Saturday, August 28, 2010

TAFAKARI A LEO: BEN CARSON, DAKTARI ALIYETHIDITISHA KUWA HAKUNA MTOTO MPUMBAVU

Dk. Ben Carson akivishwa nishani ya Uhuru na Aliyekuwa Rais wa Marekani G. W. Bush


Mojawapo ya vitabu vyake vilivyojizolea umaarufuMapacha Ladan na Laleh Bijan wa Iran ambao Operesheni yao iliyoongozwa na Ben Carson ya kuwatenganisha haikufanikiwa, walifariki wote wawili


Daktari Benjamin S. Carson (amezaliwa tar. 18 Septemba, 1951) ni daktari na mtaalamu wa Nyurolojia, na pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Nyurolojia kwa watoto katika hospitali ya Johns Hopkins huko nchini Marekani. Alitunukiwa na raisi medali ya uhuru mwaka 2008

HISTORIA YA ELIMU.

Benjamin Solomon Carson alizaliwa katika eneo la Detroit katika jimbo la Michigan. Mama yake, Sonya Carson, aliacha shule akiwa katika daraja la tatu na kuolewa na Robert Solomon Carson, aliyekuwa mchungaji mzee zaidi katika eneo la Tennesee, wakati mama yake Ben akiwa na umri wa miaka kumi na tatu tu.

Wakati Carson akiwa na umri wa miaka nane tu, wazazi wake waliachana. Mama Carson aliachwa kuwalea Benjamin na kaka yake Curtis, yeye mwenyewe. Alifanya kazi katika sehemu mbili au hata tatu kwa mara moja ili aweze kuwatosheleza watoto wake wawili. . Mwanzoni Carson alikuwa na maisha magumu shuleni. , hali iliyopelekea kuwa wa mwisho mara kadhaa katika darasa lake. Alikuwa akiitwa majina mbalimbali kutokana na hali hiyo, hivyo ikapelekea kukua kwa hasira kali ndani yake.


Akiwa amedhanmiria kubadilisha maisha ya mtoto wake, mama yake Carson akazuia muda wake wa kuangalia televisheni na kumzuia kutoka nje kila siku hadi pale atakapokuwa amemaliza kazi zake za shule kila siku. Mama yake Carson alimtaka Kusoma vitabu viwili kutoka maktaba na kuandika taarifa juu ya vitabu hivyo kila wiki, bila kujali elimu yake ndogo, hata hivo hakuweza kusoma vitu ambavyo vilikuwa vimeandikwa.


Lakini mapema, Carson alimshangaza mwalimu wake na wanafunzi wenzake kufuatana na maendeleo yake. Anakumbuka “Ni wakati ule ndipo nilipogundua kuwa sikuwa mpumbavu” anagundua baadae. Carson anaendelea kuwashangaza wanafunzi wenzake na ndani ya mwaka mmoja alikuwa na ujuzi na kuwa katika nafasi ya juu katika darasa lake.


Baada ya kugundua kuwa alitaka kuwa daktari wa magonjwa ya akili, Carson alimaliza shule na matokeo mazuri yenye heshima na hivyo alijunga na chuo kikuu cha Yale ambapo alipata shahada yake ya kwanza katika maswala ya saikolojia ya akili. Pschology. Baada ya kutoka Yale, aliendelea na shule ya udaktari ya michigan, ambapo hapo ndipo nia yake ya kuwa daktari wa magonjwa ya akili ilipobadilika na na kuwa daktari wa mishipa.

Uwezo wake mkubwa wa kuona na uwezo wake wa kufikiri haraka ulimfanya awe daktari wa upasuaji mzuri zaidi Baada ya kumaliza shule yake ya udaktari, alikuwa daktari wa mishipa msaidizi katika hospitali ya Johns Hopkins katika jimbo la Baltimore. Akiwa na umri wa miaka 33, alikuwa profesa wa hospitali na pia mkurugenzi wa idara ya upasuaji mishipa ya watoto.


KAZI ZAKE ZA MAPEMA.


Mwezi wa tisa mwaka 1987, Carson alifanya upasuaji wa kutenganisha mapacha wenye umri wa miezi saba, waliokuwa wameungana katika sehemu ya kichwa. Carson alikuwa ndiye kiongozi wa upasuaji huo mgumu, Mwaka 1997, Carson pamoja na timu yake, walienda Afrika ya Kusini, kuwatenganisha Lukas na Joseph Banda kutoka Zambia. Watoto wote wawili waliweza kuishi baada ya upasuaji na hakuna hata mmoja wao aliyepata uharibifu wa ubongo. Watoto hao wa Banda walikuwa ni watoto wa kwanza walioungana kwa upande wa juu wa vichwa vyao kuweza kuishi baada ya upasuaji. Upasuaji huo ulifanyika kwa saa 28.


Mwaka 2003, Carson alikuwa moja kati ya madaktari waliofanya upasuaji wa watu wazima waliokuwa wameungana katika sehemu ya vichwa, Ladan na Laleh Bijan. Lakini wote hawakuweza kuishi baada ya upasuaji. Alipoulizwa kwa nini alikubali kufanya upasuaji wa kubahatisha kiasi hicho alisema, ndugu hao walikuwa wamekubali bora wafe kuliko kuendelea kuishi wakiwa wameungana.


MAISHA BINAFSI.


Carson amepokea tuzo mbalimbali katika miaka mbalimbali, kama vile, Shahada za heshima za Udaktari 40, pia ni mwanachama katika chama cha American Academy of Achievement, Horatio Alger Association of Distinguished Americans, Alpha Omega Alpha Honor Medical Society Ushirikiano wa yele, (Bodi ya wakurugenzi wa Chuo kikuu cha Yale) na mashirika mengine mengi. Pia ni mwanzilishi na mkurugenzi wa The Carson Scholar Fund, ambayo huwasaidia wanafunzi kutoka katika historia tofauti tofauti walio na vipaji maalumu katika masomo.


Mwaka 2007, Carson alijumuishwa katika Chuo kikuu cha Indiana Wesley, katika Society of World Changes na kupokea nishani ya heshima ya udaktari alipokuwa akiongea katika Chuo hicho. Aliporudi, alirudi na rafiki yake alyeitwa Tony Dungy ambaye naye alikujuishwa katika jamii. Tarehe 19 mwezi wa 9 mwaka 2008, Carson alopokea nishani ya raisi ya uhuru kutoka kwa Raisi George W. Bush


UTAALAMU NA MAGONJWA.


Carson ameandika vitabu vitatu vilivoongoza katika mauzo na vilivyochapishwa na Zondervan shirika la kimataifa la uchapaji la kikristo, Vinavoitwa : Gifted Hands (Mikono Yenye Vipawa: Hadithi Ya Ben Carson) , The Big Picture, na Think Big Kitabu cha kwanza cha Historia ya maisha ya mtu, na vitabu vingine viwili ni kuhusu filosofia ya maisha yake hususani katika mafanikio yake yanayoenda sambamba na imani yake kwa Mungu.Carson ni Mkristu katika dhehebu la sabato.

Mwaka 2002, Carson aliamuriwa kusitisha kuonekana katika maeneo yenye umati wa watu, baada ya kupata matatizo ya kiafya ya kwake mwenyewe. Mwezi wa sita alikutwa na dalili za kuwa na Saratani ya Kibofu cha mkojo, lakini kwa bahati nzuri, saratani hiyo ikiliweza kukutwa katika muda muafaka.

Lakini pamoja na hayo, Carson alibadilisha mfumo wake wa maisha, Bado anafanya upasuaji kwa zaidi ya watoto mia tatu (300) kwa mwaka lakini amekuwa akijaribu kupunguza muda wake.Carson amekuwa akifanya kazi kuanzia saa 7:00 asubuhi na kumaliza saa 8:00 usiku, lakini tangu agundulike kuwa na saratani amekuwa akifanya kazi na kuondoka saa 6:15, jioni. Hii inampa muda zaidi wa kukaa na mke na watoto wake watatu (3).

Makala ya video kuhusu maisha ya Carson inayoitwa Gifted Hands: Kitabu kinachohusu, hadithi ya Ben Carson kilitolewa na Zondervan mwaka 1992, hali iliyopelekea mwaka 2009, filamu ya Televishen iliyotolewa ikiwa na Jina hilo hilo, katika TNT tarehe 07/02/2009, na kushinda tuzo ya Academi ya Gooding jr ikiongozwa na Kimberly Elise akimwelezea mama yake.

Friday, August 27, 2010

JE UMEWAHI KUZITUMIA HIZI?Nimezikuta kwenye mkoba wa Mzee Mkundi

Thursday, August 26, 2010

MLININUKUU VIBAYA!

Sikuwa na maana hiyo, nahitaji sana kura zenu!

Sunday, August 22, 2010

Friday, August 20, 2010

Labda USIMTISHE MTOTO wako!

Kaka Simon wa tatu kushoto......LOL

Kuna kitu WATU wengi hawajui kuhusu MIE Simon KITURURU,...... ila ukweli ni kwamba mkono wangu wa kulia haufanyi kazi vizuri kama inavyotakiwa ,...


... kwa KIFUPI hata UKIWA sio mbali sana siwezi nikakurushia jiwe kama nataka kukubwenga JIWE kirahisi na MKONO WA KULIA.Na tatizo lilianza kisa nilikuwa naficha siri eti kwa kumuogopa BABA.:-(


STORI fupi laini na YA KWELI :Tulikuwa tunaishi SONGEA na moja ya vitu MDINGI alikuwa hapendi ikiwa pamoja na KUWA MCHAFU , kufeli mtihani enzi hizo nikisoma SHULE ya MSINGI MFARANYAKI (kitu ambacho nilikuwa sifeli) ,....


..... nilikatazwa kupanda juu ya MITI aka kuparamia miti kimichezo.Siku moja mie na marafiki zangu tukaenda kuiba maembe aka KUTUNGUA MAEMBE yasiyo yetu shambani kwa WANAFUNZI WA SONGEA GIRLS.


Enzi hizo shamba la songea GIRLS lilikuwa kubwa na sisi tulikuwa tunaingilia upande wa UWANJA WA MEDICAL karibu na nyumba za mwisho mwisho za walimu enzi hizo za miaka ya NAINTINI EITEZ( (Kumbuka ni miaka mingi sijafika Ruvuma sijui maeneo hayo yakoje siku hizi)Basi BWANA katika kuwinda maembe bolibo na embe sindano tukaupata mti ambao mbivu zilikuwa zimenona juu kabisa.


Na mie ambaye hukatazwa kupanda miti nilikuwa kiongozi kuparamia juu kabisa kutikisa mti.Kilichotokea ni kwamba,....... katika kutikisa tawi ili kudondosha maembe tawi likakatika na kilichofuata nilijikuta chini nikijiuliza niko HAI au NIMEKUFA,..........na chaajabu hata marafiki zangu wakinisemesha nilikuwa siamini kama niko hai kwa KUWASIKIA kwa kuwa nilikuwa nahisi kuwa labda hata MFU akisemeshwa huwa anasikia.:-)


Katika kufupisha stori hii ya kweli;... ....nilivyoanguka nilitegua mkono wa kulia na baadaye nikaja stukia labda na kitu kingine mkononi kiliharibika.:-(


KIKUBWA:Kwa kuwa kwanza nilikatazwa kupanda miti na PILI miye na marafiki zangu tulikuwa tunaiba maembe ya wana SONGEA GIRLS nilifikiri sio busara kusimulia hicho kitu nyumbani. NILIFICHA maumivu na ugonjwa kisa NAMUOGOPA BABA....


.....na kwa bahati nzuri ilikuwa ni kipindi cha baridi SONGEA na maswala ya SWETA na JACKETI pamoja na MAIGIZO kuwa NIKO BOMBA yaliniwezesha kuficha nimeumia mpaka mkono ukapona kinamna. TATIZO ni kwamba mkono ulivyopona mpaka leo hauwezi kumlenga MBAYUWAYU bila msaada wa mkono wa kushoto.Kwa kifupi :


Nilijitia udhaifu wa mwili KWA KUFICHA UGONJWA kisa NAOGOPA KUCHAPWA. na BABA:-(Unajua tena AKILI ZA KITOTO).
Stori hii nimeipenda sana na nimeweka hapa ili wasomaji wa kibaraza hiki wapate kujifunza kupitia simulizi hii ya kweli ya kaka yangu Simon Mkodo Kitururu. kwa kumsoma zaidi waweza kubofya hapa

Monday, August 16, 2010

HURUMA HII YA DAKIKA ZA MWISHO SI BURE!

Akasema, 'Sihitaji kura zenu'

Kama kuna chama ambacho unaweza kukiita chama cha watu wenye kujua kuchezea watu shere basi chama hicho ni CCM. Tena siyo haba shere zao. Na hapo ndipo ninapojiuliza kuwa, nini hatima ya nchi hii baada ya uchaguzi mkuu ujao?

Nakumbuka wakati ule wa kilele cha ugomvi wa serikali na Chama cha Wafanyakazi, TUCTA juu ya maslahi ya watumishi wa umma, Mheshimiwa Raisi kwa maneno yake mwenyewe akiongea na wazee wa jijini Dar es salaam alitamka dhahiri bila kumung’unya maneno kuwa hata (Wafanyakazi) wagome miaka 8 hataongeza chochote kwani serikali haina hizo fedha, na kufanya hivyo ni kusababisha huduma muhimu za kijamii kutotekelezeka.

Mheshmiwa alienda mbali zaidi na kusema kuwa anajua viongozi wa TUCTA wana agenda ya kisiasa kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu lakini hahitaji kura za wafanyakazi. Kwa maneno yake mwenyewe alitamka ‘sihitaji kura zenu’. Kisha akadai kwamba wakiendelea na msimamo wao atawaambia Polisi wawatandike virungu na kusambaratisha mgomo wao.

Lakini leo hii baada ya kuona kuwa wafanyakazi hawakuridhishwa na matamshi yale na washindani wao wakuu CHADEMA wanayatumia kama mtaji wa kisiasa wamezinduka na kuwaongezea wafanyakazi wa umma mishahara kimya kimya.

Halafu kwa sababu walishajua wamechemsha wakawahi kuwatisha viongozi wa TUCTA ili wasitoe msimamo wao kwa niaba ya wafanyakazi, yote hiyo ni katika kuficha aibu.

Je hizi fedha wamezipata wapi?, Je huduma muhimu za kijamii si zitadorora kama walivyosema? Je hii sio rushwa ya wazi wazi kabisa? Haya maswali yanapaswa kufanyiwa tafakuri na wafanyakazi kabla ya kupiga kura, maana wakumbuke msemo usemao ‘bure ya ghali’

Na katika hali ya kushangaza muongoza kitengo cha propaganda wa CCM Bwana Hizza Tambwe, eti anadai kuwa Wananchi hawakumuelewa Mheshimiwa Raisi, hivi aliongea Kikwere, Kimakua, Kibena, Kipare au Kiswahili? Naomba mnidadavulie hapo wenzangu. Haki ya nani hivi jamani!!!
Yaani!!! Hapana jamani hili siyo kabisa!! Aaaah, naomba tuwekane wazi maana inawezekana labda katika mkutano ule na wazee wa jijini Dar es salaam aliongea Kikwere, Kikurya au Kizaramo. Lakini inawezekana Watanzania wote waliosikia ile hotuba siku ile wasimuelewe mheshmiwa kweli? Hivi ni kweli watu milioni karibu 39 wamnukuu mheshimiwa mkuu wa nchi kauli ile, halafu mkuu wa kitengo cha Propaganda anasema wananchi hao milioni 39 hawakumwelewa Rais?

Ndiyo maana nimekumbuka jinsi Jenerali Ulimwengu, katika gazeti la Raia Mwema la jumatano Agosti 11, 2010 akichambua katika safu yake ya RAI YA JENERALI alisema; ‘Msekwa ameajiri Wahuni’. Akitoa mifano ya uundaji wa chama cha mapinduzi CCM mwaka 1977 kuwa mwenendo wa chama hicho sasa ni chama-tawala, hivyo hata wahuni wamepewa ajira ya kuzungumza uhuni kwa kihuni.
Amezungumza kitu muhimu kwamba unaweza usiwe mwanamapinduzi lakini ukajiunga na chama cha mapinduzi. Sasa kwa hali hii ndiyo usemi wake unatimia kwenu wafanyakazi, tayari kitengo kisicho na wanamapinduzi kinasema hamkumwelewa mheshimiwa mkuu wa nchi.

Kwa kweli kila nikumbuka kauli ya mheshimiwa Rais na kauli ya mkuu wa kitengo cha propaganda inanishangaza sana kuona hali hii kipindi hiki. Kwanza Propaganda inayofanyika ni uhuni na inaratibiwa kihuni kwa masuala ya msingi kabisa. Na kama ilivyo Propaganda yenyewe basi kila kitu ni uhuni mtupu. Lakini waungwana hapa najiuliza maswali na kujielekeza kidogo kwenye kiini.

Ama kweli CCM ni mabingwa wa siasa za kimkakati, na mkakati wa kurejea ikulu unajengwa kwa gharama yoyote, na msije kushangaa, damu ikamwagika. Hivi ni nani asiyejua kuwa madaraka ni matamu? Nani asiyejua kuwa ajenda ya kwanza ya chama cha mapinduzi ni kushinda uchaguzi? Hivi kusudio la kitengo cha Propaganda ni lipi jamani?

Naomba kuwatahadharisha wafanyakazi kuwa hii huruma ya serikali dakika za mwisho sio bure wanataka kura zenu, ni vyema mkaanza kusoma alama za nyakati, kwani huruma hii itawahenyesha kwa miaka mitano. Msije mkatarajia kuongezewa mishahara kwa miaka mitano ijayo, itakuwa ni kujidanganya, na itakula kwenu!
Nawakumbusha hili ili mfahamu kuwa gwiji wa michezo ya kuigiza William Shakespeare aliwahi kuandika katika kitabu chake cha Timmons of Athens kwamba ‘Hakuna kinachochochea dhambi kama huruma’. Hiki ndicho ninachowatahadharisha wafanyakazi wa nchi hii.
Kama CCM wanataka kura za wafanyakazi, basi wawe wakweli wa nafsi, japo wahenga walisema kuwa mtu mzima hakosei, lakini kwa hili itabidi wakubali kuwa walikosea na mheshimiwa kama alivyozungumza na wazee pale Diamond Jubilee na kudai kuwa wafanyakazi wana hiyana, akusanye umati ule kwa mara ya pili na kukiri wazi kuwa aliteleza, na aseme ukweli kuwa fedha hizi alizoongeza kinyemela amezipata wapi?

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi hii ni rushwa hata kama watasema suala hili lilikuwa kwenye mchakato. Ina maana waziri Kapuya anatumia muda huu kuhakikisha mkuu wake anarudi kileleni hata kwa kuvunja sheria ya uchaguzi?


Kama ndiyo hali halisi ni kwanini basi iwe sasa na siyo baadaye? Tunakataa rushwa a.k.a mlungula, unaokuja kwa mtindo kama huu. Na hapa wataonesha kwamba ni huruma kwenu kuwaongezea hako kamshahara. Nasema hivi wafanyakazi msitegemee huruma hiyo ni haki yenu hivyo ili haki itimizwe ni lazima maamuzi myachukue kwa tahadhari kabisa hiyo nyongeza, la sivyo, basi na nyie, msikubali kudanyanyika, kwani kama alivyosema mwenyewe, ‘akili ya Mgaya mchanganye na ya kwenu’ basi na mie nawaambia, “huruma hii ya dakika za mwisho si ya bure, ina gharama zake, muwe macho”.


Kama hamuamini, tusubiri ile kauli ya mheshimiwa Rais(endapo atashinda tena) kuwafukuza kazi baadhi ya wafanyakazi. Kwa sasa watakuwa wanyenyekevu sana kwani wanajua bila hiyo hawawezi kuzipata kura zenu. Na mkae mkijua kwamba nchi hii ni yenu na hakuna sababu zozote za msingi kushindwa kusimamia hoja zetu.


Leo nasema hili kwa moyo mweupe kabisa, naamini kila mwenye akili atazingatia ninachosema, kwani nimesema awali kwamba akili zenu changanyeni na za kuambiwa kisha …… jazeni wenyewe. Jamani si kila mshika ngalawa anajua kupalaza mtumbwi, nina maanisha kwamba si kila kauli za huruma sasa zinalenga huruma kwenu wafanyakazi, bali kura zetu na mengine watajaza mbele ya safari.

Saturday, August 14, 2010

Friday, August 13, 2010

VISA VYA HUYU KIUMBE MWANAUME!

'Kwenye swala la mapenzi wanaume hawana mzaha'

Katika Gazeti la Mwananchi la hivi karibuni la May 18, 2010, kuna habari iliyoandikwa na mwandishi Anthony Kayanda wa Kigoma ambayo ilinisikitisha sana. Habari yenyewe ni ile iliyohusu mtu mmoja kuuwawa kwa kuchomwa kisu kifuani kwa tuhuma za kutembea na mke wa mtu.Kwa mujibu wa Gazeti hilo, tukio hilo limetokea katika kijiji cha Kitagata kilichopo katika tarafa ya Makere, Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Marehemu ametajwa kuwa ni Ally Bwisigwa ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.Ilidaiwa kwamba Marehemu alikuwa akitembea na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Perusi ambaye aliwahi kuolewa na Hassan Rashid mkazi wa Kasulu Mjini na waliishi pamoja kwa muda mrefu kabla ya mume huyo kufungwa gerezani.Baada ya mumewe kufungwa, Perusi alirudi kijijini kwao huko Kitagata na ndipo alipoanza mahusiano ya kimapenzi na marehemu.


Inadaiwa kuwa baada ya Mume huyo kutoka Gerezani alimuonya mtuhumiwa mara kadhaa kuacha kutembea na mkewe lakini marehemu aliendelea na mchezo wake huo mchafu.Inadaiwa kuwa Hassan alifanya majaribio mawili ya kutaka kumuua marehemu kwanza kwa kutaka kumgonga na pikipiki na tukio la pili lilikuwa ni lile la kumchoma kisu ambapo hata hivyo kisu hicho hakikumpata.
Nimesema kuwa tukio hilo limenisikitisha sana kwa sababu bado nashindwa kuelewa hivi inakuwaje mpaka mtu unapoteza maisha kwa sababu ya mwanamke, tena kibaya zaidi mke wa mtu!Ingawa inasemwa kwamba wanawake ni viumbe wa ajabu lakini naamini wanaume ndio viumbe wa ajabu kupindukia.
Kwa nini ninasema hivyo? Ninasema hivyo kwa sababu, wanawake kwa ujumla wao wanavyo vibweka vyao katika swala zima la mapenzi, lakini ukija kwa wanaume naamini nao wanavyo vibwekwa vyao tena vya hatari ukilinganisha na vile vya wanawake.Kwa mfano, hivi ni mara ngapi tumeshawahi kusikia baadhi ya wanaume wakiamua kujinyonga kwa sababu ya kushindwa kuwashawishi wanawake wanaowapenda?
Namini kuwa matukio ya aina hiyo yapo sana na sio kwa huko nyumbani tu bali pia hata katika nchi zilizoendelea. Linapokuja swala la mapenzi kuna baadhi ya wanaume wanakuwa kama Nyati waliojeruhiwa, na ndio sababu unaweza kukuta baadhi ya wanaume wanajiingiza kwenye vitendo viovu kama vile vya wizi au ujambazi kwa lengo la kuwashawishi wanawake wanaowapenda ili wawakubali. Wakati mwingine hujiingiza kwenye matumizi ya Pombe kupita kiasi au hata matumizi ya Bangi na madawa ya kulevya kutokana na kuachwa na wanawake wanaowapenda.
Tabia hii ya wanaume kuhatarisha maisha au hata kupoteza maisha kama tulivyoona katika tukio hilo la Kigoma ni la tangu enzi za kale. Kuna simulizi nyingi tulikuwa tukisimuliwa enzi za utoto wangu huko nyumbani kwamba kuna wakati wanaume walikuwa wakipigana ili kumgombea mwanamke na shujaa anayeshinda katika ugomvi ndiye anayemchukuwa mwanamke anayegombewa.
Inaonekana wazi kwamba uwezekano wa mwanaume kufa mapema au kuhatarisha maisha yake ni mkubwa ukilinganisha na ule wa wanawake. Na hiyo inatokana na wanaume kupenda sifa na kutaka kuwamiliki wanawake wawapendeo. Kuna matukio mengi ya kusikitisha ambayo huwa tunayasoma katika vyombo vyetu vya habari ambapo matukio kama yale ya mwanaume kumuua mwanaume mwenzie ili kumpata mwanamke ampendae ni vya kawaida kabisa.
Kwa mfano katika tukio hilo la Kigoma, licha na kukoswa koswa kuuwawa mara mbili lakini marehemu hakukoma kutembea na mke wa mwenzie, mpaka akasababisha kupoteza maisha.Hivi kumekuwa na uhaba wa wanawake kiasi cha kupelekea baadhi ya wanaume kuhatarisha maisha yao au kupoteza maisha kutokana na kumgombea huyu kiumbe mwanamke au kuna kitu kingine kinachotafutwa hapo?

Ni aghalabu sana kusikia mwanamke kamuua mume baada ya kumfumania au kumuua mgoni wake tofauti na wanaume. Kama ukipima jambo hilo kitakwimu basi utapata idadi ya wanaume ya kutosha ukilinganisha na ile ya wanawake.
Kimsingi wanaume wamewageuza wanawake kama mali zao wanazozimiliki na hiyo ndio sababu inapotokea kumfumania mkewe au mchumba wake akiwa na mwanaume mwingine mambo mawili yanaweza kutokea, kwanza atamuadhibu mgoni wake au hata kumuua kisha mke naye atasulubiwa au hata kuuawa.
Lakini, pale anapofumaniwa mwanaume mambo huwa ni tofauti sana. Kuna uwezekano mkubwa wa mke huyo kusulubiwa kwa sababu amemfumania mume na wakati mwingine hata huyo mgoni anaweza kushirikiana na mume huyu kumuadhibu huyo mwanamke aliyefumania.Nadhani kuna haja ya wanaume kujikagua upya na kubadili mwenendo wao mzima juu ya matendo yao ili kuepuka kupoteza maisha kwa jambo ambalo wangeweza kuliepuka.

Na: Yasinta Ngonyani. Bofya hapa kumsoma

Wednesday, August 11, 2010

BADO NATAFAKARI!

Bado natafakari cha kuandika

Saturday, August 7, 2010

Sunday, August 1, 2010

UTABIRI WAKE UMETIMIA?

Dada Digna

Alikuja ghafla katika tasnia ya blog kisha akatoweka ghafla, lakini nimefanya upekuzi wangu nimepata taarifa kuwa alikuwa akilea ujauzito na amejifungua binti na amempa jina la Larissa.

Nimemkumbuka dada huyu Digna Abraham kutokana na utabiri wake kutimia, Je ni utabiri gani huo? Usipate tabu msomaji unaweza kubofya hapa kumsoma.

Hongera dada kwa kutuletea kabinti kazuri, tunamuomba mungu akakuze kwa umri na kimo ili nako kaje kawe mwanablog mahiri kama mama yake. Hongera Digna