Thursday, June 25, 2009

TAKWIMU HIZI ZINATISHA!!!

Hali huku ni mbaya zaidi

Usiku wa jana nilikuwa nikiangalia kipindi cha Bunge.
Kilichonisisimua ni hoja iliyotolewa na muheshimiwa Zito kabwe mbunge wa Kigoma kupitia tiketi ya Chadema.
Muheshimiwa Zito alitoa hoja hiyo wakati bunge lilipokaa kama Kamati, na kilichonivutia katika hoja yake hiyo ambayo mwenyewe aliita kuwa ni ya kisiasa zaidi ni takwimu kadhaa alizotoa zinazoainisha maeneo mbali mbali ya kijamii hususana kiafya na vifo.

Muheshimiwa Zito Kabwe alisema kwamba, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa serikali iliyotolewa Novemba mwaka 2008 inaonyesha kwamba idadi ya Watanzania walio masikini iliongezeka kutoka 11 Milioni mwaka 2001 hadi 12.7 Milioni mwaka 2005na kwamba asilimia 75 ya watu hao masikini wanaishi vijijini.

Akiendelea kutoa hoja zake Muheshimiwa Zito alibainisha kwamba idadi ya watoto wanaokufa kwa mwaka inazidi kuongezeka na sasa kila mwaka watoto 800,000 ambayo ni sawa na idadi ya wakazi wa mkoa wa Lindi wanakufa.

Cha kusikitisha zaidi ni hili la wanawake 578 kati ya 100,000 wanaoenda kujifungua hupoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi.
Takwimu hizo zinabainisha kuwa kila baada ya dakika 60 Tanzania inapoteza mwanamke mmoja

Kwa kweli Takwimu hizi zinatisha, na sina uhakika kama kuna hatua zozote zilizoainishwa katika takwimu hizo japo kuonesha hatua zinazochukuliwa ili kupunguza au kuondoa tatizo hilo la njaa na vifo.

Wakati tulipokuwa tunaombwa kura tulibembelezwa sana na tuliahidiwa kuwa tutakuwa na maisha bora na ajira lukuki, lakini hata baada ya miaka takribani minne sasa hali inazidi kuwa mbaya kila uchao, na pengo kati ya matajiri na masikini linazidi kupanuka.

Kwa sasa niko Arusha, na mara nyingi nakuwa Karatu, kwa kweli hali ni mbaya na hasa baada ya uchumi wa dunia kuporomoka wakazi wa eneo hili wanakabiliwa na hali mbaya kutokana na kupungua kwa watalii.

Maeneo mengi ya hapa nchini yanakabiliwa na njaa na wananchi hawana hela kabisa.
Najua Mwakani watakuja tena na lugha tamu na vijizawadi wakitaka tuwape ridhaa ya kuendelea kutuogoza na kutokana na ufinyu wa uelewa hasa kwa watu wa vijijini, khanga na fulana vinatosha kabisa kupata ridhaa ya kuongoza halafu tunabaki tukiteseka kwa miaka mingine mitano………huu ni upuuzi kabisa

Sunday, June 14, 2009

CHANGAMOTO YA MZEE WA CHANGAMOTO

Rais Mstaafu wa Ghana Jerry Rawlings: Alipofanya mapinduzi na kuingia madarakani wengi walimuita Dikteta.

Naomba nikiri kuwa siku hizi nimekuwa mtu wa Kudesa. Hii nayo kanipa kaka Mubelwa Bandio mzee wa Changamoto. Link ya makala hii ameiweka hapa kibarazani akitaka kusherehesha maoni yake katika mada nyingine niliyoidesa kutoka Jamii Forum iliyouliza “Laana yetu ni nini hasa?” nami kutokana na kuvutiwa na mada hii ya mzee wa changamoto nimeona si vibaya nikiiweka hapa kibarazani kwangu ili kupata mtazamo tofauti kutoka kwa wasomaji wa kibaraza hiki


Ninapoangalia namna "tunavyokaririshwa" maana za nani ni nani, na kwanini ni yeye na kwa manufaa ya nani na nani awe rafiki na nani awe adui yake nasikitika sana. Tumepangiwa kila kitu kwa tafsiri ya wenzetu ambayo kwa hakika ni kwa manufaa yao.Mandela alikuwa "mkorofi" ( na dikteta fulani hivi) kwa kudai uhuru ambao baada ya kutambulika sasa anaonekana ni shujaa japo hajabadili alichofanya, Saddam alikuwa shujaa aliposhirikiana na wao kisha akawa dikteta alipopingana nao.
Gadafi aliyekuwa dikteta na kuonekana kama asiyewajali wananchi wake sasa kawa shujaa na "kiongozi safi" kwa kuwaruhusu "wakuu" kuingia na kukagua silaha zake japo hakuna alichobadili kwa wananchi.Luciano aliwahi kuimba kuwa "they're trying to control our minds, and treating us like swine.
They telling us who to love or hate as if they're great"Najua akitokea mtu akalazimisha baadhi ya mambo ya maana kutendeka nyumbani basi ataitwa dikteta (na kwa bahati mbaya nasi tutashabikia hata kama si tafsiri yetu).
Najiuliza akitokea "kiongozi" akalazimisha kusimamishwa kwa mikataba yote ya madini ili ipitiwe upya hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha viongozi wakuu waliosababisha mabilioni ya hasara serikalini wachunguzwe licha ya katiba waliyoshindwa kuitii kutosema hivyo hataonekana dikteta?
Je atakayelazimisha wabunge kujenga ofisi na kutumia muda mwingi majimboni mwao kama walivyoahidi wakati wa kampeni hataonekana dikteta?
Atakayelazimisha utendaji wa mikoa kulingana na rasilimali zake kuwanufaisha wananchi wake na kisha nchi nzima huyo hataonekana dikteta?
Najua kuwa atakayewafikisha viongozi wakuu mahabusu ataitwa dikteta kwa kuwa amekwenda kinyume cha katiba, lakini sijui kwa nini katiba imlinde yule ambaye ameivunja kujilimbikizia mali na kuitia serikali hasara kubwa?
Kama huyu atakayetenda haya niliyosema hapo juu, atakayevunja mikataba ya ujenzi wa miundombinu yenye utata, atakayehakikisha ahadi za wananchi zinatekelezwa na waahidi hasa wabunge, atakayeshurutisha matumizi mazuri ya rasilimali za wananchi kwa manufaa ya sehemu husika, atakayeshinikiza malipo kwa wafanyakazi ambayo mpaka sasa haijajulikana kwanini hawajalipwa ilhali waheshimiwa wanapata pesa zao bila malimbikizo, atakayehakikisha kuwa mkulima wa anapata senti zake zote alizoikopesha serikali na ambazo anatumia pesa nyingi kufuatilia kuliko atakazolipwa, atakayesimamisha ziara za nje na ndani za viongozi (zisizo za lazima) na atakayeamua Tanzania iwe ya manufaa kwa wa Tanzania kwa kutumia kila kilichopo
Tanzania ataitwa DIKTETA, basi namuombea awepo. Aje atufanyie hayo na nadhani tunamhitaji na anaweza kuwa suluhisho la awali kwa yaliyopo.
Maana sasa imekuwa kama alivyosema Kaka Evarist kuwa HAKI IMEKUWA FADHILA na twahitaji atakayeangalia haki na kama haki.
Nionavyo ni kwamba mfumo unaotumika kumpata mtu atayewania uongozi unapita katika ngazi na misaada ambayo mpaka aje kupatikana mgombea anakuwa kashirikisha "wataalamu" wa ufujaji ambao akichukua madaraka hataweza kusema lolote juu yao.
Pengine nionavyo mimi ndilo tatizo, lakini kuna ukweli kuwa tafsiri nyingine zinatufanya tuwachukie wale ambao wanaweza kutuletea mabadiliko ya kweli na badala yake tunaendeleza "kubebana na kufichana" ambako kunaendelea kutuweka tulipo.
Ni Mtazamo wangu tu na naendelea kutunza haki ya kukosea na kukosolewa.

Friday, June 12, 2009

LAANA YETU NI NINI HASA?

Tunazo rasilimali nyingi na za kutosha

Hii nimeidesa kutoka katika mtandao wa Jamii Forum, kutokana na kuvutiwa nayo nimeona si vibaya nikiiweka hapa kibarazani kwangu ili wasomaji wa blog hii waweze kuchangia mawili matatu,

Mara nyingi huwa najiuliza, hivi sisi tumelaaniwa? Na kama tumelaaniwa, ni laana gani hasa tuliyonayo? Ni nini hasa kinachosababisha tuwe hivi tulivyo? Sababu kubwa za kujiuliza hivi ni kutokana na hali yetu kimaisha, ikilinganisha na wengine karibu wote duniani. Na ukizingatia uwezo wa kirasilimali tulizo nazo. Nchi hii ina kila kitu kinachohitajika katika kuleta hali bora zaidi kwa watu wake.

1. Ina madini ya aina zote zinazoweza kupatikana duniani na zaidi (Tanzanite). Tunashindwa kuyavuna na kuamini kuwa watu kutoka nje ndio wanaoweza kutusaidia na sisi tukapata tija kwa kuwatoza 3% tu ya mapato yao. Ni nini hasa kinachotafuna akili zetu?

2. ina maji kila upande wa nchi yetu. Lakini bado mabomba yetu ni makavu na kipindupindu kinamaliza watu.


3. ina ardhi nzuri na ya kutosha kuliko nchi nyingi duniani (hakuna eneo lenye jangwa). Inatumikaje kuinua pato la mTanzania?


4. ina maliasili (hata dawa za kienyeji, misitu, mbuga za wanyama n.k.). Tunashindwa hata kuitangaza, kuitumia kupata tija. Kwanini hasa?


5. ina bahari yenye zaidi ya kilometer 1440. Maziwa yanayopakana na nchi jirani kila upande (Maziwa Tanganyika, Victoria, Nyasa). Tunayatumiaje?


6. Bahari na maziwa/mito ina samaki wa maji baridi na maji chumvi. Ila tunashindwa kuwavua, na wanaoweza kuwavua tunawakamata na hatujui tuwafanye nini.


7. Ina watu wakarimu, wenye akili na uwezo wa kufanya kazi. Kwa ujumla ina kila kitu isipokuwa hali bora kwa watu wake.

Ila wote ni watazamaji, walalamikaji na wasio na fursa yoyote ya kujiendeleza kwa uhakika na usawa. Kwa mtazamo wangu, nchi hii inakosa dira na uongozi wenye nia madhubuti ya kutumia rasilimali zilizopo katika kuleta tija. Swali ni je, kwanini pamoja na yote hayo tunashindwa kufikia malengo yetu na kudhani kuwa wahisani, matajiri duniani ndio wenye jukumu la kutusaidia kwa kile wanachopata kutoka kwao ambako wengi wao wala hawana tulichonacho hata kwa asilimia 10? Je ni laana gani inayotusumbua sisi waTanzania? Nini hasa kinachotakiwa kufanyika kujitoa kwenye laana hiyo? Nani hasa alietutupia laana kali namna hiyo?

Saturday, June 6, 2009

MIMBA MASHULENI BADO NI TATIZO!

Wengi huchanganyikiwa

Kuna wakati katika mojawapo ya makala zangu humu bloguni niliwahi kueleza juu ya mimba za utotoni. Makala hiyo niliipa kichwa cha habari kisemacho “VIBINTI NA MIMBA ZA UTOTONI!”

Hivi karibuni nimeandika kuhusu mkasa uliompata binti mmoja niliyempa jina la Anita, ingawa halikuwa ni jina lake halisi. Sioni sababu ya kurudia au kukumbusha kile nilichoandika kwa sababu naamini kuwa wasomaji wangu bado wanayo kumbukumbu ya mkasa uliompata binti huyo.

Kwa kuwa binti huyo alipata ujauzito akiwa ndio kwanza ameingia kidato cha pili na hivyo kukatisha masomo, nimeona ni vyema leo nizungumzie tatizo la mimba mashuleni.
Tatizo la mimba masuleni si geni sana kwetu, ni tatizo lililokuwepo na lipo na linaendelea kuwepo japokuwa wanasiasa na wanaharakati kadhaa wanaendelea kulipigia kelele.

Binafsi katika kusoma kwangu kuanzia shule ya msingi mpaka nilipomaliza kidato cha sita nimeshuhudia wasichana zaidi ya 40 wakishindwa kuendela na masomo kwa kupata ujauzito, Hapa nazungumzia wasichana niliosoma nao aidha darasa moja au shule moja kwa ujumla wake, achilia mbali wale waliofanikiwa kutoa na kuendelea na masomo, hapa nazungumzia wale walioshindwa kabisa kuendelea na masomo na ndoto zao kutoweka kwa kuporwa mustakabali wa maisha yao na wanaume wakware.

Tatizo la mimba mashuleni limekuwa ni sugu kuanzia shule za msingi, sekondari mpaka vyuoni kote huko hapafai. Yaani ni jambo la kawaida kabisa kusikia kuwa mwanafunzi fulani ana mimba ya mtu asiyemfahamu.
Kila mwaka kuna maelfu ya mabinti wa shule wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kupata mimba na hili sio tatizo la hapa nchini peke yake bali ni tatizo la bara la afrika, kwani ukiingia mtandaoni na kusoma takwimu kutoka vyanzo mbalimbali vya habari katika nchi nyingi za Afrika utakutana na mambo ya kutisha humo, kuna wanafunzi wengi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kujazwa mimba.

Hili tatizo sio tu linawasikitisha wazazi waliotumia fedha zao nyingi katika kumsomesha binti husika aliyepata ujauzito bali pia wanakuwa wameongezewa mzigo wa malezi ya mtoto asiyejulikana ni wa nani. Hii huwakatisha tamaa sana wazazi na ndio sababu wazazi wengi wanahofu ya kuwaendeleza watoto wao wa kike na elimu ya sekondari kwa kuhofia kupoteza muda na fedha zao bure. Kama tulivyoona kwa baba yake Anita alipokataa kumuendeleza mwanae na kutaka kumuoza kwa kile alichodai kuwa watoto wa kike hata wakisomeshwa hawainufaishi familia husika na badala yake hunufaisha familia ya wakwe zake, ingawa haikuwa hivyo kwa Anita, lakini mzee yule hatajiona kuwa alikuwa sahihi kwa kiasi fulani kutokana na binti huyo kupata ujauzito akiwa tu ndio ameingia kidato cha pili?
Hebu tuangalie sababu ambazo zinachangia wanafunzi kupata ujauzito:

Kwa kawaida mtoto yeyote wa kike akishafikisha umri wa kuanzia miaka 9 mpaka 12 anashuhudia mabadiliko katika mwili wake ikiwa ni pamoja na kuziona siku zake, hapa ndipo wazazi wanapopaswa kuzungumza na mabinti zao na kuwaelimisha juu ya kuyapokea mabadiliko hayo na namna ya kupambana na vishawishi vya wanaume na bila kusahau kuwaeleza ukweli kuhusu uwezekano wa kupata ujauzito iwapo watashiriki kufanya ngono. Namshukuru mama yetu alikuwa ni muwazi sana kwetu kiasi kwamba mimi na dada zangu tumemudu kuvuka hizo changamoto mpaka tumeweza kumaliza shule na wengine mpaka vyuoni.

Kama inavyotokea kwa mabinti na ndivyo inavyotokea kwa wavulana, nao wanapofikisha umri wa kubalehe hushuhudia mabadiliko kadhaa katika miili yao.
Nakumbuka mama aliwahi kutuambia wakati fulani, kuwa analolisema kwa watoto wake wa kike ndilo atakalolisema kwa watoto wake wa kiume vile vile, alisema hapo zamani angeweza kusema “huyu si mtoto wa kiume, yeye hana tatizo kwa sababu yeye ndiye anayefanya” lakini hali haiko hivyo siku hizi, kwani kuna gonjwa la ukimwi! Akichelea mwana ataishia kulia……
Mama yetu aliwahi kutuambia kuwa mapenzi ni kama umeme. Wote tunafahamu kuwa umeme ni nguvu inayotumika katika nyanja mbalimbali kuanzia majumbani mpaka viwandani na hutusaidia katika kurahisisha mambo mengi, lakini unapokuja vibaya ajali yake inaweza kuleta maafa makubwa na ya kutisha.

Vile vile hata swala la mapenzi nalo, iwapo mapenzi yatafanywa kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa iwe ni kimila au kidini, hakuna tatizo, lakini yakifanywa hovyo, matokeo yake wote tunayajua, ni kuishia kupata ujauzito, na katika hali ya kuchanganyikiwa mabinti wengi hufiria kutoa mimba hizo na matokea yake hupoteza maisha, wapo wanaojiuwa kwa kuwahofia wazazi, wapo wanaofariki wakati wa kujifungua kwa kifafa cha uzazi kutokana na kutohudhuria kliniki na kupata chanjo.

Wazazi wengi hawawajibiki katika kuwaelimisha mabinti zao na badala yake jukumu hilo wanawaachia waalimu ambao nao wanayo majukumu mengi ya kuandaa masomo na kufundisha,na hivyo maisha ya mabinti hao huwekwa rehani kwa wanaume wakware wenye ndimi zenye asali.


Mabinti wengi wamejikuta wakipata ujauzito kutokana na kutojua kuwa kucheza na wanaume ni sawa na kucheza na moto, na hiyo inatokana na kutopata elimu juu ya mabadiliko ya mwili na hisia za kimapenzi wanapokuwa wamevunja ungo kutoka kwa wazazi wao.

Kwa leo naomba niishie hapa, nikipata muda nitaendelea na mada hii wiki ijayo.

Wednesday, June 3, 2009

ANITA NA MIKASA YA DUNIA!

Niko Arusha kwa shughuli maalum ya kifamilia na Jumapili iliyopita nilikwenda kumtembelea rafiki yangu mpendwa Doreen niliyesoma nae huko Morogoro.
Doreen ni mwenyeji wa hapa hapa Arusha na anaishi na wazazi wake maeneo ya Unga Limited.
Niliamua kutumia usafiri wa daladala maarufu kama Vifodi, hapa Arusha kama vile na kule Nairobi nchini Kenya wanavyoita usafiri wao wa daladala matatuu.
Sikubeba simu, pochi wala sikuvaa saa niliepuka kubeba vitu vya thamani ambavyo vingewavutia vibaka.
Kwa wale msioujua mji wa Arusha na Vitongoji vyake, Unga Limited ni eneo hatari sana kwa Vibaka na wahuni hapa Arusha, huwezi kulitofautisha eneo hilo na eneo la Manzese pale jijini Dar Es Salaam au inawezekana Manzese ikawa na afadhali, au eneo la Kariobangi kwa kule Nairobi.

Niliondoka nyumbani kwa mjomba angu maeneo ya Njiro majira ya saa nne asubuhi kwa kuwa nilikuwa naenda eneo ambalo linasifika kwa uhalifu niliamua kuvaa mavazi ambayo hayatawavutia vibaka. Nilivaa Suruale yangu ya Jinz na jaketi, halafu nikavaa Kofia ya cap maarufu kama Kapelo na kisha nikavaa miwani yangu ya jua.

Kwa haraka haraka ukiniona utajua kabisa kuwa mimi ni mmojawapo wa wale wasichana walishindikana, yaani nilionekana kama muhuni fulani hivi na mvuta bhangi…
Hata Mjomba angu aliponiona alinishangaa sana, hata hivyo nilimjulisha madhumuni yangu ya kuvaa vile.

Unajua wakati mwingine unatakiwa uwe mjanja, unapoenda maeneo kama ya unga limited au maeneo mengine yanayofanana na hayo popote pale inabidi ujiweke katika mazingira ambayo hayatakutofautisha na wenyeji.

Nilifika stendi ya vifodi na kupanda basi la kuelekea mjini, maeneo ya stendi kuu, kwa hapa Arusha eneo ambalo huitwa mjini na ambalo ndipo vifodi vingi vinapogeuzia ni stendi, ambapo ndipo unapopatikana usafiri wa kwenda popote pale.

Nilifika Stendi na kupanda vifodi vya kwenda Unga Limited. Kama ilivyokuwa Dar, hata hapa Arusha abiria ni wa kugombea wakati mwingine ingawa pia nilikuta kuna utaratibu wa kupakia kwa zamu, lakini kuna wengine wanavunja huo utaratibu na hivyo kusababisha vurugu na fujo zisizo na msingi.

Nilipanda na kuchagua siti ya dirishani ili niweze kuyaona maeneo ya Unga Limited vizuri kwani ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kwenda huko.

Mwenyeji wangu aliniambia nishuke kituo cha soko mapunda kwani ana duka lake la biashara maeneo hayo na alinipa jina la hilo duka lake ambalo ni maarufu pale soko mapunda, nilimwambia Kondakta mapema kituo ninachoshuka kwani sikutaka kupitishwa kituo halafu nipotee. Kifodi chetu kilipojaa tuliondoka na ili kuhakikisha kuwa sipitishwi nilikuwa namkumbusha mara kwa mara mpaka mama mmoja alikaa jirani yangu ambaye kwa muonekano alionekana kuwa ni mbulu akanitoa wasiwasi kuwa tukifika kituo ninachoshuka atanijulisha, kuanzia hapo tukaanzisha mazungumzo nikawa namdadisi dadisi hili na lile kuhusu eneo hilo la Unga Limited.

Tulipofika eneo hilo la Soko Mapunda mwenyeji wangu huyo wa kwenye Kifodi akaniambia nishuke baada ya kumwambia Kondakta anishushe.
Nilishuka kituoni kisha nikasimama kwa nukta kadhaa nikiangaza macho yangu huku na kule ili niweze kusoma mazingira Nikavuta hatua kadhaa kuelekea kwenye duka moja mbapo nje walikaa vijana kadhaa huku wakila yale majani maarufu kama Mirungi ambayo serikali imeyapiga marufuku.

Hata hivyo la kushangaza ndugu msomaji ni kwamba hapa Arusha watu wamekuwa wakitafuna majani haya hadharani na huku askari polisi wetu wakitazama tu, kwa Arusha na Moshi Mirungi ndio ulevi maarufu wanaotumia vijana wengi.

Niliamua kuwafuata wale vijana ili niwaulize kwa mwenyeji wangu. Nilipofika pale kwa lafudhi ya kuiga ya Kiarusha nikawawasalimia “Niaje machalii wangu” wote wakanijibu kwa pamoja “powa tu sister, mambo vipi” nami nikawajibu “Powa tu”
“Mbona mnasaga bila hata soda” niliwauliza, kwa utani, kwa kawaida walaji wa mirungi hawasemi kula mirungi bali husema kusaga mirungi au kusaga mbaga, Mirungi ina majina mengi sana, mengine hata siyafahamu.
“Duh! Sister hatuna chapaa (Pesa) tunaomba ututoe hata soda moja moja basi”
Alijibu mmoja wao, nikachomoa elfu mbili mfukoni nikawapa, walifurahi sana.
“Sasa Sister karibu tusage basi” alinikaribisha kijana mwingine niliyekuja kumfahamu baadae kuwa anaitwa Saiboko.
“Kwa leo sijisikii kusaga kabisa” nilimjibu.

Nilitumia muda huo kumuulizia mwenyeji wangu ambapo Saiboko alimuita kijana mmoja kwa jina la Nyoka aliyekuwa akicheza hapo jirani na dukani walipokaa na kumwambia anipeleke kwa mwenyeji wangu.
Kwa hapa Arusha, wale vijana wadogo wadogo huitwa nyoka, jina ambalo hutumika sana kule Mererani kuwatambulisha wale watoto wadogo wanaotumishwa kule katika migodi ya Tanzanite.

Yule mtoto alinipeleka mpaka kwa mwenyeji wangu, ambapo nilipokelewa kwa shangwe na mwenyeji wangu huyo.
Tulipoteana na Doreen kwa takribani miaka mitano tangu tulipoachana kule Morogoro baada ya kuhama na kurudi jijini Dar kuendelea na kidato cha sita, kwani mazingira ya pale shuleni Morogoro sikuyapenda kutokana na matatizo ya kiafya niliyokumbana nayo.

Mwenyeji wangu alifurahi sana kukutana na mimi, kwake yeye aliona kama ndoto, kwani nilipomtumia ujumbe wa simu ya mkononi kuwa nitakuwa mgeni wake alishangaa sana na hakuamini kabisa. Tulitumia muda huo kujibizana kwa ujumbe wa simu kwa kupeana michapo na kukumbushana mambo ya shuleni wakati huo.

Baaada ya kumaliza kidato cha sita Doreen hakubahatika kuendelea na chuo kikuu na ndipo alipoamua kuwa mjasiriamali akafungua duka lake kubwa akiuza bidhaa mbali mbali, pia alinijulisha kuwa ana vibanda viwili pale stendi kuu ambapo ameajiri wasichana wawili wanamuuzia, na pia analo duka la stationary jirani na shule ya msingi ya Naura.

Wakati tunaendelea kupeana michapo ya enzi hizo mara akaja msichana mmoja aliyeonekana kuwa dhaifu akiwa amembeba mtoto mdogo ambaye naye alionekana kuwa dhaifu vile vile, alipofika pale aliniomba hela ili akale, mwenyeji wangu alimfukuza kwa madai kuwa ananisumbua, nilimzuia asimfukuze, kwani nilitaka kuzungumza nae.

“Nawe Koero hujaacha tabia yako ya umama Theresa, achana nae huyo kazi kusumbua watu kwa kuomba omba tu hapa” aliniambia Doreen akinikataza nisiongee na yule binti.

Wakati nilipokuwa nikisoma Morogoro wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniita mama Theresa, kutokana na tabia yangu ya kupenda kusaidia watu.

Nakumbuka siku moja tulikuwa tumeenda mjini siku ya Jumamosi mimi nilikwenda kanisani na wenzangu walikuwa wameenda kufanya manunuzi mbalimbali, tukakubaliana nikitoka kanisani tukutane stendi. Nilipotoka kanisani nikawafuata pale stendi nikawakuta wamekaa kwenye duka moja wakinywa soda, nilipofika niliungana nao nami nikaagiza soda yangu.
Tulipomaliza kunywa soda zetu kabla hatujaondoka kwenda kupanda basi nikakumbuka kuwa kuna dawa sijanunua, ikabidi niwaombe wenzangu wanisindikize kwenye duka la dawa lililokuwepo pale jirani nikanunue dawa zangu.

Tulipofia pale dukani, wakati nanunua dawa akaingia kaka mmoja alikuwa akitetemeka sana na alikuwa akionekana kuwa ni mgonjwa, ilibidi nimpishe kwanza anunue dawa kwani alionekana kuwa anaumwa hasa.

Alitoa cheti chake cha hospitalini kilichoandikwa dawa na kumpa yule muuzaji. Muuzaji alikiangalia kile cheti kisha akachukua Calculator na kupiga hesabu, kisha akamwambia yule mgonjwa kuwa dawa zake zitamgharimu shilingi elfu saba jumla, Yule kijana alikaa kimya, wote tukawa tunamuangalia tukisubiri atoe hela ili ahudumiwe ili na sisi tuhudumiwe, mara akaingiza mkono mfukoni na kutoa shilingi mia akamwambia muuzaji ampe panado, yule muuzaji akamwambia kuwa kwenye kile cheti hapakuandikwa panado, lakini yule kijana alisisitiza apewe panado kwanza na hizo dawa nyingine atakuja kununua siku nyingine.

Wote pale tulishikwa na butwaa ikiwa ni pamoja na yule muuzaji, lakini kama vile yule kijana alikuwa amesoma mawazo yetu, akamwambia yule muuzaji kuwa hana pesa kwa wakati ule na ndio sababu anataka apate japo panado kwanza za kupunguza maumivu halafu dawa atanunua siku nyingine akipata hela.

Nilijitolea na kumnunulia zile dawa na kuwaacha wanafunzi wenzangu na hata yule muuzaji vinywa wazi, sikushangaa sana kwani ni vigumu sana mwanafunzi kutoa kiasi kikubwa cha pesa vile kumsaidia mtu asiyemfahamu, ni ajabu eeh!

Yule kijana alinishukuru kweli nusura anilambe miguu, na alitaka kujua ninapoishi, lakini nikamwambia kuwa asijali na anione kama msamaria mwema yule aliyezungumziwa katika biblia.
Basi kuanzia siku hiyo wanafunzi wenzangu wakawa wananiita Mama Theresa, eti wakinifananisha na yule hayati mama Theresa wa Calcutta, sifa ambayo siistahili na wala siwezi kuifikia hata theluthi yake.

Sizungumzi habari hii ili kujisifu, bali nimekumbuka, baada ya Doreen kuniita hilo jina la Mama Theresa na ndipo nikakumbuka chanzo cha mimi kuitwa jina hilo.

Tuachane na habari za Morogoro, turejee Unga Limited kwa Doreen, basi nikampa yule binti kiasi cha hela ili akanunue maziwa fresh kwanza kwenye kibanda cha jirani ili mtoto anywe kwanza kwani alionekana kuwa na utapiamlo, kutokana na kukosa vyakula vyenye virurubisho na nywele za mtoto yule zilikuwa zimenyonyoka, sijui alikuwa na safura, (Mungu aepushie mbali)
Nilimchukua yule mtoto nakumpakata ili yule binti akanunue maziwa, wakati huo Doreen alikuwa ndani dukani kwake akihudumia wateja.

Yule binti ambaye alikuja kuniambia jina lake kuwa anaitwa Anita hakukawia alirudi akiwa na maziwa ya moto, niliyachukuwa na kisha nikampa kiasi kingine cha hela ili na yeye akapate chakula wakati namywesha mwanae maziwa.
Nilimuuliza jina la mtoto wake akaniambia kuwa anaitwa Elias, na alinijulisha kuwa ana umri wa miaka mitatu, ingawa alionekana kuwa na umri wa labda mwaka mmoja kutokana na kuwa nyondenyonde.
Nilimnywesha yule mtoto maziwa na kwa kuwa alikuwa na njaa aliyanywa kwa fujo na kuyamaliza, wakati wote namnywesha Eliasi maziwa, Doreen alikuwa akinitazama kwa mshangao.

“Hivi Koero ukiachiwa huyo mtoto utampeleka wapi?” Aliniuliza Doreen.
“Si namchukuwa na kuishi nae kwani kuna tatizo gani, si mtoto kama walivyo watoto wengine?” Nilimjibu.
Doreen alinijulisha kuwa yule binti anaishi ghetto na changu doa mmoja na kamfanya kama house girl wake na mlinzi wa chumba chake wakati akienda kwenye mishe mishe (Pilika pilika) zake za kujiuza.

Haikupita muda yule binti alirudi na nilipomdadisi ndipo aliponisimulia mkasa wake.

Anita ni mwenyeji wa Singida, na ni mtoto wa tatu kati ya watoto watano katika familia yao akiwa ndiye wa kwanza kuzaliwa huku akifuatiwa na kaka zake watatu na mdogo wake wa mwisho wa kike.
Alipomaliza darasa la saba alifaulu lakini baba yake alitaka kumuozesha badala ya kumuendeleza kielimu kwa madai kwamba watoto wa kike hawana faida hata wakisomeshwa kwa kuwa ni waolewaji, hivyo atakwenda kuwanufaisha familia ya mumewe.
Baada ya kuona baba yake ameshupalia aolewe ilibidi kwa kushirikiana na mama yake aende kushitaki kwa mwenyekiti wa kijiji ambaye kwa kushirikiana na mtendaji kata walimuita baba yake na kumuonya juu ya mpango wake huo na kumshinikiza ampeleke shule mwanae.

Baba yake Anita alikubali kwa shingo upande ikabidi auze ng’ombe zake mbili ili kumuwezesha Anita aende shule.
Alipofika kidato cha pili alijikuta anapata mimba ambayo nayo aliipata katika mazingira ya kutatanisha baada ya kulaghaiwa na mwanafunzi mwenzie waliekuwa wakisoma nae na kujikuta akipata ujauzito, cha kushangaza, yeye alirudishwa nyumbani lakini yule kijana aliachwa aendelee na masomo. Kama kawaida mfumo dume ukachukuwa nafasi yake.

Baada ya kurudishwa nyumbani baba yake alimpiga karibu amuue kama sio majirani kuingilia kati lakini hata hivyo alimfukuza na kumtaka asikanyage pale nyumbani kabisa na siku akikanyaga atamuua.

Anita alikimbilia Singida mjini kwa mama yake mdogo ambaye hakuwa na kazi maalum na kuishi nae hadi alipojifungua.
Hali ya maisha ilimuwia ngumu kwani hakupata masada wowote kutoka kwa mama yake mdogo, na ndipo alipokutana na huyo dada aliyemchukuwa kwa ahadi kuwa atamtafutia kazi huku Arusha, kumbe kazi yenyewe ni ya kulinda nyumba na kufanya kazi za ndani.

Maisha aliyokuwa anaisha ni ya kikatili sana kwani vijana wa kihuni walikuwa wakimuingilia usiku na kumbaka mara kadhaa pindi yule dada akishaondoka na alikuwa hampia hela kwa ajili ya maziwa ya mtoto wala mshahara na ndio sababau akawa anazunguka zunguka kwenye maduka na kwenye mabaa kuomba omba.

Habari ya Anita ni ya kusikitisha sana na nikisema niisimulie yote nitakuchosha. Kwa kifupi nilikubaliana na Anita kuwa nimpe nauli arudi Singida pamoja na mtaji wa biashara ili akirudi kule asikae bila kazi. Tulikubaliana kuwa ajiandae kwa safari Jumatatu asubuhi na ahakikishe hamwambii yule dada anayeishi naye ili kuepuka mpango mzima kuvurugika.

Doreen alizidi kunishangaa na kuonekana kama haamini juu ya kile nilichomuahidi Anita kwani alijua kuwa namdanganya tu binti wa watu. Hata hivyo siku iliyofuata yaani Jumatatu nilikwenda tena Unga Limited na kumkabidhi Anita kiasi cha pesa nilizomuahidi na ili kuhakikisha kuwa habaki pale kwa yule dada nilikodi Taxi na kuongozana naye tukiwa na mwenyeji wangu Doreeen hadi stendi na kumpakia kwenye basi la kwenda Singida na tulimkabidhi Kondakta wa basi lile kuwa ahakikishe kuwa yule binti anafika Singida na asiteremkie njiani.

Nilichukuwa muda huo kumueleimisha Doreen juu ya umuhimu wa kuwasaidia wenye shida.
Ni vyema kutoa misaada kwa wenye shida, pale unapoona kuwa kuna mtu anahitaji msaada na kama uwezo unao.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa safari yangu nilipomtembelea rafiki yangu Doreen, siku ya Jumapili.

Hapo nyuma niliwahi kuandika tatizo la mimba mashuleni, wiki ijayo nikipata nafasi nitalieleza tatizo hili kwa kina na namna tunavyoweza kuliepuka.


{Anita sio jina lake halisi}