Monday, March 9, 2009

VACATION YA ARUSHA NA USHAURI WA ASIMWE WENYE UTATA

Hizi ndizo habari zinazonifaa
Habari za siku wapenzi wasomaji wa blog hii.
Samahani kwa ukimya wa siku kadhaa uliyosababishwa na misukosuko ya hapa na pale ya kimaisha. Wapenzi wasomaji yaliyopita si ndwele bali tuganga yajayo.

Vacation yangu ya Arusha ilikuwa ni nzuri kwani ilinikutanisha na ndugu zangu niliokuwa nimepoteana nao kwa takribani miaka mitatu, na pia nilibahatika kutembelea urithi wetu yaani mbuga ya wanyama ya ngorongoro pamoja na vivutio kadhaa yote hiyo ilikuwa ni kuupa mwili raha na kutuliza akili.

Pamoja na kwamba nilikuwa na fursa ya mtandao lakini sikuwa na muda wa kukaa na kuandika kwani sikutaka kuchanganya mambo.
Katika kipindi hicho nilichokuwa Arusha nilibahatika kuzitambaulisha Blog zetu hizi kwa ndugu jamaa na marafiki na nilitumia muda mwingi kueleza faida ya blog kwani wengi niliozungumza nao walidhani kuwa kumiliki Blog ni ujasiriamali kwa maana kupata ujira.

Na nilipowaeleza kuwa hakuna ujira wowote unaopatikana, walinishangaa sana na kunihoji kuwa ina maana gani kupoteza muda wangu kwa kitu kisicho na mshiko.
Nilitumia muda mwingi kuwaeleza faida za blog mpaka wakanielewa.

Jioni moja nilikaa na binamu yangu mtandaoni aitwae Asimwe, nilikuwa namfundisha mambo mbali mbali kuhusiana na mtandao. Asimwe ndio amemaliza kidato cha sita na sasa anasubiri majibu ya mitihani kama atabahatika kujiunga na chuo kikuu kwani hiyo ndio ndoto yake.
Nilitumia muda huo kumuonesha mijadala mbalimbali niliyowahi kuiweka katika blog yangu pamoja na maoni ya wachangiaji mbalimbali waliowahi kuchangia. Pamoja na kwamba alifurahi kusoma mijadala yangu na pia kupitia blog za wanablog wengine ambao nimewaunganisha na blog yangu lakini alikuja na ushauri.

Asimwe alinitaka nibadili namna ya uandishi wangu wa blog, alidai kuwa hafurahishwi na mijadala yangu, kwamba imekaa kisiasa zaidi kitu ambacho si kizuri sana kwa umri niliokuwa nao, hata hivyo kuna maeneo alikubaliana na mimi kimtazamo lakini alinishauri nianze kuandika habari za urembo na hasa zinazohusiana na mashindano ya urembo na mavazi au hata habari za mapambo ya nyumba na bustani za maua kwani hizo ndio habari za maana ambazo zitapata wasomaji wengi hasa wanawake.
Alidai kuwa mijadala ninayoiandika inafaa zaidi kama ikiandikwa na wanaume.

Nilimsikiza kwa makini sana binamu yangu huyo ambaye pia ni rafiki yangu mkubwa. Ukweli ni kwamba sikumpa jibu la moja kwa moja bali nilimwambia anipe muda nifikirie kwani hayo mambo anayotaka niandike sio sababu ya kuanzishwa kwa Blog hii ya VUKANI.
Kwa hiyo inabidi niwasilishe ushauri huu kwa wasomaji wangu ili nao watoe maamuzi kama nibadilishe sera na kuanza kuandika habari za urembo kama nilivyoshauriwa?

Naomba kuwasilisha

9 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Dah!! Asimwe weee. Hujui kuwa wakati wa kujikomboa ni sasa? Kutegemea wanaume waandike kuhusu matatizo ya wanawake kunayafanya matatizo hayo yasiandikwe kwa hisia ama mguso halisi. Kwani umeshawahi kumuona naibi waziri Mwanaume akisoma hotuba ya waziri wake wa kike kwenye sherehe ama tukio la kinamama? Inakuwa ngumu kutilia mkazo na kuwakilisha hisia na kila kitu maana kuna vitu ambavyo vinaelezeka na kujengewa hoja na yule aliyepitia. Yaani yule "aliyenyewa na mvua" ndiye awezaye kuisifia ukajua kilichomsibu. Ndio maana uwepo wa dada zetu humu una maana na nguvu hasa katika hoja ziwahusuzo (japo uwembo nao wawahusu)
Lakini wacha nikupongeze "wa port" kwa kuwa na ujasiri wa kumueleza binamuyo juu ya kile uaminicho na hasa kwa kuwa ni ushauri.
Ila ushauri toka kwangu ni kuwa usijitahidi kulenga katika MAZOEA. Hilo ni tatizo na litaifanya jamii yote iamini kuwa vitu fulani ni vya kina fulani ama kazi fulani ni za kina fulani. Ni kama kusema ukipata maksi fulani kidato cha nne huna la kusomea zaidi ya ualimu na huko ndiko walikokwama wengi. Ama wale waaminio kuwa ukishindwa majaribio kadhaa basi achana na harakati za uvumbuzi unazotaka kufanya.
Waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali ni wale walioweza kuvuka mipaka ya mazoea, ni wale waliojifikiria nje ya kawaida na kujua kuwa wanaweza kuwa sehemu ya kubadili maisha kuelekea mafanikio zaidi. Ni wale ambao hawakubwetekwa na "mfumo wa maisha wa sasa bali wakapanga sasa mfumo wa maisha"
Basi natumai matokeo yako yakitoka, utafanya maamuzi ya nini cha kusomea na nini unataka kufanya si kulingana na mazoea, bali uwezo na utashi wako.
Dada, karibu tena
Baraka kwenu

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli ni ushuri mzuri, lakini kila mtu anafuaata moyo wake unamwambia nini.Ni kweli kama alivyosema mzee wa changamoto kuandika mambo ya hisia kwa mwanaume inaweza kuwa ngumu sana.Naamini wewe ndiye MUAMUZI kwani unajua nini unataka na una malengo gani.Na karibu tena nilikumiss

Simon Kitururu said...

@Dada Koero: Kumbe dada Koero wewe ni mwanadada!


DUH!


Napata matatizo saa nyingine kujua kama ushauri ni ushauri.:-(

nyahbingi worrior. said...

samahani fungua kurasa ya kuchangia mawazo kuhusu jumuiya ya wanablogu tanzania.

http://blogutanzania.blogspot.com/

www.ringojr.wordpress.com

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

hiyoi ndiyo dunia tuishiyo. kuna dunia nyingi sana na kuna ugumu wa kuelezea tofauti kati ya ajuaye na asiye jua. ni vigumu kujua nani yuko sahihi kwa vp katika jamii ya watu./

rejea maneno ya plato ya allegory of the cave

Christian Bwaya said...

Koero,

Sijui kwamba nitakuwa nashauri ama najisemea yale ninayoyaamini. Lakini vyovyote iwavyo, ngojea niandike.

Inapendeza sana kama kila blogu itatupa vitu vya tofauti. Kwamba unapotembelea blogu fulani basi unategemea kusoma mambo yenye mwelekeo fulani kwa kina kinachostahili.

Tunapokuwa na blogu zinazojadili mambo yanayofanana, mimi sioni kama hiyo inaweza kuwa faida. Kwani tunaweza kufika mahali pa kuandika kila kitu (general) kwa juu juu. Itafika mahali tutashindwa kutafiti tunayoyaandika na hivyo kubaki kuandika maoni yanayotokana na hisia ama ushabiki.

Miaka ile ya 2005/6, karibu kila blogu ilikuwa inajadili siasa. Na ilikuwa ukipita kwenye blogu (zote) unaweza kukuta jambo lilelile likijadiliwa. Sasa hii kwangu sikuona kwamba ni faida (kwa sababu zangu).

Nafurahi kwamba mpaka sasa tumeweza kuwa na blogu anuai zenye kuchambua masuala mengi zaidi ya yale ya siasa. Mifano iko wazi katika hili na watu wanafanya kazi nzuri.

Kwa hiyo ninataka kusema nini.

Njoo na wazo hilo jipya. Fanya kitu ambacho wengi tumeshindwa kukifanya. Tupe undani wa eneo hilo kwa kina kiasi kwamba ifike mahali tukitaka kusoma mambo yahusuyo urembo na mambo kama hayo tunafikiria vukani.

Hiyo itakuwezesha (kama nilivyogusia hapo juu) kupata muda wa kutosha kutafiti kwa kina (ikiwezekana) yale unayoyaandika kiasi cha kutupa maarifa yanayozidi maoni.

Nimepakumbuka Arusha. Hasa mwezi wa kwanza nilipokuwa nikibadili homepage adress kwenye vioski vya mtandano ili kutangaza blogu zetu.

Kila la heri dada Koero.

Koero Mkundi said...

DUH!!!!!!!!!!
KAAAAAZI KWELI KWELI.
NAHITAJI KUTAFAKARI..........

Albert Kissima said...

Mimi ninafikiri ni bora dada Koero ukaandika au kukiongelea kile kinachogusa moyo wako.
Kwa alichokiongelea Bwaya,nachelea kuwa tofauti naye kidogo.Mimi nafikiri mtu anaweza kuongelea chochote kile anachoona kina umuhimu katika jamii.Iwe siasa,michezo,sanaa na mambo mengine ya kijamii.
Kwa mfano Koero akianza kuzungumzia maswala ya urembo,mijadala kama ya kina mama wenye umri mdogo ungeibuka lini? msomi ni nani,nk.je jambo fulani ktk jamii likimgusa ambalo halihusiani na urembo afanye kitu gani? Sio kwamba alitoe wazo lake tu halafu wenye ujuzi au wenye maelezo ya kina wachangie?
Ni hayo tu.

Christian Bwaya said...

Changamoto ya Kissima nimeipata.

Labda niweke vizuri hapa. Kwanza, uandishi mahsusi (specific) haumaanishi kuingilia eneo usilolijua vyema wala kulipenda. Itashangaza leo nikija na wazo la kuzungumzia mpira wa miguu ili tu kuonyesha tofauti wakati sifuatilii masuala hayo. Uandishi mahsusi unamaanisha kuchagua eneo maalumu la kuandikia,ambalo bila shaka unalipenda na umejiridhisha kuwa na ufahamu nalo. (Hata kama mtatokea kufanana na mwingine)

Mfano mpaka sasa nikitaka picha (habari mpyampya) naenda kwa Michuzi ama kwa Mjengwa, Charahani, Miruko na wengine. Nikitaka teknolojia naenda kwa Ndesanjo ama Mushi. Siasa yuko kaka yetu Everist na Ngurumo. Mashairi na Fasihi wapo akina Serina, Mtanga, Mkwinda, Sandra. Falsafa yupo Kitururu nk. Mifano ipo mingi.

Ushauri wa kuzungumzia urembo, kwangu hapo ni mia kwa mia kwa sababu unayaweza mambo hayo kama ulivyosema.

Tena tutafurahi wakija na wengine na mawazo ya kujadili Dini/Imani, Michezo, Sayansi, Utamaduni, Malezi nk. Hii itasaidia kuboresha kazi zetu zaidi. Tukitaka kuandikia 'kila kitu' tutajikuta tunatomasa tomasa 'kila kitu' (superficially). Na pia kuwa mahsusi haimaanishi kuachana kabisa na maeneo mengine(japo mara moja moja).

Aidha, pamoja na kwamba blogu ni uwanja wa majadiliano, kuyaendesha majadiliano ya eneo mahsusi kunahitaji ubobezi wa aina fulani katika eneo husika. Hata kama wachangiaji wanatarajiwa kuwa na uelewa mpaka kuliko mwanzisha mjadala, bado 'uelewa' wa huyo aliyeanzisha mjadala katika mada husika unategemewa kuwa si haba ili kuongoza mjadala husika. Vinginevyo unaweza kujikuta ukishindwa kujua hata wanaojadili wanawazungumzia nini.

Kwa hiyo nirudie kuunga mkono wazo la kuandika urembo nikiamini tutapata maarifa zaidi yahusuyo mitindo, mapambo ya nyumba, uvaaji sahihi/kumechisha hi hi hi hi, mitindo ya kunyoa na kadhalika na kadhalika.