Saturday, April 16, 2011

MPIGA DEBE WA DALADALA AMWAGA NGELI NA KUWASHANGAZA WENGI………

Leo asubuhi nimekutana na kituko cha mwaka, naomba nikiri kwamba hata mimi nilikuwa ni mjinga kwani sikutarajia kwamba jambo hilo nililolishuhudia linawezekana. Naomba nikiri kuwa hata mie nilikuwa nawapa watu hawa mtazamo tofauti kabisa nikidhani labda mie ni mjanja kuliko wao, lakini hili nililolishuhudia asubuhi ya leo, nimenifunza jambo moja muhimu sana maishani, kwamba kamwe usimhukumu mtu kutokana na muonekano wake.


Ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili alfajiri, niko maeneo ya Msasani, nikisubiri daladala la kuelekea Kariakoo, mara likaja basi moja hivi aina ya Toyota Coster. Kama kawaida abiria wakiwemo wanafunzi tulilikimbilia na kuanza kugombea kupanda kila mtu akijaribu kuwahi kiti. Japokuwa hatukuwa wengi, lakini nilishangazwa na jinsi abiria walivyokuwa wakigombea kupanda utadhani watakosa nafasi ya kukaa. Lakini cha kushangaza ni kwamba vurugu zote zile ilikuwa ni ili kuwahi viti vya Dirishani!


Pale mlangoni alisimama mpiga debe mmoja ambapo kwa hapa Dar hujulikana kama Mateja, yaani watumia madawa ya kulevya, ambaye alikuwa amevaa nguo kuu kuu na zilikuwa chafu ajabu. Alikuwa pale mlangoni kuzuia wanafunzi wasipande. Kwa hapa Dar ni jambo la kawaida wanafunzi kuzuiwa wasipande kwenye basi na abiria wakabaki wakiangalia tu, kama vile haiwahusu. Kule Arusha mambo ni tofauti kidogo, wanafunzi huwa hawaachwi, tena kama hajavuka barabara, hasa watoto wadogo, kondakta anamfuata na kumvusha ili apande kwenye basi, kwa kweli nilishangazwa na ustaarabu wa makondakta wa daladala za Arusha.


Baada ya abiria wote kupanda, yule mpiga debe aliwaambia wale wanafunzi kuwa atachukua wanafunzi sita tu, wengine waende kwenye mabasi mengine. Pale chini kulikuwa na wanafunzi zaidi ya kumi na tano hivi na wote walionekana wakitaka kupanda kwenye hilo basi ili kuwahi shule. Yule kijana mpiga debe aliongea kwa usataarabu akiwaelewesha wale wanafunzi, akiwaambia kuwa hata yeye anajua adha ya usafiri kwa wanafunzi lakini ile gari ina Hesabu, yaani wanatakiwa wafikishe kiwango fulani cha hela kwa mwenye gari na wao wabaki na chochote, na kwa kuzingatia kuwa leo ni Jumamosi, ni ngumu sana kupata hesabu ya tajiri.


Lakini kulitokea kutoelewana kati ya wale wanafunzi na yule mpiga debe, wanafunzi walimjia juu wakimwambia aache siasa, wao wanataka kuwahi shule na hawahitaji Lecture pale. Kulitokea kutoelewana, lakini yule mpiga debe alisisitiza msimamo wake wakutaka wapande wanafunzi sita tu. Ni kweli walipopanda wanafunzi sita, aliwazuia wengine wasipande na kuruhusu dereva aondoe gari. Baadhi ya wanafunzi walioachwa pale chini walilazimisha kuning’inia mlangoni, lakini yule mpiga debe aliendelea kuwazuia huku gari likianza kuondoka mdogo mdogo..


Wakati zogo kati ya wanafunzi na yule mpiga debe likiendelea, ghafla akaibuka abiria mmoja, akaanza kumfokea yule mpiga debe, akimuonya kwamba kama hatawaruhusu wale wanafunzi wapande basi atalipeleka basi lile Polisi, yule Mpiga debe hakumjibu alikuwa akiendelea kuzozana na wanafunzi.


Yule abiria alianza kumtolea yule mpiga debe maneno ya kashfa huku akimtisha kuwa atampiga. Basi liliondoka na baadhi ya wanafunzi waliachwa pale kituoni, ndipo yule mpiga debe akamgeukia yule abiria na kumuuliza kisa cha kumkashifu wakati yuko kazini.


Yule abiria akawa kama amechokozwa, alimshambulia yule mpiga debe kwa maneno makali na kumkashifu kuwa hajasoma na ni mvuta unga tu na kibaka wa mtaani.


Yule mpiga debe akamwambia, ni kweli hajasoma, kwa sababu ingekuwa ni jambo la kustaajabisha kukuta mpiga debe msomi, hata hivyo hakuishia hapo, akamtupia swali yule abiria………


"inaonekana mwenzangu umesoma sana eh!….. hivi una degree ngapi mpaka sasa, au una masters?” Yule abiria aliendelea kumtolea maneno ya kashfa yule mpiga debe huku akisisitiza kuwa hajasoma na ni mjinga tu.


Yule Mpiga debe akaonekana kukerwa na yale maneno kutoka kwa abiria mkorofi, akamgeukia na kumwambia, kwa kiingereza, ngoja nimnukuu hapa……..


“Listen my friend, don’t judge me because of what I am doing, I have good education background than you. To be a Daladala tout does not justify that I am ignorant. For your information, I am educated enough to work for a white-collar job. I am here because of frustration, after being fired from my job; I had a nice job with a lot of benefits and privileges, I am not a fool ok!”


Wakati anamwaga kiingereza, kwanza abiria walishikwa na butwaa, na baadae wakaanza kumshangilia wakiwemo wale wanafunzi waliokuwa wakitetewa na yule abiria mkorofi. Hata hivyo yule abiria aliposikia jamaa anamwaga kiingeza, alikaa kimya asiamini masikio yake,hakujibu kitu.


Abiria waliendelea kumchagiza mpiga debe aendelee kutoa dozi kwa mshkaji, na yeye ili kupata ujiko zaidi akaendelea kumwaga ma-vitu, palikuwa ni patamu hapo…….


“You know sometimes people think all daldala touts are drug users and they are not educated ……..… No, you are totally wrong my friend, for this job I am earning more than enough, I can make your salary which you get from you Boss Indians for 10 days. Although I have been fired but I decided to work as a daladala touts rather than stealing someone’s money.”


Kisha akaendelea…..


“Why you are quiet, talk now Mr. Educated” ………… “You see,” akatugeukia sisi abiria na kutuambia ……….. “Mr. Educated have failed to speak even two English words”


Jamaa akajikakamua na kumjibu,


“Hebu ondoka na kiingereza chako cha kuombea maji, mwenyewe unajiona umeongea kiingereza hapo, hamna kitu,unachapia tu”


Mpiga debe hakumkawiza akamjibu…….


“Ok, my English is just for begging water, where is yours, if you can speak only two English words, I will give you ten thousand, right now, in front of passengers, I am not joking”


Yule mpiga debe akatoa elfu kumi na kumpa abiria mwingine aishike, ili kuthibitisha kuwa hatanii. Kumbe jamaa alikuwa ni mweupe, hajui Ngeli, yaani ilikuwa ni aibu, karibu abiria wote wakawa wana mzodoa kwa maneno ya kejeli.


Tulipofika kituo cha Namanga jamaa akashuka kwa aibu na ninadhani alikuwa hajafika safari yake, naona alishuka ili kujisitiri na aibu iliyomkumba mle ndani ya basi.


Nakwambia ilikuwa ni gumzo ndani ya basi lile kila mtu akisema lake wapo waliosema kuwa yule mpiga debe ni mpelelezi wa Polisi, wapo waliosema ni shushushu yaani anafanya kazi usalama wa Taifa. Na hilo ndilo tatizo tulilonalo Watanzania, yaani mtu akijibainisha tofauti na muonekano wake basi ataitwa shushushu…….. Basi na yule mpiga debe akapewa cheo cha ushushushu pale pale, kisa kaongea Kiingereza, kuna wengine walisema sio Mtanzania bali ni Mkenya, kwa kuwa hakuna Mtanzania anayejua Kiingereza kama vile halafu afanye kazi ya kupiga debe, ili mradi kila mtu alisema lake.


Tulifika Kariakoo kilamtu akashika hamsini zake, nimerejea nyumbani jioni hii nikaona niwashirikishe wasomaji wangu katika kisa hiki ambacho hata mie kiliniacha mdomo wazi.

13 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Haki ya nani huyu mpiga debe ningekuwepo ningeungana naye maana kila siku nimekuwa najiuliza kwa nini watu wanaweza kumuhukumu mtu bila kumjua? Yaani nimeipenda sana hii mada. Kwani hii tabia ipo na ipo sana utakuta mtu hata hakufahamu ananza kukusema fulani yule ana tabia hii na hii na hii ... natumaini wengi watajifunza hapa.

Goodman Manyanya Phiri said...

Inavutia sana kufikiri "mimi sifanyi kitu kama hicho kumhukumu (STEREOTYPE) binadamu-mwenzangu kutokana na kazi yake, umri wake, rangi yake ya ngozi, kabila lake, nchi anakotokea na mambo kama hayo".


Lakini ukweli ni kwamba kila mmoja wetu tunatumia mawazo kama hayo kwa kiwango kidogo au kikubwa na inahitajika tufanye hivyo ili kurahisisha mawazo kila tunapopata migogoro na wahusika.


Kwa mfano, swali: "UMESHIKA MIMBA NINI?" litakushangaza sana ukiulizwa na mvulana wa shule kwenye daladala. Lakini kama ni mtu mzima tena daktari kabisa anayeuliza ni sawa!


Tayari umekwisha fanya ubaguzi hapo, na kama hilo tendo sio ubaguzi, ubaguzi ndio nini??? (maana yake inawezekana kabisa ikawa mvulana huyo naye ni daktari, tena GENIUS kabisa, na amepanda daladala hilo kwa dharura ili asaidie akinamama wajawazito wakae sehemu fulani ndani ya gari hilo ili kuokoa maisha ya watoto wao baada ya kusikia TSUNAMI imeharibu barabara huko mbele).

Anonymous said...

kweli dada hiki kisa chako kimeniacha hoii ni kweli kabisa kunawatu wanaweza kumjaji mtu kutokana na anavyomuona na hii nikosa kubwa sana na hii iwefundisho kwa watu wengine wenyekudharau wengine nimeipenda hii sana big up it

Mwanasosholojia said...

Hii ilikuwa kweli kali ya mwaka da'Koero. Ni kweli si vyema kuanza kum-judge mtu from just an appearance, kazi anayofanya etc. Story nimeifurahia kweli, ilibidi niirudie mara mbili kwa utamu wake, hongera kwa uwezo wa kuelezea...swali moja tu fupi dada yangu, wapiga debe huwa najua wanabaki vituoni daladala linapoondoka, huyu aliondoka na hii daladala pamoja na huyo abiria?

Kakakuona Sijaona said...

Kweli kabisa nami naungana nanyi mliotangulia kuchangia."Don't judge a book...."Ila swali moja wapenzi ndugu zangu,hivi "akili","utambuzi", "ujuzi","werevu","maarifa",au hata "elimu"ya mtu inapimwa kwa kuongea lugha za kigeni/madarasa namiaka ya mtu aliyotumikia kwenda shule?Ni swali tu.Kuna watu wengi hawakubahatika kubeba mlolongo mrefu wa madarasa/miaka mingi ya shule,lakini mmhh ni vichwa vikali.Fact au siyo?
Ni mtazamo tu.
Nawasilisha.

Mdau Avold said...

Hilo ni somo tosha kwa wale wenye tabia za namna hiyo ya kujudge mtu pasipo kumtambua huyu ni nani na huyu ni nani! Big up Brother and i thought no one can repeat that rabish.

Raymond Mkandawile said...

Nimeguswa sana na habari hii kwani ni ukweli uliowazi kuwa watu hutoa hukumu bila kuwa na ushahidi wowote.Hatuna budi kuachana na dhana hiyo potofu na kuwa wastaarabu kapo kwa dakika moja tu.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Ina maana kwa kuwa huyu mpiga debe anaweza kuongea Kiingereza ndiyo msomi? Kuwa msomi ni lazima ujue kuongea Kiingereza? Ni usomi gani tunaouzungumzia hapa?

Kama jamii bado tunayo safari ndefu kama bado tunafikiri kwamba kiwango cha elimu na usomi wa mtu vingali vinapimwa kwa uwezo wake wa kuongea lugha ya kigeni!

Rama Msangi said...

hii nimeipenda, namna hii heshima lazima iwepo

Godwin Habib Meghji said...

Hii ina maana wamarekani na waingereza wote ni wasomi kwa sababu wanaongea kingereza. NAONA WATZ TUNA TATIZO KUBWA. TUNA-USISHA ELIMU NA UWEZO WA LUGHA. Ndio maana hata bungeni utasikia kwa LUGHA YA KITAALAMU akimaanisha kingereza na wala si technical term. kama ni kweli nimependa ustaarabu wa huyo konda/mpiga debe, ila uwezo wake wa kuongea kingereza bado haumuweki kwenye kundi la wasomi. WACHINA, WAFARANSA, WAJERUMANI SI WASOMI..ni mtazamo wangu

Anonymous said...

ndugu.Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) yaani sasa wewe ndo ujiangalie tena kwa uliyosema. kusoma au kuwa msomi hakupimwi kwa kusomea udakitari, uhandisi, usanifu majengo, sheria, nk peke yake bali hata kuwa MTAALAMU wa lugha kuanzia lugha mama hadi za kigeni (wazee wa linguafrancas kama umewahi kuwasikia) kwa hiyo wewe pia safari bado unayo kujua nani ni msomi. mwisho naona mleta mada pamoja na abiria wenzake nao wanasafari ndefu ya kujua kuwa makini na mambo ya kupewa kipaumbele kwa sababu mpiga debe amewaangalia na kujua kuwa kwa yeye kutumia point yake ya usomi wa lugha kawahamisha kwenye point ya msingi ya kuwatetea wanafunzi na kumuona yeye (mpiga debe) kama shujaa dhidi ya mpigania wanafunzi hata kama alikuwa mkosaji kwa atakavyokuwa alimchambua mpiga debe.
Naitwa; TBS

Masangu Matondo Nzuzullima said...

Anony (aka TBS):

Asante kwa hoja zako. Dhana yangu ya usomi ni pana sana; na haishii tu katika kuingia darasani na kupata ma-Ph.D. Unaweza ukawa na ma-Ph.D mia moja na bado usiwe msomi!

Kwangu mimi usomi ni ule uwezo wako wa kuyatumia maarifa uliyonayo (bila kujali kama ni ya kutoka vitabuni ama la!) katika kuyatawala mazingira uliyomo na kuyafanya yakutumikie. Ndiyo maana naamini kwamba hata kabla ya kuja kwa wazungu na elimu yao hii ya ma-Ph.D, tulikuwa na wasomi wengi tu tena waliobobea hapa Afrika. Wapo wazee kule vijijini ambao hawajui kusoma wala kuandika lakini wanaweza kukuelezea majina na matumizi ya kitiba ya miti mingi mbalimbali mpaka ukashangaa hata kama una ma-Ph.D ya Botany ! Na maarifa yote haya yapo vichwani mwao tu na wamekuwa wakiyatumia miaka nenda miaka rudi.

Nimelalamika hapa kwani ni hoja hizihizi zisizo na mashiko ndizo zinatumiwa kupimia usomi wa mtu. Ukiweza tu kuongea lugha ya kigeni eti basi wewe ni msomi na watu wanakuogopa na kukuheshimu kama huyu mpiga debe. Ndiyo maana wabunge wetu wanakazana kweli kuchanganya lugha kule bungeni ili nao waonekane wasomi hata kama wanachoongea ni pumba. Kweli?

Ni dhana hii hii pia ambapo utasikia watu wanadai kwamba matumizi ya Kiswahili Tanzania yamepunguza "usomi" na kushusha hadhi ya elimu nchini kwa sababu tu wanafunzi wa sasa hawakimudu Kiingereza sawasawa. Utaambiwa kwamba ni afadhali wakati wa mkoloni kwani wakati ule "wasomi" walikuwa kibao kwa kuwa tu wanafunzi wa wakati ule walikuwa na uwezo mkubwa wa kuongea Kiingereza.

Ngoja nimalizie na swali. Kwako wewe msomi ni mtu wa aina gani?

NYONGEZA: Mimi hata sijui kama naweza kujiita msomi; na kama kauli-mbiu yangu inavyosema katika blogu yangu, naamini kwamba sisi binadamu ni wanafunzi wa kudumu hapa duniani kwani maarifa hayashikiki, kumilikika wala kukamilika. Tunajua vitu nusunusu tu na kila siku mapya mengi yanazaliwa, mapya ambayo wakati mwingine yanabatilisha kabisa kile tunachodhani kwamba tunakijua. Ati, wewe ni msomi????

Nilishawahi kuliuliza swali hili hapa:

http://matondo.blogspot.com/2010/02/fikra-ya-ijumaa-ati-msomi-ni-nani.html

DINA MARIOS said...

heeheheheheh inafurahisha,nimecheka sana ndio maana tunaambiwa don't judge a book by its cover....