Wednesday, February 11, 2009

NDOA NYINGI NA TALAKA NYINGI!

Siku hizi hazidumu!

Hivi karibuni nilibahatika kusoma mahojiano ya Mwanamuziki wa kundi la zamani la muziki, maarufu kama Spice Girls la nchini Uingereza Geri Halliwell. Nilisoma mahojiano yake mtandaoni aliyoyafanya na Gazeti la Woman’s Day la nchini humo.
Labda niwakumbushe wale wasiolifahamu kundi hili la Spice Girls.Kundi Hili liliwahi kuvuma sana miaka ya 90 nchini uingereza likijumuisha wanamuziki wanne, Victoria, aliyeolewa na Mchezaji maarufu wa soka nchini Uingereza David Beckgham, Emma, Melanie na Geri Halliwell.

Katika Mahojiano hayo, mojawapo ya maswali aliyoulizwa na mwandishi, ni hili la yeye kutoolewa pamoja na kwamba ana mtoto. Majibu yake kwa swali hilo ndio yaliyonisukuma nikae kitako kwenye Kompyuta yangu na kuandika makala hii.
Akijibu swali hilo, Geri alisema kwamba hana imani kabisa na maisha ya ndoa, na ndoa kwake sio mojawapo ya agenda zake katika maisha.

Alisema katika kizazi hiki familia nyingi zimeshuhudia kuvunjika kwingi kwa ndoa kama ilivyotokea kwa wazazi wake. “Katika makuzi yangu nimeshuhudia ndoa nyingi zikivunjika mpaka nimefikia kuona kwamba ndoa hazina maana kabisa” alisema Geri.
Aliendelea kusema kwamba haoni ndoa hata moja ya mfano ambayo anaweza kuitumia kama Dira yake inayoweza kumshawishi kuolewa, ingawa anapenda sana kuwa na watoto wengi.

Siku hizi hapa nchini vijana wengi wamekuwa wakifunga ndoa kila uchao, lakini hata hivyo Talaka nazo zimekuwa zikiongzeka vile vile. Ndoa zimekuwa nyingi sana kwa sababu watu huoana kiholela. Kuoana kumekuwa rahisi na kusiko kujiuliza mara mbili, ukilinganisha na zamani. Kwa sababu hiyo ndoa zinavunjika sana. Kwa kuangalia ukweli huo utagundua kwamba talaka siyo nyingi sana bali ndoa za hovyo ndiyo nyingi, kwani huanza ndoa na talaka hufuata.

Wanaume na wanawake na hata wavulana na wasichana huoana bila ya kujua sababu ya kuoana kwao. huona kwa sababu wameambiwa kuna kuoana, huoana kwa sababu umri unaenda au kwa sababu watu wameona watu fulani wakiwa na furaha wakidhani ni kwa sababu ya ndoa.

Wazazi nao wanawalazimisha au kuwashinikiza vijana wao kuoa au kuolewa wanataka kuona tu kwamba nao wana wajukuu, wanataka kujua vijana wao wakiwa na wenzi wao ili wajisikie vizuri. Wanaogopa kuambiwa, ‘binti wa fulani hajaolewa mpaka sasa hivi’ au ‘vijana wa fulani wahuni tu hawataki kuoa’. Wazazi nao hawana sababu ya kwa nini vijana wao waoe au kuolewa.

Kuna haja ya wazazi kuwafanya au kuwasaidia vijana wao kujijua vizuri wenyewe, kabla hawajaingia kwenye uhusiano wa dhati wa kindoa. Inabidi kijana ajiuluze kama yu tayari kwa ndoa na je hana jambo ambalo litamzuia au kumfanya ashindwe kutimiza wajibu wake wa ndoa, kwa mfano masomo, kazi na mengine?
Je kijana anaamini nini kuhusu ndoa yaani ndoa kwake ni nini? Kama kwake ndoa ni kupata furaha, kukimbia matatizo ya nyumbani, kuzaa, kuwa huru kuamua mambo yake na sababu nyingine kama hizo inabidi ajiulize tena na tena kama sababu hizo ni sababu za msingi.

Wanaoingia kwenye ndoa siku hizi wengi hawajiulizi kama wako tayari kupata watoto. Unakuta mwanamke akizaa wanaanza kuhisi kwamba walikosea kuoana na hapo kutoka nje huanza na hata kutekelezana wakati mwingine. Hata kama wanataka watoto huwa hawajapanga namna ambvyo watawalea na kama wangependa kuwa na watoto wangapi na maswali mengine kama hayo.

Lakini, kunakushindwa kwingi katika kujiuliza ni kwa kiasi gani mtu anawaza kuwakubali wengine na kuyachukua matatizo yao. Ni vema kijana akajiuliza kama anaweza kuvumilia kasoro au udhaifu wa wenzake kama anaweza kukabili mabadiliko ambayo yanaweza kutokea kwenye uhusiano.

Siyo mtu kujijua peke yake lakini hata kumjua mwingine ni tatizo pia. Mtu anaingia kwenye uhusiano wakati hamjui vema anayeoana naye. Anamjua kwa sura na mwili ndiyo lakini zaidi ya hapo hajui kingine chochote kuhusu huyo mwingine, hajui kwamba ni Malaya, hajui kuwa ni mchoyo, hajui ni mkata tamaa, hajui kama ni “mtoto wa mama” hajui chochote kumhusu.

Unakuta watu wamekubaliana kufunga ndoa, lakini mmoja au wote hawajuani mwingine anatokea wapi hasa. Anasena tu “wazazi wake sijui ni wenyeji wa wapi, sijui Tanga vile, sijui Iringa!”

Ukweli ni kwamba bila kumjua mtu vizuri ni hatari kuoana naye. Wakati mwingine wenzetu ni watu wanaozalisha nguvu hasi nyingi duniani, wakorofi wenye kijicho, walipa visasi, wenye zarau, wapenda shari na mengine. Lakini kwa sababu wanatutendea vema katika wakati fulani tunaamini hawana tatizo.

Wasichana wengi wanakubali kuoana na wanaume ati kwa sababu siku hizi hakuna wanaume. Ni nani amesema hakuna wanaume? Msichana ameona kabisa kijana ni mgonvi na pengine ameshawahi hata kumpiga lakini anajiambia “nikimkosa huyu ndiyo basi sitoolewa tena” kisha anaolewa na wanaishi kwa mwaka mmoja tu.

Wanalazimika kuingia kwenye uhusiano ambao wanaona kabisa hautadumu. Hufanya hivyo kwa hofu ya kuwa wapweke. Wanaogopa sana kubaki bila kuolewa kwa sababu eti wamesikia mtaani kwamba wanaume hawapatikani kirahisi. Aibu tupu!
Mara nyingi vijana wanaongozwa na kuhemkwa badala ya tafakari katika kuingia kwenye ndoa. Wanapokuwa kwenye uhusiano kuhemkwa kunaisha na wanarudi kwenye hali halisi ambayo wanashindwa kuibeba.

Kuhemkwa huku ndiko wenyewe wanakokuita kupenda. Wanasema kabisa “nimependa sana siwezi kumwacha pamoja na kunipiga na umalaya wake” Ebo! Mtu ni Malaya na kama hiyo haitoshi bado huwa anakupiga halafu unasema huwezi kumwacha? Kama huo si uwendawazimu ni nini?

Mara nyingi nyingi kuhemkwa kunaisha wakiwa tayari na watoto wawili na maisha wakati huo yanakuwa yameharibika. Wengine kuhemkwa kunaishi wakiwa tayari na ukimwi, wengine wakiwa na chongo, na wengine wakiwa na BP na kisukari juu, kwa sababu ya maumivu makubwa ya kihisia.

Kuna watu wazima ninaowajua ambao nao wameshabadili wake na wanaume mara kadhaa. Kila ndoa wanayoingia inabomoka. Kisa ni kufuata mihemko badala ya kufuata hekima. Hawajifunzi ndoa ya kwanza wala ya pili, wanatembea na kosa lilelile, yote hiyo ni kuhemkwa badala ya kujua na kupenda.

Nakubaliana na Geri Halliwell kwamba, kuna talaka nyingi. Lakini kama nilivyosema, nadhani kuna ndoa za kuhemkwa nyingi, na ndizo zenye kusababisha talaka nyingi.

2 comments:

MARKUS MPANGALA said...

Kwanini watu wanaoa au kuolewa, kwanini wanaoana? Kwanini watu wanatoka nje, kwanini wanatoa talaka, kwanini wanakubali kuoana? Kwanini kuoana? kwanini iwe lazima kuoana? kwanini iwe kama ilivyo?
Sijui lakini nasema hivi, kama ndoa ni halali ya mwanadamu basi kuachana ni halali ya mwanadamu LAKINI tukumbuke hata mpanzi alipopanda mbegu zingine zilipandwa mibani na zingine mwambani, lakini zile za kwenye ardhi nzuri zilizaa udongo mzuri.
Jendoa zetu zinaongozwa kwa falsafa gani? Mapenzi yetu yanakwenda kwa itikadi gani? Au tunaiga mambo ya kununu maua,zawadi,mabusu hadharani,kukumbatiana hadharani,kuongozana kama kumbikumbi nk.?
Kwanini mtu anakuwa malaya? au kwanini anatoka nje?
SWALI: nini kinachosababisha kuwa malaya? kinachotumika kwa umalaya ni nini? Na kwanini umalaya au kutoka nje ni tabia za wanandoa? kwanini ndoa hazidumu hata tukupigana makofi ya mawili kwa tofauti ambayo tumekosa falsafa na itikadi. KUMBE tunaiga kila kitu toka ughaibuniDUH! majuzi kuna ndoa ilifungwa na sherehe ikafanywa pale jirani Movenpick nyooooooo! eti bi harusi baada ya fungate kabanduliwa na X wake!!!! ha ha ha ha ha ha niliangua kicheko..... lakini jamaa kasema hakuna noma.
SWALI kwanini wanadamu wanafunga ndoa? Muungano wa watu wawili, nini kinachowaunganisha?
NAWAZAAAAAAA lakini jibu sipati
Basi ngojeni Lucky Dube awakumbushe simulizi zake katika IT IS NOT EASY..... halafu anasema 'the choice that i made, didnt workout!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mpangala umenena hili swala pia nitete ni kwa nini tunaoana hata hatujua na wala hatuko tayari kujua.