwa ujumbe saa tano asubuhi nikiwa katika ofisi yangu kwamba natakiwa kuhudhuria mkusanyiko huo. Je ilikuwa NASIBU? ni kwanini basi niatafutwe kisha kuitwa nami nikaacha kazi zangu hata nikajumuika? Tatizo ni ubinfasi na kudhani kwamba mikusanyiko kama hii ni kueleza kero na shida zetu. KUNA TOFAUTI KATI YA WIVU NA USONGO. Ilikuwaje hata baada ya mjumuiko safari ikaenda tabata? nadhani huu ni ukosefu wa taarifa waungwana. kuna kichwa kimoja SHABAN KALUSE kingeweza kwuaelezeni mengi kabla na baada ya hapo. na mara nyingi nimekuwa na mjumuikona Kaluse, na siyo NASIBU. kawaida ya NASIBU ni kujiaminisha kwamba ndiyo ukweli, na huwa unakuwa mbali na kitendo kwahiyo hata ukaambiwa Mzee wa Lundunya sana anahitaji kumpachika Mungu maswali unaweza kubisha! WAZO TU HILI NA RUKSA KULIBISHIA WAKUUUUUU tuachane na fununu

Fadhy Mtanga said...

Hodi hodi uwanjani,
Nami niyaseme haya mdomoni,
Koero wetu yungali gizani,
Sasa anataka kutoka kizani,
Nami nina msaidia.

Nimeanza hivyo, mama mchungaji, Markus kajibu kuwa haikuwa nasibu. Haya mambo yalianza Jumamosi ya tarehe 8 Mei mwaka huu huu majira ya saa moja unusu jioni. Niliongea na Kaluse akaniambia kuwa amezungumza na Chacha kuwa anatarajia kuwasili Dar siku iliyofuata.

Nikampigia simu Chacha. Tukakubaliana nitampokea airport Jumapili mchana. Ilikuwa rahisi kwa kuwa tumekuwa na mawasiliano siku nyingi kiasi kabla.

Tulipokutana, tukaenda one way Movenpick, tukakutana na Kaluse.

Ukawa mwanzo mzuri kwani tuliweza kukutana mara mbili zaidi na Chacha na ukawa mwanzo mzuri wa kukutana mara kwa mara na Kaluse maana sasa hihesabiki tumekutana mara ngapi.

Baada ya hapo nikapata simu kutoka kwa kaka Chib anakuja Dar. Hapo tukapanga sasa kuwa hiyo tarehe 15 Mei tukutane palepale saa nne asubuhi.

Wakati huo huo kaka Kaluse akawasiliana na Markus. Mi sikuwa na namba ya bloga yeyote zaidi ya kaka Chacha na kaka Chib. Tulipokutana kaka Kaluse akanipa namba yako mama mchungaji, nikakutumia ujumbe, sijui kama uliupata maana siku tukikutana hilo ndilo shitaka la kwanza kwako.

Akaja kaka Markus (shemeji yangu huyu siku hizi).

Baada ya hapo nimekutana na kaka Chacha, Markus na Kaluse mara chungu mbovu. Ndivyo mwanzo wa urafiki ulivyo.

Sisi tulidhani na bado tunaamini huu ni mwanzo mzuri wa kuwa na ushirikiano zaidi ya jina. Na sasa, kama nilivyozungumza na kaka Kaluse, tunajipanga kuandaa siku ambayo tutaweza kukutanisha wanablog wengi waliopo hapa Bongo na wa Ughaibuni wanaokuwepo Bongo kwa wakati huo. Tunahitaji kukuza ushirikiano kwa kiwango kikubwa. Haya tunayoyaandika katika blog zetu yanagusa watu wa kada mbalimbali, hivyo ni lazima tuwe na ushirikiano wenye akili.

Kuhusu kaka Matondo, niliwasiliana naye. Amekwisharejea Amerika. Isivyo bahati kwake, alipatwa na msibwa. Hivyo siku zake hapa Bongo zilitawaliwa na shughuli za msiba na mambo yatokanayo na yaingilianayo na familia. Niliwasiliana naye wakati akiondoka. Alisikitika kuondoka vivi hivi pasi kukutana nasi. Panapo majaliwa, atarudi Bongo siku nyingine maana ndiyo nyumbani.

Maelezo ni mengi kweli hapa, kaka Markus ndo mtaalamu wa kuandika nonstop.

Tutakutana tena na tena. Ila sasa tunahitaji kupanua wigo wa kukutana kwetu.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mimi niekutana nao kadhaa ila nilishindwa kuwajulisha. nilikutana na chacha, strictly gospel basi

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Koeroooooooo!

Kudua na kugosha chedi nini? Nyika na vome.....lol!