Wednesday, March 10, 2010

AKAMWAMBIA MKEWE AMKATE KICHWA!

Karibu mgeni Sungura


Hapo zamani za kale Sungura alijenga urafiki na Jogoo, sasa siku moja Jogoo akamualika Sungura amtembelee nyumbani kwake. Basi sungura akajikusanyia zawadi zake na kumuaga mkewe kisha akaondoka kwenda kumtembelea rafiki yake Jogoo.

Alipofika alikaribishwa kwa bashasha na jogoo, na aliandaliwa chakula kitamu na wenyeji wake, baada ya kula Jogoo alimtoa mgeni wake huyo na kumtembeza sehemu mbali mbali ili kumuonesha fahari ya mji wao, Sungura alipendezwa sana na ziara hiyo.

Ilipofika jioni walirudi nyumbani wakamkuta mke wa Jogoo kawaandalia chakula cha jioni, baada ya kula Sungura alioneshwa mahali pa kulala, kisha jogoo na mkewe nao wakaingia chumbani kwao kulala. Lakini kabla sungura hajapitiwa na usingizi akasikia mazungumzo ya jogoo na mkewe huko chumbani kwao, na mazungumzo yenyewe yalikuwa ni haya.

Jogoo: Mke wangu nikate kichwa nataka kulala mie.
Mke wa Jogoo: Sawa mume wangu,

Sungura kusikia hivyo akataharuki, “He kumbe Jogoo kulala ni mpaka akatwe kichwa?
Ilipofika alfajiri akamsikia Jogoo akimuamsha mkewe tena.

Jogoo: Mke wangu, eh, hebu nirudishie kichwa changu nataka wika mie kuwaamsha watu.
Mke wa Jogoo: Haya mume wangu ngoja nikurudishia kichwa chako. watu.

Baada ya kurudishiwa kichwa chake, jogoo akaanza kuwika kama kawaida yake, ili kuwaamsha watu…Koko rikooooo ………Kucha kucheleeeeeeee………

Basi kulipopambazuka sungura akaamka na kupata staftahi iliyoandaliwa na wenyeji zake na baada ya stafutahi akapewa zawadi za kwenda nazo nyumbani kwake, lakini kabla ya kuondoka aliamualika Jogoo naye amtembelee ili kulipa fadhila kwani alipanga kumfanyia jogoo mapokezi makubwa kushinda yale aliyoyapata.

Sunguara alipofika nyumbani kwake alimsimulia mkewe juu ya safari yake na mapokezi aliyoyapata, pia hakusahau kumweleza mkewe mshangao alioupata kuhusiana na ule utaratibu wa Jogoo kukatwa kichwa na mkewe kabla ya kulala na kurudishiwa kichwa chake alfajiri ili awike.

Sungura alimtaka taka mkewe na yeye afanye hivyo siku wakitembelewa na Jogoo, kwa kuwa amemwalika aje kuwatembelea, alimtaka mkewe amkate kichwa akitaka kulala, na kukirudishia alfajiri ili amwonyeshe jogoo kuwa na yeye anaweza kukatwa kichwa na kurejeshewa asubuhi.

Ni kweli baada ya juma moja kupita Jogoo akamtembelea Sungura, na yeye alibeba zawadi kemkem kwa ajili ya wenyeji wake.

Alipofika alipokelewa na wenyeji wake ka bashasha, na kuonyeshwa ukarimu wa hali ya juu.

Kama alivyofanyiwa kule na Jogoo, na yeye Sungura alimtembeza mwenyeji wake kumuonesha mji na maeneo ya vivutio vya mji wao.

Walirejea jioni na kupata mlo wa usiku, huku wakipiga soga. Ulipofika muda wa kulala, sungura alimuonesha jogoo mahali pa kulala, na yeye na mkewe wakaingia chumbani kwao kulala.

Mara Sungura akamwambia mkewe.

Sungura: Mke wangu eh, hebu nikate kichwa mie nilale..
Mke wa Sungura: Sawa mume wangu.
Mke wa Sungura akachukua kisu na kumkata mumewe kichwa, na kukitenganisha na kiwiliwili.

Asubuhi kulipopambazuka akaanza kumuamsha mumewe,a lakini hakuamka alijitahidi kukiunganisha kichwa ili mumewe aamke lakini hakikuunga na wala Sungura hakuamka, alikuwa amekufa tayari.

Mke wa Sungura ikabidi aombe msaada kwa Jogoo, lakini Jogoo alipofika chumbani aliona damu zimetapakaa kila mahali na kichwa cha Sungura kilikuwa kimetenganishwa na kiwiliwili.
Jogoo kuona hivyo, akataharuki, lahaulaaaa…kulikoni huyu hana kichwa, aliauliza Jogoo.
Mke wa Sungura akamsimulia Jogoo kuwa utaratibu wa kukatwa kichwa kabla ya kulala aliupata kutoka kwake alipowatembelea.

Ndipo Jogoo akamwelewesha kuwa yeye huwa hakatwi kichwa na mkewe kama vle alivyofanya Sungura bali mkewe humsaidia kuficha kichwa cheke kwenye mbawa zake kila akitaka kulala na alfajiri mkewe humsaidia kutoa kichwa chake kutoka kwenye mbawa ili aweze kuwika kuwaamsha watu.

Mke wa Sungura liaposikia hivyo akaanza kulia kwa uchungu kwa kuondokewa na mumewe.

Jogoo aliporudi kwa mkewe alimsimulia masaibu yaliyomkuta Sungura.

Hadithi hii nilisimuliwa na bibi yangu Koero, siku nyingi kidogo, wakati nilipokwenda kijijini likizo. Nimeikumbuka leo nikaona si vibaya nikiiweka hapa ili tutafakari pamoja.

Je hadithi hii inatufundisha nini? Tafakari………………………

5 comments:

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Hadithi tamu hiyo!

Lakini kuna mafunzo gani tunayoyapata hapo? Najua wengine wanaweza kusema oooh ujinga wa baba na mama sungura!

lakini hata kama ni ujinga, ni mara ngapi huwa twawa wajinga katika maisha yetu ya kila siku?

Koero, umekuwa ukiandika juu ya unabii wako kwa uchaguzi ujao....

Je ni mara ngapi tumekuwa tukiwalalamikia wanasiasa bila siye kuchukua hatua?

Je ndo muda wa kukatwa kichwa umiwadia? Mh!

Ngoja nkavue samaki kwanza, ntarudi....lol

Anonymous said...

Nami nilihadithiwa hadithi hii, hivi hivi. Doh, umenikumbusha enzi za utoto.
Hadithi hii inanifundisha, 'usiamini kila unaloambiwa ama kusikia NA tujifunze kutafakari na kuchambua habari ili kuijua undani wake'.

Yasinta Ngonyani said...

Ni hadithi nzuri na ya kufunza kweli. Mimi imenifundisha si vizuri kuiga jambo usilolijua na usilokuwa na uhakika.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

kichwa kipi?? kuna vichwa vingine ni vyekundu hasa cha jogoo

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___