Thursday, April 14, 2011

MHUBIRI WA INJILI KITAANI ADUNDWA

Mhubiri akiwa kazini
Hii niliishuhudia katika viunga vya pale Mwenge jiji Dar jana wakati naenda Hospitali. Nilikuwa nimesimama kwenye duka moja la kuuza Dawa kuulizia dawa fulani ambayo niliandikiwa hospitalini. Upande wa pili wa barabara kutoka katika duka hilo kulikuwa na jamaa mmoja aliyejitambulisha kama Mtumishi wa Mungu, alikuwa akimwaga neno la Mungu, kuwaasa watu waache matendo ya Dhambi, na kumrejea Mungu.


Jasho lilikuwa likimtoka kwelikweli na alikuwa akiongea kwa jazba kama vile anagombana, lakini katika mahubiri yake alikuwa akiwananga wapita njia hususan wanawake ambao walivaa vimini au suruali za kike.


Ilikuwa kila akipita mwanamke mwenye kimini au suruali ya kike alikuwa akimwambia…….. ngoja nimnukuu hapa. ‘wewe mwanamke mwenye suruali acha dhambi, hayo mavazi uliyovaa hayampendezi mungu kamwe na ninakuhakikishia utakwenda motoni, na wewe mwanamke mwenye kimini na hakika hutauona uzima wa milele, utaishia motoni’ mwisho wa kunukuu.


Kibaya zaidi alikuwa akitumia kipaza sauti na alikuwa akiwafuata nyuma (hao wanawake) huku akiwamwagia maneno makali na ya kudhalilisha


Wakati akiendelea na mahubiri yake akapita dada mmoja ambaye alikuwa amefuatana na mvulana, sikuweza kujua kama walikuwa na uhusiano wa kimapenzi au walikuwa ni ndugu, yule mhubiri kama kawaida yake akaendelea kumwaga maneno ya kuwakashifu wanawake wenye kuvaa suruali.


Kutahamaki nikamuona mhubiri kakunjwa shati na yule kijana, aliyekuwa na yule binti, mara ghafla yule kijana akaanza kumchapa makonde yule mhubiri mara kichwa, hajakaa sawa akalambwa mtama, mhubiri chali……………..


Kisha yule kijana akamshika mkono yule dada, wakaondoka wakimuacha mhubiri akijizoa zoa pale chini. Niliondoka katika eneo lile maana umati wa watu ulianza kusogea katika eneo hilo ili kujua kulikoni.


Kilichojiri nyuma yangu sijui.


7 comments:

Albert Kissima said...

Kiukweli kuna wahubiri ambao nami huwa wananikera sana. Kwa mfano hawa wanaohubiri kwenye magari ya abiria, yani hawajali itikadi za kidini za watu, wao wanashuka verse tu, hata wakiambiwa kuwa wapo wadioyapenda mahubiri yake, yani ndio kwanza anazidisha, huwa wananikera sana watu hawa. huwa nawaona wasioijua imani yao vyema, hawtumii akili, hawatumii utashi, hawatumi elimu,maarifa wala hekima ambayo kw wakristo wanatambua kuwa hizi ni kati ya nyenzo muhimu kabisa alizowapa wakristo katika kulitafakari neno liitwalo la Mungu na hata katika maisha ya kwaida kabisa ya watu. daima huwa siwakubali kabisa watu hawa na kwa bahati mbaya sana sijawahi kukutana na mhubiri yeyote ambaye anahubiri kwa kuzingatia itikadi za kidini za watu. Huwa wanahubiri kulingana na dini zao, mawazo yao na wanataka nini. utasikia mara ndugu yangu okoka ili uende mbinguni, okoka ili uutue mzigo wa dhambi, sijui wapi ndio kuna uzima!

Goodman Manyanya Phiri said...

Biblia inasema kinaganaga kwamba Mungu kamwe hataangalia mavazi ya mtu bali anaangalia moyo au roho yake. Sasa watu wanaovuta bangi halafu kujidai wao ni wahubiri lazima wataokota makofi ya bure tu.

Hapa Afrika Kusini niliwahi mji waNelspruit kumuona "mhubiri" mmoja wa aina hiyo. Yeye alikuwa anatumia "uhubiri" kusudi apewe sigara ili avute.

Kweli ndivyo Mungu anavyotaka namna hiyo?

Pole sana, Mdogo wangu, huko Dar; lakini hayo umeyataka mwenyewe pia nashangaa kwanini hukupigwa ngumi kabisa!

Yasinta Ngonyani said...

Kila mtu sasa anahubiri atakavyo kwa kweli hii sijui ni nini?

emu-three said...

Uhubiri unatakiwa hekima...

SIMON KITURURU said...

Kuhubiri ni bonge la ujasiriamali sikuhizi kama biashara yoyote ile na wajanja hawalali njaa!


Na nasikia biashara hii ndiyo yenye mtaji mdogo kuliko yote!


Nje kidogo ya tundu:

Stori za Mtama zimenikumbusha kabla ya kuondoka Songea enzi za primary hapo shule ya Mfaranyaki enzi hizo katika kupigana kipindi cha mapumziko nilidundwa kisawasawa na jamaa mmoja aitwaye Deo . Jamaa alinibwenga ngumi ya jicho wakati naonagiza akanimalizia na bonge la mtama.

Ilichukua utaalamu sana kujaribu kutunza heshima yangu kwa kusingizia alinipaka pili pili machoni na stori kadhaa ili tu kujaribu kulainisha kuwa jamaa ni kweli alinishinda nguvu. Na tokea nipigwe hilo bonge la mtama ni miaka mingi sana ilipita kabla sijapigana tena yani !

Mtama kiboko aisee maana unaweza kujikuta uko chali kijinga vile na watu weweeee!

Goodman Manyanya Phiri said...

@Simon: Hongera sana! Yataka moyo kukiri uliwahi kudundwa. Lakini ukweli ni kwamba kila mpiganaji lazima apigwe kwanza!

Nikiwa na umri wa miaka tisa au kumi, niliwahi kumpiga kijana mwenzangu huko shuleni na ikawa sifa kweli kwamba "Goodman amelipiga jitu Penede na kuliangusha kabisa KNOCK-OUT"!


Baadaye nikajiona kweli mimi ndiye bingwa wa ngumi shuleni mpaka hapo nilipokutana na Bwana Tokoto Zwane, jamaa fupi fupi nene nene vilevile lenye kutumia mkono niliedharau sana: ISANDLA SEMFENE ("mkono wanyani") au mkono wa kushoto.

Zwane alinikung'uta pua hii mbele za mwalimu wangu wa kike na wasichana wote wa shule! Aibu kweli damu zilivyonitoka! Lakini sikurudia tena kupigana pigana hovyo shuleni!


Labda uniulize ilikuwaje nipigwe mbele za akinadada. Dada yangu mwenyewe (Monica Phiri-Ngwenya) anaenizidi kwa miaka 5 ndiye alienda kumwambia mwalimu kwamba "Goodman keshaanza tena kupigana kama majuzi" na mwalimu akaamua basi "waje wapigane mbele za shule nzima" ili eti shule ipate burudani bure!


Kwa maneno hayo tunamtakia pole sana mhubiri. Apone haraka halafu arudie kazi zake za Mungu, baada ya kujirekebisha lakini!

Markus Mpangala said...

@Kitururu, hata miye nilibwengwa ngumi ya mdomoni pale shule ya msingi Kiwanjani, kata ya mbinga mjini. duh! ilikuwa karibu na makao makuu ya halimashauri ya minga. nipigwa hadi kamasi shaaaaaaaaaaaa.

huyo mhubiri angeniTUKANIA KOERO MKUNDI ningembadilisha sura yake ifanane na kichuguuu, hata mtani wangu Fadhy ningemkaba tanganyika jeki. ha ha ha ha ha