Friday, February 6, 2009

WAPO AMBAO HAWAJAWAHI KUONESHWA UPENDO

Hawajawahi kuoneshwa upendo
Kuna mamia kama sio maelfu ya watoto hapa nchini ambao hawajawahi kuhisi upendo hata kidogo kutoka kwa wazazi kama ambavyo wangestahili kuupata. Kuna idadi kubwa ya watoto wanoenda vitandani wakiwa wapweke, wakiwa na njaa, bila ya uhakika wa usalama wa leo na hata kesho.
Sio kwamba watoto hawa wanaishi na watu wengine, hapana, huishi na wazazi wao waliowazaa, lakini wanajua kidogo sana au hawajui kabisa kuhusu upendo.

Kuna wale watoto ambao huenda kukosa upendo huko kunatokana na ugumu wa maisha ambapo wazazi wamelazimika kukimbia nyumba zao katika kuhangaika au hata kujikuta wakiwa jela na kuwaacha watoto hao mikononi mwa dunia, katika mazingira yoyote yawayo ni kwamba kuna idadi kubwa ya watoto wa aina hiyo hapa nchini.

Kama sehemu ndogo tu ya wale miongoni mwetu ambao tumebahatika kuwa na uwezo kidogo tungeamua kutumia sehemu ndogo ya ziada katika mapato yetu na sehemu kidogo ya muda wetu kuwasaidia watoto hawa, tungekuwa tumewaokoa wengi kati yao ambao kwa kawaida huishia mahali pabaya bila hiyari zao.

Hata kama msaada au vitendo vyetu kwa watoto hawa vitakuwa vinaonekana vidogo sana kwetu au kwa wengine kama ilivyo kwa matendo mengine yoyote ya upendo, juhudi hizo zingekuwa hazijapotea bure.

Kwa kadiri ambavyo misaada yetu hiyo ingeonekana midogo, bado ingekuwa ni mikubwa sana kwa kuchanganya na ya wengine.
Hebu jaribu na jitahidi sana kutoa msaada hata mdogo sana pale ambapo unaona wazi kabisa kwamba kuna mtoto mwenye mateso, ambaye una uhakika atafikia umri kama wako akiwa hajui maana ya upendo.

Jaribu kujiweka kwenye nafasi yake uone ni kwa vipi ingekuwa kama ni wewe uliyekosa upendo huo, kumbuka kwamba kizazi kilichopita kiliwezesha kizazi hiki kilichomo kuwepo kwa sababu ya upendo kwa kila binadamu mwingine bila kuangalia nasaba zao.
Hebu jitahudi kwa upande wako kuhakikisha kwamba unasaidia kufanya kizazi kijacho kije kuwepo.

5 comments:

MARKUS MPANGALA said...

Siku moja hapa mitaa ya Upanga nilimwambia binti mmoja kuwa nina wivu na wazazi wake!
Alishangaa sana. nikamweleza kwanini wazazi wako wananichulia kama mtoto wao wa kunizaa?
Kwanini wanaonyesha upendo namna hii? Akazidi kushangaa. Nikamwambia katika makuzi yangu kuna kipindi nimekaa mbali na wazazi wangu! tangu nikiwa msingi hadi sasa, nimekuwa mbali sana na wazazi wangu najisikia homa kali sana, ndiyo maana siwezi kukaa mbali kwa muda mrefu bila kuchukua mwezi mmoja kwajili ya kuwa na wazazi wangu.NAFUKUZIA UPENDO WA KWELI,ingawa wengine wanao pia

Lakini akauliza, unawajua watu waliokosa upendo? Hapo nikawaza, nikajiuliza,nikatafakari,nikahoji,nikapata jawabu.
NI KWELI wapo wapo ambao hawajawahi kuonyeshwa upendo, wapo nasema wapo tena sana orodha ni ndefu!
Jumanne wiki hii Nilikuwa Pale Ufukweni karibu na Aga Khan hospitali, nikawaona watoto wawili wamejilaza huku jua kali likiwachoma, nikadhani homa kumbe wanapumzika. Nikiwatazama umri wao ni kama 10-13, wamechoka,wamechafuka.
Moyo ulinuma,nikakumbuka maneno ya yule binti baadaye nikamwambia nilichokiona siku hiyo. Wale watoto nilichofanya ni ubinadamu tu sitasema hapa nilifanya nini.

Watu wanazaliwa, tunadundwa utadhani tupo jeshini, lakini upendo wa kweli unabaki kuwa adimu, tunaugulia.
DUH

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

tehe teeh tehe!! kwa kifupi sijalelewa na mama yangu wala baba. nimelelewa na watu wengine tuuu. familia niliyokulia ilikuwa ya kitajiri lakini sikuwahi kupendwa kwa kweli. mimi nilikuwa mtu wa kudundwa tu na kutukanwa kila aina ya matusi.

basi siku moja nikampigia simu mama mmoja niliyekuwa na uhsiano naye wa mbali. yule mama hakuwa na namba yangu kwenye 4n book yake na hivyo akaniuliza wewe nani? baada ya kumweleza, akanijibu, aaahhh kumbe ni wewe mwanangu mpendwa, hujambo? basi nikwambie nilishindwa kuongea na simu kwa sekunde kadhaa nikijiuliza kwamba kumbe na mimi huwa napendwa? naweza kupendwa na kuitwa mwanangu mpendwa? ehe?

najiuliza kama niandikie kitabu lakini naona noma, sitaki kila mtu anihurumie na kunisikitikia.

koero, umenikumbusha mbali tangu utotoni. familia yangu ilikuwa na fedha na baba alikuwa mtu mkubwa, lakini sikuwahi kuonja upendo wa kupendwa kama mtoto. nimeishi mwenge, mamangu ameishi tegeta, lakini huwa naenda kwake mara mbili au tatu kwa mwaka, sina hamu ya kwenda kwake wala kwa ndugu yeyote kwa nini? sio ukorofi, bali hali halisi, no love even if there is money, food, drinx nk.

hata kama mimi nimtambuzi, lakini umenifanya machozi yanilenge lenge hapa cafe nilipo, lakini navumilia tu. inauma sana lakini. waheshimuni wazazi wenu ninyi mnaopendwa, daaaaaaa.

Christian Bwaya said...

Ni kweli kwamba kuna watu hawajawahi kuonja ladha ya upendo. Wakati nikisoma makala hii, nikajiuliza watu wa namna hii (watoto) huwezaje kuja kupenda wawapo wakubwa ikiwa wao wenyewe hawajui maana hasa ya upendo?

Kamala, nimeguswa na maneno yako. Una nafasi nzuri ya kufanya kitu kwa ajili ya hawa wanaosemwa katika makala hii. Usisite kunandika kitabu. Nadhani una kila sababu ya kufanya hivyo.

Kazi nzuri Koero.

Subi Nukta said...

Nadhani kukosekana upendo kwa watoto ni chanzo kikubwa sana cha kupotoka kwa maadili katika jamii. Watoto wanapoukaribia ujana na kuanza kukabiliana na mihemuko ya mwili, ikiwa hawakuwahi kuoneshwa upendo, mara nyingi sana kushindwa kuonyesha upendo kwa wengine, aghalabu, hushindwa kujenga mahusiano thabiti na ikiwa wanafanikiwa ama kujilazimisha kufanya hivyo, mara nyingi huwa wanakwama katika kujenga familia bora. Wnashindwa namna ya kupenda watoto wao wenyewe wa kuwazaa (ikiwa watajaliwa kupata watoto). Watawezaje ikiwa hawajakulia upendo? Hii ni ngumu kweli pia hata kwao wenyewe, ngumu sana.

Kwa bahati mbaya wengine hujitahidi kulipiza makosa ya wazazi wao kwa kuonesha upendo kwa watoto wao kwa njia ya kuwadekeza. Kwa kuwa hawakufunzwa wala kukulia upendo, kwao huwa ni vigumu ama hushindwa kabisa kujua ni kwa namna gani warudhishe upendo kwa watoto wao, na kwa bahati mbaya, matokeo yamekuwa ni kuharibu kwa sababu ya kudekeza. Nasema hivi kwa hakika kuwa nimeyaona yakitokea katika familia niliyokulia.

Mambo mengi sana huwa tunajifunza kwenye maisha bila kuhudhuria elimu za madarasani ndiyo maana huwa tunashauriwa sana kusema na kutenda mazuri mahali ama sehemu yoyote ile ambapo watoto wapo. Kwa familia zinazozingatia hili utagundua kuwa si rahisi kumwona baba na mama wakirekebishana ama kurushiana maneno ya kejeli mbele ya watoto, mara nyingi mmoja akiona mwenzie anavuka mpaka basi ataazimu kuwa kimya kuwanusuru watoto ama wataondoka pamoja na kulumbania chumbani ama mbali. Wale wanaoshindwa kuzuia jazba na kurushiana maneno mbele ya watoto huwa wanapeleka ujumbe wa kuchanganya sana kwenye akili ya mtoto kwani mtoto anashindwa kuelewa ni kwa vipi kinywa hicho hicho kilichosema 'nakupenda mwanangu' kitoe kashfa kwa mtu mwingine anayestahili heshima? Haifai hata kidogo kuwakwaza watoto wadogo hasa kwa kuwa wanajifunza kwa maneno na matendo toka kwa watu waliowatangulia kiumri kwa kuwa hiyo ndiyo nguzo yao kuu.

Watoto wanaokosa upendo mara nyingi kwa kujua ama kutokujua hujikuta katika wimbi kubwa la mawazo mkanganyiko ya hasira, wivu, chuki, kutokuamini n.k., muda ambao akili ingepaswa kufikiria juu ya elimu na maendeleo ya mbeleni.

Nimewahi kujitolea kutembelea na kuketi na kucheza na kuimba na kuwasikiliza watoto katika kituo cha kulelea watoto yatima, Kurasini, Temeke - Dar es Salaam na katika kituo cha Faraja, Mgongo - Iringa, hata katika Kijiji cha Wazee cha Mzimbazi, Ilala - Dar es Salaam, nilichokiona kwa hawa wote ni huzuni kubwa sana katika watoto waliokosa matumaini kutokana na kukosa upendo, hilo tu. Mtoto akiulizwa ni kwa nini ametoroka nyumbani anasema, kwa sababu baba alikuwa hanipendi, au mama alikuwa hanipendi. Kwao kutokupendwa ni sawa na kunyanyaswa.

Mara nyingi watoto wanaoitwa wa-mitaani ama wanaotoka katika mazingira magumu wanahitaji upendo tu ili kurejea katika njia njema.

Upendo unaweza kubadili sura za kukatisha tamaa na zenye ukatili kuwa matumaini na huruma ya hali ya juu. Upendo wa kweli ni ule wa maneno yanayoambatana na vitendo!

Ninajua kupenda na ninajua kutokupendwa. Iwe ni upendo wa Mzazi ama Rafiki ama Ndugu ama Jamaa ama Mgeni ama Mfanyakazi nk ni kitu cha thamani na cha kujali sana! Siku zote iwepo na itawale hali ya upendo! Sitamani hata chembe moja ya chuki! Bila upendo inakatisha tamaa jamani! Inauma sana na inakera!

Create friendship.
Strengthen unity.
Spread love.
Appreciate life.
Upendo Daima!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

where there is love, there is trust, where is trust, there is friendship, where is frienship, there is peace. therefore love is peace, friendship, help, humanity, etc. I love u all