Tuesday, March 16, 2010

DAR ES SALAAM: WANAUME NA SUPU YA PWEZA!

Huyu binti naye alikuwa akijipatia pweza

Nimerejea Dar, na kama kawaida, juzi nilitoka kwenda kumtembelea rafiki yangu mmoja anayeishi maeneo ya Msasani. Eneo la Msasani ni eneo ambalo sijui nisemeje, lakini ni eneo ambalo linaishi watu wenye vipato tofauti tofauti, kuanzia wale wenye vipato vikubwa na wale wenye hali duni kabisa na maisha yanasonga mbele kama kawaida.

Hiyo ni tofauti na kwa wenzetu kule nchini Kenya ambapo sio rahisi sehemu za uswahilini kama vile kule Kibera au Kariobangi kukuta mtu mwenye kipato kikubwa amejichanganya uswahilini na kujenga nyumba yenye hadhi kwani hilo ni jambo ambalo haliwezekani, na huenda mhusika akaonja joto ya jiwe kwa kufanyiwa mchezo mchafu, hata kabla ya ujenzi.

Nilifika kwa rafiki yangu majira ya saa kumi jioni, kwani anaishi eneo ambalo lina pilikapilika nyingi sana. Nilipofika nilimkuta amekaa kibarazani kwao akijisiomea novel zake. Alinikaribisha kwa bashasha na tukaanza kukumbushana stori zetu za zamani na vituko tulivyokuwa tukivifanya enzi zetu za shule.

Mnajua maisha ya shule huwa yana mambo mengi ya kukumbukwa maana ndipo mahali ambapo kuna kila aina ya ujinga, na werevu kidogo. Wakati tukiendelea kupiga soga, nilishangaa kuona kundi la wanaume wakiwemo wazee na vijana wakiwa wameizunguka meza upande wa pili wa barabara huku kila mmoja akiwa na kibakuli chake. Kulikuwa na vitu Fulani wanaokota juu ya meza na vijiti yaani tooth picks na kula huku wakiteremshia na kinywaji kilichopo ndani ya vibakuli vyao.

Nilijishikwa na udadisi, ikabidi nimuulize shoga yangu, kuwa ni kitu gani kinaendelea pale, shoga yangu linijuza kuwa mahali pale ni maarufu kwa uuzwaji wa supu ya pweza. Shoga yangu hakuishia hapo aliendelea kubainisha kuwa supu ya pweza imeibuka na kuwa maarufu siku za hivi karibuni hususana kwa vijana kwa kuwa inasemekana kuwa inaongeza nguvu za kiume.

Kwangu mimi hiyo ilikuwa ni habari mpya, nafahamu kuwa hapa jijini hasa maeneo ya Kariokoo ni kawaida kukuta vijana wakiwa wamebeba masinia yakiwa yamesheheni vipande vya pweza, ngisi na chachandu, wakitembeza mtaani, lakini hili la supu ya pweza sikulifahamu.

Nilimuuliza shoga yangu kama ninaweza kwenda mahali pale ili kupata habari zaidi, shoga yangu huyu kwa bahati nzuri anajua kuwa mimi ni mwanablog, na hakusita kunitania, “He Koero nawe, najua hapo ushapata umbeya wa kuweka bloguni kwako, maana uliadimika kweli”
“Habari ndiyo hiyo shoga yangu hivi hapa nimeshapata udaku, maana najua wasomaji wangu wamemiss kweli longo longo zangu” nilimjibu.

Tulivuka barabara na kufika mahali pale, “Shifeya, tunaona umetuletea mgeni hapa, karibu dada” alitudaka yule kaka muuzaji wa supu. Tulilipofika pale tulikuta anazo chupa za chai kubwa maarufu kama thermos chini ya meza yake, ambazo nilijulishwa na mwenyeji wangu kuwa ndizo anazotumia kuhifadhia supu hiyo ya pweza.

Wale vijana na baadhi ya wazee tuliowakuta pale walionekana kufurahiya uwepo wetu pale na nilikaribishwa nijipatie vipande vya pweza na supu. Niliwashukuru kwa ukarimu wao na kuwaambia kuwa kwa bahati mbaya situmii pweza kwa kuwa nina mzio {Allergy} nao. Lakini ukweli ni kwamba sisi wasabato haturuhusiwi kula aina hiyo ya samaki.

Kama kawaida nilifanya udadisi wangu, kwa yule kijana muzaji wa supu, kutaka kujua sababu ya wanaume kuipenda sana supu ya pweza, “Unajua dada, supu ya pweza inafaida nyingi sana, kwanza ni kiburudisho, pili inaondoa uchovu, inachangamsha na pia…….si unajua yale mambo yetu yaleeee,”
“Mambo gani sasa, mbona hamalizii” nilifanya udadisi,
“Weweee sasa unamficha nini kwani ni mtoto mdogo huyo?” alidakia kijana mwingine pembeni aliyekuwa na bakuli lake la supu. “Unajua sister supu ya pweza, pamoja na hizo faida alizokueleza, lakini faida kubwa kabisa ni kwamba inaongeza nguvu za kiume, yaani kama mwanaume anapata supu hii ya pweza halafu akutane na mwanamke, weee inakuwa ni shughuli pevu.” Watu waliokuwa pale wote waliangua vicheko.

“Mweleze huyo akamjulishe shemeji, maana kama hayajua mambo haya, basi akiyajua itakuwa kazi kweli kweli”
“Tokeni zenu kule kwanza ninyi watu wa bara ndio mliosababisha mpaka pweza wamepanda bei siku hizi, kwani zamani pweza hakuwa ghali kiasi hiki lakini tangu mufahamu kuwa inafaa kwa majamboz, imekuwa taabu mpaka wamepanda bei” alisema mzee mmoja.

Mara akadakia kijana mwingine, “Huo sasa ni uongo, pweza wamepanda bei kutokana na kuenea kwa mahoteli na mighahawa ya kitalii hapa jijini, na ndio maana wakapanda bei”
Basi yalizuka malumbano mapaka nikashindwa nimsikilize nani na nimuache nani. Nilitoa ofa ya kuwanunulia chupa nzima ya chai iliyojaa supu ya pweza na kujiondokea zangu.

Hata hivyo kupitia malumbano yao nilikuja kufahamu kuwa mpaka miaka ya tisini pweza hawakuwa maarufu kiasi hiki na hata supu ya pweza haikuwa maarufu sana, lakini kutokana na hiyo sifa ya kuongeza nguvu za kiume, imetokea kuwa maarufu miaka ya 2000 na kuwafanya pweza kuwa ghali.

Yule kijana muuuza pweza alinijuza kuwa inamlazimu kwenda hadi Bagamoyo kuwafuatilia pweza kule, kwani hapa Ferry jijini Dar Pweza wamekuwa ni ghali mno kutokana na kupata umaarufu na pia kutokana na watu wa mahoteli na mighahawa ya kitalii kuwanunua kwa bei ya ghali.

Kule Bgamoyo napo hawakuwa ghali sana, lakini siku za karibuni wamekuwa ghali sana kutokana na wafanyabiashara wengi wa supu ya pweza jijini Dar kukimbilia kule kuwatafuta.
Kuna wakati niliwahi kudesa habari fulani kutoka kwenye kibaraza cha dada Yasinta, inayozungumzia wanaume kutumia dawa ya kuongeza nguvu za kiume maarufu kama Mkuyati, unaweza kubofua hapa ili kujikumbusha. Nakumbuka baadhi wasomaji walionekana kupingana na kile alichandika dada Yasinta. Sasa Je na hili la supu ya pweza watabisha?

Kama yupo mwenye changamoto juu ya mada hii anakaribishwa kwani mimi ni msimuliwaji tu.

11 comments:

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Da Koero, mie sina changamoto ila nadhani hiyo ni coping mechnisms ya wababa wa mujini japo sina hakika kama musoma twatumia nini....lol


lakini pia yawezekana kabisa inaletelezwa na watu waume kwa wake juu ya simulizi ya shughuli kunako kitandani na wanadhani hiyo maneno inafanywa kwa kukomoana badala ya starehe na kushiriki katika kazi ya UUMBAJI.
Utaumbaje kwa fujo na kumkamia mwenzio? si utazaa zezeta ama kichaaa?....lol

Utakuta mdada ama mama anamsimulia shogake kuwa kapata anayemfikisha na kuwa anaweza kumpiga bao 5-8 non-stop na mwenzie anadhania wake kwa kuwa wake kule nyumbani japo anamfikisha kwa bao moja tu basi ana kasoro.

na wakaka/wababa wengine wanadhani kufanya hivo kama hao wanavosimulia ni sifa :-(

Ramson said...

Chacha, inawezekana pia kuna ukweli kuwa kuna tatizo la wanauem kupungukiwa nguvu za kiume na ndio sababu ya kupanda chati kwa madawa ya kuongeza nguvu za kiume na hiyo supu ya pweza.

Sababu zinazotajwa na wataalamu kuchangiaupungufu wa nguvu za kiume ni matumizi ya dawa za hospitalini kwa muda mrefu ambapo watanzania wengi kutokana na ufahamu mdogo hujinunulia dawa over the counter bila kupata ushauri wa kitabibu, utakuta watu wNshauriana tu huko kwenye mabaa au maofisini na kisha mtu ananunua dawa na kuitumia bila kujua athari zake.

Kingine ni kufanuya mapenzi sana kama dozi asubuhi mchana na jioni, hilo nalo ni tatizo jingine, wanaume wengi hupenda kufanya mapenzi sana bila kujali afya zaowakti hicho ni chanzo kizuri sana cha ufungufu wa nguvu za kiume, lakini aaaa....hawana staha nalo...

Kuna sababu nyingi zinazotajwa kuchangia upungufu wa nguvu za kiume........

SIMON KITURURU said...

Kwangu hii supu ya PWEZA sijaifanyia utafiti bado kwa kuwa bado sijahitaji msaada zaidi ya MIND CONTROL katika kuamrisha mgambo asimamie shughuli.


LAKINI KIKUBWA kuna mambo mengine katika hili swala yanahitaji tu IMANI na ukiamini kirahisi yatengenezacho ni Placebo Effect tu.

PLACEBO EFFECT....nikiwa na maana KWA KUTUMIA MFANO MWINGINE ,...
....kuna WATU wakiumwa hata KICHWA na kupewa choki na WAMUAMINIYE ANAJUA MATIBABU wataamini hiyo CHOKI ni dawa ya kichwa,na basi kujisikia wamepata unafuu wa maumivu ya kichwa na hata kupona .

Na kunatafiti zidaizo asilimia kubwa ya HATA watumiao VIAGRA ,wengi kiwapacho msukumo WA SHUGHULI wakimeza kidonge ni KUJIAMINI KWAO BINAFSI kuwa watakabili mirindimo ya kukita ngoma na wala sio VIAGRA KIDONGE ndio iwasababishiayo uwezo wao EXTRA katika raundi EXTRA za kunesea shughuli. Kwa hiyo hata ukiwapa tu kakidonge kokote na kukasingizia ni VIAGRA kuna ambao watazidisha ujuzi wa maringo na RAUNDI kadhaa EXTRA katika kuinesea kwa ufundi shughuli.

Yasinta Ngonyani said...

mmmmmhhhh!! Mkuyati, Supu ya pweza, viagra nk, nk. Hii yote ni imani tu kama alivyosema Mt. Simon. Supu ya pweza kuongeza nguvu? Je humu kwenye supu kuna kitu kinawekwa zaidi ya huyo pweze au? Na kwa nini iwe supu sio kula tu pweza mwenyeww.

Sijui hii hali ya kukosa nguvu nadhani mwanaume wanaelewa zaidi.

Candy1 said...

Ok mimi sio mwanaume lakini mmh! This is so suspicious! Na tunaokaa nchi hizi basi sometimes huamini kitu mpaka upate "proof" (don't attack me, I am just saying).

Nilishawahi kusikia hiyo supu ya pweza (and to me I thought it was disgusting...since I don't eat it either) lakini sijapata kuiona...Je kuna uhakika upi kwamba kweli zinaongeza hizo nguvu. Na imekuwaje wanaume wako soooooo "insecure" about their abilities of pleasing a woman on bed mpaka wanatafuta KILA NJIA au kuvumbua vitu mbalimbali just for that?

Mie sielewi...I thought men were suppose to be better than that...again...I am JUST saying :-)

Godwin Habib Meghji said...

Kwanza kabisa nakubaliana na ST. Simon. Inawezekana hiyo supu inasaidia kwa msukumo wa fikra. Najua kabisa imani inaponya.

NIMEGUNDUA WATU WENGI WANAPENDA KUANGALIA TATIZO KWA UPANDE MMOJA. KWANINI WATU WANAFIKIRIA KUWA WANAUME NDIO WANA HAYO MATATIZO YA UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME? KUNA MTU ALISHAWAHI KUJIULIZA LABDA WANAWAKE WA SIKU HIZI WAMEKUWA WANAPENDA ZAIDI NGONO AU WANACHELEWA ZAIDI KUFIKA KILELENI AMA VYOTE VIWILI. hayo ni mawazo yangu tu. hayana utafiti wowote.

Sina uhakika kama kufanya ngono mara nyingi inapunguza nguvu za kiume. NINAVYOJUA MIMI NA SAYANSI NDOGO NILIYOSOMA, "MASOZI" YEYOTE INAPOTUMIKA ZAIDI KATIKA MWILI WA BINADAMU NDIO INAIMARIKA ZAIDI. Labda inawezakana Nadharia hiyo ikawa haitumiki kwa kila kiungo cha mwili

INGAWAJE SINA USHAIDI WA MOJA KWA MOJA, ILA USHAIDI WA KIMAZINGIRA UNAONYESHA ZAMANI WANAUME WALIKUWA WANAFANYA NGONO MARA NYINGI ZAIDI KULIKO SASA. tuliona zamani mtu ana wake zaidi ya mmoja na vimada kibao, Hili linaweza kuonekana kwa kuangalia zamani mwanaume mmoja anaweza kuwa na watoto wengi kwa wanawake zaidi ya mmoja. NINACHOTAKA KUSEMA NI KWAMBA, INGEKUWA SWALA LA KUFANYA NGONO MARA NYINGI LINAPUNGUZA NGUVU ZA KIUME, BASI WATU WA ZAMANI NDIO WANGEKUWA NA TATIZO KUBWA ZAIDI.

Inawezekana ugonjwa wa ukimwi pia umechangia kwa kiasi kikubwa kupoteza hamu za watu kufanya ngono. HILI NINASISITIZA KWA SABABU NINA UHAKIKA NALO KWA EXPERIENCE YANGU MWENYEWE SIJAWAHI KUWA FREE NA KUENJOY KUFANYA NGONO HATA KWA KUTUMIA ZANA, NINAPOFIKIRIA SWALA LA UKIMWI

Bennet said...

Ni kweli suala hili liko kisaikolojia zaidi, lakini kuna ukweli kwenye supu ya pweza kama unaupngufu wa nguvu za kiume lakini haitumiki peke yake kuna vyakula vingine navyo unatakiwa kula anayetaka kujua anitafute kuna jamaa yangu alitumia na ikamsaidia
Kwenye suala la kwanini supu na sio pweza mwenyewe ni kwamba pweza akikaangwa baadhi ya viinilishe hupungua, lakini supu huwa navyo zaidi kwa sababu huchemshwa kwanza akiwa mbichi ndio anakangwa baadae

mumyhery said...

Koero ukatoa ofa ya chupa moja ya supu ya pweza!!!

Masangu Matondo Nzuzullima said...

http://matondo.blogspot.com/2010/03/utafiti-upungufu-wa-nguvu-za-kiume.html

Joa Kim said...

ahsanteeee hii nimeipenda sana.... so informative and argumentive comments... ila pweza ni nouma aiseee

poker said...

PROMO DELIMA
poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
Livechat_____: delimapoker
BBM__________: 7B960959
Facebook_____: delimapoker
Phone number_: +85595678845
pendaftaran___