Monday, June 7, 2010

ETI MKUKUTA NI DAWA YA TUMBO NA UKIMWI!

Bado watu ni mbumbumbu kabisa!

Kwanza naomba radhi kwa kutoonekana mtandaoni kwa takribani wiki mbili sasa. Najua wale kondoo wangu waliozoea kupata neno kila Jumamosi watakuwa wamesononeka kutokana na mchungaji wao kutoweka neno la wiki juzi Jumamosi kama ilivyo ada.

Niko Arusha kwa sasa nikiendelea na juhudi za kifamilia za Kilimo Kwanza nikiwa nimejikita zaidi katika maeneo ya Karatu, kuliko na mashamba ya Mzee Mkundi.

Leo niko hapa Arusha mjini, nikiwa nimeamua kujipumzisha na kabla ya kurejea Karatu kesho kuendelea na shughuli za kilimo.

Ukweli ni kwamba sikupanga kublog kabisa, lakini nimelazimika kublog, baada ya kuangalia kipindi cha Uswazi kinachorushwa na TV ya East Africa yaani Channel 5.

Kilichonisukuma zaidi ni kutaka kujadili kile nilichokiona na kukisikia katika kupindi hicho ambacho kwa kweli kimeniacha mdomo wazi hadi hivi sasa.

Mtangazaji wa kipindi hicho Bwana Musa alikuwa akiwahoji vijana fulani katika maeneo ya Kinondoni ambao walikuwa kwenye maskani yao maarufu kama Camp.

Katika mahojiano hayo Musa aliwauliza vijana wale kama wanaelewa nini juu ya neno MKUKUTA.

Hapo ndipo nilipobaki hoi kutokana na majibu yaliyotoka kwa vijana wale.

Kijana wa kwanza alidai kuwa MKUKUTA ni mpango wa Elimu ya watu wazima, Musa alimuuliza maswali kadhaa kijana yule lakini alionekana kutokuwa na uhakika na majibu yake.

Kijana wa pili yeye alikuja na jibu kama la kijana aliyemtangulia lakini alikuwa na hadithi ndeeefu akijaribu kujenga hoja ya kutetea jibu lake kuwa MKUKUTA ni mpango wa Elimu ya watu wazima.

Aliyeniacha hoi kabisa kiasi cha kutamani kuzima TV ni kijana aliyejitambulisha kuwa anatokea kule Tabora ambaye alikuja hapa mjini mnamo mwaka 2005. Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la King’walu alidai kuwa MKUKUTA ni dawa ya kienyeji ya kutibu tumbo.

Alipoulizwa na mtangazaji wa kipindi hicho kuwa aliambiwa na nani kuwa MKUKUTA ni dawa ya kutibu tumbo, alijibu kuwa kuna wakati aliwahi kuumwa na tumba na ndipo alipoletewa dawa hiyo na baba yake mdogo ambapo ilimtibu ugonjwa huo wa tumbo.

Awali nilidhani anafanya masihara, lakini kwa jinsi alivyokuwa kiulizwa ndiyo alizidi kunitia kichefuchefu.

Kwa mujibu wa maelezo yake alidai kuwa dawa hiyo inapatikana hapa mjini na hata huko Tabora na Shinyanga. Alizidi kubainisha kuwa dawa hiyo ni ya mizizi na inachemshwa na kisha kunywewa na mgonjwa wa tumbo.

Kijana huyo alizidi kupiga taralila zake kwa kudai kuwa dawa hiyo ya MKUKUTA pia inatibu UKIMWI na ugonjwa wa macho ambao umesambaa hapa nchini siku za hivi karibuni.

Bila shaka wewe unayesoma hapa unaweza kudhani kuwa napiga porojo lakini iwapo kama yupo mtu ambaye alikiona kipindi hicho cha uswazi usiku wa jana na ambacho kimerudiwa mchana wa leo atakubaliana na mimi.

Hata hivyo wapo vijana wawili ambao walijitahidi kujibu swali hilo. Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Dismas alijibu kwa kifupi tu kuwa ni mpango wa kuondoa umasikini na mwenzie aliyejitambulisha kwa jina la Mkude alijibu kuwa ni Mkakati wa Kupunguza Umasikini Tanzania yaani kwa kifupi ni MKUKUTA.

Kijana huyo alikiri kuwa hana maelezo ya ziada zaidi ya hivyo alivyojibu kutokana na uelewa wake baada ya kusikia maana ya neno hilo kupitia Redio, Magazeti na TV.

Kusema ukweli tunapoelekea ni pabaya mno. Iwapo kizazi hiki tulicho nacho ambacho ndicho tunachokikiita kuwa ni Taifa la kesho lakini kinakuwa na watu ambao hata hawafahamu kinachoendelea hapa nchini ni aibu.

Nasema ni aibu kwa sababu inavyoonekana tunapoelekea huko mbeleni tutakuwa na taifa la wajinga kabisa. Tunao vijana wengi sana huko mitaani ambao hata ukiwauliza leo hii waziri mkuu wetu anaitwa nani wanaweza kukujibu kuwa anaitwa Edward Lowasa, na hiyo inatokana na sisi vijana kutopenda kujisomea na hasa kusoma magazeti na vitabu vya maarifa.

Ukikutana na wanafunzi wa siku hizi kama hatakuwa na Gazeti la udaku basi atakuwa na Gazeti la Michezo, na kama ni kuangalia TV basi vipindi wanavyovipenda ni vile vya Miziki ya Bongo Fleva au vya miziki ya Kimagharibi, na Tamthilia za kimapenzi za kimagharibi, lakini Vipindi vya maarifa hawavipendi kabisa.

Leo hii nimepitia Blog ya dada yangu Yasinta, na hapo nikakutana na habari ya Balozi wa Sweden alipoiasa Serikali yetu. Habari hiyo dada Yasinta aliitoa katika Gazeti maarufu la Mwananchi.

Mwandishi wa habari hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Mwandishi wetu, naye alikuwa na yake. Nadhani kaka Mwaipopo aliweza kuonesha hiyo dosari vizuri sana, na kama ungependa kujua alichokosoa kaka mwaipopo, basi unaweza kubofya hapa.

3 comments:

Fadhy Mtanga said...

Mama Mchungaji, usirudie kuondoka bila kuaga. Tunakusamehe kwa mara ya mwisho.

Juu ya MKUKUTA si jambo la mzaha. Hii imeonesha ni namna gani tabaka fulani lilivyoachwa nyuma katika mambo ya msingi kijamii. Pale lawama hazipaswi kuelekezwa kwao. Kuna watu walikula kodi zetu kwa lengo la kuu-advocate Mkukuta lakini hawakufanya hivyo.

Tukija pale kwa da Yasinta na ubovu wa tafsiri zetu katika lugha, ni jambo la kawaida. Waandishi wetu hawa (ndo maana Mkapa anawaponda) wanapaswa kuwa makini zaidi watafsiripo lugha ili kuandika habari.

Hii ni dunia ya mambo na vijimambo mchungaji.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Da Koero, unatiwa kichefuchefu na nini hasa? Yaani mwananchi huyo hajui unasikia kichefuchefu?

Mbona:

Mkapa alipoulizwa huko ughaibuni kwani nini Tanzania ni maskini akajibu hajui mbona hukutapika?

JK alipoulizwa naye kwani nini Tanzania ni maskini akajibu hajui mbona hukutapika?

Sumaye alipotoka Harvard akadai kuwa kwa miaka 10 alotuongoza kama PM hakujua kwa nini tuko masikini na sasa amejua hukutapika baada ya kutolewa tongotongo?

Aaagh! Waonee huruma tu hao kama huwezi kuwaonea huruma viongozi wako wakuu wa Tz! :-(

Anonymous said...

Dada Koero, kwanza naomba nikupongeze (kiukweli) kwa upambanuzi wako yakinifu wa mambo. Sipendi kutoa comment kwenye blog za watu, lakini dada unanipa changamoto. And I respect you.

Anyway nikirudi kwenye mada husika. Naamini hili swala la hawa vijana ni "wake up call" jinsi taifa letu lisivyokuwa na mwelekeo. Dada Koero, hebu nikupe mfano, juzi nilikuwa naongea na profesa mmoja wa UK ambaye amefanya utafiti wa mda mrefu sana hapa Tanzania. Aliniuliza swali...kuhusu Mkukuta kama ni kitu nakielewa. Trust me...anasema kwa research yake (ambayo alinipa) anasema Mkukuta kwa Tanzania ni jinamizi... Watu hawaelewi..zaidi ya wakubwa wa hapo hapo magogoni..and its because of that..Mkukuta haiwezi kuleta mabadiliko yoyote kabisa...now hao vijana wameprove usemi wake.....

Na Arguments za huyu profesa (anafundisha London School of Economics) anasema TZ kwa kifupi hawako serious na wanayoyafanya. akatofautisha Rwanda..ambako alisema kwamba kwa utafiti wao..wananchi wa kawaida wanaujua mpango wa serikali wa kupunguza umasikini (MKUKUTA YAO). lONG STORY SHORT, Tz..tunakalia porojo tuu.

To me, unless, sisi kama wananchi tuelewe wajibu wetu..we can hardly complain. Dada Koero, TZ hatuwezi kuendelea kwa mtaji huu. Ujanja ujanja hautufai. Hivi uliza marafiki zako..tunalalamika kwamba we are poor, serikali ni incompetent.......but ask...wangapi....watapiga kura? Infact wanafunzi (wasomi wetu wa kutegemewa) ndo wanaandamana kuisupport CCM na Kikwete..

By the way..sipingi haki yao ya kuissuport CCM, lakini naamini..hawa wasomi ndo wangekuwa mstari wa mbele kuuliza "maswali magumu"...serikali imefanya nini...

To me its so painful....and yet..we are everyday complaining!

Dada Koero, ukiandika makala kwenye gazeti..tafadhali niambie..nichangie..labda tuanze kuandika magazetini....

Masanja