Wednesday, May 6, 2009

SUBIRA,UVUMILIVU NA UBUNIFU VIKALIPA!

Kamwe sikukata tamaa

Ilikuwa ni mwaka 1999 baada ya kuwa nimetumikia shirika la umma kwa takribani miaka 20 nilijikuta nikiwa miongoni mwa wafanyakazi 70 wa shirika hilo tuliotupwa nje ya ajira kwa kile kilichoitwa ridandansi, ili kulinusuru shirika hilo ambalo lilianza kuyumba kutokana na ushindani wa kibiashara baada ya serikali kufungua milango kwa wawekezaji kutoka nje.

Baada ya kupata mafao ambayo hata hivyo hayakulingana na muda niliotumikia shirika hilo, nilikaa chini na kuanza kutafakari mustakabali wa maisha yangu ya baadae na familia yangu.

Nilikuwa bado naishi nyumba ya kupanga nikiwaa na mke na watoto wawili, wa kwanza wa kike aliyekuwa na miaka 5 na wa pili wa kiume aliyekuwa na miaka 2. Nilikuwa na jukumu zito la kuhakikisha watoto wangu wanapata elimu bora, Je hilo litawezekana baada ya kupoteza ajira? Nilijiuliza.

Katika kipindi cha miaka hiyo ishirini niliyofanya kazi katika shirika hilo, sikubahatika kujenga, ingawa nilifanikiwa kununua kiwanja maeneo ya Tabata Segerea, ambapo palikuwa ni kama porini wakati huo, tena kiwanja chenyewe kilikuwa ni cha mkopo ambao niliumaliza mwezi mmoja kabla sijapewa ridandansi.

Ukweli ni kwamba sikubahatika kujenga kutokana na maslahi kuwa madogo, kwani tulikuwa tukilipwa mshahara mdogo na kulikuwa hakuna marupurupu ya kutosha na hivyo nikajikuta nikiwa na maisha magumu.

Hata hivyo ilibidi nianzishe mradi mdogo wa kupiga picha mitaani na hata kazini ili kujiongezea kipato, ingawa sikuwa napata hela za kutosha lakini si haba, fedha nilizokuwa napata zilikuwa zikinisaidia kupunguza ukali wa maisha.

Kwa upande wa mke wangu, naomba nikiri kuwa hakuwa na msaada sana kwangu. Alikuwa ni mama wa nyumbani, lakini hakupenda kujishughulisha kama wanawake wengine. Alikuwa ni mtu wa kushinda nyumbani kutwa akijiremba na kushindana na wanawake wenzie kwa mavazi, ilikuwa kila Khanga au Vitenge vipya vikiingia hakutaka vimpite na hata mtindo mpya wa mavazi ukiingia pia hakutaka umpite, nilikuwa na wakati mgumu kumridhisha kutokana na tamaa aliyokuwa nayo.

Tofauti na wenzangu niliokuwa nikifanya nao kazi, wake zao walikuwa ni wachapa kazi, hawakubweteka, na baadhi yao walifanikiwa hata kujenga nyumba zao baada ya kuunganisha nguvu kati yao.

Waliosema, nyuma ya mafanikio ya mume kuna mke na nyuma ya anguko la mume kuna mke hawakukosea .
Hii ina maana gani? Ina maana kuwa kufanikiwa kwa mwanaume au kutofanikiwa, kunategemea na aina ya mke aliyeoa.

Nakumbauka nilishauriwa sana na baba yangu nikaoe kijijini kwetu lakini nilikataa kwa madai kwamba siwezi kuoa kijijini, kwa kuwa wanawake wa kule ni washamba, kwa hiyo nikaamua kuoa hapa hapa jijini Dar es salaam, binti wa kingindo aliyezaliwa na kukulia mjini.

Tulikuwa tukiishi Magomeni wakati huo, eneo lililojaa uswahili, ushindani na na ushabiki wa kishagingi.
Hata kwao na mke wangu kulikuwa na uswahili mtupu, dada zake wote watatu walikuwa wameolewa na kuachika na wote wako nyumbani kwa wazazi wao, sijui ni kwa nini sikuliona hilo.

Katika kipindi ambacho nilikuwa nyumbani baada ya ridandansi nilikiona kigumu hasa, kwani baada ya mke wangu kujua kuwa nimepata mafao ya kuachishwa kazi alianza kutamba kuwa wanawake pale mtaani watamkoma, alikuwa na mahesabu ya kuvaa vito vya thamani na mavazi ya gharama ili wajue kuwa na yeye anazo.

Akili yake ilikuwa ni tofauti kabisa na ya kwangu, mimi nilikuwa na mipango tofauti kabisa .
Nilikuwa na mpango wa kupandisha vyumba viwili haraka haraka kule katika kiwanja chetu kisha tuhame ili kuepuka gharama za kulipa kodi ya pango, halafu nianzishe biashara ili niweze kumudu kupambana na ugumu wa maisha.

Siku moja nikiwa nimetulia chumbani usiku nilimuita mke wangu ambaye alikuwa nje akipiga soga na wanawake wenzie, alipofika nilianza kumueleza juu ya mipango yangu, lengo likiwa ni kumshirikisha katika mipango yangu niliyokuwa nimeiratibu tangu nilipopewa ridandansi.

Mke wangu alipinga kwa nguvu zote mipango yangu niliyopanga na hakutaka kunisikiliza, kwa maoni yake alitaka eti tugawane yale mafao ili kila mtu afe na chake kwani hakuwa tayari kwenda kuishi huko porini Segerea. baada ya kumweleza kuwa nilikuwa nimedhamiria kufanya kile nilichokisema na nilikuwa sitanii, alianza kuzungumza kwa sauti kubwa na kutukana.

Nilihisi hasira zikinipanda nikaamua kuondoka na kwenda kuzurura kidogo ili kupoteza mawazo, Nilirudi majira ya saa tano usiku, nilipofika nyumbani nilipokelewa na matusi na kashfa kutoka kwa mke wangu, kwani alinituhumu kuwa nilikwenda kwa wanawake wengine kwa kuwa sasa nina fedha.

Nilijikuta nikimpiga kwa hasira na kama si wapangaji kuamka kutokana na kelele za mke wangu na watoto labda ningeua, kwani nilipandwa na hasira kupita kiasi, na tangu nimuoe mke wangu siwahi hata kumfinya, hatua ya mimi kumpiga ilimshangaza hata yeye. Ndio tulikuwa tunatofautiana lakini haijawahi kufikia hatua ya kupigana.

Wapangaji wenzangu walipofika pale waliamua ugomvi wetu halafu wakinitoa nje ili nisije nikaendelea kumpiga mke wangu kwani alikuwa akiendelea kunitukana na kunikashifu hadharani bila ya aibu.

Aliondoka usiku ule ule na taxi kwenda kwao akiwa na watoto wetu maeneo ya mwananyamala ambapo ndipo wazazi wake walipokuwa wakiishi.
Baba wa mke wangu alikuwa ni mfanyakazi Bandarini na alifanikiwa kujenga nyumba nne hapa jijini Dar es salaam mbili zikiwa Mwananyamala na nyingine mbili zikiwa Kinondoni, na hiyo ndiyo iliyokuwa ikimpa mke wangu kiburi.

Niliingia ndani na kujifungia na kujitupa kitandani, na kuanza kutafakari juu ya lile tukio. Sikupata usingizi kabisa kutokana na mawazo niliyokuwa nayo, na nilijilaumu sana kwa kile kitendo nichokifanya cha kumpiga mke wangu. Nilijiona mjinga kwa kitendo kile.

Siku iliyofuata nilikwenda ukweni kwangu asubuhi na mapema ili kusuluhishwa. Nilipofika nilipokelewa na baba mkwe wangu na baada kusalimiana waliitwa wazee kadhaa wa pale jirani ili kuweza kusuluhishwa.
Katika kikao hicho mke wangu alidai talaka na alitaka fedha za mafao nilizopata baada ya kupewa ridandansi kazini tugawane na pia kile kiwanja chetu kilichokuwa segerea kiuzwe na fedha tugawane vile vile ili kila mtu afe na chake, nilipinga wazo lile kwa nguvu zote kwani sikuwa tayari kutoa talaka, nilikuwa nawahurumia wanangu kukosa malezi ya wazazi wote wawili.

Baba yangu mkwe alikuwa ni mtu mwenye busara sana hakuafiki wazo la mwanae na aljitahidi sana kumuelewesha mwanae kuwa kile ninachotaka kukifanya sio kwa ajili yangu peke yangu bali ni kwa ajili yake na watoto, kwani si vyema kukaa katika nyumba za kupanga, na watoto wanakua. Lakini mke wangu kwa kushirikiana na mama yake pamoja na dada zake walishupalia talaka itolewe na mali igawanywe .

Wale wazee waliokuwepo katika kile kikao walijitahidi kutoa hekima zao ili kuinusuru ndoa yangu lakini haikusaidia.
Mwishowe ikaamuliwa shauri lile lipelekwe BAKWATA, baraza la kiislamu ili tuweze kusuluhishwa.

Nilirudi nyumbani nikiwa nimechanganyikiwa kabisa, sikulala usiku kucha nilikuwa nikiwaza juu ya mustakabali wa watoto wangu. Je maisha yao yatakuwaje baada ya sisi wazazi kutengana? Je watapata elimu kama nilivyokusudia?
Nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu.

Ungana nami wiki ijayo kumalizia kisa hiki chenye kufundisha….

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Koero kama haya uliyoyaandika ni kweli basi nampa pole huyo mume kwa kukataa ushauri wa babake kuwa hataki kuoa mke wa kijijini. Kwa vile ni mshamba. Na pia nasema hivi inaonekana huyo mke aliyemwoa alikuwa hajasoma au kama amesoma basi alikuwa mjinga. Kwa sababu kwanza yeye alikuwa hafanyi kazi ndio alikuwa mama wa nyumba ambayo ni kazi kubwa sana. Lakini inaoneakama alikuwa hawezi kufikiri mbali. Kwa sababu yeye alikuwa anawaza tu kuwa maridadi na kupewa kila kitu hajui wapi pesa zinatoka. Na la mwisho inaonekana hakuolewa na huyu bwana kwa penzi bali alikuwa anataka mali tu. Nasubiri kuona hiki kisa kitaishaje.

Godwin Habib Meghji said...

Nasubiria sehemu ya mwisho, Kuna kitu nakiona hapa

Anonymous said...

nasubiri hitimisho lake, nione maana tayari naona kuna darasa muhimu hapa.

Simon Kitururu said...

Nami nipo kati wasubirio kisa kimaliziwe.

Koero Mkundi said...

Haya waungwana, kutikana na maombi yenu nimeona ni vyema nikimalizie hiki kisa.
Naamini wote tutajifunza kutokana na kisa hiki cha kweli...

Mzee wa Changamoto said...

Si vibaya kujifanya mtabiri na kisha kusubiri hitimisho. Lakini nasubiri kuona jinsi wote walivyojifunza THE HARD WAY.
Nasubiri "toleo lijalo"