Friday, July 23, 2010

MARKUS, HAYATI MWALIMU NYERERE ALIANDALIWA NA NANI?

Hayati Mwalimu wakati wa kudai uhuru

Nimesoma kwa masikitiko makubwa maoni ya kaka yangu, Paroko mstaafu Markus Mpangala, kuhusiana uamuzi wa vijana wengi kujiingiza katika siasa kwa wingi na kwa namna ya pekee tofauti na miaka ya nyuma.

Naomba niweke wazi kuwa uamuzi wangu wa kutangaza nia ilikuwa ni kutaka kuamsha ari kwa vijana ili wahamasike kugombea nafasi mbalimbali za uwakilishi hapa nchini. Binafsi naamini kuwa sisi vijana tuko timamu kabisa kuingia katika kinyang’nyiro hicho. Lakini kutokana na watu wenye maono yasiyo na tija kama ndugu yangu Markus, wanaanza kuwakatisha tamaa kwa maelezo kwamba hawajaandaliwa.

Lakini hata hivyo kuna jambo moja najiuliza, hivi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Rais wa kwanza wa nchi hii baada ya kujipatia uhuru kutoka kwa Waingereza aliandaliwa na nani?

Jambo moja muhimu linalopaswa watu kama Markus kulifahamu ni kwamba historia huwa haifutiki. Na ndio maana hata leo tunaweza kujua matukio muhimu yaliyoikumba nchi yetu kabla na baada ya uhuru.

Wakati ule tulipopata uhuru, tulikuwa na wasomi wachache sana ambao wengi wao walikuwa ni makarani wa wakoloni, lakini kutokana na vuguvugu la kutaka uhuru likiongozwa na wazee wa Dar es salaam ambao wengi wao hawakuwa na elimu ya kutosha wakati huo, lakini kwa kumtumia Mwalimu Nyerere walifanikiwa kwa kaisi kikubwa.

Baada ya uhuru wale waliokuwa wakiwatumikia wakoloni wengi wao wakiwa ni makarani ndio wakajikuta wakibebeshwa majukumu katika nafasi muhimu za uongozi ambapo walikuwa hawana hata uzoefu, wa kutosha katika uongozi wa juu serikalini hususana katika nafasi za uwaziri.

Leo hii kuna mabadiliko makubwa, vijana wengi ni wasomi waliobobea katika taaluma mbalimbali, na wana uwezo mkubwa wa kupambanua mambo kwa namna ya pekee, lakini kutokana na ufinyu wa kufikiri watu wanakaa na kudai kuwa vijana hawajaandaliwa. Je, kina Rashid Kawawa, Tewa Said Tewa, Mzee Opiyo, Mzee Kisumo, Bibi Titi Mohamed, Bi, Lucy Lameck, Bi, Thabidha Siwale na wengineo wengi waliandaliwa na nani?

Ikumbukwe kwamba wakati ule kulikuwa na changamoto nyingi, tofauti na sasa, lakini wenzetu hao walifanikiwa kwa kiasi kikubwa. Leo hii vijana wanajitokeza kutaka kukushika nafasi za uongozi ili kuleta mapinduzi ya kifikra na kuleta tija hapa nchini, wengine wanaibuka na kusema kuwa hatujaandaliwa…….!

Bado nauliza, Je Hayati Mwalimu Nyerere aliandaliwa na nani?

15 comments:

Anonymous said...

Koero,

Mimi ni mmoja wa washabiki wako (japo kimya kimya) hasa linapokuja suala la kujenga hoja. Huwa ninafurahishwa sana na mtindo wa ujenzi wa hoja zako (hii imepelekea niwe na shauku ya kukutana na wewe ana kwa ana). Sasa niseme jambo moja ambalo umenikuna zaidi. Matatizo ya Watanzania yanatokana na uvivu wa kufikiri kama ulivyosema. Nchi hii ina matatizo lukuki, vijana wapo wengi tu, lakini cha ajabu huoni kabisa ule msisimko (wewe umeliita vugu vugu) wa kutaka kufanya mabadiliko. Watanzania wengi (vijana zaidi), ama wameridhika na hali ilivyo, ama wamekata tamaa! Binafsi mimi nimekuwa nakehereka sana. Kinaniuma zaidi sasa kukuta hata wale Wasaniii ambao tungewategemea kwa kutumia sanaa yao kuleta mwamko, nao wameangukia mtego ule ule wa kumuimbia Mfalme (hata kama amekaa uchi) nyimbo za kumsifu! Maskini Tanzania!!!
Ujumbe kwako Koero, songa mbele, mbegu inapoyapandwa na vijana wachache kama wewe, lazima itemea tu, na siku moja tutaona matunda yake.
Jibu la kina Nyerere waliandaliwa na nani, binafsi naweza sema ni utashi wao wa kisiasi (hawakupenda kubaki mavuvuzela - wavivu wa kufikiri)!
Naishia hapa kwa leo!

John Mwaipopo said...

koero awali ya yote of late you have changed positively. from 'mbona hamnielewi' stuff in your comments to 'hii ndio raha ya kublogu'.na kuponeza sana kwa hili, which brings to my musings on this post.

marcus mpangala nadhani ameghafilika na kusahau historia ya siasa za chii hii. nadhani wengi wetu tunakumbuka enzi za 'zidumu fikra za fulani' na 'vijana ni taifa la kesho.' najikita katika hili la pili.

nadhani ndugu mpangala ni tunda bivu lililoivishwa kisawasawa na moshi wa kuni za mti wa 'vijana ni taifa la kesho'. duniani kote sijawahi kusikia taifa lenye wazee pasi na kuwepo kwa vijana na watoto. nadhani iwe hivyo kote.

naweweseka na kutatishana tamaa kiaina kwa namana hii. pengine sie ambao hatutoki katika koo za baba au mjomba aum mama aliwahi kushika wadhifa fulani tunadhani nchi hii waliumbiwa akina fulani tu. sisi ni kuwashangilia tu.

nitatoa mifano michache. wakati anaingia kukitumikia chama Kikwete hakuwa amefika miaka 30. aliandaliwa na nani? sijui.

wakati anaingia kwenye sisa nyerere alikuwa na miaka 30-32. akiwa na miaka 39 tu alikuwa waziri mkuu. akiwa na miaka 40 tu alikuwa raisi.

nyerere hakuandaliwa na mtu bali aliona ana hisa katika nchi hii kama koero ulivyoona una hisa katika nchi hii.

nafikiri hata nyakati zina kauli ya kusema. dunia ya leo sio ile ya miaka ya 1950. wazungu wana msemo 'you cant teach an old dog new trics'. mbwa wa miaka ya 1950 na wa leo wako sawa lakini si binadamu. binadamu wa leo ni mwerevu sana. ninachotaka kusema ni kuwa kama nyerere aliweza kupambana na mikiki ya siasa za kikoloni akiwa na miaka 30, koero wa leo atashindwa nini na mikikimikiki ya siasa za ushindani za leo?

ingekuwa siasa inahitaji ma-PhD, ningezani suala la kusubiri lingekuwa na umuhimu. lakini si hivyo. siasa inahitaji malengo ya ukombozi wa hali duni ya wanakuzungukan, nia njema, elimu ya kutosha (ambayo nadhani koero anayo) na ujasiri wa kupambana.sie waoga tunaosubiri 2015 ama 2020 wacha tusubiri tu lakini itakapofika huo wakati tutakuta vijana hawa tunaosema ni taifa la kesho wamekamata nafasi. we will be wishing to rejuvenate ourselves to 2010. it will be too late.

kila la heri koero mkundi

Yasinta Ngonyani said...

Ama kweli kublog ni kuzuri, Tatizo ni kwamba kuna wengi ambao hawajiamini Yaani ni kwamba hatutaki kufunguka tumejifunga mno na pia tunaamini kuwa hatuwezi nategemea imani hii itakuja kufa siku moja. Kila la kheri Koero!!!

Fadhy Mtanga said...

Kaka John hiyo point ya mabadiliko makubwa sana kwa mama Mchungaji dole.

Markus sidhani kama alikuwa siriazi kuhusu kusubiri kwa vijana. Mara kadhaa nimezungumza naye ana kwa ana na huonesha namna anavyopenda vijana kuchukua nafasi.

Tuache hilo hajaniajiri kuwa wakili wake. Atabeba mzigo wake hapo ni shemeji yangu halafu pia mtani.

Ni kweli kama asemavyo anon hapo juu wasanii wetu nami naona wa wapi sijui.

Kama asilimia kubwa ya Watizedi ni vijana basi kuna haja ya vijana kuamka na kuchukua nafasi za uongozi. Maamuzi mengine ni ya kihafidhina kutokana na kuchoka akili kwa hao wazee. Fikiria mtu aliyejulikana kama mjamaa orijino, Kingunge hatimaye naye anatetea ufisadi, hatuoni kama wamechoka nguvu na akili?

Watu kama Makweta na wenzake tangu nazaliwa wao wapo tu bungeni. Ukitaka wao wenyewe waseme I'm tired utasubiri weeeee. Kuna haja kwa vijana kuchukua nafasi hata kama hawataki watazowea tu.

Kuandaliwa? Nani akuandae wakati waandaji hawataki kurithiwa zaidi ya kuwapa watoto na wapwa wao? Falsafa ya Darwin? Hapana. Lazima tusimame na kuungana mikono kwa dhamira za dhati.

Niseme ukweli vijana wote walioingia ktk kinyang'anyiro nawaunga mkono pasipo kujali vyama vyao. Kwangu chama si hoja, hoja ni nani?

Vijana tusonge mbele. Tuache itikadi kando, tutazame nini vipaumbele vyetu.

Nimesema sana eti eeh? Kalamu imekwisha.

Fadhy Mtanga said...

Nilipomaliza kuandika maoni hapo juu nimerudi kusoma upya maoni ya Markus. Nimejaribu kusoma neno baada ya neno kwa hatua.

Niliporidhika na kauelewa kangu nikaona nirudi hapa kutoa maoni tena.

Nilichokielewa hakuna pahala Markus kasema vijana tusubiri. Na hata maongezi yake na Muhingo, Markus anasema alikubaliana na Muhingo jambo moja kuwa vijana hawakuandaliwa. Hilo tu.

Ni kweli vijana hawaandaliwi. Lakini Markus amejaribu kutumia lugha nyepesi sana lakini kwa mbinu fulani ya kifalsafa ili kueleza mtazamo wake. Markus anasema kwa kuwa vijana hawakuandaliwi (kwa uelewa wangu) kuna haja ya kujitambulisha wenyewe. Kujitambulisha huko ndiko wanakofanya vijana wenzetu.

Ana maana gani?
Kama wazee hawajataka kuwaandaa vijana, basi vijana wameanza kujiinua wenyewe na kusema, 'nasi tupo' Nani anakataa kuwa sivyo ilivyo?

Markus ameeleza vizuri sana kuwa 2010 ni mwaka wa vijana, ila akaongeza kuwa 2015 ni mwaka wa vijana zaidi na 2020 ni wa vijana kabisa.

Kwa mantiki ya kawaida kabisa, ni kuwa kadri miaka inavyosonga ndivyo vijana wanavyozidi kukata mbuga katika duru za uongozi. Nimerudia na kurudia nione wapi huyu mtani anaonesha anapenda vijana tusubiri? Mie sijaona. Msaada tutani.

Kwanini nalivalia njuga jambo hili? Ni wiki iliyopita tu nimezungumza naye ana kwa ana na mtazamo wake ulikuwa chanya kwa vijana. Sasa nikataka nione kama mtu niliyejadili naye alikuwa ananiyeyusha huku alichokizungumza siyo imani yake bali ilikuwa changamsha mdomo?

Nikitoka hapa wacha nikasome tena.

Jamani haya ni mawazo yangu. Sasa namtetea rasmi shemeji yangu (sitaki dadaangu alale njaa)

Markus Mpangala said...

Nilipotumiwa ujumbe kuna mada inihusuyo, nilitulia na kujibu nitasoma. Baada ya kusoma, nilituma ujumbe nitachangia baada ya maoni ya wengine. Wakati naelekea nyumbani kutoka ofisini kwangu nilitumiwa ujumbe na mwanablogu kuhusu mada hii, nikamjibu nimeiona, nitasema neno. Lakini nilichoona kimenishangaza, kumbe Markus ana mawazo finyu,mvivu wa kufikiri,ameivishwa kwa moshi wa kuni, mawazo yake hayana tija. Kumbe Markus akiwa kijana hajiamini na ameshindwa kufunguka…. Nimesoma mara tano na maoni nikahitimisha huu ni UMASKINI WA FALSAFA. Kijerumani wanasema Nicht gut philosophie, wataliano wanasema poveri filosofia. Kitu usichoelewa wajerumani wanasema nicht verstehen. Nilipanga kukaa kimya, lakini haitasaidia watu wazima mnajadili matatizo ya bandia. Ni Fadhy Mtanga ndiye aliyeelewa baada ya kurudi kutoa maoni mara ya pili. Awali aliingia kwenye mtego huu. Mama mchungaji Koero pole sana, mimi nimesoma political science & public administration na history. Nikaivishwa na nondo za Educational psychology & philosophy of education, nasoma hayo hadi kesho.(sasa nasoma psychology katika THE SECRET; LAW OF ATTRACTION). Hivyo ninaposema somo la ‘insearch of identity nipo maili 600 mbele yako. Hivi ulielewa maoni yangu kweli? Mada yako ipo katika hoja mbili, KUANDALIWA na KUJITAMBULISHA lakini umeshindwa kuzichanganua, kwanini? Ulielewa kweli nilichosema? Soma maoni nasema mada na maoni ya wasomaji, wana UMASKINI WA FALSAFA. Umewaingiza kwenye mtego ambao watu wazima wanajadili hoja bandia. Hakuna mahali niliposema vijana wasubiri(uwongo huo). Hakuna mahali niliposema nawakatisha tamaa vijana(hoja bandia hiyo). Fadhy amelonga katika maoni ya pili, sijui alijuaje hilo au Mama mchungaji hakuona?. Kwanini mnataka kuwa Nyerere wa bandia? Nimesema uchaguzi huu ni ‘insearch of identity’ vijana wameamua kujitambulisha badala ya kutambulishwa(kutegemea wazee), hivyo huu ni uchaguzi wao, na zaidi ule wa 2015 ni zaidi kwao, pia ule wa 2020 ni more than you think. Ugumu uko wapi ninyi? Nani kasema vijana hawajiamini? Nani kasema tunahitaji aliyemwandaa Nyerere? Yaani tofauti na nilichosema. Ninyi ndiyo wagombea wetu au siyo jamani!!!!!! Ni vema ungeliweka maoni hayo hapo halafu mada yako ingefuata ili kutowaweka watu wazima kwenye kamtego. SUN TZU anasema hivi ‘the fighters of old first put themselves beyond the possibility of defeat and then wanted for an opportunity of defeating the enemy. To secure ourselves against defeat lies in our hand but the opportunity of defeating the enemy is provided by the enemy himself’. Mama mchungaji Koero, ‘Before setting out on revenge you first dig two graves’. Wanateolojia wanasema ‘penetrate between the line’. Na mwanamuziki Clifford Harris a.k.a T.I anasema ‘see we ain’t live the same life but represent the same struggle’.

Markus Mpangala said...

NARUDI TENA. ukitaka kuelewa somo la insearch of identity rudi kwenye moja ya mada zako ya UMRI WA UBARUBARU, nadhani pale unazungumzia kitu kinachofanana nacho yaani insearch of identity, labda hukujua na hujui kwakuwa huna hiari ya kujua. unajua kuna mambo wakati mwingine hatuna hiari nayo. nachelea kusema sana lakini nimesoma maoni yangu mara tano zaidi lakini najikuta nacheka mada yako. Najiuliza yuko wapi yule Koero mama mchungaji makini? au tatizo ni ile elimu ya makuzi niliyounganisha? lakini siamini hilo. ILA ASANTE NIMEJIFUNZA KITU JAMANI sisyo vibaya kubadilishana mawazo hivi LAKINI yawe mawazo halisi siyo ya bandia. tujaribu kudadavua tusjiingize katika mitego ya bandia manake hizi ni mada zinazotuchangamsha sana akili baadhi yetu. naona wengi mnataka kuwa nyerere lakini ajabu nyerere hawataki ninyi watizedi mnaoishi kwa mafunzo ya NICCOLO MACHIAVELLI. anayetaka kitabu chake nimwazima na aje tu ili tusahihishane . soma sana kuhusu nyerere katika kitabu cha UMAAA NI IMANI utaelewa akile anachozungumzia kuhusu kuishi na waingereza na hicho unachozungumza kuhusu KUANDALIWA. jamani TUJISAHIHISHE tusiwe na UMASKINI WA FALSAFA

Ramson said...

Ama kweli nilim-miss, Koero, maana safari hii amekuja kwa kishindo kikuu....

Kabla ya kusema lolote nimeyatafuta maoni ya mdogo wangu Markus ili nijiridhishe, kabla na mie sijasema ujinga wangu hapa au kabla ya kuingie kwenye ulimbo wa da mdogo Koero, kama alivyosema mwenyewe Markus.

Hebu tusaidieane kusoma maoni ya Markus between the line ili tujue chanzo cha mgongano huu wa hoja ni nini?

Yawezekana dada yetu huyu alikurupuka, lakini nachelea kwamba iwapo tutamshambulia sana tusije kumpoteza maana tunatakiwa kuwalinda wanablog hawa wa kike wasije toweka kama Tembo weupe....LOL.

Naomba busara itumike kupata muafaka wa huu mtego wa Koero, ambao kwa mimi naweza sema kuwa Markus ndiye aliyeanza kumtega Koero na Koero aliponasa akawatega wasomaji wa kibaraza hiki na hapa ndipo tunaposhuhudia baadhi ya wasomaji wakiingia kichwa kichwa....ama kweli hii ndio raha ya kublog....

Haya natumsome Markus tena na tena ili kujua alisema nini:

MARKUS said......

NAANZA HIVI; ni jana tu nilikuwa najadili suala la vijana na uchaguzi wa mwaka nikiwa na Mwalimu wangu Muhingo Rweyemamu(RAI). kikubwa nilikuwa nachangia mada yake iliyotoka Alhamisi wiki hii kuhusu namna vijana wanavyoamua kujiingiza moja kwa moja kushindana na wazee badala ya kusbiri. hili ni jambo zuri, lakini Muhingo na mimi tunakubaliana kuwa vijana hawakuandaliwa, na tutatakiwa kuandaliwa lkufanya hivi yaani kuthubutu kama Mama Mchungaji bila kujali umri. Tulirejea ELIMU YA MAKUZI 'Insearch of Identity' kwamba mara nyingi vijana tunataka kujitambulisha, tatizo tunakosa misingi ya kujitambulisha kwasababu hatujaandaliwa kujitambulisha. MATOKEO yake ni kwamba vijana wameamua KUJITAMBULISHA lakini hawajajua wanatakiwa kujitambulisha namna gani. Kwa uchaguzi huu tulikubaliana ni wa vijana lakini ule wa 2015 ndiyo utakuwa mzuri kwa vijana na zaidi ule wa 2020 ndiyo utakuwa haswa kwa vijana kwasababu AS MUCH AS WE DARE ndivyo tunavoamsha hari ya kufanya hivi. angalia namna vijana wanavyoshughulika na kugombea aidha udiwani,viti maalumu au ubunge, ni AS MUCH AS WE COULD ndivyo tunavyojenga nyumba. wazee naamini watashituka lakini muda umewaacha hawawezi kuzuia tena, na hata ule muda wao wa kutaka kuwaandaa vijana unakimbia, wanatakiwa nao kukimbia.

SASA mama Mchungaji mimi nakuunga mkono kwa hili UMENIKUNA HASWAAAAAA. katika hili nimejaribu kutafakari na kukufikiria tangu ulipodokeza unawania viti maalumu, nimesoma maandiko yako na kuhesabu TABIA yako kisha nikapata jawabu AS MUCH AS YOU DARE unafanana na Nakaaya SUMARI au Halima Mdee, nawapenda sana kwa jitihada zao za KUJITAMBULISHA. Hapo ndipo ninapowatamani wanawake wafikie, hapo ndipo ninapowataka wanawake wafanye.

Mama mchungaji YOUR EYES, YET MORE MY EYES,
YOUR BLOOD YET MORE MY BLOOD ...........rejea shairi la Armando Guebuza(rais wa msumbiji sasa).

July 23, 2010 9:27 AM

Markus Mpangala said...

NIPO BAGAMOYO WAUNGWANA. NIMETULIA.

ha ha ha ha! Ramson, nashukuru sana kwa mchango wako, lakini naomba tusiingize hili jambo la kushambulia. Mama Mchungaji naomba ufute kichwani hii hoja ya kukushambuliWa, kama nilivyosema tunajadili suala la msingi hapa, tusilete utani. Endapo msingi mkuu wa usanifu wa hoja unahitaji nguvu ya hoja, basi ni hoja hiyo inaweza kutanua uwezo wake wa hoja katika kuhoji.

Tukishafanya hivi tunajikuta tunaanza kujiangalia na kurudi nyuma kuweka silaha chini, KUMBE TUNAPOHOJI TUNASONGA MBELE. Lakini kama nilivyochukua sentensi za SUN TZU, kushindwa kwa adui kunatengenezwa na adui mwenyewe. Kwahiyo ninaamini kuwa tunachojadili ni mustakabali wa sisi vijana, lakini tukiweka mazingira ya kushindwa ni lazima tushindwe.

Hapo ndipo hoja inaanza. Hapo ndipo penye hekima na akili. Kwahiyo lengo la kwanza lilikuwa KUJITAMBULISHA kwa vijana, maana ni miaka mingi vijana wametumia njia za NDIYO MZEE, lakini wameanza kubaini kuwa wao wanaweza bila wazee(insearch of indentity). Hivyo wanajitambulisha hawataki KUTAMBULISHWA. Kwahiyo huko nyuma vijana waliposema NDIYO MZEE walikuwa wakisubiri KUTAMBULISHWA wakiwa WAMEANDALIWA pale chuo cha SIASA KIVUKONI. Hivyo sasa ni HAPANA, suala la KUANDALIWA kwamba ni taifa la kesho hawalitaki, na hilo ndiyo maana nikasema AS MUCH AS WE DARE. baada ya kuona baadhi ya vijana waliopenya katika msingi wa NDIYO MZEE, wakatumia mwanya ule kuwalisha vijana wenzao kuwa hakuna haja ya kusubiri wazee....

hapo ndipo WANAPOJITAMBULISHA, hapo ndipo unapoona wimbi la vijana likibuka. Mama mchungaji nilikudokeza suala la GENERATION 700, ni vuguvugu la vijana wa Ugiriki ambao wengi wao wamemaliza sekondari na vyuo vikuu, limetokea mwaka huu. wameamua kusema hawataki NDIYO MZEE, wanaamua KUJITAMBULISHA kwamba wamo. Na hilo ndilo tunaloweza kulishana na kujuzana kwa kaliba zetu.
kwakuwa wapo waliotumia kuingia kwa NDIYO MZEE wanatujuza TUJITAMBULISHE WENYEWE ili hao wazee wafyate. KUJITAMBULISHA kwa mama Mchungaji Koero ilikuwa faraja kwangu, lakini bahati mbaya hajajitambulisha mwenyewe kwa misingi yake bali ameona vuguvugu la KUJITAMBULISHA kwa vijana. Je tunaweza KUJITAMBULISHA kwa namna gani? hapo ndipo penye hekima na akili ndiyo maana vijana wanathubutu kugombea sasa, na wengine ambao wanaona hii ni utani BASI ifikapo 2015 watakuwa zaidi ya uchaguzi huu. Na ikifika 2020 itakuwa zaidi ya uchaguzi huu na ule wa 2015.

John Mwaipopo umeelewa sasa? IMEKULA KWAKO hiyo. Nilidhani Psychology imekaa vema kwako, lakini pole nasema tunakabiliwa na ZIMWI LA 'MIND CONTROL'. sijui kipi kilianza kati ya kukabiliwa na kuingiliwa na 'MIND CONTROL', maana vuguvugu bila kuliamini ni hayo ya mitego. na kuona hoja za kupanua mtasema tunakatisha tamaa. Nimetamka hili kwa wazee pale ofisi ndogo Lumumba kwamba IMEKULA KWAO, chaguzi zijazo wanakazi ngumu sana, wengine wameelewa, lakini whafidhina wanabisha. TUSUBIRI TUONE. ANZA WEWE KUCHUKUA FOMU TWENDE BUNGENI au UDIWANI

MJADALA UNAENDELEA....
NIKIPATA WAZO NARUDI TENA HAPA NINA MENGI KATIKA HILI VUGUVUGU...

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

niko bze, ila sasavijana nitaifa lijalo!!nyerere alipata uwaziri mkuu akiwa 39, akapata urahisiakiwa 40 na kuwekakatiba ngumu eti kuwarahisi lazimauwe40

ila mimi ninaimani kwamba wapigania uhuru wakiafrikawaliandaliwa na watu faulani na ndio maana ukiangalia sera za uwekezaji zanyerere kati ya waafrika na wahindi, mhhhh kuna tofauti

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Naona nimechelewa kuuona mjadala huu. Na nilichotaka kusema pengine hakina maana tena.

Tunapoandika maoni katika vijibaraza hivi na kuzama sana katika falsafa au matapo na mikondo fulani ya kimitazamo tusitegemee kwamba wasomaji wetu wote wataelewa (kwa kina) tunachotaka kukisema. Kama hoja nzima imejengeka katika kanuni ya "in search of identity", vipi mimi ambaye sijawahi kuisikia hii kanuni na udhihirisho wake? Nisipoelewa kwa kina kinachosemwa na nikatoa mchango "ulioparaganyika" ndiyo nibatizwe MASIKINI WA FALSAFA? Ni nani ajuaye kila kitu?

Ikumbukwe pia kwamba wengi wetu hatuna muda wa kusoma "between the lines" isipokuwa pengine kama ni blogu ya kifalsafa (waulize wanaokwenda kule kwa Baba Mtakatifu. Naamini huwa wanaenda huko wakiwa wamejiandaa. Ndiyo maana mara nyingi huwezi kukuta maoni kule!). Amini usiamini lakini wasomaji wengi wa hizi blogu husoma kwa haraka haraka tu na kukwapua kile wanachoweza. Kwa hivyo ni rahisi sana kuibuka na maana nyingine.

Naona Paroko ameshusha "makwotesheni" kibao pamoja na ushahidi wa "usomi" wake hapo juu (ukiwemo uelewa wake wa lugha mbalimbali). Mimi sina uhakika kama hii ndiyo njia sahihi ya kuendesha mjadala, kujenga hoja na hatimaye "kumshinda" mpinzani wako(kama mnashindana). Ukitaka kuona tatizo la mtizamo huu katika kuendesha mijadala, hebu tuanze basi kila mmoja wetu alete "makwotesheni" na ushahidi wa usomi wake kutoka katika utanzu aliosomea (Historia, Fizikia, Elimu ya Miamba, Hisabati...). Huwa nawaangalia watu wenye tabia hii kwa jicho la hati hati na kuutilia "kwesheni maka" kubwa sana usomi wao. Tazama maoni yangu kuhusu jambo hili hapa:

http://matondo.blogspot.com/2010/02/fikra-ya-ijumaa-ati-msomi-ni-nani.html

Hali hii ingeepukwa kama Paroko angeeleza kwanza kanuni ya "in search of identity" ni nini au kutoa "link" ambako watu wenye udadisi wanaweza kwenda kujisomea. Si haki kuanza kuwasikinisha watu kifalsafa wakati hujawaandaa. Hatuko kwenye hizi blogu ili kuonyesha "usomi" wetu bali kuelimisha huku tukielimishwa, kufunza huku tukifunzwa n.k.

Ndiyo maana nampenda sana Mwalimu Euphrase Kezilahabi. Nimesoma novela zake za Nagona na Mzingile zaidi ya mara 10 na kila mara huwa nafikiri kwamba nakaribia kabisa kuelewa anataka kusema nini. Uzuri wake ni kwamba ukimuuliza mwenyewe uso kwa uso hasa anazungumzia nini katika novela hizo, yeye hutabasamu na kusema "hicho ulichokielewa ndicho". Kuna kitu cha kujifunza katika jibu hili!

John Mwaipopo said...

yangu macho mie ngumbalo nisiyejua falsana, kijerumani na quotations. sikujua ili uonekane umesoma lazima uwe na quotations, hata kama zimeandikwa na wapumbavu.

Fadhy Mtanga said...

Naomba kurudi kuandika maoni kwa mara ya tatu.

Huu mjadala huu kwa mtazamo wangu umetosha sasa. Naomba kusema hivyo japo mimi si mwenye blog.

Kaka Matondo na kaka John mmetuzidi kiumri, kula chumvi nyingi si jambo jepesi. Hivyo mmejifunza mambo mengi kutuzidi. Kwa bahati nzuri nyie ni walimu, mnakutana na vichwa kama Fadhy kila uchao. Hivyo mna uzoefu wa kutosha juu yetu vijana.

Nimesoma maoni ya shemeji yangu Markus (halafu ni mtani na mahari bado hajamaliza), nimesoma ya kaka Matondo (naye ni shemeji yangu) na ya kaka John (huyu kaka kabisa) Kupitia maoni hayo nimejifunza jambo kubwa sana.

Tunasema, kublog hutufundisha kuvumiliana. Kaka yangu Chacha aliwahi kuandika maoni pahala, ukiwa bloga huwezi ugua BP. Tena humu humu kibarazani kwa muamshaji mchungaji Koero.

Kublog kunakuza mahusiano mema. Kunajenga urafiki mkubwa sana. Leo hii mimi marafiki zangu wakubwa ni wanablog wenzangu.

Jamani naishiwa maneno, ila najua wa kunielewa mmenielewa naamaanisha nini.

Upendo daima.

Markus Mpangala said...

Dhana ya kwanza ya kufikiri haitokani na msomi, bali nini kile mtu anajifunza katika maisha yake. Dhana ya pili ni ile ya kimapokeo ambayo inatokana na kilekile anachokiona na kujifunza katika maisha yake.
Maana kaka Mwaipopo anasema kwotesheni, hata za WAPUMBAVU, sawa kumbuka WAJINGA NA WAPUMBAVU uliwatambua kwakuwa ulijifunza kuwa UPUMBAVU siyo tija na elimu. Lakini WAPUMBAVU ni watu wenye jambo la kufundisha hata kwa kanuni tofauti na zile unazozijua. Labda ukweli ni sahihisho nililojifunza kwa Prof Matondo, (nitasahihisha hilo) kwamba kanuni hii inafanyaje kazi. Kwa kweli ingelieleweka vema kama mtoa mada angeliweka kiini cha hoja yake, endapo angeelewa. kwani kutoa mada alijiridhisha ameelewa.
Kwahiyo kaka Mwapipopo ninathubutu kukwambia kwangu kwotesheni hata kama ni MPUMBAVU inakitu cha kujifunza nadhani katika tasnia ya kujifunza unaelewa hilo. Kwa mantiki ya kwanza ya kujifunza ni kuelewa yatokanayo. Na mantiki ya pili wewe kuwasilisha kitokanacho.

Endapo ujinga wa kwanza ni kujionesha basi ujinga wa pili utakuwa ni KUZALIWA. Kwasababu hiyo ukiangalia yote haya utaona ni nanmna gani makuzi yetu yanajikunja na kukunjuka katika misingi ya mapokeo na kujifunza kwa asili kuna kwotesheni ya SUN TZU na methali ya KICHINA(tazama filamu ya FOR YOUR ONLY EYES). msingi hapa kaka Mwaipopo pamoja na kuwa kaka yangu ni lazima unishurutishe nifafanue kama alivyonishurutisha kama matondo. Lakini nini hasa kinachoanza kusoma kusaomewa na kujisomea? HAPO NDIPO utaona watu wanajikunjua kujua nini wanachoelewa kinachoanza. KUNA SWALI.? NITARUDI

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___