Wednesday, March 2, 2011

KAKA MARKUS, UMESIKIA WENZETU WAMEWAKATAA BABA ZAO?


Kaka Markus Honorius Mpangala,

Kwanza shikamoo! Habari za siku,

Samahani sana kwa kutowasiliana na wewe kwa muda mrefu sana, kutokana na majukumu ya sasa. Majukumu hayo yananilazimisha mimi na ndugu zangu kuyabeba japo hali zetu kimaisha hazijatengemaa.

Kaka, nakuandikia waraka huu nikiwa natumia kibatari, kwa hiyo naomba usinilaumu kama utaona makosa ya herufi.

Kaka hali zetu ni mbaya sana! Kuna wakati mimi na ndugu zako wengine tunajiuliza ilikuwaje sisi kuzaliwa katika familia hii.

Ngoja nikukumbushe mazuri ya baba yetu mpendwa licha ya kumbukizi nyingine kutia simanzi. Baba yetu wa kutuzaa, ambaye alifariki miaka kumi na moja iliyopita (Mungu amrehemu) alitujengea misingi imara ya malezi na kutunza hazina zetu.

Baba alijaa upendo, aliona mengi na upendo wake kwetu ilibidi atutunzie hayo ili wanawe tunufaike. Kumbuka Baba alitunza mbuga za wanyama, madini, mito mabonde na milima, pia alihakikisha kuwa tunapata elimu bora kwa mustakabali wa maisha yetu na vizazi vyetu vijavyo. Yaani aliwakifikiria hadi wajukuu utadhani aliwaona au kujua watakuwa wangapi! Mweeeee!

Jamani, baba yetu mpendwa, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuona mbali, kupambanua mambo na kutoa ushauri wa busara zilizotuongoza.

Kama ujuavyo katika mila zetu kuna wakati mtu anapoona umri umeenda huwa anaamua kupunguza majukumu yake ya kuongoza familia na kuteua mtoto mmoja mwenye kuonekana ana upeo na kwa kusaidiana na watoto wengine kubeba jukumu la kuongozi familia.

Mtoto huyu anakuwa ndiye kiongozi wa familia karibu kila kitu. Unakumbuka mzee mwenye mji akishachagua mtoto wa kuongoza familia hubaki mshauri. Basi hivyo ndiyo alivyofanya baba yetu.

Aliamua kupumzika na sio kupumzika tu, bali aliamua kurudi kijijini na kujishughulisha na kilimo, kwani aliwaacha baadhi ya vijana wake aliowaamini sana wamsaidie kuongoza familia yake.

Katika kipindi hicho pamoja na kuwa likuwa akiishi kijijini, lakini kaka na dada zetu wakubwa aliowapa jukumu la kuongoza familia walikuwa wakienda mara kwa mara kumuomba ushauri. Hata pale wasipofanya hivyo, akiona jambo limeenda kombo hakusita kulikemea hadharani.

Miaka kadhaa baadaye baba aliugua ghafla, pamoja na juhudi za matibabu ya hapa nchini na hata huko ughaibuni hayakufua dafu, baba alifariki dunia, huo ndio ukawa mwisho wake hapa duniani! Aah! Chozi linanitoka kaka yangu.

Baada ya kifo cha baba, ndugu zetu waliopewa mamlaka ya kuongoza familia yetu wakiongozwa na kiranja mkuu, walitutoa wasiwasi kuwa tusiwe na shaka kwani baba ametuachia misingi imara na familia hivyo haitatetereka.

Tulipewa ahadi kemkem, harara zikatushika kwamba aah! Mambo poa kabisa! Nakwambia tukajifariji, nyoyo zikapoa kwa matumaini ya kiongozi wa familia, maneno yake yalikuwa kama nyama ya ulimi, nasi tukahadaika. Maana tuliahidiwa hali bora za kimaisha, kumbe ilikuwa ghiliba.

Kaka tangu baba afariki, mambo yalibadilika, maadui zetu aliotutahadharisha baba kuwa macho nao tuliwaona wakipigana vikumbo kuja katika familia yetu na kumlaghai kiranja mkuu na ghafla tukaanza kuona wakikabidhiwa hazina zetu waziendesha na nyingine wakiuziwa kabisa.

Tunashuhudia hazina zetu zinavyotafunwa waziwazi, huku sisi wanafamilia tukibaki mikono mitupu, na tukithubutu kuhoji tunaambiwa kuwa tuna wivu wa kike, eti tule nyasi na hatujasoma.

Utaratibu aliotuachia marehemu baba ilikuwa imeamuliwa kuwa kila kiranja aliyeteuliwa kuongoza familia anatakiwa aongoze kwa miaka mitano kisha tunachagua kiranja mwingine na wasaidizi wake.

Yaani ilikuwa kuchagua kwa njia ya kugombea katika makundi, (baba aliruhusu katika familia kuwa na makundi mbalimbali na kila kundi lilitoa mwongozo wake kwa wanafamilia wa jinsi watakavyoongoza wakipewa ridhaa na wanafamilia)

Kutokana na utaratibu huo, tumejikuta tunayo makundi kadhaa lakini yenye nguvu ni mawili tu ambayo yalikuwa yamepania hasa mwaka uliopita kumuondoa kiranja mkuu na kundi lake kutokana kuiyumbisha familia na kutusababishia maisha magumu.

Mwaka jana kulikuwa na kitimtim, na ilibaki almanusura kiranja mkuu abwagwe, kama sio hila zao angengolewa. Lakini kaka hali imezidi kuwa mbaya sasa tumejikuta tunaogopa kuhoji na kuikemea hali hiyo kwa sababu tunatishiwa kuwa tutaivuruga familia na kusababisha machafuko.

Ninavyokuandikia waraka huu, kila kitu kimepanda bei, umeme wa mgao na hauna uhakika, halafu tunaambiwa kuwa kuna jamaa anatakiwa tumlipe fidia kwa kukatisha mkataba wa kutuuzia umeme, wakati mtu mwenyewe alirithi mkataba wa kilaghai kutoka kwa mtu mwingine aliyetutapeli awali na mpaka sasa shauri lake liko kwa mlao.

Mmmh! Kaka naona unataka kuniuliza huyu Mlao ni nani. Nisikilize kwanza, Mlao ni yule mtu anayesikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi. Haya naona umeelewa ila usicheke!

Kaka, wenzetu katika familia nyingine wameanza kuwashitukia viranja wao, kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia viranja hao wakizikimbia familia zao na kwenda uhamishoni baada ya wanafamilia kuwakataa hadharani.

Kama ulivyosikia walianza wanafamilia wa mzee Tusitusi, wao walimkataa kiranja wao hadharani kwa kuingia mitaani hadi akakimbilia uhamishoni kutokana na nguvu ya wanafamilia.

Nimeambiwa sababu kubwa ni kutokana na mkate kupanda bei, ukosefu wa mashamba ya kilimo na fursa za ajira kwa wale waliokwenda shule.

Baada ya tukio hilo la familia ya Mzee Tusitusi, wanafamilia wengine wa mzee Msisiri nao wakaja juu, kisa gharama za maisha zimepanda. Nao walichachamaa mpaka kiranja wao akakimbilia uhamishoni pia.

Kaka umesikia yaliyotokea kwa mzee Libelibe? Mmmh! Makubwa haya jamani! Wanafamilia wa mzee Libelibe familia yao ina neema za kila aina wakipewa kila kitu bure na kiranja wao, kama vile elimu, matibabu na huduma nyingine muhimu za kijamii, lakini wamemkataa kweupeee!!

Nao wameingia mitaani hawamtaki na wataka aondoke……, mmmh! lakini hata hivyo kiranja wao amewaua wanafamilia wengi kwa silaha za moto kwa sababu ya uasi, na amekuwa akisingizia kuwa uchochezi huo unatoka katika familia nyingine kitu ambacho si kweli kwa huyo kiranja wao kakaa muda mrefu katika uongozi wa familia takribani miaka 40, na sasa amechokwa.

Wakati wenzetu wakisema basi kwa viranja wao, sisi huku pamoja na hali ngumu ya maisha, na wizi wa waziwazi wa hazina zetu unaofanywa na kiranja wetu akishirikiana na wageni lakini sisi huku tunasema hewala baba.

Kaka hali inatisha, lakini nimeona wanafamilia wameanza kushtuka kama wanaibiwa na kutokana na kundi moja lililojaribu kugombea kushika hatamu za uongozi wa kuongoza familia likashindwa, Kwahiyo wanapita kwa wanafamilia kuwaelimisha na kuwaeleza kuwa kiranja anatupeleka kubaya, nimeona dalili za wanafamilia kuzinduka na siku si nyingi, tutashuhudia yanayotokea kwa majirani zetu.

Kaka kwa leo naomba niishie hapa

Nitakuandikia kwa kirefu wakati mwingine.

4 comments:

Goodman Manyanya Phiri said...

Asante sana, Mkuu Koero, kwa kutukumbusha mambo ya familia zetu sisi sote!


Hizo habari zinasikitisha,lakini ni mambo ya kawaida tu katika familia nyingi.

Tatizo litakuwa refu kuliko maelezo. Utakuta na huyo anayeonekana kama anaipotosha familia (kwa uongozi mbovu) hayuko peke yake bali wapo wanaomuunga mkono, "ndumilakuwili" katika hiyohiyo familia.


Kwa hiyo Kaka anapokuja kusaidia hapo baadaye labda, naye awe mwangalifu: mambo yanaweza kuharibika zaidi yalivyo sasa naye Kaka kuja kulaumiwa wakati yeye alifikiri anasaidia.


Kifupi, huwezi kabisa ukapata uongozi mzuri katika familia ikiwa uwingi katika familia hiyo ni watu wabaya, wavivu, waoga kukosoana au ni watu wenye ubinafsi na kiburi. Ole kwao wenye uchache katika familia hiyo na wale wenye uzuri uliezingirwa na ubaya wa uwingi: watalalamika weee lakini hawatapata msaada kwasababu: THE MAJORITY RULES.

Katika maandhari ifuatao nitafurahi zaidi kusikia Mwandishi yeye binafsi, nje ya kwandika haya, alifanya nini hasa kukabiliana ha uongozi huu mbovu?

Je aliogopa kusema kwakuwa eti yeye bado mdogo?

KOSA!

Aliachia ngazi tu kwakujuwa eti kiongozi wa familia yupo?


KOSA!

katawa said...

Kiongozi wa familia aliyejichagua kwa muhula unaoitwa wa mwisho naye kaanza kuogopa.Lakini anaogopa kikubwa sio kitoto kwa kuwa wakubwa hupenda kuficha woga wao.

Kikao chake cha mwisho wa mwezi uliopita alchokifanya na wanafamilia maneno yake yanaaonyesha woga juu ya mwanafamilia anayedai kuwa kura zake zilichakachuliwa.

Wanafamilia wanashtuka kuwa aliyepewa mamlaka ya kuitunza familia yupo pamoja nao kimwili lakini kiroho hayupo pamoja nao.

Kustuka ni mwanzo mzuri

Fadhy Mtanga said...

Keoro kipenzi,

Pamoja na ukimya wako. Pamoja na barua hii kutoandikiwa mimi bali ndugu yetu mwingine Markus. Nawiwa kusema ahsante sana kwa barua hii. Hakika nimeisoma vema na kuungana nawe juu ya malalamiko haya.

Familia ya Mzee Tusitusi, Msisiri na Libelibe na wengineo, zinapaswa kuwa funzo kubwa kwa familia yangu.

Ukitembelea sebuleni kwangu, nako nimesema.

Ubarikiwe sana mwanamke wewe kwa kufikiria vema.

MARKUS MPANGALA said...

Dada Koero, nimesoma barua yako. Nikipata hela nitanunua stempu ili nikutumie majibu. umenifurahisha kweli na barua yako.