Wednesday, March 31, 2010

UKIONA KINYESI KWENYE KOFIA YA MTU USIHANGAIKE KUULIZA.

Hapa ni kazi tu, katu sirudi nyuma

Kwa kauli zetu tu, au matendo yetu yanaweza kubainisha kuwa sisi ni watu wa namna gani. Lakini pia tunaweza kujiuliza, SISI NI NANI? Endapo sisi ni elimu,mavazi,sura,uzuri,uwezo wa kifedha au maisha bora n.k, bado swali linabaki sisi ni nani?

Hata kama tunaelewa sisi ni nani, lakini tunatakiwa kujiuliza, ukiwa msomi wewe ni nani na usipokuwa msomi wewe ni nani? Vivyo hivyo tujiulize tunapokuwa na maisha mazuri au pesa nyingi sisi ni nani na tusipokuwa navyo sisi ni nani?

Lakini kwa mtazamo wangu, swali la SISI NI NANI, jawabu lake ni kwamba SISI NI MAWAZO YETU. Mawazo haya yana mantiki yake katika kujiridhisha kuelewa masuala mbalimbali. Mawazo yetu ndiyo msingi wa kuchanganua hoja mbalimbali.

Lakini tunapaswa kuelewa kwamba kila binadamu anao ubongo wake na unamwezesha kufikiri. Kufikiri tu hakutoshi endapo tunakosa kuelewa uhuru wa kufikiri, hivyo basi hata mwendawazimu anaweza kufikiri na anao uhuru wa kufikiri. Nitoe mfano huu!

Nakumbuka wakati fulani, nilipokuwa kidato cha sita mwalimu wetu mmoja aliwahi kutuambia kuwa ukiona kinyesi kwenye kofia ya mtu, basi usihangaike kuuliza kujua hali ya nguo yake ya ndani ilivyo.

Yalikuwa ni maneno ambayo yalinishangaza kidogo kwa kuwa, nilikuwa na uelewa mdogo, sikuweza kung’amua alikuwa anamaanisha nini.

Lakini hata hivyo alitufafanulia maana ya maneno yake yale kwa sababu karibu darasa zima hatukumuelewa.

Kuna binti mmoja mwanafunzi mwenzetu, alianza kuwa na vituko sana darasani, na wengi wetu tulikuwa tukimshangaa, kutokana na mabadiliko yake ya kitabia ambapo alifikia kuwa kero kwa kila mtu.

Siku hiyo mwalimu wetu huyo alikuwa akitufundisha somo la biashara, lakini mwenzetu katika hali ya kushangaza alianza vituko pale darasani na kuwa kero mpaka mwalimu akamtoa nje ya darasa.

Alikuwa ni binti ambaye alikuwa akiyamudu vyema masomo, lakini hata hakuna aliyejua masaibu yaliyomkuta mwenzetu hata akaanza kuwa na vituko.

Alipotoka darasani ndipo mwalimu yule alipotoa kauli ile. Hata hivyo, mwalimu yule alituambia kuwa haihitaji mtu kutumia akili za mwanasayansi aliyegundua ‘missile’ ili kujua kuwa mwenzetu yule anatumia Bangi, alituomba tumshauri mwenzetu aache kuvuta Bangi.

Ni kweli baadaye tuligundua kuwa yule mwenzetu alikuwa amejiingiza kwenye makundi ya wavuta bangi huko mtaani na pale shuleni. Kwa kuwa alikuwa hakai bwenini ilikuwa ni rahisi kwake kupitia vijiweni ambapo ndipo alipokuwa akivuta bangi na wenzie walioshindikana makwao.

Hata hivyo uwezo wake darasani haukushuka na aliendelea kuyamudu vyema masomo yake. Kuna wakati niliwahi kuzungumza naye juu ya mabadiliko yake kitabia, alikiri kutumia Bangi na sababu ya yeye kujiingiza katika tabia ile ni kutokana na baba yake kuoa mke mwingine na kumtelekeza mama yake na kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata kutoka kwa baba yao, mama yake aliamua kujitoa roho na kumuacha yeye na mdogo wake wa kiume mikononi mwa mama wa kambo.

Mama huyo alikuwa akiwatesa sana kiasi cha kusababisha mdogo wake kutoroka hapo nyumbani akiwa kidato cha pili na kuishia mitaani, yeye aliamua kubaki pale pale nyumbani na kuvumilia mateso ya mama yule wa kambo ili amalize masomo yake na kama akifaulu aendelee elimu ya juu.

Na ili amudu kuvumilia mateso hayo ndipo alipoamua kuvuta Bangi ili kuondoa msongo wa mawazo. Hiyo ni baada ya kushauriwa na rafiki yake wa karibu.

Niliongea naye mambo mengi sana na nilijitahidi kumshauri aachane na tabia ile ya kuvuta bangi lakini nasikitika kuwa hakubadilika, kwani alidai kuwa bila bangi hawezi kuishi na mama yake wa kambo.

Bila shaka, unaweza kushangaa kuwa binti yule alifaulu na kuendelea na masomo yake ya elimu ya juu….! Sasa fikiri!

Tunazaliwa na kukulia katika mazingira tofauti, na walezi wetu na jamii iliyotuzunguka ndio wanaokuwa mainjinia wazuri wa tabia tulizo nazo leo hii, haiyumkini kuwa tabia tulizo nazo zinatokana na kile tulichojifunza utotoni kutoka kwa watu tuliokuwa nao karibu sana.

Wakati mwingine unaweza kushangazwa na tabia za mtu au matendo yake, hasa pale inapotokea mtu huyo kufanya jambo ambalo hukulitarajia. Ni vigumu sana kuamini kile kilichotendwa na mtu huyo kutokana na jinsi ulivyokuwa ukimuona.

Na baadhi ya wanazuoni wanasema watu wanaofanya matendo ya kushangaza kama hayo wakati mwingine huongozwa na ‘ubongo wa mjusi’. Huu ni ubongo unaoratibu matendo yanayostajabisha hususan tabia za kushangaza zaidi.

Hivyo ubongo wa mjusi huu unawasukuma baadhi ya watu kutenda matendo ambayo kwa kawaida hayawezi kutendwa. Ubongo huu upo kati yetu haijalishi ni msomi au siyo msomi. Matendo mengi yenye kila dalili za ubongo wa mjusi yametamalaki katika jamii yetu.

Zamani kidogo mtu msomi ndio alitumika kama kipimo cha mtu mwenye busara, mtu msomi licha ya kuheshimika katika jamii lakini pia alitumika kama mshauri katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kitaaalamu au hata ya kijamii, pale itakapohitajika ushauri katika kupata suluhu iwapo kutatokea kusigishana katika jamii.

Lakini siku hizi usomi pekee, hauwezi kupambanua kiwango cha busara na hekima alizo nazo mtu, na hii inatokana na jinsi wasomi wetu walivyofinyangwa kuanzia katika malezi mpaka huko mashuleni.

Hebu tuangalie mfano wa binti huyo niliyemzungumzia hapo juu. Je iwapo atamaliza elimu yake ya juu, tutarajie kuwa atakuwa ni mtu wa namna gani katika jamii? Siyo kwasababu ya bangi tu, bali jamii yetu ndiyo inayotutengeneza, kwahiyo hata kuwa na ubongo wa mjusi kunatengenezwa pia.

Tumekuwa tukishuhudia migogoro isiyokwisha katika vyuo vyetu vya elimu ya juu na licha ya hiyo migogoro, pia tumekuwa tukisoma kutoka katika vyombo vya habari juu ya tabia na mienendo ya wasomi wetu hawa ambao tunatarajia kesho ndio wawe viongozi wetu au wataalamu wetu katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Natambua migogoro mingi inatokana na suala la sera, lakini katikati ya sera hizo kuna wasomi ambao hutumia bongo zao kuzitunga. Lakini sera hizohizo zinatesa wengine, sitakosea kuwaita watunzi wake wana ubongo wa mjusi, ni inapotokea kwamba hatutaki kutofautiana kimtazamo, basi tunakosa kuheshimu uhuru wa kufikiri.

Nimekuwa nikisoma mijadala mbalimbali katika mitandao yetu hii, kuanzia Blogu mbalimbali, Jamii Forum na ule wa wanabidii, inashangaza kidogo pale inapotokea mada ambayo inahitaji watu watafakari na kuleta changamoto zao, lakini utashangazwa na baadhi ya wasomaji watakaochangia mada husika.

Maana kama sio kupotosha mada kwa makusudi kabisa, basi watamshambulia mtoa mada kwa matusi na kejeli ili kumshushia hadhi. Huu ni uhaini wa uhuru wa kufikiri. Haigombi kushambualia, lakini endapo kujadili mada husika kunatazamwa kwanza nani aliyetoa, inapoteza maana husika.

Wakati fulani ilitokea Mbunge wa Kigoma Mheshimiwa Zito Kabwe alitangaza kujitoa katika mtandao wa Wanabidii kutokana na tatizo hilo, kwa kuwa watu wanaacha kujadili mada husika na kukimbilia kumjadili mtoa mada kwa kumshambulia kwa kila aina ya kashfa.

Sawa, ni uhuru wa kufikiri, lakini endapo tungeweza kumshambulia mtoa mada kwa hoja ingeeleweka zaidi. Lakini kushambulia kwa kashfa na matusi ni ubongo wa mjusi, hii inatoa taswira kwamba hatujui sisi ni nani.

Lakini katika mitandao yetu tunajadili kitu gani na kwanini?.
Tatizo la kumjadili mtoa mada lilimkimbiza Mheshimiwa Zito katika mtandao wa Jamii Forum, na sasa yuko katika hati hati za kujitoa katika mtandao wa Wanabidii.

Inashangaza kuona kwamba, wasomi wetu tunaotarajia walete chachu ya mabadiliko ya kisiasa,kiuchumi na kijamii hapa nchini ndio hao ambao wameshindwa kujiheshimu. Kwao wao matusi, kashfa na kejeli ndio aina ya maoni waliyo nayo katika kuchangia mada.

Sikatai watu kutofautiana kimtizamo katika masuala mbalimbali, lakini hivi hakuna lugha nzuri inayoweza kutumia katika kufikisha ujumbe kwa njia ya busara zaidi isipokuwa kutumia matusi na kejeli? Kuna watu ambao kwa makusudi kabisa wanaficha utambulisho wao na kuwakashifu watoa mada kiasi cha kuwashushia heshima. Hawa naweza kusema wanatumia ubongo wa mjusi.

Mwalimu wetu aliposema kuwa,ukiona kinyesi kwenye kofia ya mtu, basi usihangaike kuuliza kutaka kujua hali ya nguo yake ya ndani ilivyo, hakuwa na maana nyingine isipokuwa kutanabaisha kuwa unaweza kujua kiwango cha ufahamu wa mtu kutokana na matamshi au matendo yake.

Kwamba elimu pekee haitoshi kupambanua kiwango cha hekima na busara alizo nazo mtu. Na kama elimu ndiyo kipimo cha busara, ni dhahiri leo kusingekuwepo ufisadi,ubadhirifu ambayo hufanywa na wasomi wanaotegemewa.

Nami kupitia blog hii, nimeshawatambua watu wa aina hiyo, na ninawakaribisha sana kutoa changamoto zao hapa kwa lugha yoyote waitakayo iwe ni ya matusi, kejeli au hata kukashifu, kwani hiyo haitanifanya nirudi nyuma katika kuelimisha jamii.

Nawakaribisha mstari kwa mstari, neno kwa neno bila kujali matumizi ya tamathali za semi. Kwasababu hiyo ninaomba niyanukuu maneno haya ‘Know your enemy, know yourself and you can fight a hundred battles without disaster’ (SUN TZU).

Saturday, March 27, 2010

LEO NIMEMKUMBUKA SITI BINTI SAAD

Siti Binti Saad

Siti binti Saad alizaliwa katika kijiji cha Fumba, Zanzibari mwaka 1880. Alipozaliwa alipewa jina la 'Mtumwa' hii ni kwa vile alizaliwa katika kipindi cha utumwa wa Kiarabu. Jina la Siti alipewa na mkabaila mmoja wa kiarabu.

Baba yake bwana Saadi alikuwa ni Mnyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga, lakini wote wawili walizaliwa Zanzibari. Hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana na walijishughulisha zaidi katika shughuli za kilimo na ufinyanzi kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.
Kama waswahili wasemavyo 'kuzaliwa masikini si kufa masikini' Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji. Kipaji hiki kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza. Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali wa maili nyingi na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo. Alifananishwa kuwa na mapafu yenye nguvu kama ya simba kutokana na alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila kuachia pumzi.
Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Kurani. Hivyo mnamo mwaka 1911 aliona ni bora ahamie mjini ili kubooresha maisha yake zaidi. Ujio wake wa mjini ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja wa kundi la muziki wa Taarabu la "Nadi Ikhwani Safaa" aliyeitwa Muhsin Ali. Katika kipindi hicho hilo ndilo lilikuwa kundi pekee la muziki wa taarabu lililoanzishwa na Sultani mpenda starehe na anasa bwana Seyyid Barghash Said.
Kundi hili lilikuwa ni la wanaume peke yake , wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni. Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha ya kiarabu. Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa "Nadi Ikhwani Safaa" ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonyesho mbalimbali katika jamii. Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia katika maharusi na sherehe zingine mbalimbali, inasemekana ulifika wakati ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo kutumbuiza. Siti alikuwa ni moto wa kuotea mbali na jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika. Na punde Siti alianza kufananishwa na 'Umm Kulthum', mwimbaji mahiri wa kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.

Kama nilivyosema moto wa Siti ulikuwa si wa kuusogelea karibu, mwaka 1928 kampuni ya kurekodi muziki ya Columbia and His Master's voice yenye makazi yake Mumbai India ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi na hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake utauzika. Kampuni ile haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo, na hadi kufikia 1931 santuri 72,000 zilikuwa zimeuzwa. Kutokana na kusambaa kwa santuri hizi, umaarufu wa Siti ulizidi mara dufu watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibari kuja kumwona. Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.


Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu, hivyo wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumshusha na hasa walitumia kigezo kwamba hana uzuri wa sura, nyimbo nyingi ziliimbwa lakini huu ndio uliovuma sana:-


Siti binti Saadi kawa mtu lini,
Kaja mjini na kaniki chini,
Kama si sauti angekula nini?


Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu shambulio namna hii:-


Si hoja uzuri,
Na sura jamali,
Kuwa mtukufu,
Na jadi kebeli,
Hasara ya mtu,
Kukosa akili.


Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifumatafuata. Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla, kwani katika kipindi chake watu matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru halafu wewe uliyeshitaki ndiye unayefungwa.


Utunzi wake wa wimbo wa Kijiti ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka bara, mwanamke huyu alipofika alikutana na Tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda, hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akamuua. Tajiri yule alishitakiwa na bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile, lakini kwa vile ni Tajiri alitoa pesa na kesi ikawageukia wale mashahidi na kufungwa.

Siti akatoa wimbo huu :-
Tazameni tazameni,
Eti alofanya Kijiti,
Kumchukua mgeni,
Kumcheza foliti,
Kenda naye maguguni,
Kamrejesha maiti.
Siti aliendelea kumwambia katika nyimbo zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa ajili yake.Siti aliendelea na shughuli yake ya muziki hadi uzeeni, muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita " Wasifu wa Siti binti Saadi." Wasifu huu unaonekana kuwa ndio bora zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hiki kinatumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.
Tarehe 8 Julai, 1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu. Ingawa pengo hilo haliwezi kuzibika lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni Bi Kidude
Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake, Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA), kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao "Sauti ya Siti". Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.

Wednesday, March 24, 2010

DADA SUBI, KUANDIKA MADHILA YA WANAWAKE, LABDA UWE NA MOYO KAMA WA MWENDAWAZIMU.

Hawa ndio waathirika wakubwa
Bubu hupata kusema, mambo yanapomzidi,
Na kiwete husimama, akakimbia baidi,
Ogopa moto wa chuma, sione kiko baridi,
Kama waume si wema, wake wangalikuwaje?

Hata kuku huchachama, unapomtia kedi
Na jorowe takuuma, iwapo hapana budi,
Nyundo ni nyundo kwa chuma, japo kisiwe baridi,
Kama waume si wema, wake wangalikuwaje?

Dada Subi nimeanza na shairi hilo lililoandikwa na Sheikh Amri Abedi katika kukuandikia waraka huu mahsusi kwako. Nimekuwa nikiandika kila jambo linalogusa maisha ya jamii iliyonizunguka yakiwemo yale ya kufurahisha, ya kuhuzunisha na ujinga kidogo.
Yote hiyo ni katika kujaribu kumgusa kila mtu kuanzia mwenye upeo mkubwa na yule mwenye upeo mdogo sana. Kuna wakati niliwahi kuuliza hapa kibarazani kwangu kuwa, “hivi naeleweka?” Lilikuwa ni swali ambalo wengi hawakunielewa nilikuwa namanisha nini, ingawa wako baadhi waliojaribu kuainisha mtazamo wao juu ya kile ninachowaza.
Hivi karibuni niliweka taswira inayoonesha majukumu yanayowakabili wanawake. Ingawa ni majukumu yetu, lakini nilikuwa najaribu kuonesha jinsi utekelezaji wake ulivyo mgumu kulingana na mazingira yaliyopo, licha ya kwamba tuko kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolijia. Nakumbuka nilipata upinzani mkubwa sana kutoka kwa wanaume wengi sana wakiwepo hata wale ambao sikuwatarajia.
Wakati nilitarajia mjadala ambao ungeibua namna bora ya kumuondolea mwanamke huyu madhila anayopambana nayo, lakini ikawa ni kinyume chake. Inashangaza kidogo kuona kwamba mijadala inayohusu haki za binadamu inashindwa kukubali kuwa swala la madhila yanayowakabili wanawake ni kitu ambacho kinahitaji kupewa mtazamo wa kipekee kutokana na kushushwa na kunyimwa haki zao.

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni miongoni mwa ukandamizwaji wa haki za binadamu ulio mkubwa na unaofanyika sana duniani hivi sasa. Ukandamizwaji wa mwanamke, kwa mazoea au kwa sababu ya utandawazi, kwa kukosa elimu kutokana na kubaguliwa kijinsia au kwa sababu ya wazazi kufanya uchaguzi nani asome katika familia, kutokana na uhaba wa rasilimali, wanawake wengi wamejikuta hawana elimu ya kutosha ya darasani.
Kwa kukosa elimu ya darasani wanawake wanashindwa kujua haki zao za msingi na kuepuka mila potofu ambazo zinawakandamiza, lakini pia wanakosa ajira na kipato ambacho kingewawezesha kujikimu na kumudu kuendesha maisha yao. Ikumbukwe kwamba wanawake wanafanya saba ya kumi ya watu wote masikini duniani.
Pia ni vyema ikafahamika kwamba kati ya kila wakimbizi kumi hapa duniani, wanane ni wanawake na watoto na kati ya hao, wawili tu ni wanaume. Lakini pia ikumbukwe kwamba migogoro yote ya kisiasa inayosababisha uwepo wa wakimbizi hapa duniani chanzo chake kikuu ni wanaume.
Wakati Fulani umoja wa Mataifa ulitoa taarifa juu ya haki za binadamu bofya hapa kuisoma.
Katika taarifa hiyo umoja huo ulikiri wazi kuwa kusafirishwa kwa lazima kwa wanawake na watoto kote duniani na kuuzwa na kufanyishwa kazi kwa lazima ukiwemo ukahaba, Inaaminika kuwa aina mpya ya UTUMWA hapa duniani na umekuwa ni jambo la kawaida kabisa.
Takwimu mbalimbali za mashirika ya haki za binadamu likiwemo shirika la Human Right Watch zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto milioni moja, karibu wote wakiwa ni watoto wa kike wanalazimishwa kuingia kwenye ukahaba, wakiwemo wale wa nchi masikini zaidi kama Tanzania. Hulazimishwa kuingia kwenye ukahaba kwa ulaghai wa kupatiwa kazi mijini, ndani ya nchi husika (Hili nimewahi kulizungumza katika makala zangu za nyuma).
Kwa sehemu kubwa, watoto hao hutoka kwenye familia ambazo mtu akichunguza atagundua kwamba ni masikini na umasikini wao umetokana na mfumo mbaya wa uchumi duniani. Hapa nchini idadi kubwa ya wasichana hutolewa vijijini na kupelekwa mijini hususana Dar es salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza na miji mingine ambapo huahidiwa kazi za ndani na shule lakini hakuna litimizwalo na wengine huishia kunyanyaswa na kulazimishwa mapenzi na mmoja ama baadhi ya wanafamilia na haya husababisha kukimbia nyumba bila kujua waendako na wengine kujiingiza katika maisha hatari ya ukahaba, rejea makala ya kaka Mubelwa kwa kubofya hapa
Lakini kuzungumzia swala la madhila wayapatayo wanawake inabidi uwe na moyo kama wa mwendawazimu hivi, kwani unaweza kushuhudia dhihaka na kejeli kutoka kwa wanaume utadhani hawakutoka katika matumbo ya wanawake. Inabidi tufike mahali tuuone ukweli kuwa pamoja na mgawanyiko wa majukumu kati ya wanawake na wanaume, lakini tukubaliane kuwa hatuko kwenye uwanja unaofanana kimazingira.
Kama ukilinganisha mazingira ya wanaume katika utekelezaji majukumu yao ya kila siku, na mazingira ya wanawake katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku utagundua kwamba kwa asilimia kubwa wanawake wanatekeleza majukumu yao katika mazingira magumu sana ukilinganisha na wanaume kutokana na mfumo dume uliojikita hapa duniani kwa karne nyingi tu huko nyuma.
Kwa waraka huu dada Subi ni kutaka kuweka ufafanuzi wa kile nilichokuwa najaribu kukifikisha kwa wasomaji wa kibaraza hiki ili kufungua mjadala ambao ungefika mahali tukapata suluhisho, lakini nilishangazwa na jinsi baadhi ya wasomaji walipojaribu kupotosha mada na kunishambulia dhahiri. Sijutii kwa kile nilichokifanya yaani kuweka ile mada lakini naamini ujumbe ulifika, mahali pake.
Mimi sio mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake kama baadhi ya wasomaji walivyonituhumu, lakini kama mwanamke mtarajiwa nilikuwa nayaangalia madhila wayapatayo wanawake kwa jicho la tatu, lakini kwa kuwa nimeonekana kuwa mhafidhina, sina budi kubadili aina ya uandishi wangu na kujikita kwenye kitu kingine ambacho hakitaleta kusigishana na baadhi ya wasomaji wangu.

Ni mimi mdogo wako
Koero Mkundi

Sunday, March 21, 2010

HOFU YOTE HII NI YA NINI?

Hii ndio njia wanayotumia kuingia nchini

Jana nilikuwa na Dine na rafiki yangu mmoja, binti wa Kijerumani katika mghahawa mmoja marufu ulioko maeneo ya Masaki.
Yeye, yuko hapa nchini kama Expert akiwa anafanya kazi katika sekta ya Utalii.

Wakati tukiendelea kula huku tukipiga soga, mara wakaingia Wachina kama kumi hivi wakataka waandaliwe meza ya pamoja, lakini baada ya kuingia hao Wachina, atmosphere ya pale ndani yote ilibadilika kwani karibu wateja wote waliokuwepo pale ndani ambao mostly walikuwa ni wazungu waligeuka kuwatazama.

Wachina wale walikuwa wakiongea kwa kikwao tena kwa sauti kiasi kwamba utulivu uliokuwepo pale mghahawani ulitoweka ghafla.

Yule rafiki yangu ambaye muda wote alikuwa amewatumbulia macho, alinigeukia na kuniuliza, “Ninashangazwa sana na serikali yenu kuwakumbatia Wachina kiasi hiki, mnadhani watasaidia kuinua uchumi wenu”

Kwa kifupi nilimjibu kuwa huu ni utandawazi na serikali yetu haina mkataba na taifa Fulani kuwa ndilo lenye mamlaka ya kuingia na kuishi au kufanya kazi hapa nchini, kwa hiyo yeyote yule mwenye kutaka kuja kuwekeza hapa nchini anaruhusiwa ili mradi asivunje sheria a afuate taratibu za kuingia hapa nchini basi.

“Nadhani huko sahihi”, alisema binti wa Kijerumani, “Unajua sisi inapotokea tunataka ku renew working permit zetu, kunakuwa na usumbufu mkubwa sana, ukilinganisha na hawa Wachina, wao wapo kila mahali na wanafanya biashara ambazo zilipaswa kufanya na nyie lakini hawabughuziwi kama tunavyobughuziwa sisi wazungu, imefikia mahali sasa tunahisi kubaguliwa waziwazi tofauti na hawa Wachina”

“Wewe unadhani tatizo ni nini?” Nilimuuliza.

“Sikiliza, hawa wachina ni wajanja sana wameleta miradi ya ujenzi wa barabara kama danganya toto, na katika miradi hiyo wamejipenyeza kwa kisisngizio cha expert na baada ya mradi kuisha wanendelea kuishi hapa nchini kwa kisingizio kingine cha wawekezaji ambapo hufanya shughuli ambazo zilipaswa kufanywa na nyie wazawa, na wamejipenyeza katika maeneo ya uswahilini na kuishi na wenyeji kwa ushirikiano na wamejifunza Kiswahili kiasi kwamba wamegeuka sehemu ya jamii ya chini kabisa, lakini baadae hawa watu wata take over kila kitu na kuwaacha mkishangaa, sio watu hawa jiangalieni”

“Ok, kwa nini na nyie msifanye hivyo” nilimshauri,

Haiwezekani, unajua sisi tuna utamaduni tofauti na nyie, lakini Wachina huenda utamaduni wao hauna tofauti kubwa na wa kwenu na ndio maana wameweza ku corp na society yenu bila shaka” alinijibu……….

Kwa kifupi mjadala ulikuwa ni mzito na mrefu kiasi kwamba ulichukua sehemu kubwa ya mazungumzo yetu…….any way labda nilichotaka kuwauliza hapa ni Je kuna haja ya watanzania kuhofia ujio wa hawa Wachina, au wamekuja kusukuma mbele gurudumu la maendeleo?

Tuesday, March 16, 2010

DAR ES SALAAM: WANAUME NA SUPU YA PWEZA!

Huyu binti naye alikuwa akijipatia pweza

Nimerejea Dar, na kama kawaida, juzi nilitoka kwenda kumtembelea rafiki yangu mmoja anayeishi maeneo ya Msasani. Eneo la Msasani ni eneo ambalo sijui nisemeje, lakini ni eneo ambalo linaishi watu wenye vipato tofauti tofauti, kuanzia wale wenye vipato vikubwa na wale wenye hali duni kabisa na maisha yanasonga mbele kama kawaida.

Hiyo ni tofauti na kwa wenzetu kule nchini Kenya ambapo sio rahisi sehemu za uswahilini kama vile kule Kibera au Kariobangi kukuta mtu mwenye kipato kikubwa amejichanganya uswahilini na kujenga nyumba yenye hadhi kwani hilo ni jambo ambalo haliwezekani, na huenda mhusika akaonja joto ya jiwe kwa kufanyiwa mchezo mchafu, hata kabla ya ujenzi.

Nilifika kwa rafiki yangu majira ya saa kumi jioni, kwani anaishi eneo ambalo lina pilikapilika nyingi sana. Nilipofika nilimkuta amekaa kibarazani kwao akijisiomea novel zake. Alinikaribisha kwa bashasha na tukaanza kukumbushana stori zetu za zamani na vituko tulivyokuwa tukivifanya enzi zetu za shule.

Mnajua maisha ya shule huwa yana mambo mengi ya kukumbukwa maana ndipo mahali ambapo kuna kila aina ya ujinga, na werevu kidogo. Wakati tukiendelea kupiga soga, nilishangaa kuona kundi la wanaume wakiwemo wazee na vijana wakiwa wameizunguka meza upande wa pili wa barabara huku kila mmoja akiwa na kibakuli chake. Kulikuwa na vitu Fulani wanaokota juu ya meza na vijiti yaani tooth picks na kula huku wakiteremshia na kinywaji kilichopo ndani ya vibakuli vyao.

Nilijishikwa na udadisi, ikabidi nimuulize shoga yangu, kuwa ni kitu gani kinaendelea pale, shoga yangu linijuza kuwa mahali pale ni maarufu kwa uuzwaji wa supu ya pweza. Shoga yangu hakuishia hapo aliendelea kubainisha kuwa supu ya pweza imeibuka na kuwa maarufu siku za hivi karibuni hususana kwa vijana kwa kuwa inasemekana kuwa inaongeza nguvu za kiume.

Kwangu mimi hiyo ilikuwa ni habari mpya, nafahamu kuwa hapa jijini hasa maeneo ya Kariokoo ni kawaida kukuta vijana wakiwa wamebeba masinia yakiwa yamesheheni vipande vya pweza, ngisi na chachandu, wakitembeza mtaani, lakini hili la supu ya pweza sikulifahamu.

Nilimuuliza shoga yangu kama ninaweza kwenda mahali pale ili kupata habari zaidi, shoga yangu huyu kwa bahati nzuri anajua kuwa mimi ni mwanablog, na hakusita kunitania, “He Koero nawe, najua hapo ushapata umbeya wa kuweka bloguni kwako, maana uliadimika kweli”
“Habari ndiyo hiyo shoga yangu hivi hapa nimeshapata udaku, maana najua wasomaji wangu wamemiss kweli longo longo zangu” nilimjibu.

Tulivuka barabara na kufika mahali pale, “Shifeya, tunaona umetuletea mgeni hapa, karibu dada” alitudaka yule kaka muuzaji wa supu. Tulilipofika pale tulikuta anazo chupa za chai kubwa maarufu kama thermos chini ya meza yake, ambazo nilijulishwa na mwenyeji wangu kuwa ndizo anazotumia kuhifadhia supu hiyo ya pweza.

Wale vijana na baadhi ya wazee tuliowakuta pale walionekana kufurahiya uwepo wetu pale na nilikaribishwa nijipatie vipande vya pweza na supu. Niliwashukuru kwa ukarimu wao na kuwaambia kuwa kwa bahati mbaya situmii pweza kwa kuwa nina mzio {Allergy} nao. Lakini ukweli ni kwamba sisi wasabato haturuhusiwi kula aina hiyo ya samaki.

Kama kawaida nilifanya udadisi wangu, kwa yule kijana muzaji wa supu, kutaka kujua sababu ya wanaume kuipenda sana supu ya pweza, “Unajua dada, supu ya pweza inafaida nyingi sana, kwanza ni kiburudisho, pili inaondoa uchovu, inachangamsha na pia…….si unajua yale mambo yetu yaleeee,”
“Mambo gani sasa, mbona hamalizii” nilifanya udadisi,
“Weweee sasa unamficha nini kwani ni mtoto mdogo huyo?” alidakia kijana mwingine pembeni aliyekuwa na bakuli lake la supu. “Unajua sister supu ya pweza, pamoja na hizo faida alizokueleza, lakini faida kubwa kabisa ni kwamba inaongeza nguvu za kiume, yaani kama mwanaume anapata supu hii ya pweza halafu akutane na mwanamke, weee inakuwa ni shughuli pevu.” Watu waliokuwa pale wote waliangua vicheko.

“Mweleze huyo akamjulishe shemeji, maana kama hayajua mambo haya, basi akiyajua itakuwa kazi kweli kweli”
“Tokeni zenu kule kwanza ninyi watu wa bara ndio mliosababisha mpaka pweza wamepanda bei siku hizi, kwani zamani pweza hakuwa ghali kiasi hiki lakini tangu mufahamu kuwa inafaa kwa majamboz, imekuwa taabu mpaka wamepanda bei” alisema mzee mmoja.

Mara akadakia kijana mwingine, “Huo sasa ni uongo, pweza wamepanda bei kutokana na kuenea kwa mahoteli na mighahawa ya kitalii hapa jijini, na ndio maana wakapanda bei”
Basi yalizuka malumbano mapaka nikashindwa nimsikilize nani na nimuache nani. Nilitoa ofa ya kuwanunulia chupa nzima ya chai iliyojaa supu ya pweza na kujiondokea zangu.

Hata hivyo kupitia malumbano yao nilikuja kufahamu kuwa mpaka miaka ya tisini pweza hawakuwa maarufu kiasi hiki na hata supu ya pweza haikuwa maarufu sana, lakini kutokana na hiyo sifa ya kuongeza nguvu za kiume, imetokea kuwa maarufu miaka ya 2000 na kuwafanya pweza kuwa ghali.

Yule kijana muuuza pweza alinijuza kuwa inamlazimu kwenda hadi Bagamoyo kuwafuatilia pweza kule, kwani hapa Ferry jijini Dar Pweza wamekuwa ni ghali mno kutokana na kupata umaarufu na pia kutokana na watu wa mahoteli na mighahawa ya kitalii kuwanunua kwa bei ya ghali.

Kule Bgamoyo napo hawakuwa ghali sana, lakini siku za karibuni wamekuwa ghali sana kutokana na wafanyabiashara wengi wa supu ya pweza jijini Dar kukimbilia kule kuwatafuta.
Kuna wakati niliwahi kudesa habari fulani kutoka kwenye kibaraza cha dada Yasinta, inayozungumzia wanaume kutumia dawa ya kuongeza nguvu za kiume maarufu kama Mkuyati, unaweza kubofua hapa ili kujikumbusha. Nakumbuka baadhi wasomaji walionekana kupingana na kile alichandika dada Yasinta. Sasa Je na hili la supu ya pweza watabisha?

Kama yupo mwenye changamoto juu ya mada hii anakaribishwa kwani mimi ni msimuliwaji tu.

Saturday, March 13, 2010

KOERO NDANI YA DAR.......

Foleni Jijini Dar
Hatimaye baada ya safari ndefu nimeshawasili Jijini Dar. Kama kawaida nitaendelea kuwakilisha katika blog yenu hii ya VUKANI.

Jiji letu nimelikuta vile vile, hakuna mabadiliko makubwa na foleni ya magari ndio usiseme. Kwa wale waliozoea kuendesha magari kule mikoani, hususan Arusha na Moshi, basi wakija hapa inabidi wapunguze jazba maana unaweza kujikuta unapigana kutokana na kukerwa na kile wanachoita kuchomekea, hasa Daladala, unaweza kuwa umekaa folen muda mrefu, lakini ghafla unakuta daldala hiloo limekuchomekea, yaani unatamani ushuke umlambe mtu makofi, lakini weee, watu wa Daladala ni washari ajabu, ngumi mkononi.
Ngoja nisianze porojo hapa, nikapumzike halafu tukutane kesho.................

SAFARINI DAR

Jana nilikuwa hapa
Ndugu wasomaji ninaondoka asubuhi hii kuelekea Dar. Nimekaa Arusha kwa takriban mwezi mmoja na sasa inabidi nirudi nyumbani kuungana na familia yangu. Shughuli ya Kilimo ndio imekamilika na sasa nasubiri mvua kidogo za mwezi wa nne ili mazao yazidi kupata kasi ya kukua.

Mungu akinijaalia nikifika salama Dar, nitawajuza, maana safari ni hatua.

Thursday, March 11, 2010

TARIME, TARIME YANGU.

Tarime, Tarime yangu, Tarime unapendeza
Tarime mekutwa fungu, Ufanisi kuongeza
Rorya pasipo majungu, Ulipaswa kupunguza
Tarime maisha bora, Kabisa yawezekana.


Mito, ziwa migodi, Tarime yote unayo,
Mbuga, mabonde na milima, Tarime haki unayo,
Hata ngano ungelima, Tengeneze wako mvinyo,
Maisha bora Tarime, yawezekana hakika.


Rutuba, maji, migodi, Kweli kajalia Mungu,
Mazao, nyama, madini, Tarime kwako si haba,Baridi,
joto na jua, Hizo zote hali zako,
Maisha bora Tarime, hakika yawezekana.


Tarime wewe kiungo, Afrika Mashariki,
Kenya, Uganda na Bongo, Kufika hakupingiki,
Tarime kweli kiwango, Bila wewe hatufiki,
Maisha bora Tarime, Yawezekana hakika.


Ninapatwa na simanzi, Damu kwako nikiona,
Mauaji kwako enzi, Majeraha yasopona,
Kuwa m'baya balozi, Tanzania kukuona,
Tarime damu simwage, Tarime nifute chozi.


Nakiri kweli nakiri, Hasira kwako asili,
Mejichimbia kaburi, Thamaniyo kwenda mbali,
Uukane ukatiri, Upige goti usali,Tarime nifute chozi, Tarime damu simwage.


Makazi, Afya, Elimu, Maishayo kweli duni,
Nyamongo kunyweshwa sumu, 'Mekuwa utamaduni,
Watu wako kujikimu, Uhai wao rehani,
Siyo laana Tarime, Tarime jenga umoja.


Mtimbaru, Mryanchoka, Mnchali na Mnyabasi,
Yatupasa badilika, Mwirege pia Msweta,
Amani kuimarika, Jaluo pia 'sibezwe,
Amani ii langoni, Tarime fumbua macho.


Tarime simwage damu, Watu si tambiko tena,
Uwaone binadamu, Watuwo kutouana,
Tarime muombe Mungu, Mungu atawaepusha,
Mungu wangu nakuomba, Kumwaga damu epusha.


Shairi hili nimelidesa Jamii Forum na limeandikwa na Ghati Makamba.

Wednesday, March 10, 2010

AKAMWAMBIA MKEWE AMKATE KICHWA!

Karibu mgeni Sungura


Hapo zamani za kale Sungura alijenga urafiki na Jogoo, sasa siku moja Jogoo akamualika Sungura amtembelee nyumbani kwake. Basi sungura akajikusanyia zawadi zake na kumuaga mkewe kisha akaondoka kwenda kumtembelea rafiki yake Jogoo.

Alipofika alikaribishwa kwa bashasha na jogoo, na aliandaliwa chakula kitamu na wenyeji wake, baada ya kula Jogoo alimtoa mgeni wake huyo na kumtembeza sehemu mbali mbali ili kumuonesha fahari ya mji wao, Sungura alipendezwa sana na ziara hiyo.

Ilipofika jioni walirudi nyumbani wakamkuta mke wa Jogoo kawaandalia chakula cha jioni, baada ya kula Sungura alioneshwa mahali pa kulala, kisha jogoo na mkewe nao wakaingia chumbani kwao kulala. Lakini kabla sungura hajapitiwa na usingizi akasikia mazungumzo ya jogoo na mkewe huko chumbani kwao, na mazungumzo yenyewe yalikuwa ni haya.

Jogoo: Mke wangu nikate kichwa nataka kulala mie.
Mke wa Jogoo: Sawa mume wangu,

Sungura kusikia hivyo akataharuki, “He kumbe Jogoo kulala ni mpaka akatwe kichwa?
Ilipofika alfajiri akamsikia Jogoo akimuamsha mkewe tena.

Jogoo: Mke wangu, eh, hebu nirudishie kichwa changu nataka wika mie kuwaamsha watu.
Mke wa Jogoo: Haya mume wangu ngoja nikurudishia kichwa chako. watu.

Baada ya kurudishiwa kichwa chake, jogoo akaanza kuwika kama kawaida yake, ili kuwaamsha watu…Koko rikooooo ………Kucha kucheleeeeeeee………

Basi kulipopambazuka sungura akaamka na kupata staftahi iliyoandaliwa na wenyeji zake na baada ya stafutahi akapewa zawadi za kwenda nazo nyumbani kwake, lakini kabla ya kuondoka aliamualika Jogoo naye amtembelee ili kulipa fadhila kwani alipanga kumfanyia jogoo mapokezi makubwa kushinda yale aliyoyapata.

Sunguara alipofika nyumbani kwake alimsimulia mkewe juu ya safari yake na mapokezi aliyoyapata, pia hakusahau kumweleza mkewe mshangao alioupata kuhusiana na ule utaratibu wa Jogoo kukatwa kichwa na mkewe kabla ya kulala na kurudishiwa kichwa chake alfajiri ili awike.

Sungura alimtaka taka mkewe na yeye afanye hivyo siku wakitembelewa na Jogoo, kwa kuwa amemwalika aje kuwatembelea, alimtaka mkewe amkate kichwa akitaka kulala, na kukirudishia alfajiri ili amwonyeshe jogoo kuwa na yeye anaweza kukatwa kichwa na kurejeshewa asubuhi.

Ni kweli baada ya juma moja kupita Jogoo akamtembelea Sungura, na yeye alibeba zawadi kemkem kwa ajili ya wenyeji wake.

Alipofika alipokelewa na wenyeji wake ka bashasha, na kuonyeshwa ukarimu wa hali ya juu.

Kama alivyofanyiwa kule na Jogoo, na yeye Sungura alimtembeza mwenyeji wake kumuonesha mji na maeneo ya vivutio vya mji wao.

Walirejea jioni na kupata mlo wa usiku, huku wakipiga soga. Ulipofika muda wa kulala, sungura alimuonesha jogoo mahali pa kulala, na yeye na mkewe wakaingia chumbani kwao kulala.

Mara Sungura akamwambia mkewe.

Sungura: Mke wangu eh, hebu nikate kichwa mie nilale..
Mke wa Sungura: Sawa mume wangu.
Mke wa Sungura akachukua kisu na kumkata mumewe kichwa, na kukitenganisha na kiwiliwili.

Asubuhi kulipopambazuka akaanza kumuamsha mumewe,a lakini hakuamka alijitahidi kukiunganisha kichwa ili mumewe aamke lakini hakikuunga na wala Sungura hakuamka, alikuwa amekufa tayari.

Mke wa Sungura ikabidi aombe msaada kwa Jogoo, lakini Jogoo alipofika chumbani aliona damu zimetapakaa kila mahali na kichwa cha Sungura kilikuwa kimetenganishwa na kiwiliwili.
Jogoo kuona hivyo, akataharuki, lahaulaaaa…kulikoni huyu hana kichwa, aliauliza Jogoo.
Mke wa Sungura akamsimulia Jogoo kuwa utaratibu wa kukatwa kichwa kabla ya kulala aliupata kutoka kwake alipowatembelea.

Ndipo Jogoo akamwelewesha kuwa yeye huwa hakatwi kichwa na mkewe kama vle alivyofanya Sungura bali mkewe humsaidia kuficha kichwa cheke kwenye mbawa zake kila akitaka kulala na alfajiri mkewe humsaidia kutoa kichwa chake kutoka kwenye mbawa ili aweze kuwika kuwaamsha watu.

Mke wa Sungura liaposikia hivyo akaanza kulia kwa uchungu kwa kuondokewa na mumewe.

Jogoo aliporudi kwa mkewe alimsimulia masaibu yaliyomkuta Sungura.

Hadithi hii nilisimuliwa na bibi yangu Koero, siku nyingi kidogo, wakati nilipokwenda kijijini likizo. Nimeikumbuka leo nikaona si vibaya nikiiweka hapa ili tutafakari pamoja.

Je hadithi hii inatufundisha nini? Tafakari………………………

Monday, March 8, 2010

NDIO TUKIAMUA TUNAWEZA

TUPO ndani ya siku kumi na sita za harakati, ili kuhamasisha watu katika nafasi zao kuchukua hatua kupinga kwa nguvu zote ukatili wa aina yoyote dhidi ya wanawake. Ni kweli kwamba katika zama hizi tulizo nazo kama jamii hatuwezi kuendelea kuvumilia ukatili dhidi ya wanawake.

Kampeni hiyo mahsusi ina kaulimbiu kwamba kama jamii tunaweza kuzuia ukatili wa kijinsia. Hakuna ubishi juu ya dhamira hii ni kwamba kama jamii tukiamua kukomesha ukatili dhidi ya wanawake ni kitu kinachowezekana kabisa.


Lakini msisitizo hapa ni lazima uwekwe kwenye nafsi na nafasi ya kila mtu alipo, harakati hii ni kama wokovu, haitoshi tu kutofanya ukatili wa kijinsia wewe mwenywe, unatakiwa kuwa balozi wa mabadiliko, kwa maana kwamba ili jamii yetu ifikie kiwango cha kutokuwa na uvumilivu na ukatili wowote wa kijinsia, ni lazima kutovumilia huko kuanze na nafsi ya mwanajamii wetu mmoja mmoja.
]
Haki za wanawake ni haki za binadamu, hili ndilo jambo la msingi na dira ya kutuongoza katika harakati hizi, hatuwezi kujiita taifa lenye amani na utulivu wakati wapo raia miongoni mwetu wanaoyaona maisha yao ya kila siku ni kama jehanamu.


Kwamba katikati ya kisiwa cha amani na utulivu wapo watu ambao kila uchao, maisha yao yamejaa hofu na wasiwasi, maumivu na uchungu ni sehemu ya maisha yao. Hatuwezi kujiita ni watu tunaofurahia maisha wakati jirani yetu kipigo ndio utaratibu wake wa maisha.
Na haya yanatokea si kwa sababu wao wametaka au wamejiweka katika mazingira hayo magumu, wanawake wengi wanatendewa ukatili huu eti kwa sababu tu waliumbwa kwa jinsia ya kike.


Wapo baadhi ya wanaume - sihofu kuwaita washenzi (hawana ustaraabu) - ambao kwao mwanamke ni kiumbe duni kwa kila hali, eti tu kwa kuwa ni mwanamke. Huu ni ujuha wa hali ya juu sana ambapo mwanajamii wa jamii iliyostaarabika hasitahili hata kuwaza tu wendawazimu huo.

Wapo wanaume na bahati mbaya sana, wengine ni vijana wanajua kuoa maana yake ni kuweka mjakazi ndani ya nyumba yako, kwamba wao wanakuwa ndiyo alfa na omega ndani ya nyumba. Lile wanalolitaka wao ndio linalokuwa bila kujali kwamba mke ni mwenza aliye sawa (a different but equal partner) katika kuamua na kupanga hatima ya maisha yao.
Tofauti za kijinsia hazikuumbwa ili zimfanye mwingine mnyonge kwa mwenzake, tofauti hizo zipo na ziliweka makusudi ili kuyafanya maisha ya dunia hii yawezekane, ilimpendeza Muumba wa Ulimwengu huu kwamba aweke tofauti hizo ili ziwasaidie wanadamu kukamilishana na siyo kunyanyasana.


Lakini kwa bahati mbaya wapo ndugu zetu wengine ambao hudhani kwamba ili kudhihirisha uanaume wao ni lazima kumyanyasa mwanamke, huo ni uzuzu wa kiwango kilichopea, mwanamume halisi ni yule anayejiamini na ambaye anajua kumjali mwenza wake na kumtendea kama yeye anavyopenda atendewe ndiyo msingi wa mwanamume halisi.

Ni bahati mbaya kwamba hali ya unyanyasaji wa kijinsia hapa nchini kwetu inatisha, ndiyo sababu ipo haja ya kutumia kikamilifu siku hizi za harakati, ili kuhakikisha kuweza kunaanzia katika kujishawishi kila mtu aanze kuwekeza katika kubadili tabia na mtazamo, atambue kwamba tunapozungumzia haki za wanawake, tunazungumzia haki za mama zetu, dada zetu na mabinti zetu wenyewe. Ni mwendawazimu tu anayeweza kukubali kuona mama yake, dada yake au binti yake ananyanyaswa eti tu kwa sababu ni mwanamke.

Hatuna cha kujivunia sana linapokuja suala la haki za kijinsia katika taifa letu. Katika utafiti uliofanywa mwaka 2004/5 na Idara ya Takwimu nchini, umeonesha kwamba wanawake watatu katika ya watatno hupigwa na waume zao kwa sababu za kujibishana, kuondoka bila kuaga au kukataa kufanya tendo la ndoa.

Wanawake 46 katika ya 100 wanakubali kwamba mwanaume ana haki ya kumpiga mke iwapo atajibishana naye, 47 kati ya 100 wanakubali kwamba mume ana haki ya kumpiga mkewe iwapo atazembea kuangalia watoto. 29 wanakubali ni sawa kupigwa na wanaume zao iwapo watakuwa wamekataa kufanya tendo la ndoa.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) kuhusu hali ya ukatili wa wanawake katika mikoa ya Mbeya na Dar es Salaam, takwimu zinaonesha kuwa asilimia 48 ya wanawake waliowahi kuwa na mahusiano wamewahi kufanyiwa ukatili, asilimia 60 ya wanawake waliofanyiwa ukatili hawakutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika.

Wakati asilimia 56 walisema wanaona ukatili kama sehemu yao ya maisha na asilimia 30 hawakumweleza mtu yeyote juu ya ukatili wanaotendewa. Takwimu hizi si kitu kizuri hata kidogo. Kinaonesha ni kwa kiasi gani tafsiri yetu ya Tanzania kuwa kisiwa cha amani haina mantiki wala maana.

Kwa sababu huwezi ukawa na amani wakati ambapo sehemu ya jamii yako hufanyiwa ukatili, hunyanyaswa na kuteswa ni sehemu yao ya maisha. Ipo haja ya kubadilika na kuamua kwa dhati kila mmoja kwa nafsi yake kuapa kutofanya ukatili na kutovumilia ukatili pale unapoona unafanyika.

Shirika la kutetea haki za wanawake la jijini Mwanza la Kivulini, pamoja na wadau wengine katika kampeni ya ‘Tunaweza’, limedhamiria kuwa na waleta mabadiliko milioni moja na laki sita, mpaka kampeni hiyo itakapokamilika.

Kwa msingi kwamba mtu mmoja mmoja anaweza kubadili tabia na mienendo ya watu wengine, kwa kuwapata hao, hawa ndio watakaokuwa nuru ya kuwaangazia wengine hawa watakuwa chumvi ya jamii iliyobaki katika kufanikisha mabadiliko hayo, ni muhimu ukiwa sehemu ya nuru na chumvi hiyo.

Lakini kama jamii iko haja ya kutafari upya mienendo yetu juu ya haki za binadamu, jamii yetu kwa kweli imefika mahali pasipotakiwa. Tumeanza kuwa jamii sugu inayovumilia kila aina ya ubaya miongoni mwetu eti kwa vile tu hautuhusu moja kwa moja.

Lakini tukumbuke kitu kimoja kwamba kila kinachotokea kwenye jamii yetu, taathira yake hatuwezi kuikwepa isipokuja leo itakuja kesho. Na hapo ndipo ule umuhimu wa kupigana na ukatili dhidi ya wanawake na kutovumilia kila aina ya ukatili unaotuhusu wanajamii wote kwa pamoja.

Haya ni mapambano ya wanajamii wote bila kujali rika au jinsia, haki za wanawake ni haki za familia, ni haki za jamii yetu ni haki ya taifa letu, bila kujali sisi ni wa jinsi gani.
Na kwa vile kila mmoja wetu ana nia ya kulifanya taifa letu kuwa sehemu salama na inayostahili kukaliwa na watu wastaarabu na wake kwa amani bila aina yote ya hofu, kutishia amani na utulivu wetu, ni lazima basi amani na utulivu huu uanzie nyumbani.


Kampeni hii inatualika Watanzania tuweze kupinga ukatili dhidi ya wanawake, Baba wa Taifa aliwahi kutuasa katika hekima zake kwamba inawezekana ikiwa tutatimiza wajibu wetu. Katika hili wala hatutahitaji kuhofu inawezekana kabisa kutokomeza aina zote za unyanyasaji wa kijinsia katika jamii yetu, ilimradi tu kila mtu ataamua kutimiza wajibu wake. Ndiyo tunaweza tukiamua kutimiza wajibu wetu.

Mungu ibariki Tanzania.

Makala hii imeandikwa na mwandishi Deus Bugaywa, na ilitoka katika Gazeti la TANZANIA DAIMA, wakati leo tunasherehekea siku ya wanawake leo nimeona sio vibaya kuirejea.

Hii sijaandika mimi jamani, wanaume msije nitoboa macho,..........LOL

Sunday, March 7, 2010

LEO NI SIKU YA KUZALIWA YA DADA FAITH HILARY AKA CANDY 1 WA KIBARAZA CHA MY LITTLE WORLD

Kabinti ketu Faith Hilary

Faith Hilary wa My Little World Blog

Katika viunga vya Jambiani ndani ya Visiwa vya Zanzibari, kunakopatikana zao maarufu la Karafuu ndipo historia ya binti huyu ilipoanzia.

Ikumbukwe kwamba ukanda huo wa Pwani wananchi wake bado wanaenzi tamaduni zao hadi leo hususan lile Tamasha maarufu la Mwakakogwa, tamasha ambalo naweza kulifananisha na lile tamasha maarufu kule Brazil la Samba, ambalo huwakusanya wabrazil katika viunga vya Rio De Janeiro.

Alizaliwa hapo mnamo tarehe 07/03/1991, Visiwani humo na akiwa bado ni binti mdogo wazazi wake walihamia kikazi Jijini Dar Es Salaam huku Tanzania Bara.

Binti huyu aliendelea kukua kwa umri na kimo, na alipofikisha umri wa kwenda shule, wazazi wake walimpeleka shule, akianzia na chekechea hadi alipomaliza kidato cha nne hapa hapa jijini Dar Es Salaam.

Leo hii anaposherehekea siku yake ya kuzaliwa, yuko Ughaibuni akiendelea na masomo yake ya elimu ya juu.

Ni furaha iliyoje kwa binti huyu kusherehekea siku yake hii muhimu ya kuzaliwa huku akiendelea kufukuzia ndoto yake, ambayo hata hivyo siku si nyingi zitatimia.

Pamoja na kukutakia kila la heri katika kusherehekea siku yako hii ya kuzaliwa, pia ninao ujumbe muhimu kwako:

“Dada Candy, ni jambo la kujivunia kuwa na dada mdogo mwema kama wewe. Kila jambo muhimu nililojifunza hapa duniani, kwa kiasi kikubwa lina mchangao wako, mimi na wewe naamini tutakuwa wadada wapendwa maishani, kwani kwa muda tuliofahamiana yapo mengi ya kujivunia ambayo tumejifunza. Namshukuru muumba kwa kunipa dada mdogo mwenye hekima kama wewe. Ningependa siku hii iwe ni kumbukumbu kwetu katika kudumisha undugu wetu wa hiyari”

Happy Birthday mdogo wangu Faith Hilary aka Candy1

Saturday, March 6, 2010

UKOSAPO NENO JEMA, KHERI UJINYAMAZIE.

Nakuasa usikie, usemaji ni karama,
Maneno usirukie, sema mambo kwa kupima,
Utamkapo ujue, neno halirudi nyuma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Kheri ujinyamazie, ovu huleta khasama,
Majuto yasikujia, “Laiti nisingesema”,
Mtu baa azuae, Motowe utamchoma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Ni wengi wajiponzao, kwa zao mbovu kalima,
Heshima waitakao, waseme usemi mwema,
Wale waumbukanao, ni kwa ndimi kuparama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Watazame wakuao, dunia kuwatazama,
Ni wale wapimiao, kabla ya kuyasema,
Na kimya wanyamazao, wakosapo neno jema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Neno huenda likuwe,lizidi hata vilima,
Mambo mawi liyazue, akili zende mrama,
Au mema yatukie, liwapo neno la wema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Funzo walitufunzao, wazungupule wa zama
Zama za kale na leo, walokimcha Karima,
Yawe mema tusemao, tusije zusha zahama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Mola akubarikie, na ambaye akusoma,
Na furaha ututie, uwe ni diwani njema,
Mema utuhadithie, wana kwa watu wazima,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Shairi hili limetungwa na Mshairi maarufu Afrika Mashariki Bwana Amri Abedi, nami nimeona sio vibaya kulirejea ili tujifunze pamoja.................

Wednesday, March 3, 2010

CHOZI LA MWANAMKE! NAOMBA KUTOA HOJA

Bado hamuamini tu?

Hivi karibuni nimeweka makala hapa kibarazani ambayo niliiambatanisha na taswira inayoonyesha wanawake wa vijijini jinsi wananyotekeleza majukumu yao ya kila siku.
Nimepata changamoto kutoka kwa wadau mbalimbali wakionekana kupingana na kile nilichojaribu kukionesha katika makala hiyo.
Imeonekana kama vile hawakubaliani na kile kinachoonekana machoni kwao.
Naomba leo niweke ufafanuzi hapa wa kile nilichomaanisha katika makala yangu.
Wakati mnamo tarehe 08/03/2010 ni siku ya wanawake Duniani ni vyema tukayazungumzia madhila ya wanawake bila ya unafiki wala kuongeza chumvi.

Kuzaa kwa shida:

Hivi ni nani asiyejua madhila wayapatayo wanawake sio tu wa vijijini hata wa mijini. Ni mara ngapi tunaoneshwa picha za wanawake waliojifungua katika Hospiali za mijini wakiwa wamelala wawili wawili kwenye kitanda na wengine wakiwa wamelazwa chini ya sakafu na vichanga vyao, huku vikipigwa na baridi. Huko vijijini napo kuna mengi yanasimuliwa, kuna idadi ya wanawake tena ya kutosha wanaojifungulia majumbani huku wakikosa huduma muhimu za kiafya, achilia mbali wale wanaojifungulia maporini kutokana na umbali mrefu kutoka nyumbani hadi vilipo vituo vya afya.
Sisimulii hadithi za alinacha hapa au hadithi za kufikirika, bali ninachokizungumza nina uhakika nacho na ninakifahamu kwa kuwa muda wangu mwingi nimekuwa nikiutumia vijijini hususana Arusha na Moshi.

Kulea kwa shida:

Hili la kulea kwa shida nalo halihitaji maelezao marefu, kwa kuwa kila kitu kiko wazi, kuna idadi ya kutosha ya wanawake wengi vijijini na hata mijini ambao aidha wametelekezwa na waume zao au wameolewa na wanaume amboa ni nusu wafu, yaani sio wazalishaji na badala yake huwaachia wanawake ndio wawe wazalishaji huku wakibeba majukumu mengine ya kifamilia, hebu tembelea kule feri au kwenye masoko ya mboga mboga kwa hapa jijini Dar, kuna idadi kubwa ya wanawake amboa huacha vitanda vyao aliajiri kuwahi feri kununua samaki au masokoni kununua mbogamboga na kuzichuuza. Huko vijijini napo naamini wengi mtakubaliana na mimi kuwa kuna mfumo dume ambao umetamalaki na wanawake wengi wa vijijini hawajui haki zao za msingi. Wanawake wengi wa vijijini hubeba majukumu ya kulea familia wenyewe huku wanaume wakijipa majukumu haba ambayo hayalingani na yale wanayoyabeba wake zao. Je hili nalo linahitaji ushahidi?

Kutafuta maji umbali wa kilomita kadhaa tena ya kisima:
kama kuna watu wanaotaabika na shida ya maji, basi ni wanawake na sio wa vijijini tu bali pia wa mijini, ukizungumzia shida ya maji, ni sawa na kuzungumzia madhila wayapatayo wanawake, kwa kule vijinini unaweza kukuta mke na mume wanatoka shamba na wakirudi nyumbani wakati mume anajipumzisha kivulini akipunga upepo, mke hakai chini anachukua ndoo ya maji na kwenda kutafuta maji umbali mrefu tu kwa ajili ya kuogea na kupikia. Kwa huku mijini napo, hata kama wote ni wahangaikaji kwa maan ya kutafuta mkate wa kila siku wa familia, lakini wakirudi nyumbani bado jukumu la kuteka maji linaachiwa mwanamke, niliwahi kukaa kwa mama yangu mdogo kwa muda kule kigogo., kama inavyojulikana kuwa kuna shida kubwa ya maji hasa katika maeneo mengi ya uswahilini katika jiji la Dar, nakumbuka siku hiyo tulikuwa umepanga foleni ili kuteka maji, ilikuwa ni folni ndefu ajabu, lakini cha kushangaza kila akija mwanaume na ndoo anapishwa ateke maji na kuondoka, nilipouliza niliambiwa kuwa wanaume hawapaswi kuweka foleni kwa kuwa wao eti ni watafutaji, kwa hyo wanaruhusiwa kuteka maji ili wakatafutie familia zao mkate wa kila siku. Ia walidai kuwa inawezekana mwanaume akawa anauguliwa na mkewe sasa ni vyema apewe nafasi ya kuteka maji ili awahi kumhudumia mgonjwa. Hizo ni busara za wakaazi wa Kigogo, lakini kwangu hilo halikuwa na mantiki, kwamba wanaume ni watafutaji na ndio sababu ya kupewa fursa ya kuteka maji bila ya kupanga foleni! Na wale wanawake ambo nao ndio watafutaji katika familia zao wanatambuliwa na kupewa nafasi hiyo? Je mnaona jinsi mfume dume ulivyotuingia vichwani?

Kutafuta kuni umbali wa kilomita kadhaa:

Kutafuta kuni umbali mrefu, kama ilivyo katika kutafuta maji hili nalo ni shiranga jingine linalowaadhiri wanawake wa vijijini. Wengi tunafahamu ni kiasi gani wanawake wanataabika katika kutafuta kuni umbali mrefu. Hata watoto wa kike kule vijijini wengi hukwama kuendelea na masomo kutokana na kubebeshwa majukumu mengi ya nyumbani ukilinganisha na watoto wa kiume na hili la kutafuta kuni ni moja ya majukumu ambayo watoto wa kike hubebeshwa tofauti na wale wa kiume.

Kilio cha mwanamke wa Kiafrika ni nani akisikie!?:

Niliposema kilio cha mwanamke, nilikuwa naangalia majukumu aliyobebeshwa mwanamke ukilinganisha na wanaume. Lakini pamoja na kubebeshwa majukumu yote hayo bado mwanamke huyu ameendelea kustahimili na kubeba majukumu hayo kwa unyenekevu mkubwa.
Kuna simulizi nyinge zinazohusu madhila wayapaayo wanawake katika vyombo vyetu vya habari kila uchao mpaka zimezoeleka masikioni mwa wanaume na ndio maana inaonekana kama vile wanawake ni walalamishi.
Naamini kuwa ufafanuzi huu utakidhi kile nilichoandika awali ili kuondoa shaka kwa wale ambao hawakuelewa kwamba nilitaka kufikisha ujumbe gani.