Thursday, February 25, 2010

JAMANI HIVI HUWA NAELEWEKA?

Watoto huwa werevu kung'amua

Naamini wengi hamtanielewa kwa sababu hamjui leo ninataka kuandika nini. Hata wewe unayesoma hapa huenda ukasoma mwanzo mpaka mwisho lakini ukatoka kapa kwa kuwa najua utakua ni mmoja wa vilaza wa kusoma makala za kufikirika au kusadikika.

Nimekuwa nikijiuliza, hivi ni kwani nini watu huwa hawanielewi, nimekuwa nikijaribu kuandika kwa lugha nyepesi sana lakini sieleweki. Je uwezo wangu ni mdogo katika kueleza jambo likaeleweka au wale ninaowaandikia wana uelewa finyu wa kuelewa kile ninachomaanisha katika maandishi yangu.

Inashangaza sana kuona hata wale wanazuoni ninaowaamini nao pia wamekuwa ni wagumu kunielwa. Japokuwa ninatumia lugha nyepesi lakini bado wanashindwa kunielewa. Pamoja na kwamba leo hii nimejitahjidi sana kuandika kwa lugha nyepesi tena nimejitahidi kufafanua na kutoa mifano kadhaa, bado naona kuna ugumu watu kuelewea ujumbe wangu.

Wako wapi wanazuoni wenye ujuzi wa kusoma maandiko ya wengine na kuyatolea ufafanuzi hadi watu waelewe pasi na shaka?, wako wapi malenga wetu na wajuvi wa lugha wasaidie kutafsiri maandiko haya?

Hata wewe unayesoma hapa sasa hivi yawezekana usinielewe ninataka kuandika nini, lakini nakuomba usome maandiko haya kwa makini naamini utanielewa hapo baadae kuwa namaanisha nini.

Ni mara nyingi nimekuwa nikiandika juu ya kile niandikacho na nimekuwa nikiandika kwa lugha nyepesi sana lakini nasikitika kuwa wasomaji wengi hawanielewi kabisa. Labda leo niombe ushauri kwenu kuwa ni lugha gani nyepesi ambayo itakuwa ni rahisi kwenu kunielewa? Nikisema niandike Kiingereza naamini sitaeleweka maana nakijua kiingereza changu ni cha kuombea maji tu, nikisema niandike kipare lugha ya mama yangu ndio wee nitachemsha kabisa, na kichaga nacho lugha ya baba, lahaula, nitawachekesha walionuna.

Au nijaribu kuandika kwa Kiswidi, hapo itabidi niombe msaada kwa dada yangu Yasinta, lakini na yeye najua huenda hataeleweka kwa kuwa na yeye kajifunza lugha hiyo ukubwani. Au niandike kwa Kijapani, hapo itabidi niombe msaada kwa dada Mariam Yazawa. Mwe, mwenzenu nina kazi mimi, hata sijui nilitaka kuandika nini leo.

Hebu nikumbusheni, nilikuwa nataka kuandika nini vile?

Hata hivyo naamini mmenielewa japo kidogo, na asiyeelewa basi akaombe msaada pale TAASISI YA KUKUZA KISWAHILI CHUO KIKUU (TUKI)

9 comments:

chib said...

Mimi naona umeandika kiswahili fasaha, na nimefurahia kusoma tafakuri ya kwako kwa sikuu hii ulipokuwa unaandika.
Fasiri au tafsiri ya watu itatofautiana hasa ukuzingatia mwishoni mwa mchanganuo wa mawazo yako, umeiuliza hadhira yako kuwa ... ulitaka kuandika nini vile!
Tafsiri yangu binafsi, ni kuwa ... kwa sababu unapenda kuandika kiswahili fasaha, ni matarajio yako wachangiaji wa mawazo kwenye wavuti yako ulitegemea watakuwa wanakienzi kiswahili na kuandika kwa kiswahili fasaha.
Usiponielewa na mimi basi ... ufunguo wa jumba la vilaza alikabidhiwa mtu ambaye amefariki, lakini atarudi tu, maana nyumbani ni nyumbani hata kama kumejaa tashwishi, karaha na vurumai.
Ngoja nikapate kikombe cha tangawizi.

Yasinta Ngonyani said...

Mimi naona unaandikakiswahili na kiswahili kizuri tu na kama kuna mtu asiyeelewa basi si ajabu kwani hakuna katika dunia hii aelewaye kila kitu. Ila kama unataka kuandika kwa kiswidi mimi nitakusaidia...lol ingawa umeshasema nimejifunza ukubwani lakini ni mjuzi sana ...lol. Unaeleweka mdogo wangu. Ngoja na wengine wasema nisimaliza kurasa kwa kitu kichoeleweka.

Ramson said...

Koero, mie naamini hueleweki, na kama unaeleweka labda ni wachache sana, hususan wanablog wenzio labda!
Nimekuwa nikisoma maandishi yako lakini nimeona yanakuwa kama sauti ya mwana mpotevu nyikani.

Na kama ungekuwa unaeleweka naamini yale yote unayoyapigia kelele yangekuwa yamesawazishwa au kufanyiwa kazi.

Mara nyingi nasoma maandishi yako, lakini sioni mabadiliko kuanzia katika jamii, na serikalini kwa ujumla......

Je ni lugha utumiayo, au ni maudhui katika kile uandikacho? ni swali tu najiuliza,

Au na mie inawezekana sijakuelewa?

Hivi nilitaka kusema nini vile?

Nahisi sijaeleweka!

Markus Mpangala. said...

Siku hizi tuna habari nyingi lakini hazitupatii hekima, lakini afadhali kuwa na habari nyingi kuliko kutokuwa nazo kabisa.
Ni afadhali kusema hujaelewa endapo umesoma na kujua hujaelewa. Kueleweka ni uwasilishwaji na asiyeelewa anajua ameelewa ndiyo maana anakwambaia hajaelewa.
Kuna tofauti kubwa kusema hujaeleweka kwani pengine asiyekuelewa hajasoma na kuelewa na hata akisoma hayupo makini na kuelewa. Hapo ndipo penye hekima na akili yule mwenye akili na ahesabu kwanini hajaelewa kinachoeleweka?

Mwanzo wa kuelewa ni kufahamu na kuamini na mwisho wa kuelewa ni kuuliza au kupongeza ama kutoa changamoto.... na kadiri tuonavyo ni tatizo ndiyo tatizo zaidi.

Na kwa mrindimo wa watoto kung'amua ni falsafa za kuelewa yale yasiyoeleweka, na endapo tukiwaelewa watoto tusingekuwa na hasira nao kwakuwa kuelewa tu HAKUTOSHI, na hata KUTOELEWA TU HAKUTOSHI. Ni mara ngapi tunaelewesha lakini wanaoelewa na wasioelewa wanakuwa katika kundi moja? Ni mara ngapi wanaoelewa kuwa Koero anaandika kile kwakuwa tu anajua kuandika ....lakini hapohapo atakwambia haelewa huku akisema umeandika kwakuwa ipo hivi ama vile.

Na taabu ya kwanza ni kutaka kuelewa kuwa ili uelewe ni lazima uwe na swali kwa mwandikaji au umtazmae usoni kisha utingishe kichwa kwa madaha na kujua labda utaelewa. Umesahau kuwa unapokuwa kwenye mtihani usipoelewa swali uanamwita msimamizi au mwalimu akusomee kwa madhumuni kuwa utaelewa?

Na kuelewa tu HAKUTOSHI, je tunachanganua tamathali za semi kwa kiasi gani hati tukaelewa kuwa hatujaelewa?

Na pengine kuandika kwakuwa unaelewa watakuelewa ni kazi hata ukiwa na PHD ya kuelewa.
Ni tatizo hilohilo nilikutana nalo karibuni watu tena maprofesa wazima wa kitivo cha sheria mlimani wanauliza maswali wasiyoelewa wakati wanajua wanaelewa bali wanakuuliza ili wajue kama unaelewa wakati umeandika na kuonyesha unaelewa.

Falsafa ya maisha ni ngumu ndiyo maana mzee wa JIELEWE alindika UNAFIKIRI KWA KUTUMIA LUGHA GANI? Ni kazi ngumu binadamu tunaelewa kuwa tunaelewa na naamini tumeanza kuwa wajinga toka tulipopelekwa SHULE kwani mwenendo wa makuzi ya mtoto kuelewa ni kama ngazi ya za sebule upandavyo na kushuka

sijui kama naelewa ninachoandika, ni falsafa halali na tamu kwa kuelewa tu ni umbali wa kujua uzuri wa kuelewa na ubaya wa kutoelewa.
MMMMMH MBONA SIELEWI NAANDIKA NINI?
Hivi unanielewa mwenyekiti wa VUKANI?

Jacob Malihoja said...

Mhhh! Koero mimi umeniacha hoi, sijui hata niseme nini lakini hata darasani wapo wanaosema sijui, wako wanaosema nitajaribu, wako wanaotoa majibu ya moja kwa moja wakakosa.Mimi hata sijui nitakuwa wapi.

Kimsingi mimi si mtaalamu wa Kiswahili! Halafu ni mgeni katika blog yako. Ila tafsiri ya kueleweka au kutoeleweka ni ngumu sana, inategemea zaidi nini ulichosema na nani umemlenga.

Unaweza ukasema jambo ukaeleweka, lakini ukadhani hujaeleweka kwasababu watu wamekaa kimywa, hawafanyi lolote! unaweza ukasema na watu wasikuelewe pia wakakuangalia macho tu!

Inawezekana wanaolewa hawataki kufanya lolote kwa sababu za kuathiri ubinafsi wao au ile hulka tu ya kudharau. Wengine wanaweza wakachukua hatua wakidhani wameelewa. Na wakati mwingine matokeo ya kuelewa au kutoelewa yanaweza kuwa ya aina nyingi.

Mbona Biblia ni moja lakini kuna mamia ya madhebu ya Kikristu Duniani kote! Mbona Quran ni moja lakini kuna madhehebu mengi katika Uislam! yote hii kuelewa na kutoelewa!

Sambamba na tafsiri uliyoitoa, kwamba watoto ni makini, Picha ya mtoto mbele ya mmea mchanga wa mhindi vinanipa tafsiri kuwa kuelewa ni si jambo la siku moja, ni jambo linaloanza na kukua! leo utaelewa na baada ya muda fulani utakuwa na uelewa mkubwa zaidi katika jambo hilo ulilolielewa!

Nimekuchosha kusoma?

Sisulu said...

mbongi hiyo ya wana blogu

Anonymous said...

"Kuna nyakati jibu sahihi ndio jibu bora kabisa, jibu lisilo sahihi ndio jibu bora la pili na kukaa kimya ndio jibu bovu kabisa. Pambanua Koero......

Anonymous said...

Hapa sijaelewa chochote!
Nahisi nimepotea au nimeingia ukumbi uliojaa walevi.
Mnapimana nani anjaua sana kiswahili fasaha au nini?

Hapa Nimetoka kapa kabisa!!!!

Shein Rangers Sports Club said...

Mbona mambo yote safi tu, mie naona kila kitu kinaeleweka. Sasa hao wasioelewa wafike kule ulipowashauri (TUKI).