Friday, June 12, 2009

LAANA YETU NI NINI HASA?

Tunazo rasilimali nyingi na za kutosha

Hii nimeidesa kutoka katika mtandao wa Jamii Forum, kutokana na kuvutiwa nayo nimeona si vibaya nikiiweka hapa kibarazani kwangu ili wasomaji wa blog hii waweze kuchangia mawili matatu,

Mara nyingi huwa najiuliza, hivi sisi tumelaaniwa? Na kama tumelaaniwa, ni laana gani hasa tuliyonayo? Ni nini hasa kinachosababisha tuwe hivi tulivyo? Sababu kubwa za kujiuliza hivi ni kutokana na hali yetu kimaisha, ikilinganisha na wengine karibu wote duniani. Na ukizingatia uwezo wa kirasilimali tulizo nazo. Nchi hii ina kila kitu kinachohitajika katika kuleta hali bora zaidi kwa watu wake.

1. Ina madini ya aina zote zinazoweza kupatikana duniani na zaidi (Tanzanite). Tunashindwa kuyavuna na kuamini kuwa watu kutoka nje ndio wanaoweza kutusaidia na sisi tukapata tija kwa kuwatoza 3% tu ya mapato yao. Ni nini hasa kinachotafuna akili zetu?

2. ina maji kila upande wa nchi yetu. Lakini bado mabomba yetu ni makavu na kipindupindu kinamaliza watu.


3. ina ardhi nzuri na ya kutosha kuliko nchi nyingi duniani (hakuna eneo lenye jangwa). Inatumikaje kuinua pato la mTanzania?


4. ina maliasili (hata dawa za kienyeji, misitu, mbuga za wanyama n.k.). Tunashindwa hata kuitangaza, kuitumia kupata tija. Kwanini hasa?


5. ina bahari yenye zaidi ya kilometer 1440. Maziwa yanayopakana na nchi jirani kila upande (Maziwa Tanganyika, Victoria, Nyasa). Tunayatumiaje?


6. Bahari na maziwa/mito ina samaki wa maji baridi na maji chumvi. Ila tunashindwa kuwavua, na wanaoweza kuwavua tunawakamata na hatujui tuwafanye nini.


7. Ina watu wakarimu, wenye akili na uwezo wa kufanya kazi. Kwa ujumla ina kila kitu isipokuwa hali bora kwa watu wake.

Ila wote ni watazamaji, walalamikaji na wasio na fursa yoyote ya kujiendeleza kwa uhakika na usawa. Kwa mtazamo wangu, nchi hii inakosa dira na uongozi wenye nia madhubuti ya kutumia rasilimali zilizopo katika kuleta tija. Swali ni je, kwanini pamoja na yote hayo tunashindwa kufikia malengo yetu na kudhani kuwa wahisani, matajiri duniani ndio wenye jukumu la kutusaidia kwa kile wanachopata kutoka kwao ambako wengi wao wala hawana tulichonacho hata kwa asilimia 10? Je ni laana gani inayotusumbua sisi waTanzania? Nini hasa kinachotakiwa kufanyika kujitoa kwenye laana hiyo? Nani hasa alietutupia laana kali namna hiyo?

6 comments:

Bennet said...

Kama kweli tunataka maendeleo ni lazima tufanye mapinduzi ya kilimo na kuhakikisha tuna chakula cha kutosha mpaka cha kuuza nje, wataalamu wa kilimo/mifugo hapa nchini hawatumiki kikamilifu sababu ya mishahara midogo, miundombinu, urasimu na pembejeo za kilimo

Viwanda kama UFI na ZZK ambavyo vilikuwa vinazalisha zana za kilimo tuliviua, utumiaji wa matreka ya valmet enzi zile nayo ulitushinda

Tukishafanya mapinduzi haya na mkulima akawa sio fukara tena bali tajiri au hata mtu wa kati, na watu wakawa hawana njaa watapata muda wa kufikiri zaidi na kujituma kwenye shughuli za maendeleo
Haya ni maoni yangu tu, kuyapinga ruksa

Godwin Habib Meghji said...

Kuna maswali ni marahisi kwa kuyatazama. ila ni magumu sana kuyajibu. Nilikuwa najiuliza sana swali hilo nilipokuwa mdogo. wakati nasoma shule ya msingi mapaka sekondari. Baada ya hapo nililifuta kabisa swali hilo kichwani kwangu. Ubinafsi ndio unaotuweka hapa tulipo. Na tunapoelekea ni pabaya zaidi. VIJANA SIKU HIZI ANACHAGUA KOZI YA KUSOMA ILE AMBAYO ATAPATA MWACHA WA KUCHOTA HELA. Na si kitu anachokipenda. Elimu ya uraia haipo kabisa. Itawezekana tu siku kizazi hichi kitatoweka na kuja kizazi kingine bila kukutana na mtu hata mmoja wa kizazi hichi

Yasinta Ngonyani said...

Hatuja laaniwa ila kinachotakiwa kifanyike ni mapinduzi.

Mzee wa Changamoto said...

Dada. Mfumo wetu wa siasa unatuzalishia watu wenye "system" hiyohiyo inayowaza hivyohivyo na ambayo inaingia madarakani kwa style hiyohiyo na kutakiwa kulipa madeni yaleyale waliyoyapata vilevile ili kuwa walewale. Kisha wanalazimika kutumia vitu vilevile kulipa madeni na kujilimbikizia mali zaidi ili uchaguzi ujao wawe na "ngawira za kutosha". Mimi nasema hatujalaaniwa, bali kama alivyosema Mama C hapo juu, tunahitaji kuamka. Tunahitaji DIKTETA. Ninajua kuwa wengi wamepandikizwa tafsiri ya maneno haya na watu wasio na lolote jema kwetu. Yaani mtu anayekuchukia na anayekutesa na kukunyonya ndiye anayetupangia na kututafsiria aliye Dikteta kwetu na wengi wanakubali. Basi mimi naamini kuwa huyo anayelazimika kuwa Dikteta (ambaye ninaamini atakuwa anapingana na maslahi yao ya kutunyonya) ndiye tunayemhitaji. Niliwahi kuandika kuhusu wazo hili kwa kuuliza kuwa DIKTETA NI NANI NA KWANINI TWAMHITAJI? Labda ukisoma hapa utanisaidia kuona usahihi na ukosefu wangu. Lakini bado naamini ndio suluhisho. Soma http://changamotoyetu.blogspot.com/2009/01/dikteta-ni-nani-na-kwanini-twamhitaji.html

Simon Kitururu said...

Sina jibu na naendelea kukuna kichwa!:-(

Albert Kissima said...

Tatizo ni "uzalendo"
wanene wanajali maslahi yao binafsi.
Wananchi tunalewa kwa maneno matamu, kumbe tunafanyiwa usanii tu.

Padri Karugendo kwenye makala yake katika gazeti la Raia mwema toleo namba 84 yenye kichwa cha habari, "BUSANDA:Nauliza , nijibiwe" ukiisoma nadhani utapata kitu ambacho pengine awali ulikuwa hukifahamu kuhusiana na viongozi wetu.Utagundua
ni kwa nini nchi ni tajiri, serikali ni tajiri na wananchi wanaoishi kwenye nchi tajiri na yenye serikali tajiri ni masikini.