Thursday, May 28, 2009

HEKAYA ZA BIBI KOERO!!!

UKISHANGAA YA MUSA

Hivi mnakijua kisa cha huu msemo wa “ukishangaa ya Musa utakutana na ya Firauni?
Basi leo ngoja niwasimulie kisa hiki ambacho nilisimuliwa na Bibi Koero nilipoenda kumsalimia mwaka juzi.

Kisa chenyewe sina uhakika kama ni kisa cha kweli au ni hadithi ya kusadikika na hekaya za bibi Koero katika kutoa mafundisho kwa wajukuu zake, si unajua jinsi bibi zetu walivyojaaliwa hekima kwa kutoa mafunzo kwa wajukuu zao kwa njia ya mafumbo misemo na hadithi za kufikirika ambazo zimejaa nahau na mafunzo.

Haya ungana na mimi katika simulizi za kisa hiki……

Hapo zamani sana enzi za himaya ya Firauni (Farao) kulikuwa na mivutano ya kimamlaka kati yake na Musa.(Yule Musa anyesimuliwa katika Biblia, aliyewatoa wana wa Israel kule utumwani Misri na kuwapeleka katika nchi ya ahadi)
Firauni alikuwa akishidana na Musa ambaye alikuwa akiongozwa na Mungu.
Basi ilikuwa ni kawaida watu kwenda kwa Firauni kupeleka mashauri yao inapotokea kutofautiana.
Firauni alikuwa akitolea maamuzi mashauri hayo, ambapo maamuzi yake mengi hayakuwa na haki na yalijaa utata mtupu. Lakini ikatokea baadhi ya watu wakawa hawaendi tena kwa Firauni kwa kuwa walipoteza imani kwake na badala yake wakawa wanaenda kwa Musa ambaye alikuwa akisifika sana kwa kutoa maamuzi ya haki na yaliyokubalika na pande mbili.

Basi ilitokea mtu mmoja alikuwa akisafiri kwa miguu, kutoka mji mmoja kwenda mji mwingine, na kama unavyojua zamani kulikuwa hakuna usafiri wa magari au ndege, sana sana ilikuwa ni ngamia tu.
Wakati akiwa njiani akiendelea na safari yake alijisikia njaa na kwa mbali aliona shamba la mahindi, alipofika katika shamba hilo akakata mahindi mawili matatu na kukoka moto pale pale shambani na kuyachoma kisha akala na baada ya kushiba akaondoka zake na kuendela na safari yake…
Mara mwenye shamba akafika katika shamba lake na kukuta kuna mahindi yame katwa na kuchomwa pale pale shambani na kuliwa, akaamu kufuatilia nyayo za mwizi wake..

Yule mtu alikuwa akiendelea na safari yake bila kujua kuwa kuna mtu anamfuatilia nyuma.
Wakati akiendelea na safari yake mara akaona njiwa mzuri aliyenona yuko juu ya mti, akaokota jiwe na kumrushia yule njiwa na kumpiga sawia.
Akamchukua na na kumchinja, shida ikawa ni wapi atapata moto ili amchome njiwa wake na kumla.
Alipoangalia kwa mbali aliona kuna moshi unafuka, akaamua kuufuata ule moshi mpaka akatokea kwenye kijumba kimoja cha masikini mmoja na mkewe, alipobisha hodi akatoka mama moja mjamzito kwenye hiyo nyumba. Mama huyo alikuwa peke yake kwani mumewe alikuwa hayupo alikwenda kuhemea kijiji cha jirani.
Yule mama alikuwa amekoka moto nje ya nyumba kwa ajili ya kupikia, yule bwana akaomba ambanike njiwa wake, akaruhusiwa.

Wakati anambanika yule njiwa alikuwa akinukia ile mbaya, kiasi cha kumtamanisha yule mama mwenye mji,lakini kutokana na kutomjua yule bwana akaogopa kumuomba.
Basi yule bwana alipomaliza kubanika njiwa wake na kuiva akaaga zake na kuondoka huku akitafuna njiwa wake na kuendelea na safari.
Huku nyuma yule mama kutokana kutamani sana yule njiwa akapata uchungu sana kwa kitendo cha yule bwana kuondoka bila hata kumpa kipande cha nyama,na kutokana na kuwa na kisirani na hasira mimba ikatoka.
Mumewe aliporudi akamkuta mkewe amelala nje ya nyumba akiugulia kwa maumivu ya tumbo,alipomchunguza akagundua kuwa mimba imetoka.

Alipomdadisi, mkewe akamsimulia kisa cha yule mpita njia na njiwa wa kubanika kuwa ndio sababu ya mimba kutoka. Yule bwana akawa anamuhudumia mkewe, na mara yule bwana aliyeibiwa mahindi katika shamba lake akafika pale na kukuta yale matatizo, na baada ya kusimuliwa habari ya mpita njia na njiwa wa kubanika ndipo na yeye alipoeleza kisa cha kuibiwa na mahindi na kumtuhumu mpita njia na njiwa wa kubanika kuwa ndiye muhusika.

Ikabidi waungane muibiwa mahindi na yule, mkewe aliyepoteza ujauzito kumfuatilia yule mpita njia.
Hawakwenda umbali mrefu wakamkuta mpita njia amejipumzisha chini ya mti akipunga upepo, wakamkamata na kumweleza makosa yake, mpita njia akajitetea kuwa hakuiba mahindi bali alikata na kuchoma pale pale shambani kutokana na njaa na kuhusu mimba kutoka alikanusha kuhusika kwa sababu yeye alijichomea njiwa wake na kujiondokea zake baada ya kuruhusiwa na yule mama mwenye nyumba na wala hakujua lililotokea nyuma yake.

Wale watu hawakumuelewa na wakakata shauri wampeleke kwa Musa ili kumshitaki.
Walipofika kwa Musa, wote walisikilizwa kila mtu kwa nafasi yake na baadaa ya Musa kutafakari akatoa hukumu kuwa yule bwana aadhibiwe kwa kuchapwa bakora kisha aondoke zake….
Duh!! Ile hukumu haikuwaridhisha wale jamaa, ikabidi waende kwa Firauni, wakitegemea kupata haki zaidi kwani hukumu ya Musa waliiona kama imempendelea yule mpita njia.

Walipofika kwa Firauni, kama kawaida yake aliwasikiliza wote kila mtu kwa nafasi yake, kisha akatoa hukumu.

Hukumu nyenyewe inasemaje…soma hapa chini…

Firauni akasema yule mpita njia akabidhiwe shamba avune mazao yote kisha apande upya na kuyatunza mpaka yafikie katika hatua kama ile aliyoikuta ndipo amkabidhi mwenye shamba lake. Na kuhusu yule bwana ambaye mkewe alipoteza ujauzito, akasema yule mke akabidhiwe kwa mpita njia akakae nae mpaka apate ujauzito, ukishafikia miezi kama ile iliyotoka amrejeshe kwa mwenyewe….
Duh!!! Jamaa wakachanganyikiwa na ile hukumu wakaondoka pale kwa Firauni kimya kimya na wakamua kumsamehe mpita njia kwani hakuna aliyekuwa tayari kutekeleza ile hukumu.
Na hapo ndipo ulipozuka msemo wa
“Ukishangaa ya Musa utakutana na ya Firauni”

Nikipata nafasi nitawasimulia kisa kingine kizuri cha hekaya za bibi Koero…

2 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Hata kama hakuna ukweli katika Hekaya hii ya Bibi Koero, lakini kuna mantiki ndani yake tunayoweza kuitumia katika maisha yetu ya leo. Kwanza ni kujua kile ambacho wengine husema kuwa "kwa lolote likutokealo, kuna bayta zaidi ya hilo ambalo lingeweza kukutokea". Mafunzo hapa ni mengi. Tunafunzwa kuwa si wakati wote hukumu zitasimama upande wetu hata kama mwenye kuhukumu anafanya hivyo akiamini ni kwa faida yetu. Pili ni kutambua kuwa udogo na ukubwa wa kitu utategemea unalinganisha na nini maana hawa jamaa mwanzo waliona hukumu ya Musa ni ndogo lakini walipopata ya firauni, wakaona ya Musa ni kubwa zaidi. Nnne ni kutambua kuwa hukumu zaweza kuwa za kufunza ama kukomoa. Na mara zote zenye kukomoa hazina faida kwa mhukumu, bali ni kumaliza hasira na mwishowe kujiona mjinga.
Haya yote yaliyo katika hekaya za Bibi Koero tunaona yanatokea maishani mwetu sasa. Kwa hiyo tukisoma hapa, tukaelimika badala ya kuburudika tutaibadili jamii tuishiyo

Yasinta Ngonyani said...

Nakubaliana na kaka Mubelwa! labda nami niseme machache ni kwamba hapa inaonekana hawa jamaa walikosa imani. Walitegemea jamaa atapewa adhabu ya kunyongwa. Ndi maana waliendelea kuhakikisha.