Thursday, March 24, 2011

POLE DADA YASINTA KWA KUONDOKEWA NA DA’ MDOGO ASIFIWE

Asifiwe Ngonyani 26/11/1989-23/3/2011

Dada Yasinta,


Najua itakuwa ni vigumu kwako kusoma waraka huu kutokana na msiba mzito uliokupata, na ninaamini pia kuwa waraka wangu huu hutausoma kwa wakati, labda baada ya siku tatu nne hivi. Ingawa ninatamani sana kama ungeusoma leo sasa hivi, lakini hilo bado kwangu ni jambo la kufikirika, ninabaki kusema, labda, sijui au huenda, lakini naamini pia utanielewa japokuwa itakuwa ni too late.

Dada Naomba uamini kuwa msiba huu sio wakwako peke yako ni msiba wetu sote, yaani familia ya Mzee Ngonyani na ya Mzee Mkundi au pengine na Wanablog wote wa ndani na nje ya nchi.

Ni msiba wetu kwa sababu wengi wetu tulikufahamu wewe kupitia maandishi yako katika Blog ya Maisha na Mafanikio ambapo pia tukaifahamu familia yako na familia ya Mzee Ngonyani.

Umetushirikisha kwenye mambo yako mengi na hata yale yanayotokea katika familia yako, nakumbuka ulinijulisha juu ya ugonjwa wa mdogo wako Asifiwe mwanzoni tu nilipoanza kufahamiana na wewe mara baada ya kuanza kublog, mawasiliano yangu na wewe ya mara kwa mara yalitufanya tuwe karibu kiasi cha kutengeneza undugu. Umekuwa ni dada yangu mwema na umekuwa ukinifariji kwa kila jambo linalonitokea katika maisha yangu, tumekuwa tulishauriana kwa mambo mengi na kuwa karibu wakati wote.

Ingawa hatujawahi kuonana ana kwa ana, lakini ule ukaribu wetu umenifanya nijihisi kama tumeshawahi kuonana, Nilimpenda marehemu Asifiwe kama nilivyokupenda wewe, na nilimuona kama mdogo wangu, nakumbuka wakati akiwa amelazwa pale Muhimbili mwaka jana, nilikuwa niko Arusha, lakini nilikuwa nawasiliana naye kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani mara kwa mara. Nilijikuta nikiwa naye karibu kama mdogo wangu wa tumbo moja.


Dada yangu mpendwa, Ninavyoandika waraka huu, machozi yananilenga lenga kwa huzuni, kwa kuondokewa na mdogo wetu kipenzi Asifiwe. Ni mara nyingi tunapohudhuria misiba huwa wahubiri wanatufariji kwa mahubiri matamu kutoka katika vitabu vitakatifu, mahubiri hayo mara nyingi hutupa faraja na kukubaliana na yale yaliyotokea. Miongoni mwa wahubiri wa Kikristo hupenda sana kunukuu kitabu cha Ayubu katika Biblia, ambapo tunakumbushwa jinsi Ayubu alivyopitia mitihani migumu ambayo kwa kweli inatufanya tukubaliane na matakwa ya Mungu.

Kujadili kwa nini Asifiwe ametangulia akiwa na umri mdogo wa ubarubaru, ambapo alikuwa na matumaini ya kuendelea na elimu ili na yeye atimize ndoto zake itakuwa ni kumkufuru Mungu. Inatupasa tukubali kuwa Bwana aliumba, na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.

Nakuomba usikate tamaa, bado tupo sisi wadogo zako,dada zako na kaka zako na tutaendelea kushirikiana labda kuliko hapo kabla.


Mama yangu Namsifu Japhet Mkundi, Baba Mzee Japhet Mkundi, dada zangu, Rachel, Damari, Debra na kaka zangu pamoja na mdogo wetu Jarome wote wanakupa pole na wanaiombea familia ya Mzee Ngonyani iwe na ujasiri hasa katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa mdogo wetu Asifiwe.

Ni mimi mdogo wako


Koero Japhet Mkundi

4 comments:

Fadhy Mtanga said...

nipo hapa na Shaban Kaluse na Chacha Wambura, tungali tumepigwa na bumbuwazi isiyosemekana. Da Yasinta, tupo nawe katika kipindi hiki kigumu sana kwako.
tunamuomba Mwenyezi Mungu aipokee roho ya mdogo wetu Asifiwe na kuipa pumziko la milele. Amina.

emu-three said...

POleni sana wanafamilia, kwa msiba huu mzito!

Simon Kitururu said...

Poleni sana!

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante mdogo wangu Koero kwa yote na Ahsante Familia ya mzee mkundi pia. Naaamini tupo pamoja.