Hivi karibuni nilikuwa na mjadala mzito na baba yangu kuhusiana na dhana nzima ya mtu kujiita kuwa ni msomi.Chanzo cha mjadala huo ilikuwa ni pale aliponitaka niachane na biashara niliyoianzisha ili niendelee na elimu ya juu, kwani hapendi kuwa na mtoto ambaye sio msomi. Basi hapo ndipo nilipoanzisha mjadala wa kutaka kujua kwamba msomi ni mtu wa namna gani? Au je mtu anaweza kupimwa kwa vigezo gani ili aitwe kuwa ni msomi?
Mjadala huo ulikuwa ni mzito na uliochangamsha pale nyumbani kwani kila mtu alipata nafasi ya kuchangia kwa mtazamo wake, na kutokana na mjadala huo nimejifunza mambo mengi sana kuhusiana na hii dhana ya mtu kuitwa kuwa ni msomi.
Hebu niwaulize wasomaji na wanablog wenzangu, hivi msomi ni nani?Kama mtu amesomea taaluma fulani labda tuseme, udaktari, uhandisi au udaktari wa falsafa, Je huyu anaweza kujiita kuwa ni msomi?
Nimeuliza hivyo kwa sababu kama mtu ni msomi kwa maana ya dhana ya usomi tunayoifahamu, basi atakuwa anajua kile alichofundishwa na kukaririshwa tu akiwa darasani, lakini yeye mwenyewe hajawahi kuwa na kitu chochote kipya alichobuni.
Kama ni hivyo basi sioni kama kuna mtu anayeweza kujivuna kuwa yeye ni msomi.Atajiitaje kuwa ni msomi wakati amekaririshwa nadharia za wengine pasipo kubuni kitu chake mwenyewe?Nadhani hiyo inatosha kuvunja dhana ya watu kujiita wasomi.
Hivi ni nini tofauti kati ya msomi na yule ambaye hakuwahi kuingia darasani hata siku moja?
Kwangu mimi tofauti iliyopo labda ni kwamba, mmoja ametembea sana kutoka nyumbani hadi darasani na mwingine hajawahi kufanya hivyo hata siku moja.Huyu aliyetembea sana kwenda darasani kutafua elimu, amevuliwa akili yake na kupewa akili ambayo ni nadharia za watu wengine, zikiwemo zile sahihi na zisizofaa hata kuzitazama. Lakini amezikubali hizo nadharia na hivyo anaitwa kuwa ni msomi.
Kwa mfano ukienda chuo kikuu unafundishwa hata namna ya kulitazama jambo na kulihukumu kwa kutumia akili za watu wengine. Kile ulichokuja nacho, yaani imani na ufahamu wako kuhusu maisha, uchumi na siasa vinaondolewa na kuwekewa ambacho unatakiwa ukiamini na kukitetea kwa nguvu zako zote bila kuhoji, na hiyo itakufanya uitwe labda daktari wa falsafa na kutunukiwa digrii yako ya tatu, na kuanzia hapo utaitwa msomi!
Kumbuka kwamba digrii ni karatasi zaidi kuliko maarifa, ndio maana dunia nzima inasumbuliwa na wimbi la digrii feki.Ninachojua mimi ni kwamba wasomi wengi wa vyuo vikuu na madigrii yao ni wajinga sana kwenye maeneo mengine ya maisha.
Na jambo lingine ambalo linanishangaza, ni dunia hii kuendelea kukumbatia karatasi kama kipimo cha usomi. Unaweza kukuta mtu hajui chochote, lakini kwa sababu ana makaratasi yake yanayosema amesomea Shahada ya Uchumi, basi atapewa nafasi kubwa. Kisa ni karatasi!Halafu baadae mnashangaa, kwa sababu hana anachozalisha.Sasa usomi ni kitu gani, ni karatasi, ni kukariri nadharia za watu wengine, ni kujua jambo kwa undani au ni kujiuliza na kutafuta jibu?
Kuna watu wengi ambao nawafahamu, ambao wamekariri sana elimu ya darasani, wanayo madigrii lakini ukizungumza nao, utafikiri umekutana na mtu ambaye hajawahi kutia mguu darasani hata siku moja. Na wangine wako mitaani hawana kitu,na wamekata tamaa na maisha, kisa hakuna ajira.
Kwa kuamini kwamba karatasi ndizo zinazomfanya mtu kuwa msomi ndio maana sisi vijana wengi huko mashuleni na vyuoni tunajitahidi kushindana kukariri ili tufaulu sana na kupata digrii za viwango vya juu.Tunachotaka ni karatasi ili tupate ajira na wala sio maarifa. Tunapomaliza masomo tunatoka kama tulivyoingia na pengine tukiwa tumechuja zaidi kiufahamu.
Nimewahi kujiuliza swali hili, hivi watu kama Arstotle Sophocles, na wale wajuvi wa kwanza kwanza duniani, walifundishwa na nani, walikaa darasa lipi na kupewa vyeti gani?
Hawa hawakukaa darasani, bali walizalisha maarifa baada ya tafakari kubwa na ya muda mrefu. Walijiuliza maswali ili kupata majibu, waweze kuisaidia jamii hapa duniani.
Kwa mtazamo wangu hawa ndio wasomi, kwa sababu utafiti wao unagusa kila eneo la maarifa bila kujali kama ni sayansi, biashara, tiba au sanaa.
Msomi ni mtu aliye huru kutafuta maswali kuhusu maisha yetu ya kila siku katika nyanja tofautu tofauti na kuyapatia majibu.Msomi hatembei na takwimu za watu, bali anatafuta zake na kwa njia zake. Msomi ni mtu aliyekomaa, sio kasuku aliyekariri nadharia lukuki za wengine ambazo hajawahi kuzifanyia kazi.
Bado nauliza msomi hasa ni nani?
CCM HATUHITAJI AHADI, TUNAHITAJI MTU MWENYE KUPAMBANIA WANANCHI WAKE - NDG.
ISSA GAVU
-
> CCM Yakemea viongozi wenye kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na
kukandamiza watu.
" Kwa mujibu wa ibara ya 16 inamtaja nani kiongozi, maana yake...
11 hours ago
21 comments:
tehe, tehe, tehe
msomi ni yare majamaa yanaoweza kuongea kiswahili kwa kuchanganya na kiingereza mbale ya watu ambao hawajasoma ili ionekane inavyojua kiingereza lakini isifikishe ujumbe husika ;-cheka-;
hata mimi najiuliza msomi ni nani na kwa nini nisome zaidi ili iweje? nchi kama bongo inaongozwa na wasomi lukuki kama akina JK, MWinyi mkapa nk. ahaaa Labda msomi ni yule mwenye gari zuri na anayekaa ofisi ya kyoyozi na jumba lakifahali!??
okey msomi na kama jenerali Ulimwengu yule jamaa anayeandika makala nzuri za kuwalalamiki viongozi ambao anajua hawawezi kubadilika badala ya kuelimisha jamii ili ijitambue na kujua nafasi yake (am very sory kutaja mtu kwa jina lakini huo ndio ukweli kwamba kazi zake nzuri zinamfanya aonekane alivyokuwa na uelewa mpana lakini hauleti mabadiliko yoyote kwa walengwa zaidi ya kumsifia yeye) sio ulimwengu tu na wengine.
na labda msomi ni yule jamaa anayekula na kunenepesha tumbu akiamini yuko fiti wakati ni ujinga mtupu. msomi ni prof. mkandara anayewafukuza wanafuzi wote ili chuo kibaki chenyewe bila kujali ghrama.
msomi ni wahubiri wanaotuhubilia vitu visivyoingia akilini na wasivyoweza kuvitenda wao. msomi ni yule jamaa anayemnyooshea mwenzie kidole na kumtusi ilia aachie nafasi na yeye ale.
mimi namkubali msomi kama vile bwaya, kaluse, kitururu, koero nk. wanaotumia mida yao kublogu kwa kiswahili fasaha ili waeleweke, na wanaoheshimu uhuru wa maoni na labda watafungua tovuti na kuanzisha gazeti ili hoja zao ziwafikie wengi zaidi.
namkubali marehemu Munga tehenan kwa kutafuta elimu ya utambuzi kwa gharama kubwa na baada ya kujitambua akutugeia elimu hiyo bure na sisi tukaelimika bali kujali madarasa yetu.
nimechoka kutaipu bwana ahaaa
Kwenye Blog yangu kuna gadget ya PARADOX OF OUR TIME na naipenda saana licha ya kuwa nayo kwa miaka sasa, na baadhi ya sehemu zinasema ".We have more Degrees but less common sense; more knowledge but less judgment.
.We have more experts but more problems; more medicine but less wellness....We’ve learned how to make living, but not a life; we’ve added years to life not life to years.
.We have taller buildings, but shorter tempers; wider freeways but narrower viewpoint. .We’ve been all the way to the moon and back, but have trouble crossing the street to meet our neighbor.
.We’ve conquer outer space, but not inner space.These are the time for Fast food and slow digestion; tall men and short characters.
.More leisure but less fun; more kinds of food but less nutrition; two income but many divorces, fancier houses but broken homes.
Msomi wa sasa si kama yule ambaye hakuwa na "compass' lakini akaongoza mtumbwi toka Zanzibar mpaka Arabuni. Si yule ambaye angejua nyota ile ina maana gani na itamfikisha wapi na si yule aliyejua kuwa ukichoma majani haya na haya ukapata jivu litakusaidia kuua wadudu waharibuo mazao yako. Wa sasa ni yule ambaye anaweza kurejea na kuremba kila ambacho alifundishwa kisha kukijengea hoja na ushawishi mnono wenye KUTAMANISHA hata kama hautekelezeki.
Msomi ni nani? Nami nauliza maana hapa kuna mtazamo tofauti kulingana na tuonavyo Tatizo. Na mara zote NAMNA TUONAVYO TATIZO NDILO TATIZO
Msomi? Msomi?aisee labda ni mimi na wewe Koero! pengine sababu tunaweza kuandika bloguni? sijui pengine usomi anaosema Kalama wale jamaa wasiojua kiswahili wala kiingereza. Pengine kuamua kuwa mimi ni msomi tokana na kujua kwangu kusoma maandiko ya Kilatini! sijui labda kwakuwa mungu hakusema mimi ni msomi. Inawezekana kabisa nikawa msomi lakini sijitambui kama msomi sababu usomi ni swali gumu.
Naacha nimeshindwa vibaya sana, msomi ni yule aombaye pesa ughaibuni, yule fundi wa kuandika project za kuomba pesa kwa wafadhili au yule mpambe wa msomi ambaye anamsifia mwenzake msomi. heee usomi mbona hauna ubongo wa pekee? mbona wote tuna medulla oblangata,ubongo wa kati na mbele? usomi upo wapi? unarangi gani? usomi labda kujua kuongeza na nguruwe pori toka ulaya na marekani, wenye rangi zilizochubuliwa na makatambuga ya jua kali au baridi.
LABDA msomi ni yule ajuaye UJINGA siyo usomi au yule ajuaye kwamba usomi siyo ujinga. LAKINI mbona kuna wajinga wasomi wasomao mpaka shahada za uzamili halafu wote wanasoma mistari ileile ya msomi aliyepita?
JIBU msomi ni yule atakaye anza kujitambua kama OSHO alivyowachapa bakora wanafunzi wake walipomwuliza watu wakiwauliza wao ni nani wajibu vipi! Lakini umewahi kusikia kuhusu FREEMASONS AU MASONIC, ndiyo maana dunia yote tunaweza kuwaza jambo moja ambalo wamepanga liwazwe, labda tujiulize Google Translator ni nini maana webmaster wote wanajua kiendeleacho ulimwenguni, wanajua ujinga wa wasomi. LAKINI msomi ni nani?
Swali gumu naacha nimeshindwa, nangojea wengine wa utambuzi
Samahani kwa tabia ya kuomba omba kama wasomi, pengine sijui kuomba ni dhambi au ujinga LAKINI naomba kazi katika hiyo BIASHARA YAKO ULIYOANZISHA. tafadhali dada Koero niajiri mimi au labda nakuboa? yawezekana
Mpangala sasa wewe unataka kuvuruga mada, hapa tunazungumzia jambo ambalo limnahitaji tafakuri halafu wewe unaleta sera za kuomba kazi!
Kaka ninayo email yangu kwenye blog, mambo ya binafsi, tuma email.
Usivuruge mjadala, hapa nasubiri maoni na changamoto za wasomaji wengine, wewe sio umechangia?
Kwa mtizamo wangu,nadhani pengine mtu HAJIITI msomi bali HUITWA msomi,na wanaomuita hivyo wana sababu zao za msingi (mara nyingi ni wana fani wenzie).Jamii ina uhuru wa kukubaliana na kikundi hicho cha wana fani au kukipuuza.Uluteni,kwa mfano, una mantiki zaidi jeshini kuliko uraiani ambako sanasana wanaofahamu kidogo watasema ni cheo cha nyota mbili.Lakini kijeshi uluteni ni zaidi ya hayo "mawe mawili",kuna uongozi wa moja ya vikundi vya kivita (platuni,kama sijakosea),nk.
Nadhani pia vyeti sio lazima vimaanishe usomi.Lakini again,wanaofahamu zaidi ni wale waliotunuku vyeti hivyo.Jumuiya ya wahadhiri inapoafikiana na kumteua mmoja wao kuwa profesa,kwa mfano,ina mantiki zaidi katika mazingira yao kuliko nje ya ulingo huo.Jinsi ya uprofesa huo utavyotumika ni suala jingine,na jamii ina uhuru wa kuuponda au kuuenzi uprofesa huo.
Na kuhusu vigezo gani vinavyoweza kufanya mtu aitwe msomi,nadhani pia majibu yanaweza kutofautiana kati ya walio ndani ya fani flani na walio nje ya fani hiyo.
Pia naomba nitofautiane kidogo nawe dada yangu katika hoja yako kwamba msomi lazima awe amebuni kitu.Nadhani usomi na ubunifu ni vitu viwili tofauti japo inatarajiwa msomi awe mbunifu ingawa si lazima awe mbunifu.Lakini pia kama unapozungumzia ubunifu unamaanisha kuja na kanuni (theory) mpya,then kuna mahala flani kitaaluma ni lazima uje na aidha theory mpya au uifanyie maboresho kwa iliyopo.Nje ya uwanja wa kitaaluma,huo unaweza usiitwe ubunifu lakini ndani ya ulingo huo,huo nao ni ubunifu.
Pia naomba kutoafikiana nae kwamba kile unachokuja nacho wakati unaingia chuo kikuu kinaondolewa na KUWEKEWA UNACHOTAKIWA KUAMINI...Nani anayekutaka kuamini?Labda kwa wenzetu wa sayansi ambao nyakati nyingine X ni lazima iwe X,lakini mara nyingi (japo si mara zote)huko kwenye "ungwini" ni namna mwanafunzi anavyoweza kucheza na hoja zake.Iwapo kuna mahala mwanafunzi analazimishwa kutetea hoja isiyo yake pasipo kuhoji basi hapo kuna kasoro.
Kuhusu kukutana (naomba kukunukuu)"watu wengi ambao nawafahamu, ambao wamekariri sana elimu ya darasani, wanayo madigrii lakini ukizungumza nao, utafikiri umekutana na mtu ambaye hajawahi kutia mguu darasani hata siku moja" hudhani kwamba tatizo linaweza kuwa mnahukumiana ndivyo sivyo?Yawezekana wao wanaamini mnaelewana katika mnachoongea lakini kumbe sivyo.Hudhani pia kwamba unaweza kuwa huwatendei haki kwa "kujipa mamlaka" (samahani kwa neno hilo) ya kuwahukumu?Au haiwezekani kwamba kwa vile hoja zao hazikuendana na matarajio yako ndio maana ukazihukumu kuwa ni kama za mtaani?
Mwisho,nadhani "makaratasi" (kwa maana ya vyeti) yataendelea kubaki na umuhimu wake hususan miongoni mwa wanafani husika.Kuwepo kwa vyeti feki hakuwezi kuondoa umuhimu wa vyeti halali just like kuwepo kwa noti feki kusivyoweza kuondoa umuhimu wa noti halisi.Jamii hailazimishwi kuthamini au kupuuza vyeti hivyo.Elimu itaendelea kupatikana mtaani,madarasani,kwenye karakana,semina,nk...ni kutoka katika mazingira hayo ndio wahusika watampachika mwenzao/wenzao joho la usomi,umahiri,ujuzi,ubobeaji,ujanja,nk.Watakaotuzwa joho hilo nao hawawezi kuilazimisha jamii iwathamini/iwakubali,bali matokeo ya kazi zao yanaweza kufanya hivyo.
Wadau naomba nisifunge huu mjadala, maana naona changamoto ya kaka Evarist imenitoa jasho.
lakini siamini kama nimepata majibu sahihi kulingana na hoja yangu ya kutaka kujua kwamba msomi hasa ni mtu wa namna gani?
Nadhani mada hii ni pana sana, na inahitaji tafakuri kubwa.
Sikuandika mada hii ili kubeza elimu au kuwabeza wasomi wetu hapa nchini, bali nikuwa najaribu kuangalia jambo hili katika mkabala tofauti, kwa hiyo kutofautiana kimawazo ndio njia sahihi ya kujifunza na kuyajua mambo kwa upana wake.
Bado niko kwenye utafiti, na nikirejea chuoni nitaendelea na utafiti huu, halafu nitaweka majibu yangu humu.
Bado nakaribisha maoni zaidi kutoka kwa wadau mbali mbali.
Ahsanteni sana.
Sikuwa ulingoni kwa siku kadhaa hivi. Nimependa utaratibu wa kibaraza hiki wa kutokulifunga 'jalada' kwa faida ya wasomaji ambao, kwa sababu moja ama nyingine, tunakutana na hoja ikiwa kabatini.
Kuhusu usomi. Nadhani hatuwezi kuwa na majibu yanayofanana. Pengine hata namna tunavyoutazama usomi wenyewe inatofautiana baina ya fani na fani, mtu na mtu, na kadhani.
Hata hivyo nionavyo mimi, ni kwamba kinachofanyika madarasani si kutufanya tuwe wasomi. Kumbi za mihadhara, maktaba na vyumba vya maabara vinatupanua ufahamu. Kutufanya tupate mitazamo ya watu wengine waliotutangulia. Kutujulisha maarifa yaliyopo. Huu kwangu si usomi.
Tukifikia mahala pa kuweza kuyatumia maarifa hayo ili kujua namna ya kutatua changamoto zinazotukabili sisi wenyewe pamoja na jamii kwa ujumla, hapo tunaweza kuwa wasomi.
Kwa mipaka ya tafsiri yangu, msomi ni mtu yoyote, bila kujali idadi ya madarasa aliyokanyaga, awezaye kuyatumia maarifa yake kuzikabili changamoto za maisha kiufanisi. Alikoyatoa maarifa haya si jambo la msingi.
Daktari wa SUA aliyechaifua kila aina ya kitabu cha kilimo, lakini asiweze kutusaidia kuyakabili matatizo ya kilimo nchini, kwa kisingizio kwamba eti alivyonavyo kichwani havishabihiani na changamoto za kilimo chetu, huyu si msomi. Ni sawa kompyuta isiyoweza kuzitambua data zenye format tofauti.
Nani mpimaji wa usomi wa mtu? Nadhani
jamii katika upana wake. Watu wa kawaida kabisa, hao ndio wenye vigezo vya kweli vya usomi. Sababu ni kwamba utumiwaji wa maarifa hutafsirika katika maisha ya watu. Watu wa kawaida wanaangalia namna elimu ya watu inavyowaletea unafuu wa changamoto za maisha yao.
Sikubaliani na utaratibu wa genge la mabwanyenye wa madarasa yetu wanaoiamulia jamii nani yu msomi na yupi siye. Kwa sababu ni wazi kwamba 'wasomi' hawa ni mabingwa wa kurudufu maarifa ya wenzao ambayo kwa bahati mbaya hayaleti yoyote katika jamii.
Profesa anaweza kujua vitu vingi sana katika fani husika, na ndivyo ilivyo, lakini si lazima awe msomi hata kama anaheshimika na maprofesa wenzake wanaotumia vigezo vinavyoandikika. Kama mtu hawezi kutafsiri viandikwa vyake katika maisha ya kawaida kwa maana ya kuifaidia jamii, sidhani kama ana sifa za kuitwa msomi.
Profesa anayepika tafiti zake kwa manufaa ya mafisadi, je naye ni msomi? Profesa asiye na lugha inayoeleweka na watu wanaoitwa wa kawaida, anayejijengea ukuta kati yake na jamii yake inayemhitaji, naye ni msomi?
Mashaka yangu ni haya. Ninawafahamu wanasayansi wengi waliokimbia umande, ama kushindwa mitihani, ambao maarifa yao yanaheshimika mpaka leo. Je, hawa si wasomi hata kama hawana vyeti? Hawakuwahi kuitwa madokta wala maprofesa, lakini waliweza kuyatumia maarifa yao wenyewe ambayo wasomi wa enzi hizo hawakuwa nayo!
Shule, nadhani, ingeleta maana kama utaratibu wa kupimana uelewa kwa mitihani ili kupeana vyeti hautauawa.
Albert Einstein, mwanafizikia mashuhuri aliwahi kusema, '...elimu ni kile kinachobaki, baada ya kusahau vyote ulivyofundishwa madarasani...'.
Msomaji amue hekima ya maneno haya.
Binafsi nilishtushwa na ukimya wako, nikajiuliza kulikoni?
Unajua nimesoma maoni ya wachangiaji wangu wote, ukabaki wewe tu.
Ahsante sana kwa mtazamo wako na ahsante sana kwa kunitembelea.
Bado nasubiri maoni ya wasomaji wengine........
Asante sana Koero.
Haraka mtandaoni, kwa hofu ya kuishiwa muda hutufanya tuandike kwa mcharazo. Naomba nihariri:
...shule, nadhani ingeleta maana kama utaratibu wa kupimana uelewa kwa kutumia mitihani kwa minajili ya kupeana vyeti, ungeuawa...'
Nilikuelewa.
Hata hivyo ahsante kwa ufafanuzi ili wasomaji wengine wasije potea.
Naomba kuchangia tena.
Nadhani kuna tofauti ya maana ya kitu na namna kitu hicho kinavyopaswa kuwa.Daktari wa SUA aliebukua na kupata udaktari ni msomi.Jamii ipende isipende,ili kuwa na ujuzi alofikia muungwana huyo lazima hatua flani zipitiwe,ikiwa ni pamoja na kuingia darasani,kutoa mihadhara,nk.Hizo ni taratibu za kuingia daraja la usomi.Usomi wa Msomi usipoweza kuisaidia jamii,au kutokuwa na manufaa kwa jamii,inapelekea kushuka thamani kwa usomi huo,lakini hakuondoi usomi.Kitakachotengua usomi wa mhusika ni kukiuka kanuni na taratibu za fani husika,na sio flani anapenda au flani hapendi.Ikumbukwe,walomwingiza katika daraja hilo sio jamii bali WASOMI wenzie.Wanaweza kuwa mabwanyenye wanaofikiria maslahi yao binafsi,lakini huo ndio ukweli mchungu wa maisha.Kwa mfano,Tuna viongozi wabovu,lakini kwa vile wamechaguliwa (wakati mwingine kwa kununua kura) wanaendelea kuitwa viongozi.Je wabunge wasiowakilisha VEMA wananchi wao hatuendelei kuwaita WABUNGE?
Nadhani kisifa (adjective) USOMI inatokana na kitenzi (verb) SOMA au KUSOMA.Kwa mantiki hiyo,USOMI unahusiana na KUSOMA,na nomino MSOMI ni MTU ALIESOMA.Wakati mwingine maneno ya kiswahili yanaleta maana flani yanapoelekwa kwenye lugha nyingine.Kwenye Swahili-english dictionary,ukisaka maana ya neno MSOMI kwa Kiingereza inakupa majibu yafuatayo:
msomi , pl wasomi { English: intellectual }
noun
msomi , pl wasomi { English: learned person , pl learned people }
noun
msomi , pl wasomi { English: lecturer , pl lecturers } [derived: soma V]
noun
msomi , pl wasomi { English: reader } [derived: soma V]
noun ,
msomi , pl wasomi { English: scholar , pl scholars } [derived: Swahili -soma]
noun
5 distinct results returned (chanzo:THE KAMUSI PROJECT)
Kwa mtizamo wangu unaoweza kuwa sio sahihi,nadhani kuna umuhimu wa kutofautisha MATARAJIO YA JAMII KWA "WASOMI" na MAANA YA NENO "MSOMI".
Bwaya anahoji iwapo Profesa anayepika tafiti zake kwa manufaa ya mafisadi, je naye ni msomi?Yes,ni MSOMI,lakini ANAYEKIUKA KANUNI,TARATIBU NA SHERIA ZINAZOONGOZA FANI YAKE.
Kuna baadhi ya sifa ambazo mtu akishafanikiwa kuzipata hubaki nazo kwa muda mrefu kama sio milele.Ni mithili ya ualimu,jina linaendelea kubaki MWALIMU hata pale mtu anapostaafu au kufukuzwa kazi.
Naomba kunukuu hoja nzito ya Bwaya kwamba "....Ninawafahamu wanasayansi wengi waliokimbia umande, ama kushindwa mitihani, ambao maarifa yao yanaheshimika mpaka leo. Je, hawa si wasomi hata kama hawana vyeti? Hawakuwahi kuitwa madokta wala maprofesa, lakini waliweza kuyatumia maarifa yao wenyewe ambayo wasomi wa enzi hizo hawakuwa nayo!" Binafsi,nadhani mwanzoni mwa mjadala niligusia juu ya umuhimu wa vyeti KAMA KITAMBULISHO lakini haimaanishi kwamba kutokuwa na cheti kunamuondolea mtu umahiri wake katika fani husika.Pia ili mtu aitwe msomi si lazima awe dokta au profesa LAKINI LAZIMA ASOME,iwe nyumbani,darasani au kwa njia ya posta au kujielimisha kwa elimu vitendo.HUWEZI KUWA MSOMI PASIPO KUSOMA.Utawezaje kuwa mwanasayansi kama hujasoma sayansi?
Mwisho,wakati JAMII INATARAJIA wasomi wafanye vitu kwa manufaa kwa jamii,kutakuwa na wasomi watakaotimiza matarajio hayo,na kuna wengine ambao hawatatimiza.Wote wataendelea kuitwa wasomi.Kitakachozidi au kupungua ni heshima yao kwa jamii na wanafani wenzao.Kinyume cha matarajio ya jamii kuhusu kinachotarajiwa kutoka kwa anayeitwa MSOMI hakibadili maana ya neno MSOMI...just like UONGOZI MBOVU usivyoweza kuondoa maana ya neno UONGOZI (bali kuathiri TASWIRA ya uongozi).
Swali,je kuna neno MBADALA kwa mtu aliyesoma sana lakini kusoma huko hakuinufaishi jamii?
Leo nimeamka alfajiri majira ya saa kumi na moja na nusu hivi na kukutana na maoni ya kaka Evarist, ambayo yamenisisimua sana.
Labda nikuulize kaka Evarist,
Je wale wanaotunukiwa digrii za heshima, nao tuwaiteje?
Je wanayo sifa ya kuitwa wasomi?
Je Jamii iwatambueje?
Kuhusu jina mbadala la msomi ambaye hana tija katika jamii labda tuwaulize watu wa BAKITA, nadhani hii ni changamoto kwao na kwa wadau wengine, lakini hata hivyo tukishindwa tunaweza kutohowa kutoka katika lugha nyingine kama wenzetu watakuwa walipambazukiwa mapema na kuwatenganisha watu wenye sifa hizi.
Je wadau wengine mnasemaje?
Nimesoma kwa makini maoni ya kaka yangu Evarist. Nimevutiwa na mchango wake.
Nisirudie alichosema mwongoza mjadala dada Koero. Pengine wakati tukiwasubiri BAKITA tuseme, aliyepita darasani tumwite msomaji, maana hana tofauti na msoma novo, hata kama yeye anaonekana kuchemsha ubongo zaidi. Akiweza kutumia maarifa yake kwa tija aitwe msomi.
Kwa kuzingatia mchango wa kaka yangu Evarist, naomba niulize: Hivi 'shule' zilianza -anzaje? Ni akina nani hasa walianzisha shule kama usomi hauwezekaniki bila shule? Maana yangu ni kwamba, ikiwa shule ndizo zinatengeneza wasomi, yaani haiwezekani kuwa msomi bila shule, na ikiwa pasipo shule hapana msomi, je shule hizi zilikujaje bila wasomi wasioenda shule?
Labda nisemee eneo la sayansi ninalolifahamu fahamu. Wanasayansi wengi walifanya tafiti zao kwa akili zao wenyewe bila kulazimika kufuata mwongozo wa yeyote. Inashangaza. Na si kwamba walisoma sana viandikwa na hivyo kupata ujanja wa kurekebisha nadharia zilizokuwepo. Hapana. Walitumia vipaji vyao wenyewe kuisoma nature. Hawa hawakuwa wasoma makarabrasha tu (ya wenzao), bali walitumia muda mwingi kuzisoma hali fulani , kuzifanyia kazi na mwishowe walikuja na siri zinazojadilika. Na ndio maana chuo kikuu enzi hizo kilimaanisha eneo ambalo watu wenye 'siri' hukutana kwa mijadala.
Ndio maana bado siamini kabisa kwamba kinachofanyika siku hizi si usanii maana kinaishia maili nyingi kabla ya usomi.
Haya tumsubiri kaka Evarist tumsikie atasemaje?
Nilijua mapema kabisa kwamba mada hii ni ya moto,na niliamua makusudi kuiandika ili kuwafikirisha wasomaji wangu.
basi kuna rafiki yangu mmoja kanipigia simu leo na kunishutumu juu ya mada yangu hii, kwanza nilishangaa maana najua kwamba hapendi kusoma blog,
Eti ananilaumu kuwa nawapoteza watu.
anasema, mimi nasoma chuo kikuu halafu nawaambia watu kuwa hakuna wasomi, au sitaki watu waerevuke.
Nikashikwa na mshangao, hivi kumbe watu wanasoma ili waerevuke?
Kwa hiyo wale wasiosoma hawajaerevuka!
Hiyo ilikuwa ni changamoto nyingine.
Hata hivyo nilimshauri siku nyingine aweke maoni yake humu ili wasomaji wengine wasome mtazamo wake.
Sijafunga mjadala.
Dada Koero,nadhani kabla ya kujibu kuhusu wnaotunukiwa shahada za heshima ni muhimu kufahamu kwanini wanapewa shahada za heshima.Kwa uelewa wangu mdogo,shahada za heshima hutolewa na taasisi husika (mara nyingi ni za kitaaluma) kwa kutambua mchango wa mtunukiwa katika jambo fulani.Nadhani PhD ya heshima alopewa JK huko Kenya inatoa mfano mzuri.Uamuzi wa kuwaita wasomi au la hao walopewa honorary degree nadhani unategemea zaidi suala la taaluma.Kuhusu jamii itawatambuaje,hilo linarudi tena kwenye hoja yangu ya msingi kwamba matarajio ya watoa shahada (eg chuo) na mpokea shahada (kwa upande mmoja) na jamii (kwa upande mwingine)yanaweza yasifanane.
Ndugu yangu Bwaya,naomba nifafanue tena kwamba kwa mtazamo wangu (unaoweza kuwa sahihi) usomi unaendana na kusoma.Shule ni moja tu ya mahala pa kupata fursa ya kusoma.
Kuhusu shule zilianzaje,binafsi sina jibu kwa vile sijawahi kusoma historia ya shule.Lakini lililo dhahiri ni kwamba anayekwenda shule hawezi kufundishwa na mwenzie ambaye nae hajui kitu.Ni dhahiri kuwa shule ni miongoni mwa vyanzo vya wasomi.
Bwaya,nadhani huwatendei haki wasomi kwa kuwaita wasomaji japo naheshimu mtizamo wako.Nadhani msomaji ni yule ambaye halazimiki sana kuingia ndani zaidi ya anachokisoma,kutengeneza hoja za kuunga mkono au kupinga au kutahiniwa (eg kusoma gazeti,kwa mfano).
Kuhusu "usanii" wa kazi nyingi za wasomi kuihsia kwenye mafaili,nadhani wanaopaswa kulaumiwa zaidi sio wanataaluma bali wale wanaotakiwa kufanyia kazi mapendekezo ya kitaaluma.Ikumbukwe,kazi nyingi za kisomi huishia tu kutoa mapendekezo na ni juu ya watengeneza sera kuamua kufuata mapendekezo hayo au kuyapuuza.Usomi sio udikteta kwamba kwa vile nimetafiti kitu flani na kuthibitisha kwa findings zangu basi lazima kikubalike.
Dada Koero,nadhani kilichomshangaza huyo mwanafunzi mwenzio ni nini basi kimewapeleka chuoni...maana kwa tafsiri ya mtaani ukiwa mwanafunzi unaitwa msomi(naomba nisijifanye nafahamu mawazo yake,ni hisia tu).
Nimalizie kwa kusema kuwa binafsi naendelea kuamini kuwa ili mtu awe msomi ni lazima asome.Kuhusu asome wapi,hilo ni swala jingine.Asome nini,inaweza kuwa elimu nadharia au elimu vitendo.Kiasi gani cha elimu kinastahili kumfanya mtu aitwe msomi,nadhani suala si cheti au idadi ya digrii bali content ya kile kinachompa sifa ya usomi.
Haya kaka Bwaya, umeona hoja nzito hiyo kutoka kwa kaka Evarist?
Labda niweke wazi kwamba, mimi sikwenda chuoni, ili niwe msomi, kwa sababu siamini kabisa kwamba kwenda kwangu chuoni kutanifanya niwe msomi.
Kwangu mimi namuona msomi ni yule aliyejitambua, na jamiii ikamkubali.
watu kaka Gautama Sidharata, Osho, Mama Theresa, Lenin, Dalai Lama na wengine wanofanana na hao, naweza nikawaita kuwa ni wasomi kwa sababu walijitambua na kutumia vipaji vyao kwa manufaa ya watu wengine.
Tunapokuwa chuo kikuu tunafundishwa kuhusu utandawazi, ujamaa, ubepari, na nadharia nyingine chungu mzima halafu tunaambiwa tuchague nadharia yoyote ile kati ya hizo ili tuitee, hatuambiwi tutafute nadharia zetu na kuzitetea,la hasha.
nadhani sisi tumefungwa na tafsiri kuliko uhalisia.
Kwenda chuo kikuu hakumfanyi mtu kuwa na sifa ya kuwa msomi, bali kuondoa kile alichokuwa nacho na kupewa kingine.
Kaka Evarist kumbuka kwamba kila mtu kazaliwa akiwa na kipaji chake , kinachotakiwa ni njia sahihi ya kumuwezesha mtu kukuza kipaji chake na kufikia malengo yake.
Lakini hilo halipo.
Na ndio maana siku hizi watu wanakimbilia kusomea taaluma zenye masilahi, kinachoangaliwa ni mshiko sio kipaji alicho nacho mtu.
Utakuta mtu anakwambia "Wewe unasomea Sayansi ya jamii, itakusaidia nini? Si bora ungesomea sheria, udaktari au uhasibu"
Kwa nini? Kwa sababu taaluma hizo zina mshiko, na ndio zenye maslahi.
Mimi naona hapa ndipo dhana ya usomi inapoingia mushkeli, labda tutafute neno jingine mbadala.
Naomba Nikiri kwamba, nakubaliana na Kaka Bwaya kwa mtazamo wake.
kama kuna mwenye mtazamo tofauti atuwekee hapa.
Ndio. Wakati tunawasubiri wasomaji wengine, naomba nirudi tena.
Ninukuu maneno ya Evarest aliposema "...Kuhusu 'usanii' wa kazi nyingi za wasomi kuishia kwenye mafaili,nadhani wanaopaswa kulaumiwa zaidi sio wanataaluma bali wale wanaotakiwa kufanyia kazi mapendekezo ya kitaaluma... "
Hapa ningependa kuuliza. Hivi kazi ya msomi ni ipi? Kupendekeza ama kufanyia kazi kile alichonacho? Kwa nini asubiri wengine kumfanyia kazi mapendekezo yake? Kama kweli anakiamini alichonacho, na kama ni kweli hafanyi usanii wa kitaaluma, kwa nini asichukue hatua yeye mwenyewe?
Kwa sababu, nionavyo mimi ni kwamba wasomi wa ukwelii, pamoja na kukubalika kwenye jumuiya zao za kitaaluma, wanajipenyeza katika jamii kuuza mawazo yao kwa namna yoyote iliyo halali!
Mfano rahisi. Evarest mwenyewe. Ni watu wachache wa namna yake, wamethubutu kujadiliana na watu wa kawaida kama sisi.
Evarest amekuwa akitumia maarifa yake ya sayansi ya siasa, kutuchambulia mambo tusiyoyajua. Ametumia muda wake mwingi kuandika kwenye magezeti kadhaa, hata kama mara nyingine ameibua mambo yanayowakwaza hao anaotuambia wanapaswa kutekeleza mapendekezo ya wasomi. Lakini hajasita kutoa mchango wake kwa jamii yake. Hakusubiri watu wengine watumie maarifa yake kufanya utekelezaji. Sasa kwangu, huo ndio usomi. Matumizi ya elimu.
Hata kama inakuwa kama siwatendei haki, ni kweli kwamba hao wengine ni wasomaji. Kwa sababu hata kwenye magazeti, msomaji makini ni yule ambaye huingia ndani zaidi ya anachokisoma,kutengeneza hoja za kuunga mkono au kupinga hata kama hatahiniwi.
Ikumbukwe kutahiniwa si sifa ya msingi sana ya elimu. Kutahiniwa ni kama vile mtahini anasema najua hutasoma bila mtihani, ngoja nikupe mtihani ili usome. Kwa hiyo kwa mfano wa msoma gazeti, mimi naona ikiwa anaweza kusoma bila shuruti (wakati akijua kabisa hana mtihani) maana yake huyo ni msomi kuliko yule mwingine wa darasani amabye akiwa na hakika hakuna mtihani hawezi kusoma asilani. Ushahidi wa wazi. Wanafunzi wengi wa Vyuo Vikuu wakishapewa makaratasi yao, hawakumbuki tena kama kuna kitu kinaitwa kusoma. Kumbe hawa jamaa walikuwa wanasoma sana kwa sababu gani?
Kwa kuhitimisha, nitumie maneno ya Evarest kwamba "shule ni moja tu ya mahala pa kupata fursa ya kusoma". Ni kweli. Maana sikusema kwamba wanaoenda shule hawawezi kuwa wasomi, ila nilihoji pia kwamba upo uwezekano wa mtu kuwa msomi bila shule na kwamba kwenda shule peke yake hakutoshi kumfanya mtu awe msomi. Kwa hiyo hapo nadhani tumekubaliana na Evarest kimsingi.
Usomi na shule vinahusiana, ila pia vinaweza kuwa vitu viwili tofauti.
Sasa natamani maoni yangekuwa yanaandikwa "barazani" maana naona huu ni zaidi ya uchambuzi. Nawashukuruni saaaaana saaana
usomi ni neno linalotokana na neno soma, itategemea umesomea nini lakini mantiki ya kuwa wewe ni msomi maana yake kile ulichokisoma au kuelimishwa basi umekielewa na kukifanyia kazi kivitendo na una mchango fulani katika maendeleo ya jamii kutokana na kile ulichoelimishwa au kukisoma.
Kuna idara moja ya serikali nilienda kuoji jambo nikaambiwa niwe kama msomi,na akaniambia kwa lugha hii "let it goes". Maana ya hilo neno sijui ni nini?
Post a Comment