Mheshimiwa Rais akizuindua kampeni za Zinduka malaria haikubaliki pale viwanja vya Leaders club
Hivi karibuni katika kampeni ya Zinduka Maleria haikubaliki iliyozinduliwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alizungumzia jinsi malaria inavyowamaliza watanzania, wimbo ule ule ambao umekuwa ukiimbwa na wanasiasa kila uchao.
Naamini kila mtu anajua kuwa Malaria inaua wananchi wengi sana hapa nchini kuliko hata ugonjwa wa Ukimwi, lakini cha kushangaza mpaka leo hii hakuna hatua madhubuti ambayo imechukuliwa katika kuutokomeza ugonjwa huo.
Awali nilijua kuwa Raisi angetumia kampeni hizo kuidhinisha matumizi ya DDT, dawa ambayo imefaninkiwea kwa kiasi kikubwa kutokomeza ungonjwa wa malaria katika nchi ambazo zinatumia dawa hizo hususana Zanzibar.
Nilishangazwa na kauli ya Rais pale aliposema, naomba ninukuu, "Kila siku ya Mungu, hapa nchini, wanakufa watu hadi 291 kwa ugonjwa wa malaria. Kwa maneno mengine, kila saa inayopita, wanakufa watu zaidi ya 10 kwa ugonjwa wa malaria. Hawa ni watu wengi mno. Hivyo, malaria ni Janga la Taifa letu. Lakini cha kusikitisha zaidi ni kwamba malaria ni ugonjwa unaoweza kuzuilika na kutibika. Ndiyo maana tumeamua kuwa wakati tunaendelea kushughulikia kutibu wagonjwa wa malaria, tuelekeze nguvu zetu katika kuzuia kwa kuanza juhudi za kutokomeza malaria nchini." Mwisho wa kunukuu,
Pia alibainisha njia kuu tatu za kupambana na kuushinda ugonjwa wa malaria, akisema kuwa njia ya kwanza ni kutumia dawa zenye nguvu na uwezo wa kutosha kuwatibia wale watakaokuwa wamepatwa na ugonjwa wa malaria.
Njia ya pili, alisema, ni kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua mbu na akaelezea jitihada za Serikali yake juu ya kupatikana kwa vyandarua vya namna hiyo. Alisema kuwa mpaka sasa watoto wenye umri wa miaka mitano na kina mama waja wazito wanapewa vyandarua vya namna hiyo bure, lakini mipango inakamilika kuiwezesha kila kaya nchini kuwa na angalau vyandarua viwili vya namna hiyo.
Akasema kuwa njia ya tatu ni kuhakikisha kuwa mbu wanaobeba malaria hawazaliani na wanatokomezwa kabisa.
Kwa maneno yake mwenyeweRais Kikwete alisema, "Ni lazima tuhakikishe tunawamaliza mbu wanaoleta malaria kwenye mazalia yao. Tunaweza kabisa kuhahakisha kuwa sisi tunakuwa kizazi cha mwisho kufa kwa malaria. Nchi nyingine duniani zimeweza na naamini hata sisi tutaweza. Ndugu zetu wa Zanzibar wameweza na sisi wa Tanzania Bara tunaweza pia."
Mimi nilitarajia kuwa huo ndio ulikuwa ni wakati muafaka wa yeye kutangaza rasmi matumizi ya dawa ya kuulia wadudu ya DDT, ambayo ndiyo inayotumiaka Zanzibar pia katika kuutokomeza ugonjwa huo.
Huwezi kuyataja mafanikio yaliyofikiwa na Wazanzibari katika kuutokomeza ugonjwa wa Malari bila kuitaja dawa ya DDT.
Binafsi naona kampeni hiyo ilikuwa na sura ya kisiasa zaidi kuliko kile ambacho kilitarajiwa na wananchi wengi, kwani hakuna jipya, hizo njia kuu tatu alizozitaja mheshimiwa raisi zimekuwa zikitajwa kila siku na wanasiasa na wataalamu wetu wa afya lakini hazijazaa matunda mpala leo na watu wanaendelea kuteketea.
Cha Kushangaza Kiwanda cha A to Z cha hapa Arusha ambacho ndio mtengenezaji mkuu wa vyandarua ni miongoni mwa wadhamini wakuu waliodhamini uzinduzi wa kampeni hiyo ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria, hii haiingii akilini, kwamba mtu anayetengeneza pato lake kwa kutegemea ugonjwa wa malaria akubali eti malaria iishe hapa nchini, kama sio siasa ni kitu gani, basi atakuwa ni mwenda wazimu.
Mimi naamini kuwa mheshimiwa Raisi anayo dhamira hasa ya kuutokomeza ugonjwa huu wa malaria, lakini wataalamu wetu wameshindwa kumshauri raisi wetu kufanikisha dhamira yake hiyo.
Bado nasisitiza kuwa kamwe hatuwezi kuutokomeza ugonjwa wa malaria kama hatutaruhusu matumizi ya dawa ya kuulia wadudu ya DDT.