Tuesday, January 27, 2009

NDOA ZIMEGEUKA KUWA MSAMIATI MGUMU KWA WANAUME?

Siku hizi zimegeuka kuwa msamiati mgumu kwa wanaume
Kumekuwa na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa jamii kwamba imekuaje vijana wa kiume wamekuwa ni waongo sana hasa linapokuja swala la kuoa?

Kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo idadi ya wanaume wanaoogopa kuoa inazidi kuongezeka. Utakuta wapenzi wanaambiana kwamba wanapendana na kuahidiana kuwa wataoana, lakini kitakachotokea baada ya hapo ni mwanaume kuanza kupiga chenga kwa visingizio lukuki.

Kwa nini hali hiyo hutokea?

Ukweli ni kwamba hakuna jibu la moja kwa moja juu ya tatizo hilo, lakini lipo jibu ambalo linaweza kutupa angalau tafakuri.

Siku hizi hakuna shinikizo kubwa kutoka kwa wazazi au walezi la kuwataka vijana kuoa tofauti na zamani. Labda inawezekana ni kutokana na ugumu wa maisha au kulegalega kwa maadili, ndiko kunakopelekea jambo hilo kutokuwa na msukumo mkubwa.

Kwani maisha yamekuwa magumu kiasi kwamba mzazi au jamaa wa kijana anaweza kuhisi ugumu wa kumshinikiza kijana wake kuoa. Sababu nyingine ambayo labda hii ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa ni ile tabia ya wasichana kukubali kirahisi kuishi na wanaume bila ndoa, au kuwa wapenzi ambao wanakutana kwa muda na kushirikiana katika mambo mengi kama vile wameoana, na kwa kawaida wanaume wakishafanikiwa kuupata mwili wa mwanamke, kupikiwa, na kufuliwa nguo huwa hawaoni tena sababu ya kuoa.

Na kwa kuwa kupenda kwa wanaume kunamaanisha pia tendo la ndoa hivyo upatikanaji wake unapokuwa rahisi wanakuwa hawaoni umuhimu wa kuoa.

Siku hizi wanawake wengi hawajali kuhusu miili yao, na kuigawa kirahisi kwa wanaume limekuwa ni jambo la kawaida kabisa. Na wengine hudhani kuigawa miili yao kirahisi kwa wanaume kunaweza kuwashawishi wanaume hao wawaoe, kumbe ndio kwanza wanaziba njia ya wao kuolewa.

Pia kuna dhana imejengeka miongoni mwa wanaume kwamba wanawake wa siku hizi hawaaminiki, hivyo wengi huona kwamba kuoa inaweza ikawa na maana ya usumbufu, na kwa bahati mbaya wanaume wanaamini kwamba siku hizi kumpata mwanamke wa maana ni jambo gumu sana. Kwa kufikiri hivyo, vijana wengi wa kiume huhangaika kutafuta mwanamke anayefaa bila mafanikio.

Wengi wanaamini kwamba kuna mwanamke mahali ambaye huyo hana kasoro na atakuja kukutana naye siku moja. Wengine wanahofia majukumu hasa ya kulea watoto, kwani huamini kwamba kulea ni jambo gumu sana. Pia wapo wengine wanaamini kwamba, hata mke anapaswa kulelewa kama mtoto, hivyo wanaamua kutafuta kwanza uwezo, ambao nao kuupata ni shughuli kubwa.

Wapo ambao wamefundishwa kwamba ni lazima wawe na nyumba kwanza ndio waoe, hivyo mpaka waje wapate uwezo wa kujenga wanakuwa wameshachelewa sana.

Kibaya zaidi, wapo baadhi ya wanaume, wanaona maisha bila ya ndoa ni bora kuliko yale ya ndoa.

Kwa mujibu wa baba yangu, aliwahi kunisimulia kwamba, zamani, kuoa ilikuwa kama vile ni jambo la lazima, na kijana yeyote ambaye angefikisha umri wa kuoa, halafu awe hajaoa, angelaaniwa sana na jamii, kwani angetafsiriwa kama ni mzinzi, lakini siku hizi swala hili limegeuka na kuwa ni la mtu binafsi na siyo la jamii tena.

Kwa hiyo ningependa kuwatahadharisha wasichana wenzangu kwamba wanapoingia kwenye uhusiano na wanaume wasitarajie sana kitu kinachoitwa ndoa kutoka kwa wanume hao.

Wasichana wenye hekima hawakubali kuonjwa na wanaume ili kulazimisha ndoa bali husubiri ndoa kwanza.







7 comments:

Mzee wa Changamoto said...
This comment has been removed by the author.
Mzee wa Changamoto said...

Mzee wa Changamoto said...
Mtu akikwambia kuwa JUA LIKIWAKA WAKATI MVUA INANYESHA BASI UJUE SIMBA ANAZAA basi waweza kukubaliana naye kwa sababu mbili. Moja kwa kuwa umesikia na hujafikiria na pili kwa kuwa hujasikia upande wa pili kukueleza kinaga ubaga kuwa huo ni uongo. Pengine uliyosema hapa yote yana ukweli japo yote yanaonekana kuwa ni athari fulani miongoni mwa wanaume. Sasa mbali na ukweli huo tujiulize ni kwanini haya yanatokea? Ni kwanini wavulana wawaogope wasichana? Ni kwa kuwa wapo waliogeuza ndoa kuwa mtaji. Ambao wakishazaa na mtu basi wanaona ndio "wamemfunga nira" ya kumtawala watakavyo. Wasichana hawapati mafunzo kama waliyokuwa wakipewa zamani (achana na huu uchafu wa kitchen party ninaousikia ambao 99% ya wanaofunda wameachika) na hilo linapunguza mengi ndani ya ndoa. Pia lile lilitumika kutambulisha mapungufu ya wanaume na hata namna ya ku-handle mazungumzo na mafarakano. Si unakumbuka ile mada ya wanaume kutopenda kukosolewa? Basi wakati mwingine sio kwamba hawapendi, ila style inayotumika kuwakosoa ndio inakera hasa kama ameshajiona kuwa KICHWA CHA FAMILIA. Hakuna ubishi kuwa TUMEJIPOTEZA KWA NAMNA NYINGI kuanzia imani juu ya mahusiano, imani juu ya umuhimu wa mahusiano, imani juu ya na umuhimu wa mhusiani na maisha ya mahusiano kwa ujumla. NI KWA KUWA HAKUNA HAKIKA NA TUMAINI LA UPANDE WA PILI WA MAHUSIANO. Kinachofuata hapo, ni MAISHA YA HOFU (ambayo Kaluse aliliita kuwa dubwana la kutisha) na gharama zake ndio hizi za watu kuishi kkatika maisha yenye kila kitu kuhusu ndoa lakini bila ndoa.
Labda swali langu la mwisho ni NINI TAFSIRI YA NDOA? Kama Nampenda mwenza wangu (mawazo), namwambia kuwa nampenda (maneno) na twatenda tendo la ndoa (matendo) kuna la zaidi litakiwalo (mbali na kutaka kuishi mifumo ya wenzetu?) Niliwahi kuuliza kama kuna panaposema ni lazima ifungwe kanisani ama mahala pengine sijapata jibu. Nadhani wakiishi kwa upendo wa mawazo, maneno na matendo wapo kwenye ndoa. Au sio
Blessings

Evarist Chahali said...

Nadhani kuna sababu mbalimbali zinazopelekea "wanaume kuchelea kuoa."Japo inaweza kuonekana kuwa ni excuse flani tu,lakini kupata mwenza sahihi ni moja ya mambo muhimu yanayoweza kupelekea ndoa.Mtu anayekurupuka na kuamua kuoa for the sake ya kuoa tu si ajabu akaishia kutumia muda mwingi wa ndoa hiyo mahakamani,baraza la usuluhishi,nk kutafuta mwafaka wa hatma ya ndoa husika.Kuna wengi waliokimbilia kuoa kwa ajili ya "kufuata kanuni za dini",kuwapendeza wazazi,kujijengea heshima mbele ya jamii,nk lakini baadhi yao wanatamani wangetafakari kwa makini zaidi kabla ya kuchukua uamuzi wa kuoa.However,hii haimaanishi kuwa kuwa ndoa nyingi zinakwenda mrama.Ni BAADHI tu.Hoja yangu hapa ni kwamba kwa vile mke (au mume) ni mwenza wa milele katika maisha,NI LAZIMA mhusika ajiridhishe vya kutosha kabla ya kuchukua uamuzi huo.Na ni vigumu zaidi kwa Wakristo ambao sheria za ndoa hazihalalishi talaka (nadhani iko hivyo kama sijakosea).

Vilevile kuna sababu kama UCHUMI au MALENGO YA MAISHA.Kama mtu hamudu maisha yake mwenyewe basi ni dhahiri akichukua mtu mwingine (ambaye kuna uwezekano mkubwa akawa tegemezi)atakuwa na wakati mgumu maradufu.Na wapo baadhi ya wale ambao wamejipangia kuwa masuala ya ndoa/kuanzisha familia yatafuata baada ya kukamilisha malengo flani katika maisha.

Pamoja na sababu nyingine,nadhani pia kuna suala la maamuzi binafsi (rational choice) yanayotokana na uchambuzi wa faida na hasara ya tendo (cost-benefit analysis).

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

labda mzee wa changamoto kaongea vizuri na kuuliza maswali mazuri kwamba ninani wa kuniambia sasa nimeoa tofauti na mimi na yule nimuowaye!

ndoa ninini na nikaujina fulani ambako sipendi kukasikia. eti mnaenda kanisani harafu padre anasoma vitabu vilivyoandaliwa na wazungu, anawavalisha chuma cha mviringo, eti sasa mu-mwili mmoja. harafu padre mwenyewe ni single!!!!

wengine mnasubili wazazi wawapangie, hamjui kama nyie na wazazi wenu ni tofauti kabisa japo mliwapitia wao kuja duniani. hakuna maadili kumomonyoka hapa kwani hakunaga maadili jumla ambayo kila mwanadamu analazimika kufuata, ieleweke hivyo!!

binadamu wa leo amejifananisha na mali sana kiasi kwamba anahofu juu ya mali.

hata hivyo koero umeongelea mapungufu ya wanauma kana kwamba wanawake ni malaika. nyie mnasubili kupelekwa tu! kwa nini usiniambie unanipenda na tuishi sote? umekamilika binti na waweza amua pia. msisubili kutongozwa, mtadanganywa, tongoza wenyewe!!

maisha hayajawahi kuwa magumu wala kuwa rahisi, ni tafsiri tu. wanaume tunafuliwa pikiwa, nk. lakini pia nasi kuna vitu tunatoa!

mwanamke ni muhimu agawe mwili wake kwa mwanaume kama anataka kuzaa na mwanaume hivyo hivyo. nahitaji mwanamke anayehitaji mwanaume!

kuogopa kulea watoto nao ni uchizi kwani wewe mbona ulilelewa?

unawaonya wasichana wenzio wasitoe --- mpaka waolewe, inafuatana na tafsiri yako ya ndoa. pia kumbuka kuna wasichana wasiotaka kuolewa lakini wanataka --- sasa hao unawaambiaje?

kweli mwanamke ni muhimu sana kwa mwanaume lakini mke pia inabidi awe imara sio kujilegeza legeza. binafsi napenda mke anayejiamini asiyeniona kama mungu wake, mke wa kunibishia na kunipa changamoto, sio lelemama. mke asiyetanguliza mala wala utajiri mbele yangu. I love women 4 I love my mom, sis, gf, womenbloggerz, etc

Simon Kitururu said...

DUH!

MARKUS MPANGALA said...

Mmmmmmmmmmmmmhhhhhhhhhhhhhh! miye simo kabisaaaaaa

Esther said...

naomba comments juu ya ushauri wa watu walionishauri juu ya TITUS MATHIAS TOSSY WIKI ILIYOPITA. KWANI ALIKUWA MWINJILISTI MSABATO LEO ANAISHI UZINZINI NA HAWALA. USHAURI