Monday, February 9, 2009

KUSENGENYA: TABIA ISIYO NA MWISHO MZURI

Mwisho wake ni maumivu

Hebu chukulia umechelewa kufika kazini , unapofika ofisini unasikia sauti za wafanyakazi wenzako wakizungumza kwa ndani, unapofungua mlango na kuingia, ghafla wananyamaza na kukuangalia kwa mshangao!
Jiulize walikuwa wanazungumzia nini?

Kwa kuangalia mfano huo kwa haraka utagundua kwamba walikuwa wanazungumzia jambo linalokuhusu au walikuwa wanakusengenya. Kwa mujibu wa watafiti mbalimbali, imethibitishwa kuwa wanawake na wanaume wote wanasengenya, labda kinachowatofautisha ni uwiano kwamba wanawake ndio wasengenyaji wazuri zaidi ya wanaume.

Hebu jaribu kutembelea kwenye saluni za kike, utakuta hakuna kinachozungumzwa huko zaidi ya kusengenya, tena kibaya zaidi ni usengenyaji wa kubomoa na kuharibu umaarufu wa watu wengine. Kama wamemtembelea mwenzao au kuhudhuria mazishi ya msiba unaomhusu mwenzao, shuhudia mazungumzo yatakayotawala wakati wanarudi.

Njia nzima mjadala utakuwa unahusu maisha ya mwenzao, kwamba hana hiki , hana kile, au mazishi hayakuwa mazuri kama ya fulani, pia hata kulinganisha thamani ya jeneza la maiti na umaarufu wa mhusika. Utawasikia wakisema “kuringa kote kule kumbe si lolote wala si chochote, ndani kwake kubaya, hana hata kitu cha thamani ukilinganisha na mavazi yake na umaarufu wake”.

Litazungumzwa hili na lile ilimradi tu kumbomoa mhusika. Hivi karibuni niliamua kufanya kautafiti kadogo pale ilipo biashara yangu kwa kuwauliza baadhi ya wateja wangu na wapita njia wengine. Nilizungumza na baadhi ya wanawake pamoja na wanaume kadhaa kuhusu hili suala la kusengenya. Dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Sharifa, alithibitisha kuwa ni kweli sisi wanawake tunaongoza kwa kusengenya, lakini alitetea kuwa kuna tofauti ya kusengenya na kumzungumzia mtu au watu kwa mazuri na mafanikio yao.

Sharifa alibainisha kuwa sio vibaya kumzungumzia mtu kutokana na mafanikio yake, kwani hiyo kuwapa fursa ya kujifunza kulingana na mafanikio ya mwenzao, pia hata wanapozungumzia mapungufu ya mtu, hiyo ni kwa ajili ya kujifunza kutokana na mapungufu ya mwenzao. Dada mwingine aitwae Bupe, alisema kuwa hata wanaume nao husengenya, yeye alishawahi kumfuma mvulana ambaye punde tu alitoka kufanya naye mapenzi akiwasimulia wenzake jinsi yeye (Bupe) alivyo awapo kitandani, kuanzia mwili wake hadi namna anavyofanya mapenzi.

Ukweli ni kwamba hakuamini tukio lile kwa sababu mvulana aliyemwamwini na kuamini kumkubali kuwa mpenzi wake baada ya kumtongoza kwa muda mrefu, angeweza kusimulia yale yote aliyoyasikia. Kibaya zaidi hata wale waliokuwa wakisikiliza ule utumbo walionekana kwa nje, kuwa ni watu wenye busara. “Usiwaone wamekaa kwenye makundi wakizungumza ni wasengenyaji wazuri sana, tena usidhani wanajadili jambo la maana, sanasana wanazungumzia wanawake wale waliotembea nao alisisitiza Bupe”.

Kijana mmoja aitwae Dikupila ambaye anamiliki saluni ya kunyoa nywele jirani na ofisi yangu, kwa upande wake aliyewatetea wanaume kuwa siyo wasengenyaji, kwani hayo ni mambo ya wanawake. “Sisi wanaume kusengenya! Haiwezekani, hayo ni mambo ya wanawake, sana sana ukikuta mwanaume anajadili udhaifu wa mpenzi wake hadharani basi ujue huyo jamaa anamatatizo makubwa ya kiakili” alisema Dikupila.

Watu wengi wa jinsia tofauti niliobahatika kuzungumza nao walikuwa wanakiri kusengenya lakini walikuwa wanajaribu kutengeneza fasili ya neno kusengenya kwa namna ya kukidhi haja zao. Kwao kusengenya walisema ni mtu kutafuta namna ya kujifunza kuwa bora kupitia makosa ya wengine. Je tabia hii inaweza kuachwa? Wengi walikiri kwamba siyo rahisi tabia hiyo kuachwa kwani imekuwa ndiyo sehemu ya maisha, kwamba haiwezekani watu kukaa pamoja na kuacha kuzungumza matukio na yanapozungumzwa matukio, ni lazima yatawahusu watu hivyo kujikuta watu wanasengenya.

Na tabia hii imejikita kila mahali kuanzia nyumbani, mitaani, hadi maofisini, mashuleni na vyuoni. Binafsi naamini kwamba tabia inaweza kuachwa kwa watu wakijikita zaidi katika kufanya kazi na kuwa wabunifu, hasa maofisini. Kama ni suala la mazungumzo iwe ni ya kuleta ufanisi na tija katika kazi kwani waajiri hulipa mishahara kutokana na ufanyaji wetu wa kazi na uzalishaji.

Utakuta mtu anafika kazini amechelewa na akifika anaanza kusengenya, atazungumzia hili na lile wakati muda unaenda na muda wa kazi ukiisha anafunga kazi na kuondoka. Ukichunguza utakuta tangu asubuhi hakuna chochote alichofanya zaidi ya umbea. Watu wa aina hii wanakuwa wa kwanza kulalamika mishahara ikichelewa. Yapasa watu kubadilika na kutia shime katika ubunifu.

Majumbani na mitaani vilevile nako hapafai. Kwa mfano utakuta mtu ana saluni yake na ana wateja wengi wanasubiri kuhudumiwa lakini wahusika utawakuta wanatumia muda mwingi kusengenya na hivyo kupoteza muda bure. Wale wateja wenye haraka kwa kawaida huwa wanaondoka na kutafuta mahali pengine. Hivyo ikiwa watu watajirekebisha kwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha tabia ya kusengenya naamini nchi hii uchumi wake utakua kwa kiwango kizuri na kila mtu atafaidi matunda ya jasho lake.

Ni vema kama mtu hawezi kusema jambo lolote zuri kuhusu mwenzake akakaa kimya, kwani ni njia bora ya kusitiri heshima yake.

3 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Nasio aliwahi kuimba kwenye wimbo wake wa Dangerous akasema "don't worry about the pretty things you hear them (they) say, don't trust no enemy can trust no friend". Japo lugha zaidi ni patois ambayo grammar yake (kama ipo) ni tofauti na kiingereza, lakini analosema ni kuwa kusimuamini mtu kwa kila anachosema machoni mwako. Ndilo lililomkuta Dada Bupe. Well, kusengenywa hakufai kwa namna yoyote ile, japo wapo wasikiao masengenyo wakabadilika kutokana na kuogopa kuwa wahanga wa yaliyowakuta wenzao. Ndio yale ya ukiona mwenzio ananyolewa. Sasa wanaposengenya mtu mwenye kazi nzuri na pesa nyingi wakati maisha ya watoto wake ni duni kwa kuwa tu anaendekeza ulevi, kama kuna aliyepo pemeni na akasikia hayo na yeye ni kama asengenywaye ujue inaweza kuwa "turning point".
Lakini Da Koero, mara zote athari za usengenyaji hutokana na hatua azichukuazo msengenywaji.
Akiamua kuendeleza ubishani na magomvi nao anawapa la kusema, akiamua kujifunza kitu na kujijenga kutokana na mapungufu atakayojifunza atakuwa amenufaika. Lakini sasa, ni mpaka ajue anachosengenyewa na nia hasa ya kusengenya ni kumsema mtu na asijue kuwa anasemwa.
Kwa hiyo usengenyaji si mzuri kama ulivyosema na unapaswa kuachwa, na badala yake watu wawe na ujasiri wa kuhoji na kueleza hisia zao kwa "wapendwa" wao uso kwa uso maana hilo litaonesha wajali na litajenga zaidi.
Amani kwako na kwenu pia

Simon Kitururu said...

Tatizo ni jinsi jamii iuchukuliavyo usengenyaji mpaka tuna magazeti kibao ambayo kinamna ni ya kisengenyaji na ndiyo yanunuliwayo kwa wingi kwa sababu jamii inahamu yakujua yasiyo ya maana MPAKA kama ni kweli mheshimiwa ni kweli ana chupi moja au LA.:-(

Nachojaribu kusema ni ; katika usengenyaji mengi ni uongo na yasiyo na manufaa.

Udhaifu wa kuvumilia uongo uliopo mpaka UKWELI ujitokeze ndio usababishao tutapetape kujitetea au hata kugombana ili kutaka kuharakishia umati ujue usengenywayo ni ya uongo.

Naamini kama ni mvumilivu na usengenywayo ni ya uongo, toa muda tu UKWELI utajulikana na asengenyaye atajulikana mpaka ni kwanini anataka kudadisi na kuongelea yasiyomuhusu.

MARKUS MPANGALA said...

nawaza, nawaza. kaka zangu wamemaliza yote ASANTENI