Akasema, 'Sihitaji kura zenu'
Kama kuna chama ambacho unaweza kukiita chama cha watu wenye kujua kuchezea watu shere basi chama hicho ni CCM. Tena siyo haba shere zao. Na hapo ndipo ninapojiuliza kuwa, nini hatima ya nchi hii baada ya uchaguzi mkuu ujao?
Nakumbuka wakati ule wa kilele cha ugomvi wa serikali na Chama cha Wafanyakazi, TUCTA juu ya maslahi ya watumishi wa umma, Mheshimiwa Raisi kwa maneno yake mwenyewe akiongea na wazee wa jijini Dar es salaam alitamka dhahiri bila kumung’unya maneno kuwa hata (Wafanyakazi) wagome miaka 8 hataongeza chochote kwani serikali haina hizo fedha, na kufanya hivyo ni kusababisha huduma muhimu za kijamii kutotekelezeka.
Mheshmiwa alienda mbali zaidi na kusema kuwa anajua viongozi wa TUCTA wana agenda ya kisiasa kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu lakini hahitaji kura za wafanyakazi. Kwa maneno yake mwenyewe alitamka ‘sihitaji kura zenu’. Kisha akadai kwamba wakiendelea na msimamo wao atawaambia Polisi wawatandike virungu na kusambaratisha mgomo wao.
Lakini leo hii baada ya kuona kuwa wafanyakazi hawakuridhishwa na matamshi yale na washindani wao wakuu CHADEMA wanayatumia kama mtaji wa kisiasa wamezinduka na kuwaongezea wafanyakazi wa umma mishahara kimya kimya.
Halafu kwa sababu walishajua wamechemsha wakawahi kuwatisha viongozi wa TUCTA ili wasitoe msimamo wao kwa niaba ya wafanyakazi, yote hiyo ni katika kuficha aibu.
Je hizi fedha wamezipata wapi?, Je huduma muhimu za kijamii si zitadorora kama walivyosema? Je hii sio rushwa ya wazi wazi kabisa? Haya maswali yanapaswa kufanyiwa tafakuri na wafanyakazi kabla ya kupiga kura, maana wakumbuke msemo usemao ‘bure ya ghali’
Na katika hali ya kushangaza muongoza kitengo cha propaganda wa CCM Bwana Hizza Tambwe, eti anadai kuwa Wananchi hawakumuelewa Mheshimiwa Raisi, hivi aliongea Kikwere, Kimakua, Kibena, Kipare au Kiswahili? Naomba mnidadavulie hapo wenzangu. Haki ya nani hivi jamani!!!
Yaani!!! Hapana jamani hili siyo kabisa!! Aaaah, naomba tuwekane wazi maana inawezekana labda katika mkutano ule na wazee wa jijini Dar es salaam aliongea Kikwere, Kikurya au Kizaramo. Lakini inawezekana Watanzania wote waliosikia ile hotuba siku ile wasimuelewe mheshmiwa kweli? Hivi ni kweli watu milioni karibu 39 wamnukuu mheshimiwa mkuu wa nchi kauli ile, halafu mkuu wa kitengo cha Propaganda anasema wananchi hao milioni 39 hawakumwelewa Rais?
Ndiyo maana nimekumbuka jinsi Jenerali Ulimwengu, katika gazeti la Raia Mwema la jumatano Agosti 11, 2010 akichambua katika safu yake ya RAI YA JENERALI alisema; ‘Msekwa ameajiri Wahuni’. Akitoa mifano ya uundaji wa chama cha mapinduzi CCM mwaka 1977 kuwa mwenendo wa chama hicho sasa ni chama-tawala, hivyo hata wahuni wamepewa ajira ya kuzungumza uhuni kwa kihuni.
Amezungumza kitu muhimu kwamba unaweza usiwe mwanamapinduzi lakini ukajiunga na chama cha mapinduzi. Sasa kwa hali hii ndiyo usemi wake unatimia kwenu wafanyakazi, tayari kitengo kisicho na wanamapinduzi kinasema hamkumwelewa mheshimiwa mkuu wa nchi.
Kwa kweli kila nikumbuka kauli ya mheshimiwa Rais na kauli ya mkuu wa kitengo cha propaganda inanishangaza sana kuona hali hii kipindi hiki. Kwanza Propaganda inayofanyika ni uhuni na inaratibiwa kihuni kwa masuala ya msingi kabisa. Na kama ilivyo Propaganda yenyewe basi kila kitu ni uhuni mtupu. Lakini waungwana hapa najiuliza maswali na kujielekeza kidogo kwenye kiini.
Ama kweli CCM ni mabingwa wa siasa za kimkakati, na mkakati wa kurejea ikulu unajengwa kwa gharama yoyote, na msije kushangaa, damu ikamwagika. Hivi ni nani asiyejua kuwa madaraka ni matamu? Nani asiyejua kuwa ajenda ya kwanza ya chama cha mapinduzi ni kushinda uchaguzi? Hivi kusudio la kitengo cha Propaganda ni lipi jamani?
Naomba kuwatahadharisha wafanyakazi kuwa hii huruma ya serikali dakika za mwisho sio bure wanataka kura zenu, ni vyema mkaanza kusoma alama za nyakati, kwani huruma hii itawahenyesha kwa miaka mitano. Msije mkatarajia kuongezewa mishahara kwa miaka mitano ijayo, itakuwa ni kujidanganya, na itakula kwenu!
Nawakumbusha hili ili mfahamu kuwa gwiji wa michezo ya kuigiza William Shakespeare aliwahi kuandika katika kitabu chake cha Timmons of Athens kwamba ‘Hakuna kinachochochea dhambi kama huruma’. Hiki ndicho ninachowatahadharisha wafanyakazi wa nchi hii.
Kama CCM wanataka kura za wafanyakazi, basi wawe wakweli wa nafsi, japo wahenga walisema kuwa mtu mzima hakosei, lakini kwa hili itabidi wakubali kuwa walikosea na mheshimiwa kama alivyozungumza na wazee pale Diamond Jubilee na kudai kuwa wafanyakazi wana hiyana, akusanye umati ule kwa mara ya pili na kukiri wazi kuwa aliteleza, na aseme ukweli kuwa fedha hizi alizoongeza kinyemela amezipata wapi?
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi hii ni rushwa hata kama watasema suala hili lilikuwa kwenye mchakato. Ina maana waziri Kapuya anatumia muda huu kuhakikisha mkuu wake anarudi kileleni hata kwa kuvunja sheria ya uchaguzi?
Kama ndiyo hali halisi ni kwanini basi iwe sasa na siyo baadaye? Tunakataa rushwa a.k.a mlungula, unaokuja kwa mtindo kama huu. Na hapa wataonesha kwamba ni huruma kwenu kuwaongezea hako kamshahara. Nasema hivi wafanyakazi msitegemee huruma hiyo ni haki yenu hivyo ili haki itimizwe ni lazima maamuzi myachukue kwa tahadhari kabisa hiyo nyongeza, la sivyo, basi na nyie, msikubali kudanyanyika, kwani kama alivyosema mwenyewe, ‘akili ya Mgaya mchanganye na ya kwenu’ basi na mie nawaambia, “huruma hii ya dakika za mwisho si ya bure, ina gharama zake, muwe macho”.
Kama hamuamini, tusubiri ile kauli ya mheshimiwa Rais(endapo atashinda tena) kuwafukuza kazi baadhi ya wafanyakazi. Kwa sasa watakuwa wanyenyekevu sana kwani wanajua bila hiyo hawawezi kuzipata kura zenu. Na mkae mkijua kwamba nchi hii ni yenu na hakuna sababu zozote za msingi kushindwa kusimamia hoja zetu.
Leo nasema hili kwa moyo mweupe kabisa, naamini kila mwenye akili atazingatia ninachosema, kwani nimesema awali kwamba akili zenu changanyeni na za kuambiwa kisha …… jazeni wenyewe. Jamani si kila mshika ngalawa anajua kupalaza mtumbwi, nina maanisha kwamba si kila kauli za huruma sasa zinalenga huruma kwenu wafanyakazi, bali kura zetu na mengine watajaza mbele ya safari.