Friday, July 31, 2009

UFISADI: JE TANZANIA INAHITAJI YALIYOTOKEA GHANA 1979?

Ndugu wasomaji wa Blogu hii ya Vukani, leo nimeona niwawekee hii makala ambayo nimeidesa kutoka mtandao wa Jamii Forum.
Nilipousoma niliona ni vyema niwashirikishe wasomaji wa Vukani nao wapate kutafakari kama kuna haja ya kuwaiga wenzetu ili kutokomeza ufisadi hapa nchini.

Naomba kuwasilisha..................

Wale wanaoupinga ufisadi kwa dhati naomba mtafakari iwapo nchi yetu imefikia mahala ambapo pengine linahitajika tukio kama lile la Ghana la June 1979 ambalo kwa kiasi kikubwa limetokea kuwa ni fundisho kubwa kwa mafisadi na wale wanaowalinda. Mapema mwezi huu Rais Barack Obama alitembelea Ghana, nchi ya kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kupata heshima ya kutembelewa na kiongozi wa Marekani mwenye chimbuko la Bara hili.

Hakubahatisha katika kuichagua Ghana – na hasa kutokana na yale aliyoyatamka nchini humo kuhusu Afrika na viongozi wake. Aliwapasha kikweli kweli – kwamba wao ndio wahusika wa kwanza kwa yote yaliyo mabaya ndani ya tawala zao. Kwa hivyo asingeweza kutamka hayo kama angekuwa Tanzania, Nigeria au Kenya kwa mfano. Alichagua nchi angalau aliona inaweza kuwa mfano kwa wengine. Aliisifia sana Ghana kwa demokrasia iliyojijengea na inayoridhisha, uongozi mzuri na utawala bora, pamoja na udhati katika kupigana na ufisadi.

Lakini yote haya hayakuja bure, kwani ule msemo usemao “Usione vinaelea, vimeundwa” unaelezea vizuri sana hali hiyo ya sasa ya Ghana. Baada ya kupinduliwa kwa Kwame Nkrumah mwaka 1966, Ghana iliingia katika kipindi cha tawala za kijeshi na za dhulma. Hata ule wa kiraia uliokuwapo kwa muda mfupi (wa Dr Kofi Busia mwanzoni mwa miaka ya 70) ulikuwa hivyo hivyo -- ufisadi na kulindana ulikithiri kwa kiasi kikubwa sana – kama vile ilivyo hapa Tanzania. Hatimaye mwaka 1979 serikali ya kijeshi ya Jenerali Fred Akuffo iliamua kurudisha utawala wa kiraia.

Vyama vya siasa vikaruhusiwa, ikatayaarishwa katiba mpya na uchaguzi ukafanywa. Lakini kabla ya rais mpya wa kiraia, Hilla Liman kuapishwa, Luteni Jerry Rawlings wa kikosi cha Anga naye alifanya mapinduzi. Akawakamata majenerali wote waliokuwa wakipinduana huko nyuma, kuanzia Akwasi Afrifa, Ignatius Acheampong na Fred Akuffo na maafisa wengine watano. Mahakama maalum iliundwa, na kwa haraka haraka iliendesha kesi na kuwahukumu kuuawa kwa kupigwa risasi, tukio lililofanywa katika ufukwe wa Accra mapema June 16, 1979. Baada ya tukio hilo, tarehe 24 Septemba 1979 Rawlings aliruhusu utawala wa kiraia uendelee na hivyo Hilla Liman aliapishwa kuwa rais.

Rawlings alisema ilibidi majenerali hao wahukumiwe vile kwa sababu siyo tu waliipora nchi na kuifilisi huku wakilindana, lakini pia walishinikiza kuwepo kipengele cha “kinga” katika Katiba ya Kiraia waliyoiunda, kwamba wasiweze kushitakiwa kwa makosa yoyote – ya rushwa na utawala mbovu – walipokuwa madarakani. Rawlings alisema alijitolea kufanya hivyo kwa sababu, ungeingia tu utawala wa kiraia, watawala wale wa zamani wasingewajibishwa, kwa maana ya kushitakiwa, wangeendelea kutanua na mapesa na mali waliziowaibia wananchi.

Kwa hivyo utawala bora uliopo Ghana sasa hivi umetokana na fundisho kubwa la kihistoria lisilosahaulika na limekuwa kama “onyo kali” (deterrent) kwa wengine. Ingawa Rawlings alirudi kuipindua tena serikali ya Liman, hiyo haikuondoa kile alichokifanya kwa nchi yake, kubadilisha mwelekeo wa nchi yake liyoonekana ikienda kusiko, na kikubwa ni kupiga rungu kubwa ufisadi kwa vitendo na siyo kwa maneno. Sisemi kama ufisadi hakuna Ghana, upo, lakini unashughulikiwa vilivyo kwa vyombo husika vilivyo huru, visivyoingiliwa na mamlaka za juu. Hivi majuzi waziri wa Nje wa zamani chini ya utawala wa Rais aliyeondoka John Kuffuor alikamatwa kwa rushwa kuhusiana na uagizaji wa mchele kutoka nje.

Alikamatwa kimya kimya bila hata ya umma kupiga kelele sana kwanza – kama ilivyo hapa kwetu. Kuna baadhi wanasema kitu kama hicho kingefaa pia hapa, kwani ufisadi umekithiri kupindukia, na kulindana kwa hali ya juu na kusafishana kwa wakubwa ndiyo umekuwa kitu cha kawaida na huku umma hauna nguvu zozote za kuweza kurekebisha mambo. Mimi naona tulijadili hili

3 comments:

Fadhy Mtanga said...

Da Koero ahsante kwa kudesa historia yenye kuvutia.

Mi naziunga mkono jitihada za wanaharakati wa Ghana. Ufisadi si jambo la kuchekewa hata kidogo. Ufisadi ni uuaji mbaya kuliko hata ule uliofanywa na mafashisti.

Kwanini nasema ufisadi ni uuaji mbaya? Ufisadi unapopelekea kuwafanya wananchi wateseke, kwa kupata huduma za jamii katika kiwango cha chini, nini tunategemea? Mama mjamzito anapofariki kwa kukosa huduma wakati kuna pesa zingeweza kuboresha huduma hiyo, zinahodhiwa na wachache, tafsiri yake ni nini?

Wananchi wanapoathirika kwa maji yenye sumu kwa sababu ya ufisadi wa kundi fulani la wenye nguvu, lugha ipi ni sahihi?

Ipo haja. Nachelea kusema hivyo. Haya mambo yanaumiza sana.

Kama Waghana wameweza kujaribu kujenga misingi mizuri ya uadilifu, tunashindwa nini?

Albert Kissima said...

Sio siri ufisadi umetuumiza na utazidi kutuumiza.

Mbaya zaidi kwa kadiri mda unavyokwenda ufisadi unazidi kushamiri mbali na jitihada ndogo za kukabiliana nao.


Kesi za wanaotuhumiwa na ufisadi zaendeshwa kifisadi fisadi, hatma ya kesi zenyewe haieleweki.


Ghana kulikuwa na pengine hadi leo kuna wazalendo, wale wanaoipenda nchi yao na watu wao.


Hapa kwetu Wazalendo kama hawa wa Ghana huwa wanafichwa pasipojulikana,wanatoweka kama upepo.Wanaharakati wengine wazalendo husoma mazingira,huogopeshwa na hufyata mkia.



Labda niulize swali,


inaaminika kuwa serikali yetu ipo kumi bora duniani kwa kuwa na Mashushushu, kwa nini, kipi chatafutwa, hofu ya nini? Ni kuwalinda wananchi?

Mzee wa Changamoto said...

Wala hatuhitaji yaho ya Ghana tuu. Pengine tuunanishe na mengine mengi kutoa ya kwetu. Wao walikuwa na matatizo lakini sisi tumevuka hapo. Hatuna matatizo kwenye nchi yetu, bali nchi yetu ni matatsasa hivi.
Nasubiri hivyo vifukavyo moshi vitakapotoa kishindo tuone atakayebabuliwa uso ni nani?
Na tunakoelekea ndio itakuwa NJIA PEKEE ya kujikomboa. Inasikitisha kusema haya lakini nadhani tunaweza kukumbuka aliyoimba Bob Marley kwenye wimbo wake BURNING AND LOOTING
Ndiko tusongako sasa Dadangu na wapendwa wengine